Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Fedha na Mipango

Hon. Dr. Ashatu Kachwamba Kijaji

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Kondoa

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Fedha na Mipango

NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwanza kabisa nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema, aliyeniwezesha siku ya leo kufika salama na kusimama mbele ya Bunge lako Tukufu kwa ajili ya kuchangia hoja iliyowasilishwa jana na Mheshimiwa Waziri wa Fedha na Mipango.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, napenda niwatakie Ramadhani njema na saumu zenye kukubaliwa wale wote wanaofunga mwezi Mtukufu wa Ramadhani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyosema naomba sasa nichangie hotuba ya Mheshimiwa Waziri wa Fedha na Mipango katika baadhi ya hoja zilizopendekezwa na kuchangiwa na Waheshimiwa Wabunge katika Bunge lako Tukufu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja ya kwanza ambayo napenda kuitolea ufafanuzi ni hoja iliyoletwa na Kamati yetu ya Bajeti nayo ilikuwa inapendekeza kwamba ni muhimu kitengo cha kusimamia Deni la Taifa kufanya tathmini ya ulipaji wa deni la Taifa kwa kuzingatia mapato ya ndani badala ya kutumia vigezo vingine kwa lengo la kuifanya Serikali ikope zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hoja hii napenda kusema kwamba, jambo la msingi ambalo tunatakiwa kujiuliza, ni kwa nini tunakopa? Nim-quote mwanafalsafa mmoja alisema; “What matters is not how much you have borrowed, but for what you have borrowed.” Kwa hiyo, hilo napenda tuliseme vizuri kabisa kwamba kinacho-matter zaidi siyo kiwango gani umekopa, lakini umekopa kufanyia nini?

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hili napenda kuliambia Bunge lako Tukufu kwamba deni ambalo tunaendelea kulilipa kama Serikali, Serikali yetu ilikopa kwa ajili ya kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo ili kufungua fursa za kiuchumi kwa wananchi wetu na Taifa letu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi sote ni mashahidi, miundombinu ya Taifa letu inaelekea kuwa mizuri, sasa tunaona Taifa letu limefunguka kwa kiwango kikubwa, ni rahisi sasa kusafiri kutoka mkoa mmoja kwenda mkoa mwingine bila tatizo lolote. Ni rahisi kusafirisha bidhaa zinazotoka Sumbawanga kufika Dar es Salaam kwa muda wa siku moja au siku moja na nusu. Hii yote ni miradi iliyotekelezwa kupitia mikopo iliyokopwa na Serikali yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, katika hili tunajifunza kwamba uchumi wa Taifa letu unafunguka, ajira zinaongezeka katika Sekta za Kilimo, Sekta za Usafirishaji; na hii ni muhimu sana tuweze kuelewa tunapoliongelea deni letu la Taifa. Katika hili, wachumi wanasema, bottleneck inflation inaondoka kwa sababu sasa bidhaa inayozalishwa kutoka sehemu moja inaweza kusafirishwa na kufika sehemu nyingine ambako bidhaa hizo hazipo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kiashiria kilichopendekezwa na Kamati yetu ya Bajeti ni sahihi, kinatumika katika kupima kiwango cha uhimilivu wa deni letu la Taifa. Vile vile kuna viashiria viwili vinavyotumika na hiki kilichosemwa ni kimojawapo kati ya hivyo. Kiashiria cha kwanza ni kiashiria ambacho kinapima uwezo wa Taifa letu kuendelea kukopa (solvency indicators). Katika solvency indicators kuna viashiria vidogo vitatu, cha kwanza ni thamani ya sasa ya jumla ya Deni la Taifa kwa Pato la Taifa letu (present values to total public debt) ambayo nayo inaonekana bado tuko vizuri tunaweza kuendelea kukopa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, indicator ya pili ni thamani ya sasa ya deni la nje pekee kwa Pato la Taifa (present value to external debt). Nayo pia tupo katika level nzuri, hatujafika hata nusu ya viashiria ambavyo vimewekwa. Kiashiria kilichopendekezwa na Kamati yetu ya Bajeti ni hiki kiashiria kidogo cha tatu ambacho ni thamani ya sasa ya deni la nje kwa mapato ya ndani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hili kwa sasa hivi tuko asilimia 145.3 ikilinganishwa na ukomo wa asilimia 250. Kwa hiyo, kwa uhalisia kabisa, bado Taifa letu linaweza kuendelea kukopa kwa sababu viashiria vyote vitatu kwa ajili ya ukopaji vinaruhusu Taifa letu kuendelea kukopa. Katika hili, siyo kwenye kukopa tu, kiashiria cha pili kikubwa ni kiashiria kwa ajili ya uwezo wa Taifa lolote lile kulipa ambayo ni liquidity indicators.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika liquidity indicators kuna viashiria viwili vidogo, kiashiria cha kwanza ni ulipaji wa deni la nje kwa mapato ya ndani ambayo kwa sasa tupo katika asilimia 11.5 ikilinganishwa na ukomo wa asilimia 20. Kwa hiyo, bado tuna uwezo wa kulipa madeni yetu kama Taifa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kiashiria kidogo cha pili, ni ulipaji wa deni la nje kwa kutumia mauzo ya bidhaa nje ambapo Taifa letu tuko katika asilimia 7.8 ukilinganisha na ukomo wa asilimia 20. Kwa hiyo, viashiria vyote vya kukopa na vya kulipa vinaonesha bado Taifa letu la Tanzania tuna uwezo wa kukopa na tuna uwezo wa kulipa bila tatizo lolote kabisa. Hiyo ilikuwa ni hoja ya kwanza ambayo nilipenda kuitolea ufafanuzi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja ya pili ambayo pia Waheshimiwa Wabunge wengi wameichangia inahusu hilo hilo Deni la Taifa lakini katika nyanja nyingine, ambapo walisema takwimu zinaonesha kuwa kiasi kikubwa cha mapato ya ndani kinakwenda kulipia Deni la Taifa na hivyo Serikali kushindwa kugharamia masuala mengine ya maendeleo, ukatolewa na mfano.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hili, napenda kuliambia Bunge lako Tukufu kwamba kama nilivyosema kwenye hoja ya kwanza, Serikali yetu hukopa kwa ajili ya kugharamia miradi ya maendeleo. Katika hili nilitegemea tupongezwe kwa sababu Serikali imeweza kulipa Deni la Taifa katika kipindi cha mwaka huu kwa kiwango kikubwa kwa kutumia mapato yetu ya ndani. Ndiyo ile niliyosema katika jibu la kwanza kuhusu liquidity indicators.

