Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mbulu Mjini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. ZACHARIA P. ISSAAY: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi. Nitoe tu mchango wa kushauri Serikali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la kwanza, mfumo wetu wa kukusanya mapato hivi sasa si mzuri. Tungeweza kukusanya kodi na ushuru au nchi ingeweza kupata hela ya kutosha hasa katika viwanda kwa kudhibiti mianya na kuweka utaratibu mzuri wa ukusanyaji kodi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashauri mfumo mzima wa kusanyaji kodi utazamwe. Hivi sasa kodi zinalipwa katika utaratibu ambapo wale wanaolipa wanapangiwa kiwango kikubwa sana kutokana kwamba wengi wao huwa hawako kwenye mfumo ambao unaipa Serikali kodi. Ukusanyaji huu uungane na ule wa viwanda vikubwa sasa tunapata wakati mgumu pale ambapo mfumo wa ukusanyaji wa kodi ndani ya viwanda na makampuni haujakaa vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, hivi sasa Watanzania wanaogopa sana kutumia mifumo hii ya kielektroniki katika kukusanya mapato. Mfumo huu ni mzuri, mimi ni mdau wake kwa takribani miaka 10, shida iliyopo ni uelewa kwa wafanyabiashara na wadau wanaopaswa kutumia mfumo huu ili nchi ipate mapato ya kutosha. Kwa hiyo, nashauri kama itawezekana kufanyike utaratibu wa mfumo huu na viwango vile vya kodi kupungua ili kundi kubwa la ukusanyaji wa mapato waweze kuingia katika utaratibu huu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la tatu, katika taarifa hizi tulizowasilishiwa, upelekaji wa fedha katika ngazi za Serikali za Mitaa hasa fedha za miradi ni mdogo sana. Tunapata wakati mgumu sana sisi Wabunge, bajeti hii tunapokaa hapa hatimaye tunapopitisha lakini mwishoni tunaenda kuwaambia wananchi malengo ya Serikali yetu au Serikali yao kuhusu miradi ya maendeleo. Sasa pale ambapo fedha za miradi ya maendeleo hazitapelekwa katika ngazi za Serikali za Mitaa miradi mingi ya maendeleo inakosa fedha na hatimaye sasa tunaingia mgogoro wa wachaguliwa na wananchi waliotuchagua lakini pia miradi mingi inakosekana na huduma inakuwa duni. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, upelekaji huu wa fedha ukisimamiwa kwa kuzingatia mpango mzima wa bajeti na kwa kuona kwamba umuhimu wa miradi ya maendeleo na uendeshaji wa Serikali unapelekewa fedha kwa vyovyote vile miradi mingi ya maendeleo itafanikiwa. Hivi leo hata tukipiga kelele kwa Waziri na timu yake bila pesa kupatikana nadhani Waziri hatabadilika kuwa fedha na hatutaweza kufanikiwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nne ni suala la Mfuko wa Maji. Naomba jambo hili litazamwe na namna pekee ya kuondoa kero ya maji nchini ni kutafuta mfumo mzuri wa kuona fedha za miradi ya maji zinapatikana kama ilivyo kwa Mfuko wa Mawasiliano na huu Mfuko wa Maji upate fedha za kutosha na pengine taarifa yetu iletwe baadaye ili tuweze kuona na kuishauri Serikali namna gani Mfuko huu wa Maji unapata fedha za kutosha ili miradi ya maji vijijini iweze kutatuliwa. Hivi sasa hali ni mbaya sana katika miradi ya maji na hasa miradi mipya na vile viporo lakini pia hali ni mbaya katika upatikanaji wa fedha na kwa vyovyote vile hatutafanikiwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tano, madeni ya watumishi na wazabuni wenzangu walishaongea sitaongelea, nashauri malipo ya wastaafu yawe na mfumo wa wazi ambao unaonesha dira sahihi na kiwango kizuri. Hivi sasa wastaafu wetu au watumishi wanapoelekea kustaafu wengi wao wanakata tamaa na kuona kwamba ni wakati mgumu sasa unakuja kwao. Pengine tuone namna ya kuboresha malipo yale ya wastaafu na utaratibu wa wazi ambao hauwabugudhi wala kuwatesa wale