Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018

Hon. Yussuf Salim Hussein

Sex

Male

Party

CUF

Constituent

Chambani

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018

MHE. YUSSUF SALIM HUSSEIN: Mheshimiwa Mwenyekiti, Bismillah Rahman Raheem, nakushukuru kunipa fursa ya kuwa mchangiaji wa mwanzo kwa siku hii ya leo kwenye hotuba iliyo mbele yetu. Nisiwe mwizi wa fadhila nami niungane na wenzangu kumpongeza Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri, Katibu Mkuu pamoja na Watendaji wote wa Wizara ya Ardhi. Pongezi hizi zinatolewa kwa usimamizi mkuu wa wawili hawa au watatu hawa lakini wameshirikiana vizuri na watendaji wao ndiyo maana wakaweza kupongezwa na kila Mbunge anayesimama leo hii. Ni ombi langu kwao isije ikawa sifa ya mgema.

MHE. YUSSUF SALIM HUSSEIN: Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze na suala la migogoro ya ardhi, kuna migogoro mingi sana ya ardhi hapa nchini, sina haja ya kuitaja lakini nataka nimshauri tu Mheshimiwa Waziri pamoja na timu yake sasa hizi sifa zao basi ziende katika kutatua haya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama eneo la ardhi ndani ya nchi hii liliopimwa ni asilimia 15 ndiyo eneo ambalo limepimwa na kupangiwa matumizi ni dhahiri kwamba mna kazi kubwa ya kufanya ili kuweza kupima eneo kubwa zaidi na kupangiwa matumizi ili kupunguza hii migogoro.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa faida za kupima ardhi na kupanga matumizi zimeonekana wazi, mimi kama Mjumbe wa Kamati nilipoenda Kilombero pale imeonekana tumejifunza, tumeona na wananchi wanafaidika sana, kwa sababu ile faida ya kupata Hati Miliki ya yale maeneo yao inawafanya wao sasa kuenda mbele kiuchumi na kufaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hili sasa tatizo liko wapi, sasa hapa Mheshimiwa Waziri nadhani utanielewa wewe unaelewa vizuri zaidi lakini kwa mtazamo wangu mimi ninawaomba katika Serikali ni vizuri Waziri Mkuu leo yupo mkae katika Serikali, huu mkanganyiko wa kwamba watumishi wengi wa ardhi wako kwenye Halmashauri au wako chini ya Halmashauri ama TAMISEMI wako kule, na wewe sasa unataka kuipima ardhi ili wananchi wapate hati miliki pamoja na kupanga mipango ya ardhi na hawa watu sasa hawawajibiki moja kwa moja kwako, nani atawapatia vifaa vya kufanya hiyo kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri bajeti hii iko kwako, bajeti hii iko TAMISEMI, bajeti hii iko wapi? Sasa hili kama Serikali mkae ili kusiwe na conflict of interest hapa kwenye hii Wizara ama katika eneo hili ili vifaa vya kupimia ardhi vipatikane, wataalam wapatikane, ardhi ipimwe ili kuondoa matatizo. Serikali mpo Waziri Mkuu yupo mkae kama Serikali muondoe haya mambo ya kupeleka hawa TAMISEMI, hawa wapi, hawa wapi, mimi kwa mtazamo wangu ni mipango ya kiujanja ujanja iliyokuweko hapo, wekeni wazi hii Serikali ya Hapa Kazi Tu mfanye kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la pili niendelee kukupongeza kwa namna ambavyo umeweza kutumia busara na hekima kubwa kuwahamasisha wamiliki wa ardhi wakaweza kulipa kodi ya pango, ni kitu kimoja kizuri sana kimeleta tija na kila mmoja ameona faida yake. Tunakuomba uendelee kutumia approach hii ya kuwaelimisha na siyo nguvu, wanaomiliki ardhi kama ambavyo unatumia waendelee kulipa kwa faida ya nchi hii na pato la Taifa liongezeke. