Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Fedha na Mipango

Hon. Ali Hassan Omar King

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Jang'ombe

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Fedha na Mipango

MHE. ALI HASSAN OMAR KING: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Awali ya yote nimshukuru Mwenyezi Mungu ambaye ametujalia siku ya leo kuwa hai hapa na tukafika katika Bunge lako Tukufu na kuweza kujadili bajeti hii ya Wizara ya Fedha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nakushukuru wewe kuweza kunipa nafasi hii kuweza kujadili lakini kwanza kabla sijaanza kuchangia kitu ambacho nataka kukisema nina mambo kama nane, jambo moja tu ambalo ni muhimu sana kuzingatia.

Katika kitabu hiki cha rangi ya waridi ambacho walizungumza Kambi ya Upinzani wakasema kwamba wanawashukuru waliofanya utafiti mpaka wakaandika kitabu hiki, lakini hiki kitabu kimeandika Bajeti Kuu, hakijaandika bajeti ya Wizara ya Fedha. Sasa pamoja na reseach hiyo halafu bado watu wako nje ya beat, watu wanaimba nje ya key, sasa sijui haya mambo yataendaje.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hili linakuja kwa sababu ukiajiandaa sana kukosoa basi mwisho unakosolewa wewe, kwa hiyo ndilo nilitaka nitoe taarifa tu kwamba hiki kitabu kiko nje ya beat tena kiko nje ta key kinazungumzia Bajeti Kuu, ikifika siku hiyo ya Bajeti Kuu sijui kutaelezwa nini, ukikitafuta utakiona.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo ninalotaka kuchangia la mwanzo, nataka kuchangia katika Fungu Namba 10 la Wizara ya Fedha. Fungu Namba 10 ni Tume ya Fedha ya Pamoja. Katika kitabu cha Mheshimiwa Waziri ukurasa wa 40 na ukurasa wa 41 amezungumzia Tume ya Pamoja ya Fedha. Katika Tume hiyo ya Pamoja ya Fedha amesema kwamba imefanya mapitio ya study tofauti za masuala ya kodi. Sasa na mimi nizungumze masuala hayo ya kodi ambayo labda mengine kwa kuwa mambo haya yanapita huko na haya yapite huko. Jambo lenyewe ni hili kama lifuatalo:-

Mheshimiwa Mwneyekiti, tunajua tumepitisha Petroleum Act pia tumepitisha Oil and Gas Revenue Management Act, 2015 ambavyo vimelenga kuifanya kwamba Zanzibar kuwa inashughulika na mafuta na gesi ambayo wanachimba kule na Tanzania Bara watashughulika kwa upande wao, lakini kitu kimoja ambacho ninataka kikaangaliwe katika Tume hii ya Pamoja ya Fedha ni kwamba bado Sheria za Kodi ni za Muungano.

