Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018

Hon. Ester Alexander Mahawe

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018

MHE. ESTER A. MAHAWE: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa ulinzi wake kwetu sisi sote. Pili, naomba kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri na Naibu wake wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa kazi kubwa wanayoifanya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni ukweli usiopingika kwamba Mawaziri hawa wanafanya kazi kubwa na nzuri sana ya kuhakikisha wanaondoa kero zote zisizo za lazima, hasa migogoro baina ya wakulima na wafugaji. Miaka michache iliyopita tulishuhudia mapigano na uvunjifu wa amani baina ya wananchi mbalimbali kwa sababu ya ama kuingiliana kimipaka ama wasio na uwezo wengi kunyang’anywa ardhi zao na matajiri wachache. Hata hivyo, tangu Mheshimiwa Lukuvi pamoja na Naibu wake Mheshimiwa Angelina Mabula waingie kwenye Wizara hii, kero hiyo imepungua kwa asilimia kubwa sana. Hivyo, naomba tena kutumia fursa hii kuwapongeza sana kwa kazi nzuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, siku zote penye mafanikio hapakosi changamoto. Niendelee kuiomba Wizara hii kuendelea kupanga miji yetu na kutoa elimu juu ya matumizi mazuri ya ardhi. Kwani ardhi haiongezeki bali watu ndiyo wanaongezeka sasa ni wakati muafaka wa Serikali yetu kuweka mipango madhubuti ya kuhakikisha kunakuwa na matumizi sahihi ya ardhi ili kuliondosha Taifa letu lisiingie kwenye migogoro isiyo ya lazima huko tuendako.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa tunayo Tume ya Taifa ya Mipango ya Matumizi ya Ardhi na kwa mujibu wa sheria No.6 ya mwaka 2007 inayoipa Tume hii mamlaka ya kupanga Ardhi kwa matumizi endelevu ili kuondoa umaskini wa wananchi wetu. Basi niliombe Bunge lako Tukufu litenge bajeti ya kutosha ili kuwezesha Tume hii kuweza kutekeleza majukumu yake kama ilivyokusudiwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi sote tunafahamu kuwa wanaochangia uchumi wa nchi hii kupitia kilimo ni wanawake, lakini kwa bahati mbaya sana sheria za kimila zinamnyima mwanamke haki ya kumiliki. Katiba ya nchi pamoja na Sheria ya Ardhi zote zinatambua mwanamke kumiliki ardhi lakini sheria za kimila zinamfanya mwanamke ku-access ardhi na siyo ku-own ardhi. Hii inafanyika kupitia mumewe au wazazi wake. Pale owner ambaye ni mume au mzazi anapofariki mwanamke huyu hunyang’anywa ardhi hiyo kwa kuonekana ardhi ni mali ya mwanaume.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu katika hili ni kwamba, tunaomba sheria hizi za kimila ziletwe Bungeni, zitazamwe upya ili ziweze kumpa haki mwanamke kumiliki ardhi. Naomba pia nizungumzie kwa ufupi migogoro baina ya wakulima na wafugaji. Tatizo hili bado ni kubwa sana katika maeneo mengi ya nchi yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo basi, ningeshauri Serikali iweke mpango mkakati ili kuweza kutenganisha maeneo ya kilimo na ufugaji. Pia, wafugaji wetu wapatiwe elimu ya kutosha ili waweze kuacha kufuga kizamani bali waweze kufuga kisasa na kibiashara zaidi. Hii itasaidia sana kupunguza migogoro isiyo ya lazima.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho, niipongeze Ofisi ya Rais kupitia MKURABITA. MKURABITA wamesaidia sana kushirikiana na Halmashauri mbalimbali nchini kurahisisha ardhi na kuwapatia wananchi hati za kimila. Hati hizi zimesaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza migogoro ya kimipaka baina ya wananchi. Vile vile, wananchi wameweza kutumia hati hizo kukopa fedha katika benki mbalimbali na kuwasaidia kufufua wajasiriamali. Hali hii imepunguza sana kwa kiasi kikubwa umaskini kwa wananchi wetu. Hivyo basi, naomba sana Wizara hii ya Ardhi iweze kushirikiana na MKURABITA ili wananchi wengi hasa wasio na uwezo waweze kumiliki ardhi.