Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Fedha na Mipango

Hon. Khadija Nassir Ali

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Fedha na Mipango

MHE. KHADIJA N. ALI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru nami kwa kunipatia nafasi ya kuchangia kwenye Wizara hii ya Fedha na Mipango. Kwanza kabisa napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa afya ya kuweza kusimama hapa leo lakini pia napenda kuwapa heri ya mfungo wa Ramadhani Waislam wote duniani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa vile dakika zangu ni chache, naomba sasa nijikite moja kwa moja kwenye mchango wangu na nitaanza kuongelea mtiririko mzima wa fedha za miradi ya maendeleo. Mwaka wa fedha 2015/2016, fedha zilizotengwa kwenye bajeti ya miradi ya maendeleo ilikuwa ni bilioni 1,031.7 na kwa mwaka wa fedha 2016/2017, fedha zilizotengwa ilikuwa ni bilioni 791.9.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ingawa Serikali imepunguza budget ceiling ya hizi fedha za maendeleo lakini bado tatizo la kupeleka fedha hizi kwenye miradi imekuwa ni changamoto kubwa. Mfano, katika mwaka wa fedha wa 2016/2017, Wizara iliidhinisha jumla ya shilingi bilioni 791.9 lakini mpaka kufikia Machi, 2017 Serikali ilikuwa imepeleka jumla ya shilingi bilioni 18.8 ambayo ni sawa na asilimia mbili tu ya bajeti ambayo imeidhinishwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu kwa Serikali juu ya hili ni kwanza, Serikali kupitia Bunge iidhinishe bajeti ambayo itaweza kwenda ipasavyo na siyo kuidhinisha bajeti kubwa ambayo haitaweza kwenda. Bajeti za Wizara ziendane na kasi ya makusanyo ya mapato.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu wa pili; muda muafaka sasa kwa Serikali kuhakikisha fedha zote zinazoidhinishwa kwa ajili ya matumizi ya maendeleo zipatikane kwa wakati ili kuendana na kasi ya Mheshimiwa Rais ya kujenga Tanzania ya viwanda. Ushauri wangu wa tatu; Serikali isitegemee sana fedha za wafadhili kwa sababu fedha hizi hazina uhakika wa kutosha, zinaweza kuja au zisije au zikaja kwa kuchelewa na hili linaweza kuathiri maendeleo ya miradi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla sijamaliza kuongea kwenye hili suala naomba Waziri atakapokuja kuhitimisha anipe majibu ya maswali haya yafuatayo:-

Huu mpango wa Serikali kuhamia Dodoma; Je, Serikali imetumia kiasi gani cha fedha katika mpango huu? Pili; Je, mpango huu umeathiri vipi fedha za umma ambazo zingeweza kupelekwa kwenye miradi ya maendeleo? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sasa niingie kwenye suala la misamaha ya kodi. Serikali imekuwa ikitoa misamaha ya kodi kila mwaka lakini bado misamaha hii haitolewi kwa uwazi kwa maana ya kwamba mimi na wewe na wananchi wengine hatujui misamaha hii inatolewa kwa vigezo gani. Wabunge na wananchi tunahitaji kujua projection ya misamaha hii lakini pia tunahitaji kujua uhalisia wa misamaha hii, pia ushauri wangu kwa Serikali ni kwanini isiwe ina-publish misamaha hii ili tuweze kujua kiwango na watu ambao wanasamehewa hizi kodi ni akina nani na wanatolewa kwa vigezo gani? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sasa nigusie kidogo issue ya deni la Taifa. Kwa mwaka wa fedha 2016/2017 malipo ya deni la Taifa ilikuwa ni bilioni 8,000 matumizi ya kawaida kwa mwaka huu yalikuwa ni bilioni 8,009.3 na kwa mwaka wa fedha 2017/2018 malipo ya deni la Taifa yanatarajiwa kuwa bilioni 9,461.4 na matumizi ya kawaida yanatarajiwa kuwa bilioni 9,472.7. Naipongeza Serikali kwa hili, kwa kuwa wameweza kuongeza bajeti ya malipo ya deni la Taifa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, rai yangu kwa Serikali ihakikishe kuwa fedha hizi zinatolewa kwa wakati ili nchi iondokane na madeni yanayosababisha nchi kulipa fedha nyingi yaani ile fedha inayotoka kama riba ingawa Serikali inasema kwamba deni la Taifa ni himilivu lakini lazima Serikali iendane……………..

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)