Kwa hiyo, tuna uwezo mzuri wa kuweza ku-service deni letu bila tatizo lolote. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ulipaji wa Deni la Taifa ni wajibu wa kisheria kabisa na hatuwezi kukwepa kama nilivyosema mwanzo, tumekopa kwa ajili ya miradi ya maendeleo. Tuliingia makubaliano pia ambayo ni ya ukopaji pamoja na umuhimu wa kulipia miradi iliyotekelezwa miaka ya nyuma wakati mikopo hiyo ilipopokelewa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile ulipaji wa Deni la Taifa kwa kutumia mapato ya ndani ni mojawapo ya sifa kama nilivyosema ya kuonesha uwezo wa kukopa zaidi na uaminifu. Tena tumeweza kulipa kwa mapato yetu ya ndani. Kwa hiyo, tunaonesha kwamba pamoja na kwamba tuna miradi ya maendeleo, lakini kipaumbele chetu ni kulipa ili tuweze kutengeneza sifa nzuri ya Taifa letu. Sisi sote ni wanadamu, tunaishi katika uchumi wetu na tunafahamu ukiwa na deni lazima kulilipa na ndicho ambacho tumekifanya. Kwa uhakika kabisa na miradi yetu ya maendeleo tutaweza kuitekeleza baada ya kuonesha kwamba Taifa letu lina dhamira ya dhati ya kulipa madeni ambayo tumeyakopa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja ya tatu ambayo ningependa kuitolea ufafanuzi ilikuwa ni kuhusu Serikali kulipa shilingi bilioni 796 kati ya kiasi hicho inachodaiwa na wazabuni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kamati ya Bajeti nayo ilipendekeza pia kuwa kwamba tuweze kuwalipa Wazabuni, Wakandarasi pamoja na Watumishi wetu. Tumekuwa tukiliambia Bunge lako Tukufu, Serikali yetu ina lengo la dhati kabisa la kulipa wakandarasi, watumishi, wazabuni pamoja na watoa huduma wengine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali yetu imekuwa ikilipa madeni haya kulingana na upatikanaji wa mapato kama ambavyo Sheria ya Bajeti Namba 11 kifungu 45(b) kinavyotuelekeza kufanya. Katika bajeti yetu ya mwaka huu wa fedha, tulitenga kiasi cha shilingi bilioni 626 ili kulipa madeni haya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hadi kufikia mwezi Machi, kwa kuonesha dhamira njema ya Serikali yetu, tumeweza kulipa shilingi bilioni 796 zaidi hata ya bajeti tuliyotenga kuonesha kwamba dhamira ya Serikali ni njema, tunataka kulipa madeni haya, tunawathamini wazabuni wetu wanaohudumia Shule yetu, Magereza pamoja na Majeshi yetu mengine. Tumekuwa tukiwalipa mwezi hadi mwezi na kitakwimu tunalipunguza deni hili kulingana na mapato ya Taifa letu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kuzuia madeni haya yasiendelee kulimbikizwa, Wizara ilitoa angalizo na mwongozo kwa Maafisa Masuuli wote, kwamba hawaruhusiwi sasa kuendelea kulimbikiza madeni haya. Ninavyoongea, kwa mwaka huu wa fedha hakuna deni lolote ambalo tumelimbikiza. Kwa hiyo, hii ni nia njema na lengo bora kabisa la Serikali yetu kuhakikisha kwamba sasa tumejiandaa kuwalipa watu wetu wanaotoa huduma, tunafahamu wanavyosumbuka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwongozo huu uliotolewa na Mlipaji Mkuu wa Serikali, niseme tu kwa Maafisa Masuuli kwamba yeyote atakayekiuka mwongozo huu atakuwa amejifukuzisha kazi mwenyewe, kwa sababu Wizara imekuwa ikipeleka pesa kila mwezi kwa ajili ya malipo ya watoa huduma na wazabuni wetu.

