Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CHADEMA
Constituent
Bukoba Mjini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. WILFRED M. LWAKATARE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Hatuwezi kuendelea kukaa hapa tunaambiwa Wizara inakusanya, watu wanafungiwa maduka kwa kudaiwa kodi, watu wanafunga biashara kwa kulemewa mizigo, wanataka kukamuliwa huku hakuna mashudu, maziwa sijui yatoke wapi, wakati Waziri na Timu zake na vyombo vyake wanakusanyia kwenye pakacha linalovuja. Ukweli wenyewe tunapigwa mno, tunakusanyia kwenye pakacha. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mbaya zaidi juzi inaripotiwa kwamba kuna mtumishi wa TAKUKURU amepiga ile mbaya, hebu Waheshimiwa Wabunge fikirieni vyombo ambavyo Mheshimiwa Rais amezungumza kwamba sasa anaviamini, vyombo vya ulinzi na usalama ndiyo vimsaidie kudhibiti mapato na mianya ya rushwa, TAKUKURU anakuwa ndiyo mpigaji mkubwa, hii haiwezekani. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka Waziri anapokuja hapa kuhitimisha atueleze yeye na timu yake sasa kwa awamu hii wamejipangaje kuzuia pakacha hili linavyovuja vinginevyo watu wanakatishwa tamaa na wanapata hofu, tunawaonea watu kwa kuwatoza kodi inayokwenda kuvuja, hilo la kwanza. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, kila Kamati ya Bunge iliyokuja hapa na Mawaziri wengi waliokuja hapa wanalalamika bajeti haitoshi yaani kwa maana nyingine Mheshimiwa Mpango na Naibu wake shemeji yangu, kwa lugha nyepesi ya Mheshimiwa Rais wanatuletea bajeti hewa, hizi ni bajeti hewa yaani watu wanapewa eight percent ya bajeti yao ambayo sisi kama Wabunge tunakuja kukaa hapa Madaktari, Profesa na watu wa kada mbalimbali mnakuja mnapitisha 100 kwa 100, mwisho wa siku ripoti inakuja kwamba mnapitisha eight percent maana yake ni kwamba hata performance ya Serikali ni eight percent katika eneo hilo husika, tunafanya nini?
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, Mheshimiwa akija hapa atueleze tunamalizianaje, hizi bajeti hewa, bajeti hewa ya safari hii iwe ya mwisho, hatutaki tena bajeti hewa. Tunataka apange mambo machache yanayoendana na kile anachokusanya, asijipangie mambo mengi akawapa watu kiu kumbe wanaishia kunawa kula hawali, hilo haiwezekani. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, watu wanazungumza kwamba wawape pesa kwa muda mchache uliobaki, ukitoa pesa mwishoni ni sawa na una gari la V8 unaweka mafuta ukiongeza speed ikaanza 200 ujue valve zimefunguka zinakunywa mafuta ile mbaya, sasa hii pesa ya kutolewa mwishoni, zinapigwa hatutaki mchezo huo. Pesa zitoke kwa ratiba ambayo imepangwa na kwa muda husika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la wafanyabiashara wa Bukoba Town, nimekuwa napiga kelele hapa, Mheshimiwa tutataka Marshall Plan ya Bukoba – Kagera, tumeumia sana na shemeji yangu amekuwa anakuja ukweni unapendelea watu waendelee kulala maturubai? Tunataka
Marshall Plan ya Bukoba Town, wafanyabiashara wana madeni hamuwalipi, walipeni basi madeni yao ya ku-supply huduma Serikalini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho ni road license, wadau wanaomba hii road license ya kutoza gari ambalo liko under grounded miaka saba au nane na mbaya zaidi unakamata gari linalotembea lipo kwenye biashara eti mpaka lile deni la gari ambalo lipo garage liligongwa au lilianguka lilipiwe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba utaratibu huo ubadilishwe hata kama ni kuweka kwenye mafuta bora road license iwekwe kwenye mafuta, kwa njia hiyo hutalipata gari linalotembea kwa sababu limekwenda kunywa mafuta na tutakuwa tumemalizana kuliko kuwaonea watu, watu wanakamatiwa vyombo vyao, watu wanashindwa kuelewa na imekuwa ni chanzo cha rushwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya hapo sitaki kugongewa kengele, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia.