Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Ilemela
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote, napenda kumshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa fursa hii ambayo amenipa na kunipa afya njema na hatimaye kuweza kusimama katika Bunge lako Tukufu na kuweza kujibu baadhi ya hoja ambazo zimetolewa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla sijaendelea, naomba nichukue fursa hii kutoa pole kwa wananchi wa Mkoa wa Mwanza na mikoa ya jirani ambao jana wamepatwa na tetemeko na hususan Jimbo langu ambalo karibu Kata saba zote zimepitiwa na tetemeko hilo. Tunamshukuru Mungu kwamba madhara hayakuwa makubwa sana na tunamwomba Mungu amrehemu yule Askari ambaye amepoteza maisha. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimpongeze sana Mheshimiwa Spika, Naibu Spika, pamoja na Wenyeviti wote wa Bunge hili kwa kazi nzuri ambayo mnaifanya na mmekuwa mkituongoza vizuri katika shughuli nzima ya kuendesha Bunge letu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, nampongeza sana Mwenyekiti wa Kamati yetu pamoja na Makamu wake ambao wamekuwa wakitupa ushauri kupitia Kamati ya Bunge ya Kudumu ya Ardhi, Maliasili na Utalii ambayo tumekuwa tukifanyanao kazi vizuri. Namshukuru sana pia Waziri Kivuli ambaye naye amefanya kazi nzuri katika kuwasilisha hotuba yake. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile nachukua fursa hii kuwashukuru sana wananchi wa Jimbo langu la Ilemela kwa kuniamini. Nashukuru Chama cha Mapinduzi kwa kuniamini, lakini Serikali pamoja na Viongozi wa Dini ambao wamekuwa pamoja nasi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia naungana na wachangiaji wote waliotangulia kumpongeza sana Mheshimiwa Rais wetu, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli kwa kazi nzuri sana ambayo anaifanya. Kwa kweli, amekuwa ni kiongozi wa mfano, kiongozi wa vitendo, kiongozi ambaye anasimamia kauli zake. Nasi wasaidizi wake tunasema tutakuwa tayari kumsaidia pale ambapo tunahitaji kusaidia kwa kadiri alivyotuamini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza Waziri wetu Mkuu pamoja na Makamu wa Rais. Kwa kweli wamekuwa wakitupa ushirikiano mzuri na kutupa maelekezo mazuri ya kuweza kufanya kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapokea pongezi zilizotolewa na Waheshimiwa Wabunge. Naomba nichukue fursa hii kuwashukuru sana, lakini niseme pongezi hizo hazikutustahili sisi peke yetu, ni sisi pamoja na ninyi Waheshimiwa Wabunge kwa sababu, ushirikiano mliotupa umefanya pia kazi yetu iwe rahisi. Kwa hiyo, nasi tunawashukuru sana. Maandiko yanasema, “moyo usio na shukrani hukausha mema yote.” Hivyo hatuna budi kuwashukuru Waheshimiwa Wabunge wote kwa ushirikiano wenu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, shukrani na pongezi mlizozitoa, kwetu sisi ndani ya Wizara ni chachu ya kuzidi kuongeza kasi ya kutenda kazi vizuri na kuweza kusaidia jamii ambayo muda wote inategemea utendaji wetu. Nawashukuru sana pia Watendaji wetu ndani ya Wizara ambao wamekuwa wakifanya kazi nzuri sana katika kuona kwamba, shughuli hizi zinafanyika vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa namna ya kipekee kabisa, nimshukuru sana Waziri wangu, Mheshimiwa Lukuvi. Ni Waziri ambaye amekuwa ni mentor wangu mzuri, ni kiongozi ambaye anaweza kuelekeza vizuri, ni kiongozi ambaye anasimamia maamuzi, ni kiongozi ambaye kama ni mwanafunzi mzuri, kwa kweli utafuata nyayo. Mheshimiwa Waziri nakushukuru sana kwa sababu umenifanya niwe kama nilivyo katika Wizara hii ambayo ina changamoto nyingi sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda sasa niseme kwamba Sekta ya Ardhi inakabiliwa na changamoto nyingi. Wote ni mashuhuda, tumeona namna ambavyo Waheshimiwa mmechangia katika kutoa hoja zenu. Katika michango yenu jumla ya Waheshimiwa Wabunge 77 wamechangia; 40 wamechangia kwa njia ya kuzungumza na 37 wametoa kwa maandishi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sehemu kubwa ya michango ya Waheshimiwa Wabunge waliyoitoa, imejikita katika suala zima la utawala wa ardhi ambapo sehemu hii inahusu migogoro ya matumizi ya ardhi baina ya watumiaji mbalimbali wakiwemo wakulima, wafugaji, wawekezaji na hifadhi zetu ambazo zipo nchini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, kuna suala la kutolipwa kwa fidia kwa wakati kama ambavyo mmesema, lakini kuna ucheleweshwaji wa utoaji wa Hakimiliki za Ardhi. Yote haya yako katika utawala wa ardhi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sehemu ya pili ambayo pia imezungumziwa na Waheshimiwa Wabunge wengi sana ni suala zima la upimaji na ramani. Katika maeneo haya limezungumziwa suala la uhaba wa wataalam wa upimaji na vitendea kazi, gharama kubwa za upimaji, umuhimu wa kuimarisha mipaka ya nchi, migogoro ya mipaka ya Vijiji, ya Kata, Wilaya kwa Wilaya, lakini pia migogoro kati ya wananchi kwenye vijiji pamoja na hifadhi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa Mipango Miji, nako Waheshimiwa wengi wamezungumzia. Maeneo mengi waliyozungumzia upande huu walikuwa wakitoa kama ushauri; suala la kuharakisha zoezi la urasimishaji wa makazi katika miji mbalimbali ambalo tayari limekwishaanza; Waheshimiwa Wabunge wameishauri Wizara kuongeza kasi ya uaandaaji wa mipango kabambe, ushauri tumeupokea, lakini pia limezungumziwa suala la uhaba wa watumishi na vitendea kazi katika Halmashauri mbalimbali. Tunakiri uhaba huo upo na ni kikwazo kikubwa katika kupanga miji yetu ili kuwa na miji salama.