Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. DKT. CHRISTINA G. ISHENGOMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimshukuru Mwenyezi Mungu aliyeniwezesha leo kupata nafasi na kuweza kuchangia angalau kwa maandishi. Pili, nichukue nafasi hii kukupongeza kwa kazi nzuri, pamoja na Mheshimiwa Spika, na Naibu Spika na Wenyeviti wenzako. Nizidi kuwapongeza Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri, Katibu Mkuu, Wataalam na watendaji wote kwa kazi nzuri wanayoifanya, nawaombea Mungu wasonge mbele kwa kazi yao nzuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sote tunajua kuwa Morogoro ni mkoa ulioweka historia, kwa migogoro ya wafugaji na wakulima. Nichukue nafasi hii kuipongeza Serikali kwa kazi nzuri inayoendelea nayo, ya kupima, kurasimisha na kutoa hati miliki kwa wananchi. Upimaji wa ardhi na kuwamilikisha wananchi kwa kupewa hati ya kumilikisha ardhi hii ni mkombozi wa kutatua migogoro. Naomba nimwambie Mheshimiwa Waziri na Naibu Waziri, upimaji wa vijiji na mashamba pia ni utatuzi tosha wa migogoro.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ilifikia wakulima kushindwa kwenda mashambani na hasa Mbigili, Kilangali na sehemu za wakulima wa Mpunga Wilayani Kilosa kama Mabwerebwere. Kundi kubwa la wanawake, ambao ndio wakulima wakubwa, kweli, hali ilikuwa mbaya mpaka mapigano.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mifugo pia ilifikia wakati ikakatwakatwa mpaka wengine kufa. Mifugo ilihamia katika Wilaya zote za Mkoa wa Morogoro, Kilosa, Gairo, Mvomero, Morogoro Vijijini, Morogoro Manispaa, Kilombero, Malinyi na Ulanga.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru na kuipongeza Serikali kwani baadhi ya Mawaziri walifika na hasa Mvomero na Kilosa ili kuona na kutatua migogoro hii kwa kusaidiana na Uongozi wa Mkoa na Wilaya, nawapongeza. Tatizo kubwa lilikuwa ni kutafuta malisho na maji katika ardhi iliyo wazi ambayo haijapimwa kisheria.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru na kupongeza Serikali ya Uingereza Sweeden na Dernmark kwa kupitia kwenye Mashirika yao ya Maendeleo DANIDA,SIDA,na DFID, kwa ufadhili wao wa upimaji ardhi mpaka kutoa Hatimiliki na kujenga Masjala ya Ardhi katika Wilaya ya Kilombero, Ulanga na Malinyi. Naamini, upimaji kiasi chini ya Serikali umefanyika Mvomero na kidogo Kilosa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, upimaji ardhi ni gharama, Nashauri na kuiomba Serikali yangu ya Chama cha Mapinduzi, fedha ziendelee kutafutwa, kama tulivyosaidiwa na nchi rafiki zetu kwenye mradi huu wa Kilombero, Ulanga na Malinyi, kusudi wananchi wote katika Wilaya hizi, kila mmoja apimiwe ardhi yake na kupewa hati miliki. Wakati mwingine tunashauri, taasisi Mheshimiwa Waziri, hata maeneo ya taasisi zetu zikapimwa na kupewa Hati miliki za maeneo yao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Serikali yetu ione kuwa upimaji ardhi na matumizi bora ya ardhi ni muhimu kwa utatuzi wa migogoro ya ardhi. Nishauri maeneo yote ya wilaya zote za Morogoro yapimwe na wananchi wapewe hati miliki zao. Matumizi bora ya ardhi kwa kuchanganua ni wapi kilimo, mifugo, ifanyike na kadhalika. Hii itasaidia wananchi na kwa kuambatanisha na miundombinu kama mabwawa na majosho. Sasa hivi tumetulia kwa sababu malisho yapo baada ya mvua kunyesha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama ikiwezekana Mikoa/ Wilaya zote zenye migogoro, ardhi yao ipimwe. Pia Hati miliki inaweza kutumika katika kuomba mikopo. Naomba benki (CRDB, NMB, NBC) wazipokee.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Shirika la Nyumba (NHC) pamoja na Watumishi Housing, natoa pongezi kwa Serikali kwa kazi hii, liko tatizo nyumba hizi ni ghali. Nashauri, Serikali itathmini tena ili gharama zipungue, wananchi na hasa vijana wapate pa kuishi na kumudu maisha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wataalam wa ardhi ni wachache, kwa hiyo, nashauri kwa kupitia Chuo Kikuu cha Ardhi, Chuo cha Tabora na Morogoro udahili uongezeke.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuunga mkono hoja.