Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki

Hon. CAN.RTD Ali Khamis Masoud

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mfenesini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki

MHE. KAN. MST. MASOUD ALI KHAMIS: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi hii ya kuchangia kwa dakika hizi chache.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nampongeza Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri, Makatibu na watendaji wote wa Wizara hii kwa kazi nzuri wanayoifanya. Muendelee kushika uzi huo huo wa utekelezaji wa majukumu yenu kama mlivyopangiwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa ni dakika tano, naomba nichangie kitu kimoja, Wizara hii ni nyeti sana, ni Wizara ambayo inaonesha uso wetu nje ya nchi. Ikiwa leo Bunge linaamua kuiwekea siku moja ya kuchangia ni dhahiri kwamba Wabunge wengi hawataweza kutoa mchango wao wa kutosha wa kuweza kuboresha ofisi zetu kwa Watendaji walioko nje ya nchi. (Makofi)

Hivyo, naiomba ofisi hii iendelee kufikiria zaidi jinsi ya kuipatia nafasi Wizara hii ipate michango mingi ili iweze kuboresha zaidi na kuonesha sura nzuri nje ya nchi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mambo muhimu yanayotakiwa kufanywa nje ya nchi kwa sasa ni pamoja na kuboresha majengo yetu. Majengo mengi ya Wizara hii nje ya nchi hayapo katika hali nzuri. Kweli tuna uhaba wa fedha, lakini bado utumike utaratibu mwingine wowote utakaowezekana kuhakikisha tunaonesha sura nzuri nje ya Taifa letu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa wale ambao hawajafika, sisi wengine tumeona, nchi mfano ya Msumbiji, hali ya Msumbiji siyo nzuri. Ukiangalia na sisi tabia hii tuliyoipata sijui tumerithi wapi? Tabia ya kwamba mtu nyumba yako ikichakaa unahama, ni tabia gani? Nyumba ikichakaa hurekebishwa na baadaye uendelee kuishi ndani ya nyumba hiyo. Balozi amehama kwa kuwa nyumba imechakaa, amepangishiwa nje. Tunapoteza fedha nyingi sana kwa kupangisha nyumba.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sasa hivi naishukuru Wizara hii kwa kazi nzuri waliyoifanya ya kutumia fedha katika kipindi hiki kifupi kwa ajili ya pango la Balozi kutengeneza ile nyumba ya Balozi kule Msumbiji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, bado naiomba Serikali na Wizara hii waendelee kuweka kipaumbele kuhakikisha jengo la ghorofa tisa nchini Msumbiji linamalizika haraka kwa kuwa hii ni njia moja itakayotukomboa na kuhakikisha kwamba tunafanya kazi nzuri, tunaboresha nyumba zetu na wafanyakazi wetu wanaishi katika mazingira mazuri. Ni kweli, nchi nyingi tulizo na Ubalozi hatuna majengo mazuri, lakini kama Wizara na Serikali itatoa kipaumbele kutoa fedha za kutosha, nina uhakika Watendaji katika Wizara hii wanaweza kufanya kazi nzuri sana na ya kupigiwa mfano.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.
Naomba niachie nafasi wengine.