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine lililozungumziwa na Waheshimiwa Wabunge, ni la maendeleo ya nyumba. Hili limezungumziwa na Waheshimiwa Wabunge wengi sana. Kubwa hapa lilizungumziwa kuhusu gharama kubwa za ujenzi wa nyumba kwa wananchi, imekuwa gharama ni kubwa kwa hiyo, vipato vyao ni vidogo na hawawezi kumudu kulingana na bei ambayo imewekwa na National Housing. Pia, mmezungumzia uhaba wa nyumba kwa watumishi katika maeneo hasa ya vijiji. Haya yote tumeyapokea kwa sababu ni michango; ni hali halisi ambayo ipo, lakini bado tutazungumzia majibu yake kwa baadaye.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ambalo limezungumziwa ni suala la Mabaraza ya Ardhi na Nyumba katika Wilaya zetu. Upande huu umezungumziwa uhaba wa watumishi wa mabaraza katika Mabaraza yetu kwenye Wilaya, lakini pia mkazungumzia suala zima la azma ya Serikali ya kuwa na mabaraza haya katika kila wilaya. Ni kweli, hatujaweza kutimiza azma hiyo, lakini nia ya Serikali ni njema na tutaendelea kuifanyia kazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kutoa utangulizi wa maeneo ambayo Waheshimiwa Wabunge wameyachangia, naomba sasa nianze kujibu hoja mbalimbali ambazo zimetolewa, nikianza na hoja kutoka kwenye Kamati yetu ya Bunge ya Kudumu ya Wizara ya Ardhi, Maliasili na Utalii ambayo imetoa hoja mbalimbali. La kwanza amezungumzia ufinyu wa bajeti katika Tume yetu ya Mipango ya Matumizi Bora ya Ardhi ambayo imekuwa ikipatiwa rasilimali kidogo kulingana na kazi wanazozifanya na ndivyo jinsi ambavyo mmeliona suala hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda niwahakikishie kwamba Serikali imekuwa inatoa fedha kulingana na bajeti inavyopata katika Tume ile. Kwa sasa Tume ile inalo Fungu lake, inayo Vote yake Na. 3 ambayo sasa imeanza kutengewa bajeti kuanzia mwaka 2016. Mwanzoni ilikuwa iko ndani ya bajeti ya Wizara kwenye Fungu Na. 48, lakini kwa kasi ambayo yao na kazi wanayofanya, wameweza kufanya majukumu yao kulingana na pesa waliyopata na wanafanya kazi nzuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kwa mafungu kadiri yatakavyozidi kuongezeka, tutawaongezea kwa sababu Tume hii ni muhimu sana katika kufanya shughuli za upangaji miji yetu katika maeneo yetu hasa katika mipango ya matumizi bora ya ardhi. Kwa hiyo, niseme tu kwamba tumepokea maoni hayo na tutazidi kuyafanyia kazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka wa fedha huu wa 2017/2018 Serikali imeipatia Tume vibali vya ajira kwa watu saba. Kwa sababu wakati mwingine pia utekelezaji wake haukuwa mzuri sana kwa sababu hawakuwa na personnel ya kutosha. Kwa hiyo, wataongeza wataalam wengine saba ambao ni kutoka katika kada mbalimbali kwenye eneo lao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, Serikali kupitia Wizara yangu itaendelea kuipatia Tume ushirikiano mzuri, hasa wa rasilimali fedha na watumishi pamoja na vitendea kazi ili waweze kufanya ile kazi ambayo wote tumeitambua kwamba ni muhimu, Tume hii ifanye kazi yake vizuri katika kusaidia katika mpango wa matumizi bora ya ardhi katika maeneo yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala pia la kuongeza kasi ya elimu kwa umma kwa matumizi ya ardhi ambayo yameonekana kwamba kwa watumiaji mbalimbali imekuwa ni shida. Katika kutekeleza jambo hili, majukumu ya kuandaa mipango ya matumizi bora ya ardhi, ngazi ya Kata na Vijiji, Tume hutoa elimu kwa timu za usimamizi wa ardhi kwenye vijiji na hususan katika Halmashauri. Hili limekuwa likifanyika na kumekuwa na ushirikiano mzuri sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, timu ya kusimamia mipango ya matumizi bora ya ardhi katika Wilaya hujengewa uwezo wa kuratibu na kupanga utekelezaji na usimamizi huu wa mipango ya matumizi bora ya ardhi nchini. Hivyo, katika mwaka wa fedha 2016/2017 Tume ilitoa elimu katika Halmashauri 24 nchini. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, Tume imekuwa ikifanya kazi yake vizuri, pamoja na ufinyu wa bajeti ambao umekuwa ukitokea. Pia Tume hii huandaa vipindi maalum vya elimu kwa umma. Hii yote ni katika kupanua uelewa katika maeneo yetu ili kusaidia kujenga uelewa wa pamoja. Imekuwa ikitumia njia mbalimbali ikiwemo kutumia vyombo vya habari, maonesho ya Saba Saba, Nane Nane, Wiki ya Utumishi na kadhalika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, haya yote yanafanyika ili kuweza kupanua wigo wa kutoa elimu. Vipindi hivi pia vimekuwa vikihusisha sheria, taratibu na miongozo ya kupanga na kusimamia matumizi bora ya ardhi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mpango wa Elimu kwa Umma umeandaliwa kwa kushirikisha wadau wa matumizi ya ardhi kama Taasisi za Umma na Asasi Zisizo za Kiserikali. Care International Tanzania, Haki Elimu, Ardhi Oxfarm na Ujamaa Community Resource Team. Hawa wote wamekuwa wakishiriki katika zoezi hilo. Kwa hiyo, kazi inayofanyika ni nzuri kiasi kwamba ni kiasi cha kufuatilia tu zile programu zinapokuwepo ili watu waweze kujengewa uelewa mzuri zaidi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala lingine wamezungumzia kuwa Serikali itenge fedha za kutosha ili kuyafikia maeneo mengi zaidi nchini yenye migogoro ya mipaka ya ardhi. Katika suala hili Serikali itaendelea kutenga fedha kadri zinavyopatikana. Aidha, Wizara pia itaendelea kushirikiana na wadau wa Sekta binafsi ili kufikia maeneo mengi katika kutoa elimu na masuala ya ardhi ili kuepusha migogoro hii. Kwa hiyo, Serikali peke yake haiwezi, ndiyo maana tunashirikisha sekta binafsi ambazo zipo katika taaluma hii ili kuweza kufikia wananchi wengi kwa wakati.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukosefu wa fedha pengine unakuwa nao ni kikwazo sana, lakini Serikali itaendelea kuishughulikia changamoto hii katika kuweza kupata rasilimali hiyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Kamati imetoa ushauri katika mambo mengi na sisi tunayachukua na tumeyapokea kama yalivyo, wamezungumzia suala la Serikali ihamasishe Halmashauri kukopa ili kutekeleza miradi ya kupima viwanja. Hilo tumelipokea. Kuwezesha Bodi ya Mfuko wa Fidia ya Ardhi iweze kutekeleza majukumu yake tumelipokea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile kuhusu Wizara kuendelea kufanya kazi kwa pamoja na wadau wengine, tumelipokea na tunaendelea kulifanyia kazi; kuhusu Sheria ya Ardhi kwamba iboreshwe na kusimamiwa kikamilifu ili kuondoa migogoro baina ya watumiaji ardhi, huo ushauri tumeupokea, tunaendelea kuufanyia kazi; kuongeza kasi ya kutoa elimu nimesema tunaendelea, kwa hiyo, ushauri huo tumeupokea na tunaufanyia kazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwamba Serikali itenge fedha za kutosha kwa ajili ya kuanzisha Mabaraza ya Ardhi. Kama nilivyosema kwenye utangulizi, nia ya Serikali ni kuwa na mabaraza haya katika nchi nzima. Tuseme tu kwamba kwa mujibu wa Sheria ya Mabaraza ya Ardhi ya Na.2 ya mwaka 2002, kila Wilaya inatakiwa kuwa na Baraza. Lengo la Serikali ni kuwa na Mabaraza haya katika kila Wilaya. Hadi kufikia 15 Mei, 2017 Serikali tayari ilikuwa imeshaunda Mabaraza 97 kati ya yale Mabaraza 100 tuliyokuwa tumekusudia kuweka, ambapo kati ya hayo Mabaraza 53 tayari yanatoa huduma; na Mabaraza 44 hayajaanza. Kwa hiyo, nia ya Serikali ni njema na tunaendelea kuifanyia kazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka wa fedha 2017/2018, Serikali inatarajia kuajiri watumishi 291 na kati ya hao, watumishi 98 ni ajira mpya katika Mabaraza. Kwa hiyo, tuna imani tukishawapata hao, basi yale maeneo yote ambayo yana upungufu wa watumishi hao katika Sekta hiyo, watakuwa wamepata. Kwa hiyo, nawaomba sana Waheshimiwa Wabunge tuwe na uvumilivu, Serikali ina nia njema na itaweza kufanya haya yote kadri ya muda unavyoruhusu na bajeti inavyoruhusu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja nyingine ilitolewa kwamba, Serikali iangalie namna ya kupunguza gharama za ujenzi wa nyumba za National Housing. Hili zimezungumzwa na wachangiaji wengi, lakini Kamati pia imelizungumza. Naomba niseme kwamba Serikali imepokea ushauri huu, lakini pamoja na hayo Mheshimiwa Rais alishatolea maelekezo, kwa sababu wengi walilalamikia gharama kwamba zimekuwa kubwa. Tumekuwa tukilieleza siku zote kwamba pengine gharama kubwa inachangiwa na National Housing kufanya kila kitu wao wenyewe; kwa kuweka miundombinu ya barabara, maji na umeme.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, hili tayari Mheshimiwa Rais ameshalitolea maelekezo kwamba Taasisi zinazohusika na huduma, kabla National Housing hawajaweza kufanya uwekezaji wao, basi kama ni barabara iwe imeenda, miundombinu ya umeme iwe imesogea na maji yawe yamekwenda. Wakiweza kusongeza huduma hizo, ni wazi gharama ya nyumba itapungua. Kwa hiyo, hili linafanyiwa kazi na Mheshimiwa Rais ameshalichukulia hatua.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hili limefanyika hata kwenye hizi nyumba za Iyumbu zinazojengwa sasa hivi hapa, tayari maelekezo yalishatolewa. Kwa hiyo, nina imani kwamba kwa sababu maelekezo yamekwenda katika Halmashauri zote katika kutekeleza agizo la Mheshimiwa Rais, Waheshimiwa Wabunge ambao mnataka kuwekeza katika maeneo yenu kwa kuwashirikisha National Housing, basi nadhani tukitekeleza hayo pia kwao itakuwa ni rahisi sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, National Housing wako tayari kwenda maeneo yote na siyo National Housing peke yake, hata Watumishi Housing ambao wanajenga nyumba za watumishi nao wanahitaji kuwa na miundombinu hiyo hiyo ambayo inatakiwa kuwekezwa. Hii itapunguza sana gharama za nyumba ambazo tunazungumzia. Kwa hiyo, hili tumelichukua na Rais amelitolea agizo na litatekelezwa kadri ambavyo miradi itakavyozidi kuwekezwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja nyingine ilitaka Wizara ihakikishe Manispaa ya Dodoma inatekeleza dhima iliyokuwa ikifanywa na CDA na kupeleka huduma ya jamii ya miundombinu. Hii ilikuwa ni hoja ya Kamati na walizungumzia Iyumbu na nimeshaizungumzia. Kwa hiyo, suala la miundombinu limewekwa sawa.
Mheshimiwa Mwenyeiti, kuna suala lingine ambalo limezungumziwa, kuhusu kusimamia utekelezaji wa Sheria ya Mipango Miji kwani kuna changamoto nyingi. Niseme tu kwamba Sheria Na. 8 ya 2007 inazipa Halmashauri zetu za Wilaya na Miji pamoja na Manispaa mamlaka ya kupanga na kudhibiti uendelezaji wa miji. Wizara kama msimamizi mkuu, kwa Waraka wake Na.1 wa mwaka 2006 unaoelekeza taratibu za kufuata katika kubadili matumizi ya ardhi na mgawanyo wa viwanja na mashamba, hili linasimamiwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile Wizara ilitoa Waraka Na. 4 mwaka 2006 ambao unatoa maelekezo ya miongozo ya udhibiti ya undelezaji miji. Kwa hiyo, jukumu hili bado liko katika Halmashauri zetu kwa sababu sheria zipo. Tukiangalia tu Wizara peke yake tunaweza pengine tukachelewa kudhibiti hili suala.
Mheshimiwa Mwenyeiti, naomba sana katika hili Halmashauri zetu Sheria Na. 8 ya mwaka 2007 hii ya Mipango Miji lazima isimamiwe katika maeneo hayo. Haya yote yataepusha hizo changamoto ambazo tunazisema. Kwa hiyo, Wizara kama msimamizi, tuko karibu sana na Halmashauri kushirikiana nazo, lakini Waheshimiwa Wabunge ni jukumu letu pia kuhakikisha kwamba tunapoona hali inakuwa siyo nzuri, kwa sababu tunahitaji miji iliyopangika na miji ambayo ni salama, ni jukumu letu pia kuwakumbusha wataalam wetu kuweza kusimamia mambo hayo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala la mipango kabambe ya miji ambayo inatakiwa isiishie kupanga tu miji mikubwa, bali ipanue wigo wake. Hili linafanyika na sasa hivi kuna kujumla ya mipango kabambe 26 ambayo iko katika hatua mbalimbali. Mpaka sasa mji wa Mtwara pamoja na Musoma mipango yake kabambe imekamilika toka mwezi Mei na Mheshimiwa Waziri alikwenda kuzindua. Kwa hiyo, mipango mingine bado iko kwenye mchakato na tutaendelea kufanya hivyo. Wizara imeandaa programu ya utayarishaji wa mipango kabambe kwa nchi mzima ikiwemo miji midogo ambayo inakua kwa kasi. Kwa hiyo, hili tunalichukulia kwa uzito wake na tutaendelea kulisimamia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, upande wa hoja za hotuba ya Waziri Kivuli, ametoa hoja nyingi sana. Niseme tu kwa ujumla wake pamoja na zile ambazo nimemaliza kuzijibu kwamba tunaandaa pia kitabu ambacho kitajibu hoja zote, maana kwa muda uliopo siwezi kuzijibu zote, nitajibu chache tu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala la kupima ardhi ya Mkoa wa Morogoro kama mpango wa dharura ili kupunguza migogoro; wameongelea kwenye hotuba hiyo. Niseme tu Tume inaendelea na mipango ya matumizi bora ya ardhi. Kama nilivyosema awali na hata katika kujibu maswali tunapojibu, Morogoro ilichukuliwa kama eneo ambalo Serikali ilikuwa inaliangalia kwa jicho pana zaidi kutokana na migogoro yake iliyokuwepo. Ndiyo maana zile Wilaya tatu ambazo sasa tunapima ardhi yote, imeanzia Morogoro, ni kwa sababu ya tatizo hilo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, hili nalo tunalichukua, hivyo vipande vya ardhi vyote vitapimwa na kuwekewa alama za kudumu ili kuweza kuepusha hii migogoro.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hili ambalo limeongelewa kwenye maeneo ya Hembeti, Ndimboho, Buguma, Mkindo, Kigugo, Kambara vilivyopo katika bonde la Mto Mgongola Wilaya ya Mvomero, nadhani Serikali itachukua taratibu zake vizuri kuweza kuona kwamba tunafanyaje, kwa sababu hali halisi kila mmoja anaifahamu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Tume inashirikiana na programu ya kurasimisha ardhi katika Wilaya tatu nilizowaambia. Kwa hiyo, hatua zinachukuliwa na tunaendelea. Vile vile Tume inashirikiana na Halmashauri za Wilaya Mvomero na asasi za kiraia kama ile ya PELUM Tanzania TFCG na IWASHI katika kutoa elimu. Lazima elimu iwafikie ili waweze kutambua ni nini kinatakiwa kufanyika. Kwa hiyo, haya yanafanyika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine, Kambi Rasmi imeongelea kuhusu changamoto kubwa ya kibajeti katika Wizara na wakashauri pengine Serikali iongeze nguvu katika kushirikiana na Sekta binafsi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mradi wa Urasimishaji katika eneo la Kimara ni mojawapo ya mfano ambao tunaweza kuusemea. Mradi huu lengo lake pia ulikuwa umekusudia kurasimisha viwanja 6,000, lakini mpaka tunavyoongelea sasa, viwanja 4,333 tayari vilikuwa vimeshapimwa na Hatimiliki zimetolewa 82 na kuna barabara ya urefu ya kilomita tisa imetengenezwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ile speed ndogo ya kutoa hati inachangiwa na wananchi wenyewe. Kama Wizara imeweza kupima viwanja 4,333 kati ya 6,000, ilikuwa imekusudiwa watu wote 4,333 wawe wamechukua hati. Sasa hiyo huwezi kusema kwamba ni tatizo la Wizara. Ni tatizo la wananchi ambalo tunasema tunawapa elimu ili waweze kuona manufaa ya kurasimishiwa maeneo yao ili pia waweze kutumia zile hati katika shughuli za maendeleo. Viwanja vimepimwa lakini watu hawachangii. Ni jukumu letu Waheshimiwa Wabunge kuendelea kuhamasisha wananchi wetu kuchukua hati zao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitumie fursa hii kwa wale wote ambao