Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

Hon. Mendard Lutengano Kigola

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mufindi Kusini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

MHE. MENDRAD L. KIGOLA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa namshukuru Mwenyezi Mungu na mimi kupata nafasi, ili niweze kuchangia Mapendekezo ya Mpango wa Taifa wa mwaka 2018/2019.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze na kuipongeza Serikali, katika miaka miwili Serikali imefanya mambo makubwa sana na Wabunge kwa macho yetu kwa masikio yetu, tumesikia na tumeona. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapopanga mpango wa miaka ya mbele lazima uangalie miaka ya nyuma umefanya nini. Serikali miaka ya nyuma tukichukua reference kwa kweli, imefanya kazi nzito sana na mambo yanaonekena. Nikianza kutoa mifano, Serikali ilipanga kununua ndege na kweli ndege imenunua. Serikali ilipanga kutoa elimu bure na kweli kazi hiyo imeanza kutoa elimu bure kwa watoto wetu. Serikali ilipanga kupanua Bandari ya Dar es Salaam na kweli Serikali inapanua Bandari ya Dar es Salaam. Serikali ilipanga kujenga bomba la mafuta kutoka Tanga mpaka Uganda, Serikali inafanya na tunaona na tunasikia. Serikali ilipanga kununua meli kule Bukoba na Mheshimiwa Rais tumeona hata juzi akisema pale, tunaona Serikali inafanya. Serikali tunaona kila inachopanga na inasema, tulipanga hiki tumefanya moja, mbili, tatu, ndiyo utekelezaji tunaoutaka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, natoa pongezi kubwa sana kwa Mheshimiwa Rais wetu Dkt. John Pombe Magufuli kwa kweli, anasimamia vizuri. Ndiyo maana nataka tuende kwa data, ameahidi nini amefanya nini na anasema kila mmoja tunaona kitu kinachofanyika. Leo, sasa Serikali imeleta mapendekezo ya mpango, yaani Wabunge tutoe mapendekezo, sio tulaumu, tutoe mapendekezo tunataka nini. Sasa na mimi nataka nitoe mapendekezo yangu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, bahati nzuri nimesoma vizuri mwongozo, nimesoma vizuri mapendekezo ya Serikali ambayo imeleta kwa Wabunge tutoe mapendekezo. Kuna maeneo ambayo lazima tupendekeze ili Serikali ikae vizuri na Serikali ili ifanye kazi vizuri lazima iwe na fedha. Bahati nzuri Serikali imesema kuna mapungufu kidogo katika ukusanyaji wa kodi, hiyo na mimi nakubaliana kabisa, sasa tunafanyaje? Naomba niishauri Serikali, kwenye eneo hili lazima tuhakikishe kwanza tunatoa elimu ya kutosha kwa walipa kodi wetu ili mtu anapolipa kodi asione kama adhabu, aone kama ni hiyari yake kutoa kodi bila matatizo yoyote. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kinachotakiwa ni kutoa elimu ya kutosha kwa wafanyabiashara, hilo la kwanza. Pili, vitendea kazi lazima viwepo. Kwa mfano, sasa hivi wafanyabiashara wengi zile mashine ambazo tunatumia kwa ajili ya kukata risiti mashine zile hazipo, bado ziko chache wengine hawana, nyingine wanasema mbovu. Kwa hiyo, hatuwezi kukusanya mapato kama vitendea kazi bado havieleweki. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili, sasa hivi ukusanyaji kodi sio lazima uende TRA, naomba Serikali itafute mfumo mzuri, wewe unaweza hata ukawa barabarani unatembea ukatumia hata M-Pesa ukalipa kodi. Kwa mfano, kama wewe ni mfanyabiashara au kama wewe mtu una magari yako kwa mfano hata insurance, kama mtu anataka kulipa insurance siyo lazima aende TRA au aende wapi, analipa kwa njia ya M-Pesa tu. Kwa hiyo, nataka niseme hivi tuhakikishe kwamba tunaweka vitendea kazi vimekaa vizuri kwa walipa kodi wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo ni la msingi sana, nimeona kwenye taarifa ni uvujaji wa mapato. Hii ni njia ambayo Serikali inaweza kuidhibiti na bahati nzuri mnajitahidi sana kudhibiti mianya, zile njia za panya, njia za nini sasa hivi hazipo zimepungua sana naipongeza. Na mimi naiomba Serikali iendelee kutafuta mbinu kuhakikisha kwamba, kile kiasi ambacho kinakusanywa kinatumika vizuri, hakivuji, hakuna mianya ile ya uvujaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo naipongeza Serikali kwenye Wizara ya Afya. Wizara ya Afya hata Mheshimiwa Ummy leo amejibu swali hapa vizuri sana kwamba Wizara ya Afya zamani ilikuwa na uwezo wa kupewa shilingi bilioni 29, lakini sasa hivi tuna uwezo wa kuipatia Wizara ya Afya shilingi bilioni 296 kama sijakosea, ni kiwango kikubwa sana. Katika hiyo, tumekwenda vizuri, katika fedha hiyo