Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Serengeti
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. MARWA R. CHACHA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru sana. Naomba na mimi nichangie kwenye mpango huu mambo machache, lakini ya msingi sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama kuna Wabunge huwa hawaielewi hii Serikali, mmojawapo ni mimi huwa siielewi, ninazo sababu za msingi mnisikilize wote mkae kimya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nchi hii ni ya wakulima na wafugaji, unapokuja kwenye mikoa iliyopo Kanda ya Ziwa, wafugaji waliopo kandokando mwa hifadhi na mapori ya akiba na misitu wana kilio kikubwa sana. Ng’ombe wa wafugaji wa mikoa ya Mara, Simiyu, Mwanza mpaka huko Kagera inataifishwa na Serikali hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi maskini ambao tegemeo lao ni mifugo, leo unapiga mifugo mnada, unamuacha mfugaji akiwa maskini akiwa ana watoto wanamtegemea yeye, akiwa na rundo la familia nyuma wanamtegemea yeye awalipie ada za chuo kikuu na shule za sekondari, leo mmepiga minada, watu wetu wamebaki maskini. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Jimbo la Serengeti ng’ombe wameuzwa, watu wanalia. Mama mmoja ng’ombe wameuzwa wote, mama akapigwa miaka mitatu jela na kulipa faini ya shilingi 800,000, ameacha familia haina chochote, mnatupeleka wapi ninyi Serikali ya CCM? Mnasema ninyi ni Serikali ya wanyonge, mnatesa wafugaji. Mimi nawaambia wafugaji wa Kanda ya Ziwa wale wa Mikoa ya Simiyu, Biharamulo, Serengeti na Mkoa wa Mara hii Serikali ya CCM 2020 ishughulikieni kweli. Haiwezekani wafugaji wetu waendelee kuteswa na Serikali hii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashindwa kuwaelewa, njoo kwenye viwanda. Nchi hii tuna viwanda vya kuchakata mazao ya mifugo vingapi, kiwanda kipo kimoja tu, tena cha mjasiriamali mmoja Mtanzania yupo pale Mwanza, ndiye mwenye kiwanda kikubwa ambacho angalau. Tembea kokote huko hakuna wana bucha tu wanaita viwanda, hakuna kiwanda ni butchery. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka Waziri Mheshimiwa Mpango, tuambie mna mpango gani kuhusu viwanda vya kuchakata mazao ya mifugo, mtuambie hapa. Ukienda hata kwa yule ambaye ana kiwanda pale Mwanza analalamika kweli, kodi kibao, hakuna namna ya kumsaidia yule mjasiriamali, tumsaidie kwa ajili ya kusaidia wafugaji wetu wa Kanda ya Ziwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka Mheshimiwa Mpango uniambie, mifugo ya nchi hii ambayo kimsingi tuna mifugo mingi, mna mpango gani maana kiwanda ni hicho cha huyo na kiwanda kingine kipo huku Rukwa yule Mbunge mstaafu yule Mzee Mzindakaya, kinakaribia kufa kile. Tumeshindwa kuwasaidia watu wetu ili wawe na viwanda vya kwao wenyewe. Kwa hiyo, nikisema siwaelewi, siwaelewi kweli na wananchi hawawaelewi kweli. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye fedha za maendeleo, mwaka wa fedha uliopita zilitengwa shilingi trilioni 11.8 kwa ajili ya maendeleo, zikatoka shilingi trilioni
6.5 sawa na asilimia 55, fedha za maendeleo hizo. Kwenye bajeti ya mwaka huu, fedha zilizotengwa za bajeti ni kama shilingi trilioni 12 kwenye robo ya kwanza zimetoka shilingi trilioni 1.3 sasa piga zipo robo nne. 1.3 trilioni mara nne ni ngapi, utaona ni kama asilimia 44, hapo wanasema hapa kazi tu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye Jimbo langu la Serengeti, Mkoa wa Mara barabara ya lami inayounganisha Mkoa wa Mara na Mkoa wa Arusha, tangu Mheshimiwa Kikwete aliondoka mzee mpaka leo na aliyekuwa Waziri wa Ujenzi wa barabara ni Mheshimiwa Magufuli, tangu hapo barabara ya kuunganisha Mkoa wa Mara na Mkoa wa Arusha imekuwa ni ndoto. Kibaya zaidi aliyepewa tender kujenga barabara ile ni rafiki yake na Magufuli na ndiyo huyu amempa kujenga uwanja wa Chato sasa hivi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka Mpango unapokuja tuambie yule mkandarasi mliyempa kilomita 50 miaka zaidi ya mitano ameshindwa kumaliza kilomita 50, bado mnaendelea nae? Barabara ya kuunganisha Mkoa wa Mara na Mkoa wa Arusha “baakerwa” wameshindwa! Barabara hiyo kipande cha Mugumu - Nata mwaka wa fedha 2016/ 2017 kilitengewa shilingi bilioni 12, mwezi wa 12 2016 wakatangaza tender mpaka leo wanatafuta mzabuni, sema hamna hela bwana msitudanganye hapa! (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye maji nako ni aibu. Mwaka jana zimetengwa zaidi ya shilingi bilioni 600 kwenye maji, zimetoka asilimia 18. Kwenye nchi hii shida kubwa ya watu wetu ni maji, ukienda vijijini ni maji na ukienda mijini ni maji, unatoa asilimia 18 tu halafu unasema hapa kazi tu, hapa kazi kwa kitu gani...mura nu tune ng’ana [unatafuta jambo]. (Kicheko/Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hali ni mbaya sana, barabara sasa hivi wameanzisha kitu kinaitwa TARURA.