zoezi hili linaendelea ikiwemo na Mkoa wa Mwanza katika zile Wilaya za Nyamagana na Ilemela, lakini tunao wenzetu wa Musoma, Lindi, Kigoma, Ujiji na Sumbawanga; nawaomba sana, zoezi hili ni kwa nia njema ya kutaka kuwasaidia wananchi. Kwa hiyo, pale ambapo urasimishaji unafanyika, nawaomba sana wananchi, kwanza mchango siyo mkubwa ukilinganisha na gharama halisi ya upimaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niseme kwamba nia ya Serikali ni nzuri. Kwa hiyo, watumie fursa hii ya sasa ambayo ipo. Mkishaweka mipango kabambe katika maeneo yenu, unaweza kukuta urasimishaji tena hauna nafasi na tusingependa tufikie hapo. Kwa hiyo, hatua tuliyonayo sasa ni vizuri wananchi wanakaifanyia kazi iliwaweze kufaidika na zoezi hili linaloendelea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Waheshimiwa Wabunge wameongelea suala la migogoro kati ya mpaka wa Kisopa King’azi na Mloganzila; fidia ilishalipwa kama ambavyo ilikuwa imetajwa katika masuala mazima ya uendelezaji na hii iko katika Wilaya ya Kisarawe ambayo ilikuwa imeanzishwa kwa GN hiyo 117 ya tarehe 28 Novemba, 1980. Katika ule mgogoro uliokuwepo pale, wale ambao walikuwa wameendeleza walikuwa tayari Serikali imelifanyia kazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mujibu wa GN 69 ya 29/1/2016, eneo hilo la Ubungo ilimega sehemu ya Kinondoni ambayo ilijumuisha maeneo ya Kisopa na King’azi, Mloganzila hiyo ilikuwa ni chanzo cha migogoro. Napenda kulitaarifu Bunge lako Tukufu kuwa Wizara itashirikiana na TAMISEMI ili kupata suluhu ya mgogoro huu. Kwa sababu kama kunakuwa na mgongano wa GN au kunakuwa na mgongano wa kijiji na kijiji, bila kuwa na elimu kwa wale hasa walioko katika maeneo yale inaweza ikaleta shida; suala la mipaka wakati mwingine linakuwa lina shida.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mara nyingi Wilaya mpya inapoanzishwa siku zote inakuwa na changamoto zake, hasa upande mmoja unaposhindwa kuridhia ama kuachia baadhi ya maeneo. Kwa hiyo, migogoro kama hii inakuwepo tu, lakini Serikali itaendelea kushirikiana na TAMISEMI kuhakikisha mgogoro huu unakwisha katika maeneo hayo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kulikuwa na hoja nyingine inayosema Serikali imalize ufafanuzi kuhusu mgogoro wa mpaka kati ya vijiji na hifadhi ya wanyama Serengeti, ambayo imezungumziwa hasa katika maeneo ya Vijiji vya Marenga, Nyamakendo, Mbalimbali na vijiji vingine kama vilivyo, hivi vyote katika Wilaya ya Serengeti vina mgogoro na hifadhi kama ambavyo ilivyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, namshauri tu Mheshimiwa Mbunge kuwa ni vema tukasubiri maamuzi ya Mahakama, sababu hili suala liko Mahakamani na hatuwezi kulitolea maamuzi hapa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala lingine ambalo lilikuwa limezungumziwa na Kambi Rasmi ya Upinzani kwamba Serikali ieleze Bunge sababu za kuipa TRA mamlaka ya kukusanya kodi ya majengo ambayo ilikuwa ni chanzo muhimu kwa Halmashauri zetu. Tumesema TRA ilipewa jukumu la kukusanya kodi ya majengo ili kuimarisha mfumo wa ukusanyaji kodi. Hii yote ilipangwa kwa nia njema katika kurahisisha ukusanyaji maduhuli ya Serikali na zoezi limeanza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile limezungumziwa suala zima la kupanga rates ambazo pengine wakati mwingine zinaweza kuwa ziko juu au zipangwe kulingana na viwango. Hii tumechukua kama ushauri ambao tunaweza kwenda kuufanyia kazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wamezungumzia suala la kutatua migogoro ya eneo la mnada wa Pugu Kajiungeni na UKIVIUTA, Kipawa. Eneo la Mnada wa Pugu Kajiungeni lipo chini ya Wizara ya Kilimo na Mifugo na eneo hili limevamiwa na wananchi na kuendelezwa. Utatuzi wa mgogoro huu utahusisha wadau mbalimbali ikiwemo Wizara yenyewe ya Kilimo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba wavute subira kwa sababu itafanyiwa kazi. Vile vile kuhusu UVIKIUTA, suala hili lilifikishwa Mahakamani na Mahakama ilitoa ushindi kwa UKIVIUTA. Kwa hiyo, nalo tayari lilishatolewa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna lingine limeongelewa kwamba Wizara iandae takwimu za hati ambazo zipo. Ushauri umezingatiwa, tutalifanyia kazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wameongelea pia suala la Wakuu wa Wilaya kuingilia majukumu ya Mabaraza ya Ardhi. Suala hili, kwa mujibu wa Sheria ya Mabaraza ya Ardhi, Sura Na. 216 kama ambavyo imerejewa mwaka 2002, Mabaraza ya Ardhi na Nyumba Wilaya ni chombo huru cha kuamua migogoro ya ardhi. Hivyo haipaswi kuingiliwa na chombo chochote katika kutekeleza majukumu yake. Kwa hiyo, masuala haya yako kisheria na tunasema yataendelea kusimamiwa chini ya sheria husika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala la kuhamisha ajira ya Watumishi wa Sekta ya Ardhi kutoka Halmashauri kwenda Serikali Kuu. Serikali itaendelea kutekeleza ile dhana ya D by D, hatuwezi kusema leo tunaibadilisha hapa kwa sababu tayari utekelezaji wake unakwenda vizuri na wote tunaona, lakini hayo yote yatafanyika kwa utaratibu ambao Serikali imepanga.
