Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018

Hon. Riziki Shahari Mngwali

Sex

Female

Party

CUF

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018

MHE. RIZIKI S. MNGWALI: Mheshimiwa Mwenyekiti, niruhusu nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Waziri kwa mageuzi makubwa aliyoyafanya na anayoendelea kuyafanya katika Wizara hii. Namtakia kila la kheri na ni matarajio yangu kuwa tutafika mahali pazuri pa kuwa na Wizara na Taasisi zinazowajibika ipasavyo. Katika sekta hii muhimu sana kwa maendeleo ya kijamii katika nchi yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na pongezi na dira hizi naomba nimshauri Mheshimiwa Waziri, kupitia kwa kina bila hiyana hotuba ya Kambi ya Upinzani na kuyafanyia kazi mengi ya mapendekezo yake. Sote katika Bunge lako hili Tukufu tupo kwa maslahi ya wananchi wetu na si vinginevyo na hivyo tukishirikiana itapatikana tija zaidi nchini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba pia nimshauri Mheshimiwa Waziri, kushughulikia kwa kina suala la kuwapatia na kuwahakikishia watumishi wa umma nchini makazi bora na ya uhakika katika maeneo mbalimbali. Hivi sasa NHC inaonekana kuweka mkazo zaidi katika kujenga na kuuza badala ya kupangisha hata kwa watumishi wa umma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, watumishi wa umma kwa asili yao si watu wa kudumu katika maeneo yao ya kazi bali katika maeneo yao ya kuzaliwa. Hivyo msisitizo unapowekwa katika kuwauzia nyumba watumishi panatengeneza mazingira ya kuwafanya watumishi wa umma, kutaka kubaki maeneo waliyopangiwa na wakati mwingine kutumia hata njia chafu kuhakikisha kuwa hawa hawahamishwi. Hali hii si zuri kwa kujenga kada ya watumishi wa umma waadilifu na walio tayari kutumikia popote nchini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata Wabunge wako wengi nikiwemo mimi mwenyewe, tumehangaika kwa zaidi ya mwaka na nusu sasa kutafuta makazi ya kukaa hapa hapa Dodoma, Makao Makuu ya Serikali. Hii ni dalili wazi kuwa Wizara hii na Serikali kwa ujumla haijatoa kipaumbele au haijajipanga ipasavyo katika eneo la makazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana.