Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Kigoma Kusini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. HASNA S. K. MWILIMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niungane na wachangiaji wenzangu kwa kuwapongeza Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri, kwa kuchapa kazi ya kusimamia Wizara hii na kupunguza migogoro ya ardhi nchini na migogoro ya wakulima na wafugaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kuzungumzia migogoro ya mipaka ya vijiji na hifadhi, natambua Mheshimiwa Waziri ni mzoefu wa kupunguza migogoro ya ardhi na kwa kuwa migogoro ya hifadhi na vijiji vilivyosajiliwa vinamgusa kwenye Wizara yake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimwombe sana tena sana Mheshimiwa Waziri Lukuvi tushirikiane kwa ukamilifu sana na Wizara ya Maliasili na Utalii na TAMISEMI ili basi mgogoro wa hifadhi na Vijiji vya Sibwesa na Kalilani, unaweza kutatuliwa na kwisha ili basi wananchi na hifadhi wenyewe waweze kufanya shughuli za kimaendeleo na kufanya mahusiano ya kijamii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, upungufu wa watumishi wa ardhi; niombe kwa Mheshimiwa Waziri akipata watumishi wa ardhi, basi atukumbuke Halmashauri ya Uvinza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nizungumzie suala la NHC, kwanza nimpongeze Mtendaji Mkuu wa Shirika la Nyumba la Taifa Tanzania (NHC). Kwa kuchapa kazi na kwa kasi kubwa anayofanya ya kuwajengea Watanzania nyumba za bei ya kati ambayo Watanzania wengine wamemudu kununua. Rai yangu katika hili tuombe NHC nao waweze kutoa fursa kwa Watanzania kulipa asilimia 10 na baadaye walipe kila mwezi hadi hapo mkataba utapokwisha ndio wapewe Hatimiliki.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hii ya kulipa asilimia 10 halafu zilizobaki mtu alipe ndani ya miezi mitatu kwa kweli inatunyima fursa Watanzania wengi kuweza kununua nyumba hizi na wadau ni wengi, mtu anaweza kuwa na nyumba Dar es Salaam akapenda kuwa na nyumba pia Arusha, lakini kwa utaratibu wa kulipa 10% halafu miezi mitatu awe amemaliza kwa kuchukua mkopo Benki, hili ni gumu. Sababu ni kwamba, wapo Watanzania tayari wana mikopo mingine benki ya biashara, sasa akichukua mkopo benki kwa ajili ya kununulia nyumba mikopo inakuwa mingi inamzidia. Hivyo, nimwombe Mheshimiwa Waziri, aone namna ya kuchukua mfumo wa NSSF mtu analipa downpayment ya miezi mitatu kisha kila mwezi analipa pango hadi amalize.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimwombe pia Mheshimiwa Waziri, NHC waje Uvinza kutujengea nyumba za bei za kati na bei za nafuu katika ukanda wa Ziwa Tanganyika. Ziwa hili lina mandhari nzuri sana na viwanja tunavyo. Sambamba na hili tunaomba pia waje kujenga Uvinza, viwanja vikubwa kwa ajili ya ujenzi wa nyumba hizi tunavyo na huku kwa vile ni Wilaya mpya watumishi wengi wa Serikali na Taasisi mbalimbali hawana nyumba za kuishi, hivyo tunawakaribisha NHC kuja kujenga nyumba za bei nafuu na kati.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema haya, niendelee kumpongeza Mheshimiwa Waziri na Mheshimiwa Naibu Waziri kwa kazi nzuri wanayoifanya kwenye Wizara. Naomba kuunga mkono hoja kwa asilimia mia moja.