Mheshimiwa Mwenyekiti, utaratibu wa kuhamisha ajira za watumishi katika Sekta ya Ardhi kutoka Halmashauri, unakinzana na dhana hii ambayo Wabunge wanaipendekeza. Ili kuongeza huduma kwa wananchi, Wizara imefungua ofisi za Kanda, kwa hiyo, tutashirikiana na Watumishi wa Ardhi kwenye Halmashauri kuona kwamba kazi hizi zinafanyika katika utaratibu mzuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Waheshimiwa Wabunge wamezungumzia suala la Serikali kuwa na vipaumbele vya kutekeleza kulingana na mapato yake kuliko kuwa na vipaumbele vingi ambavyo wakati mwingine havitekelezeki.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niseme kwamba Serikali imekuwa ikitekeleza majukumu yake kwa kuweka vipaumbele muhimu ikiwa ni pamoja na kutekeleza bajeti kulingana maoteo yanayopangwa katika projections zetu tunazozifanya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo, suala la kuwa na vipaumbele vingi sidhani kama ni sahihi sana kwa sababu wakati mwingine unapanga ukitarajia kwamba maoteo yanakwenda kufanya kazi katika utaratibu uliopangwa. Isipokuwa wakati mwingine ufinyu wa bajeti unafanya usitekeleze jukumu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, huwezi kusema kwamba usipange, maana hizi ni projection ambazo ni lazima uziandae. Kwa hiyo, unapoandaa unategemea pia utapata pesa na tunafanya kazi kwa cash budget, kwa hiyo, lazima pia haya nayo tuyazingatie. Pia fedha ya Serikali inatolewa kutegemeana na makusanyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nami nawaomba tu Waheshimiwa Wabunge, tusisitize katika kukusanya pato la Serikali ili tuweze kuhudumia bajeti zetu ambazo tumezipitisha. Ni vema wananchi walipe kodi zao kwa wakati ili kuwezesha Serikali kutekeleza majukumu yake. Usipolipa kodi kwa wakati, matokeo yake shida inakuwa ni hiyo. Sasa hivi watu mpaka wafuatwe na Polisi, Summons za Mahakama ndiyo walipe kodi. Kwa nini?
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama tukiwa wazalendo kweli, kila mmoja akatimiza wajibu wake; unajua unatakiwa kulipa kodi ya ardhi kila mwaka, wewe lipa. Kwa nini unangoja mpaka uletewe Summons? Wakipelekewa Summons za Mahakamani, kesho yake unaona foleni kubwa iko kwenye Ofisi za Wizara. Sasa hivi ukienda TRA hapaingiliki katika zile kodi za majengo. Watu wamejaa pale, wanashinda pale. Kwa nini unangoja mpaka ufikie hatua hiyo? Lipa kodi kwa wakati ili uondoe usumbufu. Tukiweza kuwajibika, haya yote hayatakuwa tena na usumbufu katika utekelezaji. Kwa hiyo, ni jukumu letu kuona ni jinsi gani tunasaidiana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kupitia hoja mbalimbali za Kambi Rasmi ya Upinzani, naomba sasa nianze kujibu hoja za Waheshimiwa Wabunge mmoja mmoja na nitaziunganisha zile zinazofanana ili kwenda na wakati na kwa zile ambazo nitakuwa nimezijibu wakati najibu hoja za Kamati pamoja na Kambi Rasmi ya Upinzani, nitaziruka na sitazirudia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Innocent Bilakwate, Mheshimiwa Abdallah Ulega na Mheshimiwa Zuberi Kuchauka, walikuwa wanazungumzia suala la kupunguza urasimu katika upimaji ardhi kwa wananchi wa vijiji ili kuwaondolea usumbufu. Wizara yangu imepunguza sana gharama. Walikuwa wanazungumzia gharama na kupunguza urasimu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara yangu imepunguza sana gharama na hata kama kwenye bajeti mmesikia, tumezidi kupunguza gharama. Lengo letu ni kuhakikisha usumbufu kwa wananchi haupo. Kwa hiyo, ni jukumu letu kuwahamasisha wananchi wetu waweze kuona umuhimu wa kupima maeneo yao ili waweze kuwa na umiliki halali ambao utawasaidia pia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lengo la Wizara ni kuendelea kuhakikisha tunawawezesha wananchi. Unamwezesha kwa kutumia ile ardhi yake; ukiweza kumpa Hakimiliki kisheria tayari utakuwa umemsaidia. Kwa hiyo, niseme kwamba Wizara itaendelea na utaratibu wa kupata vifaa vya upimaji ili waweze kupimiwa kwa urahisi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa habari njema tu, kama mmesoma magazeti ya jana, tayari kuna tender imetangazwa kwa ajili ya ununuzi wa vifaa hivyo na ile No objection tuliyokuwa tunaisubiria kutoka World Bank, nayo tayari imetoka. Kwa hiyo, tuna uhakika vifaa hivi mtakwenda