TARURA sijui iko chini ya nani? Ukija kimsingi Madiwani na Mkurugenzi ndio wasimamizi ambao wapo karibu na wananchi, barabara zimeondolewa kwa wala barabara hazipo chini ya Mkurugenzi tena, hazipo chini ya Baraza la Madiwani wala Mbunge, zipo chini ya kitu kinaitwa TARURA. TARURA ina mapembe, wao wenyewe ndio wanajua walime barabara ipi na waache ipi, mimi sielewi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wamekomba engineers waliokuwa kwenye Halmashauri za Wilaya na Manispaa wamekwenda TARURA, Halmashauri za Wilaya hazina wahandisi sasa hivi. Mheshimiwa Mpango unapokuja utuambie mpango wenu ni kuua Halmashauri au mna mpango gani? Kwa sababu kwenye mapato mimi sijawahi kuona. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Halmashauri zilikuwa zinakusanya mapato vizuri sana, property tax, ushuru wa mabango na ushuru mwingine mwingi walikuwa wanakusanya. Leo Serikali hii inayojiita Serikali makini imechukua mapato ya Halmashauri hata ushuru, ushuru unakusanywa unapelekwa Serikali Kuu halafu ushuru wenyewe umeshindwa kukusanya, Halmashauri zinakaa hata kuendesha vikao imeshindikana. Mtuambie mna mpango gani hizi Halmashauri, mna mpango wa kuziua Halmashauri kwa kuzinyng’anya vyanzo vya mapato? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nawaambia Madiwani nchi nzima, wawe wa CCM ama CHADEMA wote muungane pamoja, ninyi ndiyo mnatafuta kura za Wabunge na Rais. Madiwani wote wa CCM na CHADEMA unganeni muishughulikie hii Serikali ijue kwamba ninyi ndiyo wasimamizi wakubwa wa miradi ya maendeleo. Haiwezekani Baraza la Madiwani, haiwezekani Halmashauri zinyang’anywe mapato, haiwezekani! (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hii Serikali inaitwa Serikali ya bomoa bomoa. Mmewakuta wananchi, enzi hizo mlikuwa hamuwapimii viwanja, walijenga kwenye squatters ndiyo utaratibu uliokuwepo, leo mnabomoa hovyo hovyo. Serikali makini, Serikali ya wanyonge! Mimi naangalia kilio, eti Rais anabomolea watu wa Dar es Salaam halafu anakimbilia Mwanza anasema, eti Mwanza ndiyo walimpa kura, hivi Mwanza ndiyo walimpa kura nchi hii nzima! Sasa kwa kuwa Mwanza ndiyo walimpa kura, aache mwaka 2020 uone maeneo mengine watamshughulikia kama hana akili. (Kicheko/Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu ajira. Viwanda hakuna, ukija kwenye nchi hii, hivi wamemaliza wanafunzi wangapi vyuo vikuu, wapo wapi, ajira ziko wapi? Mnasema Serikali ya viwanda, hamjajenga vyuo vya kati vya ufundi, vyuo vya VETA, unakuja Mkoa mzima unaweza kukuta Chuo cha VETA kimoja au mikoa mingine haina. Mimi hata pale Serengeti nataka kufungua kiwanda, lakini ukitafuta hata fundi tu wa kuongoza ile mitambo hayupo, mkoa mzima hayupo! Hata nchi hii wa kuhesabu ni wachache, sasa tunaenda wapi? Elimu ya ufundi iko wapi tuambieni. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Mpango unapokuja hapa sema mpango unasema nini kuhusu VETA kila Wilaya, tungelikuwa na VETA kila Wilaya tungekuwa na vijana mafundi wazuri tu ambao wangekuwa wanachakata. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nendeni hata Kenya hapo msiende mbali, msiende Ulaya, nenda hapo Kenya uone vijana wanavyofanya kazi, wana mafunzo mazuri na wanajiajiri. Leo unasema, kwa mfano hivi mwalimu ambaye amemaliza chuo kikuu ana Bachelor of Arts atajiajiri kwenye nini maana kazi yake ni kufundisha, anaenda kujiajiri wapi, akajenge shule, umempa mtaji? (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye afya. Ninyi Serikali ya CCM nisikilizeni. Sera yenu ya afya inasema kila kijiji kiwe na zahanati na kila kata iwe na kituo cha afya. Njoo Serengeti tuna vituo vya afya viwili tu, Kituo cha Nata na Ilamba, hata hivyo vituo viwili bado havijakamilika vizuri vina mapungufu kibao, lakini sera yao inasema kila kata iwe na kituo cha afya, hakuna.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mtuambie pesa mnayojidai mnasema mnakusanya zipo wapi? Mimi nataka waniambie wanasema wanakusanya matrilioni, tunataka kuona huko mtaani ukienda hakuna pesa wananchi wanalalamika, hata Wabunge wanalia. Wananchi wanalia kweli, sasa mtuambie hizo pesa mnakusanya mnalalia au mnafanyia nini! (Makofi/ Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuchangia.