Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Fedha na Mipango

Hon. Devotha Methew Minja

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Fedha na Mipango

MHE. DEVOTHA M. MINJA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba na mimi nichangie kwa maandishi hotuba ya Waziri wa Fedha na Mipango. Baada ya kumsikiliza sana kwenye uhamasishaji wa Wabunge kuunga mkono hoja ya Wizara hii ni lazima tushauri ili kusaidia maendeleo ya Taifa letu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wafanyabiashara kama wadau muhimu wanaotegemewa na Taifa kuongeza mapato, wako katika wakati mgumu sana na wengi wamefunga biashara zao hasa katika kipindi hiki cha Serikali ya Awamu ya Tano kutokana na kuelemewa na kodi nyingi zisizo na tija. Kwa nini wafanyabiashara wasipewe fursa wezeshi za kuwezesha wafanye biashara hizi wapate faida na waweze kulipa kodi bila kukimbizana? Serikali lazima ifungue milango ya biashara na kuwaona wafanyabiashara ni marafiki na wadau muhimu wanaotakiwa kusaidiwa ili biashara zao kuwa endelevu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika taarifa ya Waziri, kwa nini hajaleta taarifa za hali za biashara, kwa nini hajasema wafanyabiashara wangapi wamefunga biashara, wawekezaji wangapi wamehamisha uwekezaji au wamesitisha uwekezaji wao? Waziri angeleta status ya hali ya biashara nchini na challenges zilizopo ili tuone mikakati ya Serikali ya kufufua biashara hizi au kuhamasisha wafanyabiashara kurudi kwenye biashara zao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nchi za Afrika Mashariki mfano Rwanda mifumo yao ya kukusanya mapato ni rafiki na kila mfanyabiashara anajikuta anaona umuhimu wa kulipa kodi/mapato kwa faida ya Taifa lake. Kwa nini tusiige mfumo huo ambapo hata ukitokea biashara imekufa wanapeleka wataalam wa biashara, wanazungumza nao na kuwapa indoor training jinsi ya kufufua biashara badala ya hivi sasa biashara ikifa hamna anayejali hata Serikali haioni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Benki ya Wanawake (TWB), tumesikia hadithi za kuwa benki hii itapeleka matawi mikoani. Je, kwa nini Benki hii ya Serikali iliyoanzishwa kwa ajili ya kutoa ahueni kwa wanawake imebaki kuwa ya watu wachache kwa maana ya mikoa michache? Benki zingine zimeanzishwa nyuma baada ya TWB sasa hivi zina matawi karibu kila mkoa, kuna shida gani kwa nini benki hii ya Serikali isifungue matawi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, interest ya Benki hii ya Wanawake ni kubwa hata kuzidi Benki ya Posta, kwa nini? Lengo la benki hii ni kusaidia wanawake wapate fursa za kukopa na kuendeleza ujasiriamali lakini cha kushangaza inaonekana kuwa na interest za juu hali inayopelekea wanawake wengi kushindwa kumudu gharama hizi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali iwe na mipango mipya ya kupata vyanzo vya mapato, wataalam wabuni vyanzo vipya vya mapato kupitia miradi mipya ya kilimo, uvuvi na mifugo ambapo zipo nchi zimeendelea kwa kutegemea blue economy yaani uvuvi tu. Kwa nini Serikali isifikirie uwekezaji kwa maana ya kuwa na wataalam ambao watalipatia Taifa mapato badala ya hivi sasa inakimbizana na wavuvi haramu na kuingia gharama nyingi za kuharibu nyavu?

Mheshimiwa Mwenyekiti, baadhi ya wawekezaji wameanza kufunga viwanda. Kwa nini Serikali haifanyi utafiti na kuja na mawazo/mbinu za ku-retain wawekezaji badala ya kukaa kimya na kusubiri wawekezaji wapya?