Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018

Hon. Joram Ismael Hongoli

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Lupembe

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018

MHE. JORAM I. HONGOLI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kupata nafasi nami kuchangia kwenye Wizara hii, nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Waziri na Naibu Waziri kwa kazi kubwa wanayofanya kuhahakisha kwamba wananchi wanapata makazi bora lakini pia kutatua migogoro ya ardhi nawapongeza sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu ya muda niseme mambo machache hasa kuhusu watumishi wa Idara ya Ardhi. Halmashauri nyingi hasa hizi Halmashauri za Wilaya, Halmashauri za vijijini hizi hazina watumishi wa kutosha wa idara hii ya ardhi, hasa Maafisa Ardhi wateule. Wilaya ya Njombe mpaka sasa hatuna Afisa Ardhi Mteule, tukitaka kusaini hati tunamtumia Afisa Ardhi Mteule wa Halmashauri ya Mji, kwa hiyo, mara nyingi tunapotaka kusaini hizi hati zimekuwa zikichelewa kwa sababu na yeye ana majukumu ya Halmashauri yake. Kwa hiyo, niombe Mheshimiwa Waziri ukishirikiana na TAMISEMI tuweze kupata Afisa Ardhi aweze kutusaidia kuweza kupata hati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hati za viwanja zimekuwa zikichelewa na kwenye Halmashauri yangu tuna wananchi wengi ambao wana mashamba ya chai na wangependa wapate hati ambazo zingeweza kutumika kwa ajili ya kupata dhamana kwenye mikopo na sehemu mbalimbali, lakini zimekuwa zikichelewa kwa sababu tu hatuna Afisa Ardhi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, uzoefu unaonyesha kwamba maeneo yote ambayo yana Maafisa Ardhi Wateule ndio maeneo ambayo migogoro inapungua sana, kwa hiyo, wanafanya kazi kubwa sana za kupunguza migogoro, lakini maeneo ambayo yanakuwa hayana Maafisa Ardhi Wateule migogoro inakuwa mingi. Kwa hiyo, tukiajiri Maafisa Ardhi Wateule wa kutosha katika Halmashauri zetu naamini migogoro mingi itapungua. Mfano ni pale Halmashauri ya Mji wa Njombe, tulikuwa na migogoro sana ya ardhi miaka ya nyuma, lakini sasa hivi imepungua na inaendelea kupungua kwa sababu tuna Afisa Ardhi ambaye anafanya kazi vizuri sana. Tunaomba Halmashauri zetu zote ziwe na Maafisa Ardhi Wateule na maafisa wengine wawepo ili kasi ya upimaji wa ardhi na kasi ya utoaji wa hati iweze kuongezeka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili ni kuhusu mikopo ya nyumba. Nampongeza Waziri kwamba kuna mpango wa kuanza kukopesha nyumba kwa wenye vipato vidogovidogo, mpango huu umejikita sana kwenye maeneo ya mijini, tuende vijijini ambako kuna wakulima wadogo wadogo na vijana ambao wanafanya kazi za bodaboda na shughuli ndogondogo waweze nao kumiliki nyumba. Tufuate utaratibu ule wa VIGUTA ambao wanajenga nyumba za bei rahisi sana. Wanajenga nyumba mpaka za shilingi milioni 15, shilingi milioni 25 lakini wanajenga nyumba za ghorofa moja mpaka za milioni 60 na wamejenga maeneo ya Kibaha pia sasa hivi wanajenga maeneo ya Dodoma.

Kwa hiyo, twende vijijini hawa wakulima wetu wadogo wanahitaji nyumba, naamini kwamba kupitia shughuli zao za kilimo, kupitia shughuli zao za bodaboda na ujasiriamali mdogomdogo wakiwekewa utaratibu mzuri wanaweza wakamiliki hizi nyumba, wanaweza wakajenga nyumba na wakarudisha hizo fedha kupitia hizo shughuli zao za kila siku kwa maana ya bodaboda au ujasiriamali na kilimo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme pia juu ya bei viwanja. Bei ya viwanja bado iko juu kwenye baadhi ya maeneo. Kuna maeneo hasa viwanja vile ambavyo vinapimwa na makampuni au mashirika mbalimbali kwa kushirikiana na Halmashauri, viwanja hivi vinauzwa bei ya aghali sana. Kwa mfano, utakuta kiwanja kinauzwa shilingi milioni 10, shilingi milioni 20 eti kwa sababu tu barabara imetengenezwa au maji yamepelekwa. Ukiangalia utakuta kwamba wananchi wa kipato cha chini ambao wana uwezo mdogo wa kupata hizi fedha hawawezi kumiliki hivi viwanja kwa sababu ni vya bei ya juu sana. Tuweke utaratibu mzuri wa kuhakikisha kwamba tunathibiti bei za hivi viwanja, tukiacha hivi makampuni haya kama hali iliyopo utakuta kwamba wananchi wa chini watashindwa kumiliki viwanja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia wanaoweza kununua hivi viwanja shilingi milioni 10, shilingi milioni 20 ni wale watu wenye uwezo tu, ni wale watu wenye kipato cha juu. Utakuta hawa wananchi wenye kipato cha chini wanazidi kwenda pembezoni, wanaondoka katika maeneo yale kwa sababu hawana uwezo wa kumiliki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo naunga mkono hoja. Ahsante sana.