bahati nzuri Serikali imeangalia kwamba umuhimu wa watu lazima tuwe na afya nzuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nitoe msisitizo, Serikali ihakikishe kwamba vituo vya afya vijijini vinamaliziwa kujengwa, kuna maboma mengi sana, bado hatujamaliza vituo vya afya. Kuna zahanati, tuna maboma ya zahanati bado hayajaisha nchi nzima, lazima tujitahidi tuhakikishe kwamba kwenye sekta ya afya tunapeleka fedha za kutosha na bahati nzuri kwenye mpango umeongea, lakini bajeti inayokuja kwa sababu tunaongelea mpango halafu tunakuja kuupangia bajeti. Naomba kwenye sekta ya afya tuangalie tumeipatia fedha ya kutosha kwenye bajeti inayokuja na mpango ueleze vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu sekta ya maji. Sekta ya maji vijijini naiomba Serikali, bado iongeze nguvu kubwa sana. Kwa sababu hata kwenye Jimbo langu la Mufindi Kusini wananchi wanapata taabu sana ya maji, lakini katika mpango, bahati nzuri Waziri wa Fedha ameeleza vizuri kwamba, ataiangalia sekta ya maji, naomba aiweke kipaumbele zaidi. Tuhakikishe kwamba miundombinu yote ya maji, kama kuna matenki, kama kuna visima, tuhakikishe kwamba wananchi wana uwezo wa kupata maji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, miaka ya leo hii mwananchi hawezi kutembea kilometa 10, kilometa 20. Kuna sehemu nyingine nimeona watu wanachota na punda kilometa ngapi, hayo ni mambo ya zamani sana, naiomba Serikali ihakikishe kwamba sekta ya maji imekaa vizuri, wananchi wetu wapate maji ya kutosha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikija kwenye sekta ya umeme, bahati nzuri umeme vijijini Serikali imekaa vizuri na wameshafanya survey tayari kwenye vijiji vingi. Hata kwenye Jimbo langu la Mufindi Kusini wamekuja, tumeona wamefanya survey na Serikali imeahidi, imesema kila kitongoji kitapata umeme na kila kaya itapata umeme. Tumeona hatua zimeanza kufanyika, lakini nataka niiombe Serikali, tuhakikishe kila tulichopanga tunatengeneza time frame, tusije tukaahidi halafu tukachukua muda mrefu sana, kwa sababu sasa hivi tunaweka na muda, ukiahidi kitu lazima kuwe kuna progress ya kazi, lakini bahati nzuri kwenye vijiji vyetu mmenza tayari, survey imeshafanyika, sasa tunategemea Serikali ianze kupeleka nguzo katika vijiji vyetu na katika mitaa yote ambayo imeshapimwa tayari. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niongelee tena suala lingine ambalo ni la muhimu sana. Wenzangu wameshaongea, hasa Wabunge wanaotoka Rukwa ambalo ni suala la kilimo hasa kilimo cha mahindi inaonekana bado kuna tatizo na tatizo tunaongelea ni soko. Nafikiri kuna kilimo cha matumizi ya chakula, kuna kilimo cha biashara. Kwa mfano, nataka nikwambie Tanzania bahati nzuri kila mikoa imepata neema, ukienda Kaskazini wenzetu utakuta wanaongelea labda karafuu, ukienda Magharibi huku utakuta wanaongelea masuala ya pamba, ukienda Kusini wanaongelea masuala ya korosho, ukienda mikoa ya Rukwa Kusini tena wanaongelea masuala ya mahindi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama kwenye korosho Serikali inaweza ikatafutia soko korosho na ika-subsdise fedha. Kama kwenye pamba Serikali inaweza ikapeleka fedha kwenye pamba, basi ipeleke fedha hata kwenye kilimo cha mahindi ili watu wa mahindi waweze kuhakikisha kwamba kilimo kinaenda vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nikuambie kitu kimoja, Tanzania ni nchi ambayo inategemea zaidi kilimo cha mahindi kuliko kilimo kingine. Nitoe ushauri kwamba kama Serikali itashindwa kununua mahindi ya wakulima, mahindi yakaozea kwenye maghala basi iruhusu ifanye open market, kama kuna uwezekano wa watu kuuza nje, wauze nje. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, bahati nzuri nataka nikumbuke Mheshimiwa Rais alisema vizuri sana, kwamba tusiwagandamize wakulima wa mahindi. Kama debe litauzwa hata shilingi 100,000 basi liuzwe laki moja ili mkulima apate. Wewe kama unaona unashindwa kununua basi lima. Na sasa hivi bahati nzuri mvua zinanyesha sehemu kubwa sana, lakini isionekane kwamba wakulima wa mahindi hatuwa-support, tuwape uhuru. