Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Fedha na Mipango

Hon. Sebastian Simon Kapufi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mpanda Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Fedha na Mipango

MHE. SEBASTIAN S. KAPUFI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Awali ya yote naomba niwatakie ndugu zangu Waislam mfungo mwema, ili waendelee kupata baraka za Mwenyezi Mungu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa nikikipitia kitabu cha Waziri na taarifa za Kamati, nikaanza na sehemu ambayo ilikuwa inazungumzia hoja mbalimbali na hatua ambazo Wizara imekusudia kuchukua kwa maana ya kukabili changamoto. Wanasema kuendelea kuwianisha mapato na matumizi kwa kuhakikisha kuwa mgawo wa fedha utaendana na upatikanaji wa mapato.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nasema jambo hili ni jema, lakini kama alivyosema Mheshimiwa Waziri kwamba, kuhakikisha kuwa mgawo wa fedha utaendana na upatikanaji wa mapato, fedha hizo zinazopatikana bila kuwafikia walengwa tabu ipo na ni tabu kubwa. Kwa hiyo, naomba ikiwa amesema hizo ni hatua za kukabili, kweli hilo jambo tulifanyie kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna changamoto nafahamu. Kuna changamoto kwa maana ya mashine za kielektroniki, niendelee kusema jambo hili ni jema, lakini waendelee kufuatilia suala la udanganyifu katika mashine hizo za kielektroniki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuchelewa kwa fedha kutoka kwa washirika wa maendeleo inaendelea kutukumbusha kwamba, ni vizuri tukajenga uwezo wetu binafsi kwa sababu unapokuwa unatamani kusafiri, lakini kwa nauli ya kutoka kwa jirani, hiyo safari iko mashakani. Niendelee kuomba Mheshimiwa Waziri kwa maana ya kujenga uwezo wetu wa ndani, ili hata kama fedha za wadau wa maendeleo zitakuwa hazipatikani tutakuwa tuko sehemu salama.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba elimu kwa maana ya miradi ya ubia kwa wadau mbalimbali, wadau hao tusiwasahau Madiwani. Tutakapokuwa tukizungumzia elimu kwa miradi ya ubia Madiwani ni kiungo muhimu kwa sababu wanatufanyia kazi kubwa kule. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mafanikio Mheshimiwa Waziri amezungumzia mafanikio kwa maana ya kupunguza malimbikizo ya madai ya Watumishi, Wazabuni na Wakandarasi yaliyohakikiwa hadi Machi, 2017, Serikali imelipa kiasi cha shilingi bilioni 796.3. Nasema kwa hatua hiyo ni jambo jema, lakini tuendelee, malalamiko huko ni mengi na kwa kweli eneo hili tukilifanyia kazi tunaamsha ari ya watu kufanya kazi, lakini na wale wengine kama ni Wazabuni au ni wadau muhimu wa maendeleo wanapokuwa wakilipwa, maana yake wanashiriki zaidi kwenye kufanya shughuli za maendeleo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna tatizo la upelekaji fedha za maendeleo. Mimi kule kwangu Katavi hivi ninavyoongea hawajapata OC, hawajapata fidia ya vyanzo vya mapato kwa maana ya General Purpose Grant, suala la National Water Supply Sanitation Program, hawa watu fedha zote katika maeneo hayo hawajapata. Kwa hiyo, tunapozungumzia suala zima la kupeleka mbele maendeleo naiona shida kubwa katika maeneo hayo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, namna pekee ya kuenzi watumishi na hasa wale wastaafu, mafao ya wastaafu na mirathi ilipwe kwa wakati. Hapa nilikuwa naendelea kupongeza, najua kuna program wanasema mfumo wa TEHAMA unaoitwa Saperion mpaka Machi, 2017 inaonesha wastaafu 96,989 wamewekwa kwenye mfumo, hili ni jambo jema, lakini niendelee kusisitiza namna pekee ya kuwaenzi wastaafu ni kuwalipa kwa wakati ili watu hawa waone kwamba, nchi inawaheshimu kwa utumishi walioufanya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, napongeza suala la utoaji elimu kwa Maafisa Mipango. Hapa kuna Maafisa Mipango 183 kutoka Sekretarieti za Mikoa na 237 kutoka Halmashauri kwa maana ya kuwajengea uwezo wa kutafsiri vipaumbele vya Kitaifa. Ni vizuri kuwajengea uwezo kwa sababu, watu hawa tunao kule katika maeneo yetu, wanapokuwa wanafahamu nini tufanye, elimu hiyo wataishusha kwa watu wengine pale, kwa hiyo tutakuwa tunaimba wimbo mmoja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nafahamu tunaambiwa kwamba, 2016/2017 kukua kwa Pato la Taifa ilitoka 7.2 kwenda 7.3 na kwa maana ya 2017 tunakusudia kukua kwenda 7.4 ni jambo jema, lakini ninachoomba Mheshimiwa Waziri wananchi hawa wanatamani tunapozungumzia habari hii ya ukuaji huu wa uchumi walione bubujiko kwenye mifuko yao. Namna pekee ya kuweza kuimba ukuaji wa uchumi uende sambamba na hali halisi katika mifuko yao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kuyasema hayo yote, najua pia kwamba, mfumuko wa bei unabaki tarakimu moja na nakisi ya bajeti ya Serikali isiyozidi asilimia 4.5 ya Pato la Taifa yote hayo nasema ni mema. Eneo la sekta ya ujenzi, naona hapa tunaambiwa kwamba, imekua kwa asilimia 13. Sekta ya Ujenzi kwa mimi ninayetoka Katavi naona namna pekee tutakayoweza kufanya kwa sababu, leo ukiuzungumzia mfuko wa simenti katika maeneo ya kwetu, bei ya mfuko wa simenti wakati nikiona sekta hii inakua, natamani tuone namna ambapo mkazi wa Katavi anapokwenda kuununua mfuko 20,000/= anapokwenda kununua mfuko zaidi ya 20,000/= ni namna gani na yeye atakuwa sambamba na ukuaji wa sekta hii ya ujenzi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kuyasema hayo, kwa upande wangu naomba niishie hapo. Nakushukuru sana na naunga mkono hoja.