Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Fedha na Mipango

Hon. Ritta Enespher Kabati

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Fedha na Mipango

MHE. RITTA E. KABATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze na kumpongeza Waziri, Mheshimiwa Dkt. Mpango; Naibu Waziri, Mheshimiwa Dkt. Ashatu Kijaji, Katibu Mkuu na Watendaji wote wa Wizara kwa uwasilishaji wa bajeti yao hapa Bungeni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati Serikali ikifanya juhudi za kurasimisha biashara zisizo rasmi, Wizara ya Fedha kupitia TRA haioneshi juhudi za makusudi kuwakomboa wananchi wa hali ya chini kuinuka kiuchumi na kuweza kuchangia pato la Taifa kutokana na taratibu ngumu zilizowekwa kwa wafanyabiashara katika kuanzisha na kuendesha biashara zao. Taratibu hizo ni pamoja na:-

(i) Kumkadiria kodi mtu anayetaka TIN ya biashara na anatakiwa alipe kadirio hilo kabla ya biashara kuanza;

(ii) Kumtaka mfanyabiashara aambatanishe invoice yake ya EFD receipt wakati wa kuwasilisha invoice ya mradi kwa mtu aliyempatia huduma kabla hata yeye hajalipwa, mfano Idara za Serikali ambapo malipo yenyewe hayalipwi kwa wakati;

(iii) Kuwataka wafanyabiashara kununua EFD machine kwa fedha zao chache za mtaji wakati EFD ni machine inayoiwezesha TRA kukusanya mapato yake. Ni kwa nini tusifanye kama TANESCO ambapo mita ya umeme inakuwa mali ya TANESCO hivyo kuipunguzia gharama ya ufuatiliaji wa madeni ya kodi? Mheshimiwa Rais wetu wa Awamu ya Tano alitoa na kuzigawa bure ili zisaidie kukusanya kodi lakini utaratibu huo ulifanyika kwa kipindi kidogo tu na haukuendelea tena;

(iv) Kuzuia ugawaji wa Tax-Clearance kwa mfanyabiashara anayedaiwa kodi jambo ambalo si sahihi kwani kunamkwamisha mfanyabiashara huyo kuendelea kufanya biashara ili aweze kupata fedha ya kulipia deni la kodi anayodaiwa ukitilia maanani kuwa hata leseni haitolewi kwa mtu asiyekuwa na Tax Clearance. Kwa nini usiwepo utaratibu mwingine wa kumruhusu huyu mtu akaendelea kufanya biashara wakati mwingine anakuwa anakadiriwa makadirio ya kodi makubwa kuliko pato halisi. Akinyimwa Tax Clearance anashindwa kuomba kazi matokeo yake anafunga biashara. Serikali inawavunja moyo wasifanye biashara halali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naipongeza Serikali kwa kuanza kulipa madeni ya wazabuni kiasi cha shilingi bilioni
796.22 kati ya kiasi cha shilingi trilioni tatu kinachodaiwa. Hata hivyo, bado wazabuni wengi wanadai labda ni vizuri Serikali itangaze katika magazeti wazabuni waliohakikiwa na wale waliolipwa madeni ili waweze kujua sababu kuna wengine walikuwa wanadai lakini hawajui hatima yao mpaka leo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Benki ya Wanawake ilianzishwa ili kuweza kuwasaidia wanawake kupata mtaji wa biashara baada ya kuona udhalilishaji mkubwa wanaopata katika baadhi ya taasisi. Mwaka 2010 Serikali ilitoa ahadi ya kuipatia Benki ya Wanawake shilingi bilioni 10 kwa miaka mitano maana yake shilingi bilioni mbili kila mwaka. Mwaka 201/2012 – Serikali ilitoa shilingi bilioni mbili; 2012/2013 – Serikali ilitoa shilingi bilioni 1.75 na 2013/2014 – Serikali ilitoa shilingi bilioni 1.5. Jumla Serikali imeweza kutoa shilingi bilioni 5.75. Je, shilingi bilioni 4.25 itatolewa lini?

Mheshimiwa Mwenyekiti, TIB (Tanzania Investment Bank), Tanzania tunaelekea kwenye uchumi wa viwanda lakini bila kuiwezesha benki hii tutapata shida sana, sababu ndiyo benki itakayosaidia kuwezesha miundombinu ya viwanda. Serikali iliahidi kuipatia mtaji wa shilingi bilioni 500 na tena shilingi trilioni tatu lakini walipatiwa shilingi bilioni 150 tu. Je, nini mkakati wa kuisaidia benki hii?

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.