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sasa utakapokuja kujumuisha utuambie wale ambao wanamiliki mashamba makubwa, wanamiliki ranchi lakini hawajaziendeleza, hawazifanyii kazi ni wangapi na je Serikali ina mpango gani? Pamoja na hayo nipendekeze kabisa kwamba mashamba yale makubwa ambayo hayajaendelezwa pamoja na ranchi yatumike sasa kuwagawia au kuwaazima kwa muda hawa wafugaji wakati mkiendelea kufikiria ili kupunguza migogoro na vita vya wakulima na wafugaji wakati kuna maeneo kama haya ambayo hayajaendelezwa na watu wanayamiliki. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba kuongelea suala la Kigamboni, ni takribani miaka tisa sasa wananchi wa Kigamboni kwenye ule mradi wa Kigamboni nyumba zao hawawezi kuziuza, hawawezi kutengeneza, hawawezi kufanya kitu chochote wanasubiri mradi, lakini ni miaka tisa mradi haujaanza, Mheshimiwa Waziri hatujui kwamba huu mradi utaendelea kuwepo au hautakuwepo. Kama hautakuwepo wananchi wale kwa muda wa miaka tisa mmewazuia kufanya chochote mtawafidiaje na kama utakuwepo katika kipindi chote hiki mtawafidiaje. Naomba Serikali ijipange hapa ili wananchi wale muwaondoe katika ugumu ule ambao mmewapa hivi sasa, wanakaa wanasubiri mradi, miaka tisa ni mingi sana kwa maendeleo ya mtu binafsi, kwa Serikali ni kidogo, lakini kwa maendeleo ya mtu binafsi ni miaka mingi sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu suala la National Housing, ninaomba Serikali pia ipo, National Housing inafanya kazi moja kubwa sana na kila Mtanzania leo hii anaona kazi inayofanywa na National Housing, wanastahili sifa kweli, wanajitahidi sana. Kuna nyumba za gharama nafuu ambazo wananchi maskini wanatakiwa wanunue zile nyumba lakini ukiziangalia siyo za gharama nafuu kulingana na patol mwananchi wa Tanzania uwezo wake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nyumba hizi siyo za gharama nafuu kwa sababu ya mambo mengi, moja kama kodi ya VAT kwa vifaa vya ujenzi itaondolewa kwa watu hawa wa National Housing wataweza kujenga nyumba hizo na Mtanzania yeyote ataweza kununua, lakini kama kodi ya VAT haitaondolewa basi suala hili litaendelea kuwa gumu kwao. Vilevile gharama nyingine zinaongezeka wao wanapojenga zile nyumba wanaweka gharama za kuweka maji, umeme, barabara ambazo wao wanapaswa kuweka wenyewe. Sasa Serikali ipo, kama mmeamua kujenga nyumba hizo sehemu fulani, kwa nini Serikali haipeleki maji, ikapeleka umeme, ikapeleka barabara kwenye eneo lile kabla ya watu wa National Housing hawajaanza kujenga? Serikali ni moja lakini kwa nini kunakuwa na conflict of interest?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini nchi za wenzetu wanafanya hivyo, ukienda nchi zote za Arabuni na Ulaya kabla ya lile eneo kuendelezwa huduma muhimu za barabara maji na umeme zinapelekwa kwanza, barabara, maji, umeme, shule, masoko yanapelekwa kwanza halafu ndiyo nyumba zinajengwa wananchi wanaenda kuhamia pale ikiwa huduma zote muhimu zipo. Kwa nini kwenye nchi yetu inashindikana?

Kwa hiyo, nikuombe tu Mheshimiwa Waziri kwamba hili nalo mliangalie katika Serikali ili watu hawa wafanye hiyo kazi kwanza kabla ya kupeleka ujenzi katika eneo basi huduma hizi muhimu ziende ili kupunguza gharama. Mkiendelea kwamba watu wa National Housing walipe gharama za kuvuta maji, walipe gharama za kuvuta umeme, walipe gharama za kutengeneza barabara, wananchi wa Tanzania kwa kipato chao wataendelea kushindwa kuzinunua nyumba hizi na mtazijenga mtaziweka zitakuwa hazileti ile faida iliyokusudiwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, ninaunga mkono hoja ya Kambi Rasmi ya Upinzani, lakini niendelee kukupongeza Mheshimiwa Waziri nikuambie kaza kamba, narudia isije kuwa sifa ya mgema, tunategemea kipindi kijacho tuendelee kukusifu zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru.