Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CUF
Constituent
Tanga Mjini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. MUSSA B. MBAROUK: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kwanza nianze kuunga mkono hoja ya Kambi Rasmi ya Upinzani. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini baada ya kusema hayo, nami nina yangu machache ya kuzungumza.
Mheshimiwa Naibu Spika, labda kwanza nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu ambaye ametujalia afya njema na kuweza kukutana katika Kikao chetu hiki cha Bunge na hatimaye kuipitia taarifa hii ya Intergovernment Agreement Between the United Republic of Tanzania and the Republic of Uganda Concerning the Pipeline System of the East African Crude Oil Pipeline Project.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, nami nina yangu ya kushauri. Kwanza, nishukuru kwamba mradi huu umekuja kwenye Jimbo letu la Tanga ambayo itakuwa ndiyo last destination. Vilevile niwashauri wale ambao mradi huu utapita katika maeneo yao, katika mikoa nane, wilaya 24 na vijiji takribani mia moja na ushehe.
Mheshimiwa Naibu Spika, niombe kwanza tushirikishe wananchi wetu katika suala hili lakini vilevile na Serikali nayo itoe maandalizi maalum kwa sababu wananchi wengi huu mradi wamekuwa wakiusikia juujuu, lakini hapa nishukuru kwamba Kamati yetu ya Nishati na Madini imelifanyia kazi vizuri na imetoa baadhi ya tahadhari na hata Kambi Rasmi ya Upinzani katika baadhi ya maeneo ambayo nikipata nafasi nikayataja huko mbele, imetoa tahadhari, lakini makubwa zaidi ninayoona ni haya yafuatayo.
Kwanza, Serikali iwe makini katika kila hatua kuepuka tabia ya kusaini mikataba ambayo baadaye inakuja kuonekana kuwa mikataba mibovu kama ilivyosemwa na Kamati.
Mheshimiwa Naibu Spika, lingine ni kuhusu malipo ya fidia, yazingatie bei ya soko la ardhi iliyopo sasa na pasiwe na visingizio. Kwa mfano katika eneo la Chongoleani wananchi kule wamelipwa eka moja kwa thamani ya shilingi milioni mbili na baadhi walikuwa wakitaka ufafanuzi zaidi kujua kwa nini wanalipwa pesa hiyo kwa sababu wapo watu ambao walikuwa wamenunua, ule ni Ukanda wa Pwani kabisa, wapo watu waliokuwa wamenunua eka moja kwa zaidi ya hata milioni 10, lakini baada ya kutaka ufafanuzi tukaenda kwa Mkuu wa Mkoa wakaitwa wataalam wa ardhi wao wakasema tu moja kwa moja kwamba bei ya milioni mbili iliwekwa kabla hapajawekwa miundombinu.
Mheshimiwa Naibu Spika, hilo kwa kweli lilileta taabu kidogo kwa sababu binafsi kwa maoni yangu niliwahi kuwaeleza kwamba lazima mjue wakulima hawa maeneo yao ambayo yalikuwa ndiyo chanzo chao cha mapato yanachukuliwa. Zao kubwa katika maeneo ya Chongoleani ni minazi, mihogo, midimu, milimao, michungwa na mambo mengine.
Mheshimiwa Naibu Spika, labda nikueleze tu, ndimu katika maeneo ya Chongoleani imekuwa na faida kubwa sana kwa sababu mdimu mmoja unaweza kutoa visalfeti viwili na kila kiroba cha ndimu kikifikishwa katika soko la Dar es Salaam ni sawasawa na Sh.40,000. Kwa hiyo, mti mmoja wa mdimu unaweza kutoa katika zao la awamu moja Sh.80,000 ya Kitanzania.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo niliiomba Serikali kwamba kwa kuwa wananchi wale maeneo yao yanachukuliwa basi watafutiwe maeneo mbadala. Vilevile pia kama tunavyojua kwamba kuna thamani ya ardhi na thamani ya mimea, kwa hiyo, yote hayo niliitaka Serikali iyazingatie. Sasa nawashauri Waheshimiwa Wabunge wengine ambapo mradi huu utapita wawe makini na hilo ili tusije tukawarudisha wananchi wetu katika lindi la umaskini.