Kwa hiyo, sisi kama moja ya Wajumbe wa Baraza la Madiwani katika Halmashauri tunazotoka, tuhakikishe pesa hizi zinapokuja kwenye Halmashauri zetu, zinatumika vizuri kulingana na maelekezo ambayo yanakuja na pesa hizo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja ya nne ambayo ningependa kuitolea ufafanuzi ni utekelezaji wa ahadi ya shilingi milioni 50 kwa kila kijiji, mtaa na shehia. Nimeona jana imesemwa kwa uchungu sana na Waheshimiwa Wabunge wameendelea kuisema. Napenda niseme kwamba hoja hii ilitolewa ufafanuzi pia wakati wa bajeti ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, lakini siyo vibaya mimi kama Naibu Waziri wa Fedha pia nikaweza kuisemea kidogo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama ambavyo imesemwa na Waheshimiwa Wabunge wengi kwenye hoja hii, ni kwamba kwa mwaka huu wa fedha Serikali yetu ilitenga shilingi bilioni 59.5 kwa ajili ya kuanza utekelezaji katika pilot areas. Wakati tunaendelea kutaka kutekeleza hili, zipo changamoto ambazo zimegundulika na hatuwezi kufanya makosa ambayo yaliwahi kufanyika huko nyuma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto ambazo zimeonekana ni pamoja na changamoto zilizolikumbuka Taifa letu kutokana na utekelezaji wa JK Fund. Hatutaki tena katika hizi milioni 50 kwa kila kijiji changamoto hii iweze kujirejea. Lazima tujifunze kutokana na makosa yetu na tuweze kuyarekebisha na kuhakikisha kila kinachotolewa kinawafikia walengwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto ya pili ambayo imesababisha tuchelewe kutekeleza hili, ni wananchi kuwa na mtazamo hasi wa fedha hizi kwamba ni fedha za bure. Tunahitaji kufikisha elimu ya ujasiriamali kwa wananchi wetu, wapate elimu waweze kujua fedha hizi siyo za bure. Fedha hizi wanawezeshwa ili atakayewezeshwa leo iwe ni revolving fund aweze kuwezesha na wengine. Kwa hiyo, ni lazima tuandae wananchi wetu ili waweze kuzipokea na kuweza kuzifanyia kazi ambayo ilikusudiwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia tumegundua changamoto nyingine kuhusu vijiji vingi kuwa na vikundi ambavyo havijasajiliwa kisheria. Katika hili, vikundi havijasajiliwa kisheria na vipo vingine ambavyo vinasajiliwa specifically ili vipate fedha hii. Kiuchumi hiki ni kitu ambacho hakiwezekani, kwamba kinasajiliwa kikundi, kinasubiri pesa ili waanze utekelezaji, tunategemea nini? Ni kurudia makosa yale yale ambayo yalitokea huko nyuma na hili hatutaki tena liweze kutokea katika shilingi milioni 50 hizi, tunahitaji zionekane zina impact iliyokusudiwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyosema, Waheshimiwa Wabunge ni Madiwani viongozi katika Halmashauri zetu. Katika Halmashauri zetu, tunaona changamoto pia za utekelezaji wa asilimia tano za own source ya Halmashauri zetu kwenda kwa wanawake na asimilia tano kwenda kwa vijana; utekelezaji wake haujakaa vizuri. Kwa hiyo, baada ya kugundua haya yote, Baraza la Taifa la Uwezeshaji Kiuchumi chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu pamoja na Ofisi ya Rais, (TAMISEMI) wanaandaa utaratibu mzuri na utakapokuwa umekamilika, fedha zote hizi zitatolewa katika vijiji vyote ambavyo Serikali yetu iliahidi na tutaweza kutekeleza kwa asilimia mia moja ndani ya miaka mitano ya utawala wa Mheshimiwa Rais wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja nyingine ambayo napenda kuitolea ufafanuzi ilikuwa ni ushauri kuhakikisha kuwa pensheni