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunasema kwamba inaweza ikatokea njaa, tuwafundishe jinsi ya kuhifadhi mahindi, lakini tusiwafundishe kuuza kwa bei ndogo ili wapate hasara, wakulima wanalalamika. Tuseme wahifadhi mahindi, lakini wawe wanaweza kulima zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo nimeliona, hili naipongeza Serikali kwa upande wa mbolea, Serikali imetoa bei elekezi kwa wafanyabiashara, imesimamia vizuri na imefanya vizuri sana. Sasa hivi wakulima wana uwezo wa kununua ile mbolea lakini ukienda kwenye Mjimbo yetu mbolea bado haijafika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano Jimbo la Mufindi Kusini hata Wilaya ya Mufindi sasa hivi ndio tunalima lakini mbolea ya kupandia haipo. Naomba Waziri wa Kilimo atusaidie kwenye hili, mbolea ya kupandia ifike miezi hii; miezi hii Mufindi kule ndio tunalima sasa hivi. Mbolea ya kupandia ukileta mwezi wa 12 hatuwezi kuoandia mahindi, tutakuwa tumeshachelewa, tunaenda na muda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naiomba sanaSerikali kwa upande wa kilimo ihakikishe kwamba mbolea inafika kwa muda unaotakiwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni kuhusu gesi; hili suala la gesi kwanza ni neema. Tumepata neema kubwa sana kwamba uchumi wa nchi ili upande tumefanikiwa kupewa gesi na gesi inatoka Mtwara lakini ili gesi ipate soko ni lazima tupanue wigo. Kama kuna viwanda vinatakiwa kutumia gesi basi tuwaruhusu watumie gesi iliSerikali iweze kukusanya hela nyingi sana na fedha nyingi sana tunaweza tukapata kutoka kwenye masuala ya gesi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna viwanda vingi kwa mfano mikoa ya Pwani hiyo nimeona wamejenga viwanda vingi sana. Sasa vile viwanda kama havitatumia gesi, tutazalisha gesi nyingi halafu tunasema soko tunashindwa kumbe viwanda vile havitumii gesi. Naiomba Serikali basi ihakikishe kwamba viwanda vyote vinatumia gesi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine hata Mufindi tuna viwanda vingi sana, kama kweli mtatuletea gesi na viwanda vya Mufindi, kwa mfano tuna Kiwanda cha Chai kikubwa sana, katika Afrika nadhani ni kiwanda cha kwanza, tuna Kiwanda cha Karatasi, katika Afrika nadhani ni cha kwanza na tuna viwanda vya mbao. Vile viwanda vyote vikitumia gesi, nadhani gesi itapata soko kubwa sana na Serikali itakusanya mapato makubwa na bajeti tuliyopanga ya mwaka 2018/2019 tumesema Serikali itakusanya shilingi trilioni 32.47. Sasa hizi shilingi trilioni 32 kama hatutapata revenue kutoka kwenye gesi, tutapata wapi? Tukitaka kufanikiwa makusanyo makubwa lazima tuhakikishe tunafanya makusanyo makubwa kwenye gesi, tunaweza kufikisha hilo lengo la shilingi trilioni 32.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuhakikishe tunakusanya mapato kutoka kwenye madini, tutapata hizo shilingi trilioni 32, tunapata mapato kutoka kwenye maliasili na utalii tunaweza kufanikiwa. Kama hatutakusanya kwenye vyanzo vikubwa tukategemea kwamba tutakusanya kutoka kwenye sigara, vinywaji maana kwenye vinywaji ndiyo tunapandisha hata bei, hii hatuwezi kufikia lengo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lazima tuhakikishe kwamba kwenye vyanzo vikubwa kwanza vile tunakusanya mapato ya kukamilika halafu tunakuja kwenye vyanzo vidogo. Ukisema kwamba labda utategemea minada ya kuuza haya masoko ya pembeni ya wakulima wadogo wadogo hii haitasaidia. Tuhakikishe kwamba tunakusanya kutoka kwenye vyanzo vikubwa ili tufikie lengo tulilojiwekea la shilingi trilioni 32.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu upande wa wafugaji na wenyewe lazima waheshimiwe sana. Kuna sehemu nyingine nataka nimshukuru Waziri wa Mambo ya Ndani, sasa hivi ule ugomvi wa wafugaji na wakulima umepungua sana, naipongeza sana Serikali, ni jambo zuri sana hilo, sasa hivi hatujasikia malalamiko makubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Serikali isimamie vizuri kuhakikisha kwamba wafugaji wanalindwa kwa sababu na wafugaji lazima tuwaheshimu, wanafuga ng’ombe na tunapata nyama, bila nyama hatuwezi kuishi. Ukiangalia katika Afrika nchi ya kwanza kwa ufugaji nadhani ni Ethiopia kama sikosei na ya pili ni Tanzania, kwa hiyo lazima tuwaenzi. Lazima kuwe kuna mpangilio mzuri ili isitokee kugombana kati ya wafugaji na wakulima. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naipongeza Serikali naona kwenye hilo imefanikiwa na sasa hivi inakwenda vizuri na huo mpango wa kudhibiti wafugaji na wakulima ili waende vizuri. Wafugaji wafuge mifugo hatuwakatalii, wakulima na wenyewe walime kama inavyowezekana, hii itakuwa ni vizuri sana na watu watakuwa na maisha mazuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niishie hapa, nakushukuru sana. Ahsante sana.