Mheshimiwa Naibu Spika, lazima tujue kwamba kilimo ni uti wa mgongo wa Taifa letu. Kwa kuwa Serikali kwa kushirikiana na Serikali ya Uganda tunaamua kuchukua maeneo yale ya wananchi, basi lazima wananchi wale tuwatafutie maeneo mbadala kwa ajili ya shughuli zao za kilimo. Kwa mfano, katika eneo la Chongoleani lipo shamba la mkonge linalomilikiwa na Kampuni ya Amboni Limited ambayo sasa hivi imebadilisha jina inaitwa Cotel Company Limited. Shamba lile limekuwa haliendelezwi, kwa hiyo, naiomba Serikali hususan Mheshimiwa Rais alifutie hati shamba lile la Amboni ambalo liko eneo moja linaitwa Mwanyungu na wananchi wale ambao maeneo yao yamechukuliwa wapewe maeneo ya Mwanyungu sasa katika shamba la mkonge ili waendelee na shughuli zao za kilimo.
Mheshimiwa Naibu Spika, nasema hivi kwa sababu wengi wamekuwa wakilalamika kwamba maeneo yamechukuliwa lakini fedha waliyolipwa haikidhi kwenda kununua mashamba au ardhi maeneo mengine. Wale ambao nyumba zao zimepitiwa na mradi pamoja na kwamba ni nyumba za tope lakini kwa fedha waliyopewa labda mtu anaweza akawa ana eka nne amepata labda shilingi milioni nane na fidia ya mimea labda amepata shilingi milioni nne, shilingi milioni 12 leo huwezi ukajenga nyumba yenye hadhi na ya kisasa, kwa sababu lengo letu ni kwamba wananchi wetu waishi katika maisha bora na nyumba ambazo zina huduma zote za kibinadamu. Kwa hiyo, mimi niombe tu kwamba Serikali iwe makini katika kufidia wananchi wetu lakini pia kuwapatia maeneo mbadala ya kilimo.
Mheshimiwa Naibu Spika, lingine ni kuhusiana na suala zima la first priority kwa wale wakazi ambao wanapitiwa na mradi. Kwa mfano, zimetajwa ajira hapa takribani 10,000 ambazo zitajitokeza katika mradi, lakini kutakuwa na zile ajira ambazo ni permanent takribani 1,000. Sasa hatukuchanganuliwa hapa katika hizi ajira 1,000 labda zitagawanyika vipi ki-percentage, kwamba katika 1,000 asilimia kadhaa itatoka Uganda, asilimia kadhaa itatoka Tanzania. Tuwe makini hapa, tusije tukakuta zile ajira 1,000 zote zinatoka kwa wananchi wa Uganda.
Mheshimiwa Naibu Spika, niombe tena viongozi wa ngazi mbalimbali ambao wanapitiwa na maeneo ya mradi kuanzia Waheshimiwa Wabunge, Madiwani, hata Wenyeviti wa Vijiji na Vitongoji wawe wanashirikishwa kwa karibu katika zoezi zima la mradi huu. Kwa sababu lengo ni mradi huu uwe na manufaa kwa Watanzania isije ikawa tena mradi umekwishaanza panaanza manung’uniko ya hapa na pale.
Mheshimiwa Naibu Spika, binafsi nashukuru katika Jimbo langu nimeshiriki kwa asilimia kadhaa au kwa asilimia takribani 70 katika haya masuala yote ya mradi, ndiyo maana umeona pia hata Tanga hapakutokea manung’uniko mengi kuhusiana na mradi huu. Kwa hiyo, naishauri Serikali kule ambapo mradi huu utapita wananchi, Viongozi wa Vijiji, Mitaa, Madiwani, Waheshimiwa Wabunge washiriki kikamilifu. Waelewe in and out katika kila kinachoendelea katika mradi huu ili baadaye tusije tukaja tukabeba lawama.
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile pia nawakumbusha Waheshimiwa Wabunge, mtakaposhiriki kikamilifu katika mradi huu tukawatetea wananchi wetu itakuja kuwa ni sababu mojawapo ya wewe kurudi tena humu Bungeni.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, nakushukuru.