kuvipata na kazi itafanyika na watu watapimiwa, tuwahamasishe tu wajitokeze kwa wingi ili waweze kupimiwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala lingine ambalo limeongelewa na Wabunge kama wanane; ameongea Mheshimiwa Mama Makilagi, Mheshimiwa Paresso, Mheshimiwa Shekilindi, Mheshimiwa Mwassa, Mheshimiwa Bashungwa, Mheshimiwa Bilakatwe, Mheshimiwa Chumi na Mheshimiwa Allan. Wamezungumzia kwamba Serikali itenge fedha kwa ajili ya kuanzisha mabaraza. Nilishalizungumzia lakini bado limejirudia. Lengo letu bado lipo pale pale, tumechukua hoja zetu na tutafanya kama ambavyo imekusudiwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika ule utaratibu wa maeneo ambayo pengine hayana Wenyeviti, nachukua fursa hii kumwomba sana Mkuu wa Mkoa wa Singida pamoja na Mkuu wa Mkoa wa Tabora; tunajua huko kuna matatizo na Wenyeviti ambao muda wao tayari ni kama ulikwisha lakini Wizara ilishawaandikia barua kwa ajili ya kuleta mapendekezo katika hatua ile. Mpaka leo hawajatoa na limejitokeza hapa kama ni tatizo. Kwa hiyo, nawaomba sana Waheshimiwa Wakuu wa Mikoa katika maeneo hayo watusaidie ili tuweze kutatua tatizo hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia suala la uwezeshaji Mabaraza nalo limezungumzwa na Mheshimiwa Paresso tena, likazungumzwa na Mheshimiwa Makilagi, yamejirudia katika maeneo hayo. Mabaraza yana changamoto nyingi na ndiyo maana yamezungumzwa sana. Wengine wamezungumzia suala la kutoa elimu kwenye Mabaraza ya Kata. Napenda niwakumbushe tu Waheshimiwa Wabunge kwamba suala la Mabaraza ya Kata yapo chini ya TAMISEMI. Kila tunapokwenda katika ziara tumekuwa tukishirikiana nao kuweza kutoa elimu katika yale mabaraza kwa kutumia wale Wasajili wetu wa Mabaraza kwenye yale maeneo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tulishasema kwamba Halmashauri yoyote iliyopo tayari, Wizara ipo tayari kutoa wawezeshaji wakisaidiana na Mwanasheria wa Halmashauri kuweza kuwapa elimu wale Wajumbe wa Mabaraza waweze kufanya kazi yao vizuri. Hii ni kwa sababu haya yapo chini ya TAMISEMI, lakini kwa sababu yote yanasimamia Sekta ya Ardhi, basi tunashirikiana kuhakikisha tunawapa elimu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la elimu lilizungumzwa na Waheshimiwa Wabunge hapa ni kwamba wapewe mafunzo ambayo imezungumzwa pia na Mheshimiwa Chumi, Mheshimiwa Bilakwate na Mheshimiwa Allan ili waweze kufanya kazi yao vizuri. Tutaendelea kusaidiana na Halmashauri zetu. Lengo letu ni kuhakikisha kwamba hawa watu wanapata elimu na wanawasimamia masuala yote ya ardhi katika maeneo yao kwa sababu wao ndio hasa waliopo kwenye zile changamoto.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kupitia Bunge lako hili, nawashukuru sana viongozi wa Mkoa wa Katavi na Sumbawanga, Wakuu wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya pamoja na Wakurugenzi, wamechukua hatua mahususi ya kuweza kuanza utaratibu wa kutoa mafunzo ya mabaraza hayo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, Wilaya ya Kalambo walitoa mafunzo ya siku ya zaidi ya 20 kutaka kuwezesha yale Mabaraza. Jambo hili linawezekana pale ambapo dhamira ya dhati katika maeneo na viongozi husika wakiliona kwamba ni changamoto, inawezekana kuyapatia ufumbuzi. Nitumie fursa hii kuwapongeza na nitoe rai kwa mikoa mingine kuweza kuiga mikoa hii miwili ambayo imeweza kufanya kazi nzuri katika kuelimisha Wajumbe wa Mabaraza waweze kufanya kazi zao vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Mbaraka Kitwana alikuwa anazungumzia mgogoro wa Shamba la Utumani lenye ukubwa wa hekari 4,000 na shauri hili lipo Mahakamani, kwa hiyo akataka sasa watu wa Mafia wafanyiwe ugawaji. Sasa nasema, hili suala bado halijafikia hatima yake. Kwa hiyo, haliwezi kufanyika jambo lolote katika utaratibu huo, lazima hatua za Kimahakama ziishe ili tuweze kwenda kwenye hatua nyingine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia Mheshimiwa Shangazi amezungumzia suala la Mnazi Sisal Estate la Lushoto ambalo nalo amelizungumzia. Taratibu za kufuta zimekwama kutokana na miliki za shamba hili kuwekwa dhamana benki. Hii ni kwa sababu kuna wamiliki wengi wa mashamba wengine walichukulia mikopo na hasa kwa Korogwe, Mkoa wa Tanga, mashamba mengi sana yamechukuliwa mikopo benki.
