Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
HE. MAIDA HAMAD ABDALLAH: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa nafasi hii. Naipongeza sana Serikali kwa juhudi zake za kuleta maendeleo nchini. Nampongeza sana Mheshimiwa Waziri wa Fedha na Mipango, Naibu wake na timu yake yote ya wataalam inayowasaidia kutekeleza kazi zao vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, moja kwa moja niende kwenye utaratibu wa kupunguza umaskini. Vigezo vya MKUKUTA I na II ni kuwa na wastani wa kila mtu kutoka Sh.770,464.3 mwaka 2010 hadi Sh.1,918,928/= mwaka 2015 kwa mujibu wa Mpango wa Taifa 2016/2017. Pia kasi hiyo inaendana na matarajio ya kutoka asilimia 24.5% iliyokuwepo mwaka 2015 na kushuka hadi kufikia 16.7%. Njia kubwa ya kuondoa umaskini ni pamoja na kujitosheleza kwa chakula.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sote tunafahamu kwamba upatikanaji wa chakula kwa wingi chanzo chake ni upatikanaji wa mbegu bora, tafiti na umwagiliaji na bajeti ya kutosha kwenye mahitaji ya kilimo. Ni kwa nini bajeti ya kilimo inaendelea kutengwa ndogo ambapo inahitaji mipango ambayo inaweza kuendeleza kilimo na kuweza kujitosheleza kwa chakula ili kuondoa umaskini?
Mheshimiwa Mwenyekiti, wanafunzi au wahitimu waliochukua mikopo kwa ajili ya kujiendeleza. Wahitimu hawa waliingia mkataba na Bodi kwa kukubali kulipia 5% baada ya kumaliza masomo bila riba. Jambo la kusikitisha au linalowashangaza wengi ni kwa nini wameitwa wadaiwa sugu wakati wengi wao wapo kwenye Wizara za Serikali?
Mheshimiwa Mwenyekiti, pili Serikali imewashtukiza kwa kuongeza riba ya kutakiwa kulipa asilimia 15 badala ya 5% iliyokuwa awali. Ni kwa nini kwa vile wapo kwenye Wizara, Serikali isiwe inakata marejesho ya mikopo hiyo bila riba baada ya kurudi kwenye Wizara zao? Sheria ya kuongeza riba kwa mikopo hiyo ni kuwapa adhabu, kwani wengi wao ni maskini sana, hawana uwezo wa kifedha na hawataweza kujiendesha kimaisha. Ni vema kubaki na 5% kama awali ya mikataba yao inavyosema.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ilitoa kauli kwamba mwaka 2015, Benki ya Wanawake ilifikia mtaji wa shilingi bilioni 20, lakini pia ilifungua vituo vya kutoa mafunzo na mikopo katika mikoa mbalimbali, jumla ya wananchi 12,874 wakiwemo wanawake 9,693. Nataka kujua miongoni mwa wananchi waliopatiwa elimu hiyo kwa upande wa Zanzibar, imejipanga vipi? Kwani mtaji wa Benki ya Wanawake, baadhi ni michango ya hisa za Waheshimiwa Wabunge toka Zanzibar na hati za uthibitisho zimetolewa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Tume ya Pamoja ya Fedha, katika hotuba ya Mheshimiwa Waziri, kwa ujumla mashirika tisa yanayotekeleza masuala ya Muungano kwa sehemu kubwa mtaji wake ulitokana na Tanzania bara. Ni kweli, swali, je, kama mtaji umetokea upande mmoja wa Muungano, lakini upande wa pili ukawa umewekeza na rasilimali, taratibu za kimapato kwa mujibu wa sheria za nchi na Katiba ya 1977 zinasemaje?
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.