Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
2
Ministries
nil
MHE. FATMA H. TOUFIQ: Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza Waziri wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Naibu Waziri, Katibu Mkuu pamoja na watendaji wote kwa kuandaa hotuba ya Wizara ya makadirio ya Bajeti ya mapato na matumizi ya Wizara kwa mwaka wa fedha 2017/2018.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Ofisi za Ubalozi zimekuwa na changamoto kubwa ya majengo. Ofisi za Balozi zimepanga ofisi, makazi ya mabalozi na makazi ya maafisa ubalozi. Hakuna eneo, Serikali inamiliki majengo ya balozi zake kwa asilimia mia moja kama tunavyoona baadhi ya nchi nyingine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kila mwezi Serikali inatumia fedha nyingi kulipia kodi. Ikumbukwe kwamba mara nyingi Serikali huchelewesha kupeleka fedha katika Balozi hizi, hivyo kuleta fedheha sana kwa Ofisi za Balozi zilizopo ughaibuni. Nashauri Serikali ikaweke bajeti ili Ofisi zetu za Ubalozi zijenge Ofisi zetu huko nje ya nchi ambako Balozi zetu zinawakilisha. Ni vizuri kodi za pango zikalimbikizwa ili ziweze kujenga majengo badala ya kulipa kodi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baadhi ya Balozi za nchi yetu zilipewa viwanja tangu miaka ya 1980. Nashauri Serikali iweke mkakati wa muda mrefu na mfupi ili kujipanga na kuanza kuendeleza viwanja hivyo. Kama upo uwezekano wa kuviendeleza viwanja hivyo kupitia mikopo ya benki, mortgage finance, higher purchase system na njia nyingine ni budi Serikali ikaona jambo hili na kutekeleza mapema ili majengo hayo yaendelezwe. Tukiacha kuendeleza tunaweza kunyang‘anywa, kwani viwanja vingi vipo katika maeneo maalum (Diplomatic Quarters).
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la upungufu wa wafanyakazi nalo ni tatizo kubwa. Ofisi nyingi za Ubalozi zina maafisa wachache sana. Hivi sasa tuna dhana ya diplomasia ya kiuchumi, ni budi Serikali ikaona umuhimu wa kuweka wataalam mbalimbali katika Ofisi za Ubalozi kama wachumi, wanasheria, wenye utaalam wa utalii, Maafisa Uhamiaji ili kuendana na kasi ya diplomasia ya kiuchumi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wageni wengi wafikao katika shughuli za uwekezaji na shughuli nyingine za kibiashara hukosa taarifa za kutosha kutoka taasisi na Wizara. Nashauri suala la matangazo kwa njia mbalimbali zitumike na hasa njia za mitandao ya kijamii kama facebook, twitter, websites na nyingine nyingi ambao zitaleta tija ili kufanya nchi yetu itambulike zaidi Kimataifa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru na naunga mkono hoja.