Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Fedha na Mipango

Hon. Ruth Hiyob Mollel

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Fedha na Mipango

MHE. RUTH H. MOLLEL: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi nami niweze kuchangia hoja iliyoko mezani. Na nichukue nafasi hii pia niwatakie kheri ndugu zetu Waislam, Ramadhan Karim kwa wote, Mungu awajalie mmalize mfungo salama. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara hii ya Fedha na Mipango ni moyo wa Serikali. Nasema moyo wa Serikali ni kama moyo wa binadamu unavyofanya kazi, kama usipofanya kazi vizuri kila kitu kinatetereka. Kwa hiyo, ninapenda kusisitiza unyeti wa Wizara hii ya Fedha na mipango. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama tunavyojua katika mwelekeo wa Serikali ya Awamu ya Tano ni kwamba, hii ni Serikali ya Viwanda. Katika kuangalia mpango wa miaka mitano, nikaangalia mpango ule wa mwaka mmoja, nikaangalia pia hotuba ya Mheshimiwa Waziri wa Viwanda, vimetajwa viwanda vingi sana ambavyo vinahitajika kufanyiwa kazi, vingine kufufuliwa, vingine kujengwa upya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kumwomba Mheshimiwa Waziri atakapohitimisha hoja yake atuambie hii Tanzania yetu ya viwanda ni viwanda vya aina gani? Kwa sababu ni lazima tujue kama viwanda tunavyozungumzia ni agro-processing, kama ni textile industries, kama ni machinery, ili tuweze kuwa na lengo ambalo Serikali iweze kujipanga maana unapoainisha kabisa, kwamba, kama alivyofanya Mwalimu Nyerere yeye alikwenda kwenye Textile Industry, tukaona viwanda vingi vya nguo na resources zote zikapelekwa kwenye hayo maeneo kwa ajili ya kuleta ufanisi na ku-create ajira. Sasa ningependa Mheshimiwa Waziri atakapohitimisha hoja yake atufungue macho kidogo, kujua hivi viwanda tunavyovizungumzia ni vipi ambavyo Serikali inajikita kuviamsha?

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeona viwanda vingi, ni jambo jema, lakini kwa resources tulizonazo hatuwezi tukapeleka hapa kidogo, hapa kidogo, hapa kidogo. Ni lazima tuainishe maeneo madhubuti ambayo tunajua baada ya miaka mitano tunajua hii Serikali tutaipima kwa viwanda gani vilivyokamilika na vinavyofanya kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hilo pia linaendana na kuelimisha Watanzania. Nchi nyingine za duniani ukienda Mauritius au Singapore au Malaysia unakuta mpaka tax driver anajua mwelekeo wa nchi yake. Je, Watanzania wote tunajua mwelekeo wa nchi yetu? Kama ni laa, basi kazi kubwa ifanyike ili kusudi kila mtu aweze kujua nini mwelekeo wa nchi yetu katika hii Sera ya Viwanda Tanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hiyo itasaidia hata na wakulima kama ni agro-processing, wakulima watajipanga, kila mtu atajipanga na Serikali pia itajipanga kama ni kupeleka mbolea, kama ni kuhakikisha mashamba makubwa ya pamba, itajipanga vizuri na wataalam. Maana mwaka 2015 tulihitajika tuwe na Mechanical Engineering, Manufacturing Engineering, kama 17,000, lakini lengo halikufikiwa, kwa nini halikufikiwa? Ni kwa sababu bado hatujaainisha ni kitu gani tunataka kufanya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu suala la mapato ya ndani. Hili jambo limezungumziwa na watu wengi kuhusu kodi ya majengo. Kodi ya majengo ina historia, Mheshimiwa Waziri anafahamu. Kwanza walikuwa wanakusanya TRA wakashindwa, jukumu hili likapelekwa kwa Halmashauri (TAMISEMI) wakafanya vizuri sana wakakusanya, sijui ni kitu gani sasa kimekuja hapa katikati kuona kwamba hili suala tena lirudishwe TRA.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa taarifa kidogo tu ya mkoani kwangu Dar es Salaam, Kinondoni na Ubungo walikuwa wamepanga kukusanya bilioni 10.5 Kinondoni ilikuwa wakusanye bilioni 7.5, Ubungo shilingi bilioni 3.0, wote ilikuwa wakusanye hizo pesa. Jukumu hili lilipoondolewa
wakaambiwa watapewa bilioni mbili, mpaka leo hawajapewa hata senti tano na hatujui kama hizi pesa zimekusanywa au hazijakusanywa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wote tunakubaliana kwamba Serikali imeingia katika Sera ya D by D na unapotekeleza Sera ya D by D upeleke resources, upeleke na wataalam. Kitendo cha kunyang’anya property tax kwenye Halmashauri za Jiji na Manispaa ni sawa na kuwaambia wasifanye kazi, kwa sababu huduma zote za jamii zinapatikana kwenye Serikali za Mitaa ndiko kwenye afya, maji, barabara, ndiko kwenye kila kitu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa inakuwaje kwa sababu Serikali Kuu imekasimu madaraka kwa Local Government, ni kama baba unasema mtoto wangu wewe nenda ukafanye A, B, C, D, chukua hela hizi, chukua resources hizi, sasa unainyang’anya tena halafu unategemea itafanya nini? Tunaomba Mheshimiwa Waziri ili akajitafakari, najua Sheria ilipita hapa lakini hiyo sheria ikatazamwe upya, kwa sababu mpaka sasa TRA wameshindwa kukusanya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tulipokuwa Iringa tumekuta TRA Iringa wameshindwa kukusanya, wanawatumia tena hao hao watu wa Local Government kukusanya kuwatumia kama agency. Kama wao hawawezi kukusanya kwa nini wasiwaachie Local Government wazikusanye hizi pesa? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunakuja kwenye suala la fedha za miradi. Fedha za miradi tumekwenda kwenye Mikoa fedha za miradi hakuna, tumekuja hata kwenye Wizara, fedha za miradi hazipo hata kwenye Wizara katika taarifa zilizopita sasa hivi kwa mfano kilimo wanapata three percent, viwanda eighteen percent. Sasa ni kwanini Wizara isiende na realist budget. Kama bajeti ya kupeleka kwenye Wizara fulani ni bilioni mbili basi ipelekwe hiyo bilioni mbili na ipatikane, kuliko kusema unapeleka bilioni 100 kwa mfano kilimo halafu hakuna pesa inayokwenda. Hii ni unacceptable kwa kweli. Twende na uhalisia ile pesa iliyokusanya ndiyo hiyo igawanywe na hiyo iweze kupatikana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakwenda kidogo kwenye suala la Muundo wa Wizara. Najua Tume ya Mipango iko chini ya Wizara sasa hivi, Tume ya Mipango ndiyo think tank ya uchumi na mipango. Nikiangalia hata bajeti waliyopelekewa haitoshi, sasa katika hii dhana ya Tanzania ya viwanda ikiwa Tume ya Mipango ambayo ndiyo think tank ambayo inatakwa ikae na kufikiri, kupanga na kupangua haipati bajeti, tutafika huko tunakwenda? Sioni kama tutafika huko tunakokwenda. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Mheshimiwa Waziri atakapokuja kumalizia hoja yake atuambie mwelekeo wetu wa viwanda ni upi na ni viwanda gani ambavyo Serikali ina mpango wa kuhakikisha kwamba itakapofika 2020 vitakuwa vinafanya kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.