wastaafu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sita, tulifanya ziara mimi na timu yetu ya Kamati ya TAMISEMI, tulienda kule Njombe, jengo la Hospitali ya Mkoa wa Njombe ni kubwa na linajengwa kwa shilingi bilioni 3.2 mpaka kukamilika, lakini miradi kama hiyo katika mikoa mingine nchini na katika Wilaya zingine inajengwa kwa shilingi milioni karibu nane mpaka tisa na hata zaidi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashauri kuwe na mfumo na utaratibu unaoangalia matumizi ya fedha katika manunuzi ya umma na jinsi ya kutekeleza miradi kwa kuzingatia mfano wa Hospitali ya Njombe. Matumizi sahihi ya fedha yanaweza yakasaidia nchi pia kuona ni namna gani kile kidogo kinachopatikana kinakuwa na thamani katika utekelezaji wa miradi ya wananchi na miradi ya huduma na utoaji wa huduma Serikalini. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, saba, ni Wakaguzi wa Ndani katika Halmashauri, wakaguzi hao mara nyingi wanafanya kazi katika utaratibu ambao sio mzuri. Nashauri Idara ya Ukaguzi wa Ndani katika Halmashauri zetu wapewe nafasi ya kuwa Idara inayojitegemea na Serikali ianzishe mfumo huu toka Taifa hadi Halmashauri ili wasiwe wategemezi kwa Wakurugenzi na watendaji wa Halmashauri kwa jinsi ambavyo wao ndiyo jicho la Halmashauri pale walipo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nane, semina kwa Madiwani. Madiwani bila kufanyiwa semina wakapewa kazi ya kusimamia miradi ya maendeleo ni kazi bure. Nashauri Serikali ione umuhimu ya kutenga fedha kwa ajili ya semina za majukumu, wajibu na usimamizi na uendeshaji wa Halmashauri wao kama wawakilishi wa wananchi ili waweze kufanya kazi yao na kwa makusudi yaliyokusudiwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tisa, ajira Serikalini. Tunashindwa kuajiri watu sasa kwa sababu hata mfumo ule wa kuwastaafisha watu unakuwa si rafiki kwa wale wanaoelekea kustaafu na kwa hivyo hela hatuna hivyo vijana wengi wanakosa ajira. Ingewezekana tungepunguza hata umri wa kustaafu sasa lakini tuboreshe pensheni ya kustaafu ili kustaafu kuwe miaka 50 kwa hiari na lazima 55. Hali hii itafanya wastaafu waone wanalipwa pensheni inayolingana na maisha yao yajao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kumi, kuimarisha Benki ya Kilimo. Hivi sasa tunazungumza suala zima la upatikanaji wa fedha, lakini bila kuboresha Benki ya Kilimo ambayo ndiyo itachukua wananchi wengi na watanufaika na huduma yake na kutazama utaratibu wao ulio rafiki katika kukopesha wakulima, kwa vyovyote si rahisi uchumi wa kawaida ukamfikia mwananchi na mzalishaji na mjenga uchumi wa nchi kwa kadri ambavyo inawezekana kuleta tija.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kumi na moja, Tume ya Mipango iboreshwe, irudi Ofisi ya Rais kama Kamati ilivyoomba lakini ijengewe uwezo na iweze kuwa chombo/ taasisi inayoweza kushauri Serikali kuhusu uchumi wa nchi. Chombo hiki kikisimamiwa kikakaa vizuri kinaweza kitatufikisha katika hali ambayo itatujenga zaidi kiuchumi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho ni misamaha ya kodi isiyo na tija. Hivi sasa si kweli kwamba misamaha yote ya kodi inayotolewa ina tija kwa nchi yetu. Kama itawezekana nashauri kuwe na chombo kinachosimamia mfumo huu na kutazama msamaha uliotolewa kwenye kampuni au taasisi fulani una tija kwa nchi, kizazi kijacho na uchumi wa nchi kwa siku za baadaye. Misamaha haiwezi kuepukika kutokana na hali halisi inayojitokeza, lakini si misamaha yote ina tija kwa hivi sasa. Naona jambo hili likitazamwa linaweza likajenga uchumi wa nchi lakini likaongeza pia mapato Serikalini na tutafanikiwa sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi, naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja.