Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki

Hon. Cosato David Chumi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mafinga Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki

MHE. COSATO D. CHUMI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nimezungumza mara kadhaa na Mheshimiwa Waziri wa Fedha na wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, lakini bado nahisi hakuna uelewa wa pamoja kuhusu suala hili na hasa kuhusu umuhimu wake katika suala zima la FDI. Nashauri Wizara i-take lead hata kwa kuishauri mamlaka kuu kuhusu nafasi ya suala hili hasa katika dhana nzima ya kuelekea uchumi wa viwanda ambao kwa hakika tunategemea pia wawekezaji kutoka nje ambao wangependa kuhakikishiwa masuala muhimu kama Avoidance of Double Taxation na hili la Promotion and Protection of Investments.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na jitihada za kutenga fedha za kukarabati majengo, upo umuhimu wa kutafuta mbinu mpya hata kwa utaratibu wa PPP, kadri taratibu zinavyoelekeza ili tujenge kwenye viwanja ambavyo viko maeneo ambayo ni prime, lakini pia hata kimahusiano, viwanja kama pale Maputo, tumepewa zaidi ya miaka 30 iliyopita, hatujaweza kujenga. Nchi husika pamoja na mengine mengi inaweza kuona kuwa hatujali au hatuthamini mchango wao wa sisi kupewa viwanja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, posting (downsizing ni sawa na downgrading); ninafahamu kwamba kuna maafisa wamerejeshwa, lakini hatujapeleka Maafisa Balozini. Kuna nchi Balozi yupo peke yake bila maafisa, suala ambalo linaathiri sana utendaji. Nchi kama China, Belgium (EU), France, Italy, Uganda, Sweden, Ujerumani na kadhalika, kimajukumu Balozi kukosa Afisa inadumaza jitihada zote za kuelekea uchumi wa viwanda.

Mhashimiwa Mwenyekiti, kwa bahati nzuri Mheshimiwa Waziri, Katibu Mkuu na Naibu Katibu Mkuu wamekua vituoni, hivyo nina imani wanapata feeling ni kwa namna gani utendaji wa kazi unakuwa mgumu kwa Mabalozi wasiokuwa na Maafisa. Kuna dhana kuwa posting ni kama privilege, ninashauri kama suala hili liko juu ya uwezo wa Wizara, kwa uzoefu wao Waziri, Katibu Mkuu na Naibu Katibu Mkuu waieleze mamlaka kuna athari za Mabalozi kutokuwa na Maafisa vituoni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wapo Mabalozi ambao kitaalam na kitaaluma siyo wanadiplomasia, tunajaribu kufikiria Balozi wa aina hiyo awe hana Afisa, atafanya kazi katika mazingira gani? Hata nchi husika zinapata shahada kuwa ni kama tunapunguza mahusianao kwa ku-down size staff.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la Honorary Consul Lubumbashi limezungumzwa sana kutokana na umuhimu wa DRC Congo katika uchumi wetu lakini pia halina gharama za kifedha. Je, limefikia wapi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la malalamiko kuhusu unyanyasaji wa house girls Arabuni limejitokeza mara kadhaa na hata Kamati yetu imelijadili kwa kukutana na baadhi ya wadau na Waheshimiwa Wabunge wenye familia zao Arabuni na hususan Oman.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala hili ni vizuri Wizara ikashinikiza ipasavyo na Wizara ya Kazi na Ajira ili kuwepo utaratibu ambao utaondoa ukakasi unaoanza kujitokeza kiasi kwamba suala hili linaweza kuathiri mahusiano yetu na nchi hizo. Uganda wamefanikiwa sana katika suala hili, wapo wanaotaka wasichana wazuiwe kwenda kufanya kazi Arabuni, lakini kwa upande mwingine watu wanataka fursa kufanya kazi nje. Wafilipino wamefanikiwa katika suala hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaamini Serikali ikiweka utaratibu mzuri, jambo hili ni la manufaa kwa Taifa kiuchumi, lakini pia kimahusiano. Ni matarajio kuwa baada ya michango ya Wabunge Mheshimiwa Waziri kwenye majumuisho atasema lolote hasa kushauri wanaofanya kazi ya uwakala wa kupeleka wafanyakazi wa ndani Arabuni kuwasiliana pia na Balozi zetu kwa taarifa tu. Kimsingi suala limejadiliwa sana katika social media na kwa hisia kali sana, ni muhimu Serikali/Wizara kulisemea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni ukweli kwamba mtumishi wa umma anafanya kazi sehemu yoyote ndani ya Serikali. Hata hivyo ni faida zaidi kuwatumia watumishi pale ambapo wanakuwa na tija zaidi. Kwa mfano, maafisa waliorejea hasa watu wa uchumi ambao wamejengewa uwezo kwa kufanya kazi nje, baadhi yao wamepata mafunzo kuhusu diplomasia ya uchumi. Ni matarajio kuwa kuelekea uchumi wa viwanda, maafisa hao kwa uzoefu na taaluma yao wangeweza kuwa msaada mkubwa kwa Wizara. Hata hivyo, waliporejea wamehamishiwa Wizara, bado ninashawishika kuamini kuwa ilikuwa ni tija kuwa-retain watumishi hao kwa kuangalia pia waliingiaje Wizarani?

Mheshimiwa Mwenyekiti, waliokuwepo enzi Mheshimiwa Jakaya Kikwete akiwa Waziri wa Wizara hii watakumbuka alivyotoa wazo la Wizara kupata maafisa wa fani ya uchumi. Good enough wamekaa na kupikwa katika nyanja hii hapo Wizarani na Balozini, lakini ghafla kumeingia uoga kwa kuwahamishia kwenye Wizara nyingine, sijui uoga huu unasababishwa na kitu gani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya uteuzi wa baadhi ya Wakurugenzi kuwa Mabalozi nje ya nchi, waliopo wanakaimu, nashauri Mheshimiwa Waziri na Katibu Mkuu, pamoja na kuwa uteuzi ni suala la mamlaka kuu, ipo nafasi ya kushauri ili Wizara kupata watendaji ambao siyo makaimu kwa nia ya kuleta ufanisi zaidi.