kwa wastaafu inatoka haraka na kwa wakati ili kupunguza usumbufu kwa wazee wetu. Ushauri huu kama Wizara tunaupokea, lakini ninavyofahamu, wastaafu wote wanaolipwa pensheni kupitia Wizara ya Fedha na Mipango, hata baadhi ya mifuko wanalipwa sambamba na mishahara ya wafanyakazi kila mwezi kwenye akaunti zao. Kwa hiyo, hakuna ucheleweshaji wowote ambao unatokea hasa kwenye pensheni ya kila mwezi kwa wastafu wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyowahi kuliambia Bunge lako Tukufu, tulikuwa tukiwalipa miezi mitatu mitatu, wakalalamika na sisi tukafanya analysis ya kutosha tukajiridhisha na sasa tunawalipa kila mwezi na wote wanapata pesa zao siku ambayo mishahara ya Serikali inalipwa. Niseme tu kwamba hili tunalichukua, kama ipo baadhi ya Mifuko ya Hifadhi ya Jamii ambayo hailipi pensheni za kila mwezi kwa wakati, tutalifanyia kazi, tutalisimamia vizuri kuhakikisha wazee wetu wanaweza kupata pensheni yao kwa wakati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hili la Mifuko ya Hifadhi ya Jamii, Kamati yetu pia ilishauri kwamba Serikali itimize ahadi yake ya kutoa non cash bond kwa ajili ya shilingi trilioni 2.6 ya mfuko wetu wa PSPF. Katika hili naomba kuliambia Bunge lako Tukufu kwamba nimekuwa nikijibu maswali na nikilieleza Bunge lako Tukufu kwamba Serikali ilikuwa inakamilisha tathmini na sasa tathmini imekamilika kwa ajili ya hii shilingi trilioni 2.6 ambalo ni deni la kabla ya mwaka 1999 pamoja na malipo pia ya mifuko mingine ambayo iligharamia miradi mbalimbali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, dhamira ya Serikali yetu ni njema kabisa na sasa tuko kwenye hatua za mwisho kuhakikisha kwamba hii non cash bond inaweza kuandikwa na kuanza utekelezaji wake mara moja baada ya uhakiki na tathmini kuwa imekamilika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja nyingine ilitoka Kambi Rasmi ya Upinzani kwamba Serikali iielekeze Mifuko ya Hifadhi ya Jamii kuwekeza kwenye miradi yenye faida na ya haraka hususan maeneo yanayochochea ukuaji wa uchumi kama vile reli na bandari. Katika hili naomba kuliambia Bunge lako Tukufu kwamba Serikali yetu kupitia Mamlaka ya Usimamizi wa Sekta ya Hifadhi ya Jamii imetoa miongozo ambayo imeainisha maeneo ya uwekezaji kwa kuzingatia faida na tija kwa jamii. Mojawapo ya maeneo hayo ni kama ilivyopendekezwa na Kambi Rasmi ya Upinzani kwamba ni ujenzi wa miundombinu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, katika miongozo hiyo, Mamlaka ya Usimamizi wa Sekta ya Hifadhi ya Jamii kwa kushirikiana na Benki Kuu inaweka ukomo wa uwekezaji kwa kuzingatia athari za uwekezaji na siyo faida ya haraka. Unaweza ukapata faida ya haraka halafu baadaye uwekezaji ule ukawa siyo endelevu. Hilo haliwezi kutekelezeka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tutatekeleza lile ambalo ni lenye faida endelevu kwa ajili ya mifuko hii kama tunavyojua wateja namba moja wa mifuko hii ambao ni wastaafu wetu ili waweze kuendelea kulipwa kwa wakati na muda unaotakiwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kuna hoja ililetwa kwamba Serikali iweze kutoa taarifa ya hesabu za robo mwaka za kila Mfuko wa Hifadhi ya Jamii. Katika miongozo hii niliyoitaja ina kipengele inayojielekeza mifuko hii kutoa taarifa kwa wateja wao kila robo mwaka. Kwa hiyo, hili lipo na linatekelezwa na mifuko yetu yote ya hifadhi ya jamii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hili