Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Fedha na Mipango

Hon. Dr. Christine Gabriel Ishengoma

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Fedha na Mipango

MHE. DKT. CHRISTINE G. ISHENGOMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kupata nafasi hii kuchangia kwa maandishi ndani ya Bunge lako Tukufu. Napenda kutoa pongezi kwa Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri, Katibu na Wataalam wote katika Wizara hii ya Fedha na Mipango.

Mheshimiwa Mwenyekiti, fedha za maendeleo zilizotolewa Hazina ni shilingi bilioni 5.8 kati ya bilioni 740.15 ya fedha zote zilizoidhinishwa na Bunge (sawa na asilimia 0.8), namna hii ya utoaji fedha za maendeleo kidogo (asilimia 0.8) ni dhahiri kwamba Hazina haijafanya vizuri kadri ilivyopangwa awali katika mambo ya maendeleo. Naishauri Serikali kuwa mara fedha zinapopatikana ziwe zinatolewa kadri zilivyopangwa na kupitishwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kumshauri Mheshimiwa Waziri kuwa ingawaje bado deni la Taifa linalipika, tuwe tunalipa kadri ipasavyo. Serikali ijitahidi kwanza kwa vyovyote vile kulipa deni hili la Taifa, jambo hili litasaidia kuendelea vizuri na miradi ya maendeleo kwa hiyo, pale inapowezekana Serikali iendelee kulipa na kupunguza deni hili la Taifa badala ya kuongezeka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inaweza kutoa au kulipa suala hili kipaumbele. Hata hivyo, naipongeza Serikali kwa kipindi hiki, kulipa Shilingi Trilioni 4.64 kwa deni la Taifa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashauri Serikali ihakikishe na kujitahidi ili madeni ya watumishi wote yaendelee kulipwa,ili kuwapatia moyo wa kufanya kazi kwa bidii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukusanyaji wa mapato; Serikali kusimamia mkakati kabambe wa ukusanyaji wa mapato kutoka kwa wafanyabiashara kwa kutumia mashine za kielektroniki (EFD). Ni vema kuwafuatilia wafanyabiashara ili wanaopaswa kulipa kodi wakalipe ni dhahiri wengine wanakwepa eti, hawana mashine au mashine mbovu, kiasi cha kupoteza mapato mengi. Wafanyabiashara hasa wafuatiliwe ili tuweze kupata mapato ya ndani yanayostahili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mradi wa milioni 50 kwa kila Mtaa na kila Kijiji; ni kweli mwaka 2016/2017 hazikutolewa, tafadhali vikundi vya wajasiriamali wanazisubiri kwa hamu. Nashauri hizo shilingi bilioni 60 zilizotengwa kwa 2017/2018 jitihada iwepo, zipatikane na kutolewa kama ilivyopangwa. Naomba niwaambie Mheshimiwa Waziri, kuwa wananchi wanazisubiri sana, nashauri Serikali isichelewe kuanza kutoa fedha hizi angalau kwa awamu, isikike kuwa fedha hizi zimeanza kutolewa, hivyo itekelezwe kama ilivyopangwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu huduma kwa wastaafu; nawapongeza kwa kazi nzuri ya Serikali kwa kuwatambua wastaafu. Nashauri Serikali iendelee kuangalia pensheni zao, bado wale waliostaafu zamani pensheni zao ni ndogo sana. Wastaafu wanaomba na pia nashauri kwa sababu waliifanyia kazi nzuri Serikali yao, mara mishahara inapopandishwa na wenyewe angalau wapandishiwe pensheni yao ili kumudu maisha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu suala la mikopo, ni dhahiri kuwa wananchi kupokea mikopo kwa kutumia hati ya ardhi, bado benki nyingi hawatambui. Ni vema zijulikane benki zinazokubali hati hizi ili wananchi wa kawaida hasa waweze kupata mikopo. Nashauri Serikali, Benki ya Kilimo pamoja na mambo yote iweze kuongezewa fedha ili wakulima wakope kwa urahisi ingawaje matawi ya benki hii bado hayajasambaa mikoani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wote tunatambua kuwa asilimia 65 ya Watanzania wanategemea kilimo, pia viwanda (Tanzania ya Viwanda) vinategemea malighafi ya kilimo, ni kwa nini Serikali isichukue jukumu la kuongeza fedha kwenye Benki ya Kilimo ili wakulima wakope. Pia Serikali iangalie jinsi ya kuwaongezea fedha, Tanzania tunataka maendeleo ya viwanda ni vema wakulima tuwawezesha kwa njia ya mikopo nafuu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.