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo linapokuwa limewekwa dhamana ya benki, huwezi kuanza kufanya taratibu nyingine. Kasoro hizi ambazo zinatokana na hiyo, Halmashauri inaagizwa pia itume tena ilani katika shamba hilo ili benki waweze kupewa nakala ya ilani hiyo na ufutaji utaendelea baada ya taratibu zote kukamilika. Kwa sababu kuwa na dhamana isiwe ni kikwazo. Tumeni tena ilani na benki wapewe nakala ili wajue pamoja na kwamba wana dhamana hiyo, lakini shamba hili lina changamoto zake. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Mwakasaka alizungumzia suala la nyumba za NHC, watu kununua kwa wingi na kupangisha. Sina uhakika na malalamiko yake labda angetupa mfano mzuri ni wapi, kwa sababu Tabora, Uyui na Igunga kuna nyumba zimejengwa pale, hazijapata wapangaji na hazijanunuliwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa aliyenunua na kuhodhi nyingi ni zipi? Kwa sababu hiyo ni case study ambayo iko wazi kwamba nyumba zipo, lakini hazijanunuliwa. Ni vyema akatufahamisha ni wapi ambapo nyumba zimenunuliwa na mtu mmoja halafu anaanza kupangisha ili tuweze kuchukua hatua.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Lupembe vile vile amezungumzia nyumba ambazo zimejengwa lakini zinakaa idle. Niseme kwamba nyumba kukaa idle wakati mwingine Halmashauri pia zinakuwa zinahusika. Mnaomba kujengewa, zinajengwa. Zikishajengwa zimekamilika, hamko tayari kuchukua. Sasa hii kidogo inakuwa ni shida. Ndiyo maana tukasema, Mheshimiwa Kalanga alikuja na wazo la kwamba watu wapewe miaka mitano kulipa lakini Shirika la Nyumba linatoa miaka 10 kwa mpangaji mnunuzi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nitoe maelekezo katika nyumba zilizojengwa ambazo Halmashauri hazijawa tayari kuzichukua, utaratibu wa shirika utabadilika kuliko kuacha ziharibike, zitakwenda kwenye ile sera ya mpangaji mnunuzi na zitauzwa kwa mtu yeyote aliyeko tayari kununua ili zile nyumba ziweze kupata wapangaji. Ikienda kwa mpangaji mnunuzi, maana yake una miaka kumi ya kuweza kulipa. Mheshimiwa Kalanga aliomba miaka mitano, lakini National Housing wameweka miaka 10. Kwa hiyo, bado nafasi tunayo ya kuweza kutumia nyumba hizi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sana, kwa sababu tusipofanya hivyo, haya mambo wakati mwingine tunaweza tukawa tunawalaumu wawekezaji, tunalaumu National Housing lakini sisi wenyewe tunaohitaji pia tunakwamisha. Niwape mfano mzuri wa Jimbo la Busokelo, waliomba wakajengewa nyumba nzuri za mfano na tayari wamechukua; na Jimbo la Momba pia nao wamejengewa nyumba nzuri na zinafanya kazi na wanakwenda hatua nyingine ya pili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Halmashauri zetu, mnapohitaji muwe tayari pia kuhakikisha kwamba mnakwenda kuzichukua nyumba zile ili kuepusha uwekezaji unaokwenda kudumaa. National Housing hawawezi kusonga mbele kama wanawekeza halafu haziendi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Sakaya ameongelea wawekezaji wa miradi mbalimbali kwamba wapewe ardhi kuenenda na maeneo yanayofaa katika miradi husika. Viongozi wa Vijiji wapewe elimu. Hili tumelichukua kwa sababu Sheria ya Ardhi iko wazi na inatoa utaratibu mzima wa ugawaji ardhi. Sasa katika hili nadhani ni elimu tu izidi kutolewa kwa watu wetu waweze kujua ni jinsi gani ya kuweza kusimamia haya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna tatizo la ujenzi holela ambalo limeongelewa na Mheshimiwa Kigola. Nadhani nimeliongelea kwa upana wakati nazungumzia masuala ya uandaaji wa mipango kabambe na kuhamasisha wananchi kutojenga ili kuepuka hili. Wizara inashirikiana na mamlaka za upangaji katika maeneo hayo ili kuandaa mipango kabambe na hili suala litakuwa limepungua.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Cosato Chumi ameongelea kupewa baadhi ya Watumishi nyumba za CDA. Wizara haihusiki moja kwa moja na utoaji wa nyumba hizi katika kupangia watumishi, lakini haya yamepokelewa na yanaweza kufanyiwa kazi kulingana na maombi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la Watumishi wa CDA kutawanywa katika maeneo mengine, hili pia lipo chini ya Wizara husika kwa sababu CDA sasa hivi ipo chini ya Manispaa ya Dodoma, maana yake ipo chini ya Ofisi ya TAMISEMI. Hivyo, Wizara inayohusika kwa kushirikiana na Wizara yetu, kwa sababu wako pia Watumishi wengi tu wa Sekta ya Ardhi, basi tutaona ni jinsi gani bora ya kuweza kutatua hilo tatizo na hasa katika kuwapanga watu katika maeneo yanayotakiwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nadhani muda umekuwa finyu na mambo ni mengi. Naomba uniruhusu tu nizungumzie suala moja la asilimia 30 ambayo imezungumziwa. Ndugu zangu suala la asilimia 30 limezungumziwa na Waheshimiwa Wabunge nane.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nirudie tena; baada ya ile Sheria ya Bajeti mwaka 2016 tulivyoipitisha ya kuondoa mambo ya retention, asilimia 30 haipo tena. Ndiyo maana tulisema na nikipita katika ziara nawaambia kwamba Halmashauri zinazopanga bajeti ya asilimia 30 kutegemea Wizara, tunapotosha bajeti zetu, kwa sababu hiyo iliondolewa katika bajeti iliyopita.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pesa zinazokuja kwenye Halmashauri, zinatokana na OC ambayo Wizara inakuwa imepangiwa shilingi bilioni kumi kwa mwaka 2016/2017 kwa nchi nzima na zinatolewa kutegemeana na zinavyoingia. Kwa hiyo, haiji kama asilimia 30 ambayo wewe unaiweka. Kwa hiyo, unapoweka kwenye bajeti yako asilimia 30 kwamba unadai Wizara, kibajeti kidogo inakuwa haiko sahihi sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba pia nisisitize katika hili maana limekuwa likijirudia, hakuna asilimia 30 kama 30 inavyorudi kule. Kinachokuja ni OC kwa ajili ya kuziwezesha Halmashauri zetu kwa shughuli za sekta na pesa hizo lazima zifanye kazi ya Sekta ya Ardhi na siyo Mkurugenzi kupanga matumizi yake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba sana, zitakuja kwa kadri zinavyoingia kutegemeana na bajeti ya Wizara iliyowekwa kuliko hiyo ambayo ninyi mnaitegemea sasa kwamba ni asilimia 30, inapotosha kila kitu katika maelezo yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naunga mkono hoja na nawashukuru kwa kunisikiliza.