Mheshimiwa Mwenyekiti, maana yangu ni kwamba pato kubwa linalotokana na mafuta na gesi huwa linatokana na kodi, sasa hizi kodi bado ni za Muungano kwa kuwa hizi kodi bado ni za Muungano, Tume hii nayo basi ikakae na ikatazame kwa sababu watu wanazungumza wataalam zaidi ya asilimia 90 ya mapato ya mafuta na gesi ni kodi lakini kama zikiwa hazikuelezwa kodi hizo kama hazitokuwa za Muungano ina maana kwamba bado patakuwa pana utata. Sasa zikaelezwe hizo kodi ambazo zitatokana na mafura na gesi nazo pia ziwe tofauti na Sheria za Kodi ambazo ni Sheria za Muungano, hilo ni moja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa Tume hii ipo kwa maslahi ya kuangalia study na kuangalia masuala ya kodi na kufanya mapitio kama ilivyoelezwa na Mheshimiwa Waziri katika ukurasa wa 41 basi pia tukaangalie Tanzania Bara na Zanzibar ni sehemu ambazo hazijapakana kwa mipaka mikubwa, masafa ni madogo sana. Katika masuala ya bidhaa ambazo zinakwenda Zanzibar kuwekewa zero ratekwa masafa madogo inakuwa haiko vizuri ni bora tukatumia ile compensation arrangement kuliko tukatumia zero based arrangement.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama suala hili litakwenda litaafikiwa na litazungumzwa vizuri kwa sababu masafa yetu madogo, zero based mara nyingi watu wanatumia kwa masafa marefu na zero based ina gharama kubwa ina maana kwamba lazima uanze kuweka mambo ya administration katika customs zote, uanze kufanya masuala hayo, jingine ni magendo yanaweza yakaimarika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hili nashauri katika Tume ya Pamoja ya Fedha ijaribu kuangalia hili kwa sababu mara nyingi inakwenda hivyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Fungu 21 - Hazina; Wabunge wengi sana walisema kwamba fedha hawajaziona lakini ukienda katika Kitabu cha Maendeleo cha bajeti, Fungu 21- Hazina iko pale village empowerment na imewekewa fedha zake shilingi bilioni 60. Tukitazama katika vitabu hivyo tutaona. Sasa mimi nazungumzia katika kitu kimoja. Mwaka huu tumesema kwamba tutafanya pilot study lakini miezi tayari inataradadi nafikiri bado nafikiri bado tutakuwa hatujafanya pilot study.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kwa sisi wengine wenye Majimbo na ambao tumechangamka haraka baada ya kusikia fursa hii kwa wananchi, tulijaribu kwenda kuhamasisha, tulisajili vikundi, tulitoa elimu kwa vikundi tayari tulikwishajipanga. Jang’ombe tayari tulishajipanga. Kama hiyo pilot study inataka kufanyika ghafla basi tuleteeni Jang’ombe kwa sababu tumeshatoa elimu na vikundi viko imara na vikundi vimehamasika na vinafanya kazi yake vizuri, kwa hiyo tutakapokwenda tukafanye hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumze jambo moja, hili jambo tulisema kwamba kwapilot study ndiyo shilingi bilioni
59.5 lakini iweje na mwaka unaofuata iwe bilioni 60? Na wakati vijiji vinajulikana au mitaa inajulikana idadi yake kwa fedha hizi ambazo tumezitenga kwa mwaka wa pili ni kidogo na fedha hizi mwaka wa mwanzo hazikutoka hatujui kama tumelishwa samaki wa kuchora au vipi! Kwa sabbau bado hazijatoka. Sasa Je, na hizi za mwaka wa pili zitatoka sambamba? Kwa hiyo, hapo namwomba Mheshimiwa Waziri ajaribu kuja kuangalia suala hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu Fungu la Deni la Taifa, tunakubali Serikali ikope, nchi maskini ili iweze kuendelea ikope na tumefurahi kuona kwamba katika Deni la Taifa tunalipa, tunaishukuru na tunaipongeza sana Serikali yetu. Miradi ambayo inayofanyika tukikopa leo wanakuja kulipa wa kesho na kesho kutwa. Watakuja kulipa watu kwa miaka 20 au 25 mbele ambao hawajatumia, sasa miradi ambayo itakuwa inafanyika kwa kukopa fedha hizi basi at least iwe ina record nzuri, iwe inajulikana katika kila hatua kwa maana gani?

Mheshimiwa Mwenyekiti, inawezekana umekopa umsomeshe mtu mpaka Chuo Kikuu, lakini kumbe yule mtu akamalizia primary lakini mkopo uliochukua ni wa Chuo Kikuu. Sasa tupate faida ile ya kusoma mtu Chuo Kikuu na huo mradi tunaosema ukubwa wake uwe vilevile ambavyo ulitarajiwa na usije ukawa ni mradi ambao ni mfupi ambao faida yake ni ndogo. Tutakuja kuwalipisha watu deni kubwa kuliko faida ya mradi ambao upo kwa sababu deni tutalipa mbele. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni kuhusu Msajili wa Hazina Fungu Namba 7. Katika Fungu Namba 7 siku zote Serikali inahangaika kutafuta mapato lakini…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante nashukuru sana. Naunga mkono hoja.