la Mifuko ya Hifadhi ya Jamii kulikuwa na mapendekezo pia kwamba Ofisi ya Msajili wa Hazina ichukue usimamizi. Napenda kuliambia Bunge lako Tukufu kwamba Mamlaka ya Usimamizi wa Sekta ya Hifadhi ya Jamii pamoja na Msajili wa Hazina na Benki Kuu hushirikiana katika kuisimamia mifuko hii ya hifadhi ya jamii. Kila mmoja ana majukumu yake na kila mmoja anatekeleza majukumu yake kama yalivyowekwa katika sheria na taratibu za nchi yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo tunaomba watu hawa watatu; Mamlaka ya Usimamizi wa Sekta ya Hifadhi Jamii, Msajili ya Hazina na Benki Kuu wote kwa pamoja waendelee kunya kazi yao kwa pamoja ili kuhakikisha mifuko hii ya hifadhi ya jamii inafanya kazi kwa faida, kwa ajili ya wateja wao ambao ni wastaafu wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kulikuwa na hoja kwamba kwa mujibu wa ripoti ya Benki Kuu mfumuko wa bei umepanda kutoka asilimia 5.4 mwezi Machi, 2016 mpaka asilimia 6.4 mwezi 2017.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuliambia Bunge lako Tukufu kwamba mfumuko wa bei uliongezeka kutoka asilimia 5.1 mwezi Aprili, 2016 hadi asilimia 6.4 mwezi Aprili, 2017 ni sahihi na hii sote tunafahamu sababu kuu inayosababisha mfumuko wa bei ni tatizo la bei ya chakula.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sote ni mashahidi, sababu kubwa iliyotokea ni hali mbaya ya hewa katika msimu wa kilimo wa mwaka 2015/2016 kulikosababisha upungufu wa mazao ya chakula katika masoko ndani ya nchi yetu. Hata hivyo, mfumuko wa jumla wa bei umeendelea kudhibitiwa na kubaki katika wigo wa tarakimu mmoja ambapo Serikali yetu imeahidi kwamba ni lazima tutahakikisha mfumuko wa bei unabaki katika tarakimu mmoja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuliambiwa tuseme na mikakati ambayo tunaitekeleza. Katika hili tunaendelea kuimarisha miundombinu ya masoko yetu na barabara kama nilivyosema mwanzo ili kuwezesha usafirishaji wa chakula kutoka eneo moja kwenda eneo lingine iwe ya urahisi na kuweza kuhakikisha kwamba upungufu wa chakula haupo kwenye maeneo ambayo hayakupata mvua za kutosha. Pia tunaendelea kutoa ruzuku ya pembejeo, kuimarisha huduma za ugani na uimarishaji wa miundombinu ya umwagiliaji ili kupunguza utegemezi wa mvua katika kilimo chetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia tunaendelea kuongeza uzalishaji wa mazao ya chakula na kuimarisha upatikanaji wake katika masoko yetu. Serikali yetu, ni wiki mbili tu zilizopita imeweza kutoa chakula kupeleka katika zile Halmashauri zilizoathirika zaidi na uhaba wa mvua na hii tumepeleka katika lengo hili hili la kuhakikisha stabilization ya bei ya chakula ili kuhakikisha kwamba mfumuko wa bei hauvuki ile digit moja kama nilivyosema mwanzo.

Hoja nyingine zilitoka kwa Waheshimiwa Wabunge mbalimbali, nayo ilikuwa ni kuhusu Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi kuongezewa bajeti pamoja na kuha…

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa mzungumzaji)

NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kumalizia kwa kusema kwamba nawashukuru Waheshimiwa Wabunge wote waliotoa hoja madhubuti na mijadala mizuri yenye tija kwa ajili ya uboreshaji wa bajeti yetu ya Wizara ya Fedha na Mipango.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kumalizia kwa kusema, naunga mkono hoja, hoja iliyowekwa mezani na Mheshimiwa Waziri wa Fedha na Mipango, ahsante sana.