Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

Hon. Masoud Abdalla Salim

Sex

Male

Party

CUF

Constituent

Mtambile

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

MHE. MASOUD ABDALLAH SALIM: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Awali ya yote namshukuru Mwenyezi Mungu Subhanahu Wataala kunijalia uzima na afya njema kuweza kuchangia mapendekezo ya Mpango huu wa mwaka 2018/2019.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niwapongeze wananchi wangu wa Jimbo la Mtambile kwa kuendelea kuniamini na kunipa baraka zote, halikadhalika nikipongeze Chama Wananchi CUF kwa kuendelea kuwa imara katika harakati mbalimbali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya hapo nataka nianze kumwambia ndugu yangu Dkt. Philip Mpango wa Waziri wa Mpango, yeye mwenyewe kwanza alikuwa Mwenyekiti wa Tume ya Mipango kwa muda wa miaka kumi, sasa kama si hivyo naomba basi niendelee kwa kusema kwamba mpango huu ambao umetuletea ningependa kujua kwanza tathimini ya mpango uliopita umefikia hatua gani na wakati huu mpango huu mpya, hilo lilikuwa la kwanza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kile kinachoitwa mkakati wa Tanzania ya viwanda kuelekea uchumi wa kati, ni kwamba Serikali mara kadhaa imekuja hapa Bungeni ikituambia kwamba ina mkakati wa kufufua viwanda vilivyobinafsishwa. Serikali mara kadhaa imekuwa ikituambia viwanda vyote vile ambavyo vilibinafsishwa lakini baadaye wakapewa wawekezaji ambao hawaviendelezi watatajwa majina yao na kitajulikana nini cha kufanya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ningependa kujielekeza katika viwanda vilivyobinafsishwa katika Mikoa ya Lindi na Mtwara, vile viwanda vya korosho, Mheshimiwa Waziri utuambie leo hii viwanda vya korosho vilivyobinafsishwa ambavyo asili yake/mwanzo wake kulikwepo na mkopo kutoka Italy na Japan kwenye miaka ya 1980 dola milioni 20, zikachukuliwa kujengwa viwanda vile ili kuondokana na tatizo la kuuza korosho ghafi nje ya nchi.

Leo viwanda vimebinafsishwa, vimechukuliwa, mmewapa mliowapa, mmepeana sadaka kwa watu mnaojuana. Mheshimiwa Waziri naomba unipe ujasiri na utuambie hapa viwanda vile mmewapa akina nani?

Mheshimiwa Mwenyekiti, uchunguzi unaonekana mmepeana wenyewe kwa wenyewe kwa bei chee, vigogo wa Serikalini, utuambie ni akina nani na kwa nini haviendelezwi? Leo bei ya korosho ghafi Mikoa ya Lindi, Mtwara, Pwani na Morogoro imefika shilingi 3,800; lakini mnasema kwamba watu wale mtawaita, mpaka leo hawapo. Mtuambie mmewapa akina nani? Mtuambie Kiwanda cha Lindi Mjini nani anayemiliki? Newala One nani anayemiliki? Newala Two nani anayemiliki?, TANITA yote One na Two ni nani anayemiliki? Kwa nini hamtuambii? Kwa nini hamko wazi kutuambia viwanda hivyo? Na mnasema kwenye Katiba ukurasa wa 20 kwenye haki na wajibu kuna haki ya usawa, kwamba watu wote ni sawa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimuulize Mheshimiwa Waziri haki sawa iende kwa nani? Na wale wasiotenda haki? Nashangaa kwamba leo mmesema mtatuletea majina ya watu wote waliochukua viwanda hawaviendelezi, mkasema mko wazi, lakini leo hakuna kitu, wengine mnawataja, wengine hamuwataji, shida! Hilo ni tatizo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo, kuna kiwanda mtuambie cha kusindika samaki (TAFICO) Dar es Salaam hatua yake imefikia wapi? Anayemiliki ni nani? Mtuletee Bungeni mtueleweshe, wananchi wanalalamika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nije kwenye suala zima la wafanyabiashara wadogo wadogo. Kuna malalamiko makubwa ya jinsi gani ya hali ya maisha wakati huu ilivyokuwa ni ngumu. Mzunguko wa pesa umekuwa ni mdogo, wafanyabiashara mbalimbali katika masoko ya vyakula na mboga mboga wamekuwa wakilalamika, Kariakoo maduka yamefungwa wateja wamepungua, Mheshimiwa Waziri Mpango anasema uchumi umeimarika, uchumi kuimarika kuna takwimu zenu mnazosema umeimarika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini mimi niseme, si muda mrefu hapa Mheshimiwa Mbunge wa Mtwara au Lindi kule Kusini amezungumzia tatizo la wakulima wa mbaazi. Leo mbaazi kilo shilingi 150, shilingi 200, shilingi 300. Mheshimiwa wewe mwenyewe unajua kwamba kuna Sheria ya Bajeti ya mwaka 2015 kifungu cha 43(1) kinaeleza kwamba ikiwa fedha zilizoidhinishwa na Bunge hazikutosha kutokana na majukumu yake Serikali inaweza kuwasilisha Bungeni bajeti ya nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama kweli mnawapenda wananchi wa Lindi na Mtwara Serikali mnashindwa nini kuleta hapa Bungeni kuongeza bajeti ya kununua mbaazi za Lindi na Mtwara na maeneo mengine kama ya huko Babati?

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninyi mnazungumzia MKUKUTA kumbe MKUKUTA wa maneno. Serikali leteni hapa bajeti ya nyongeza ili sisi Wabunge tuweze kuidhinisha ili wakulima wale ambao wamegharamika kwa gharama kubwa ya kulima mbaazi, mbaazi zao zisiharibike, lakini leo wapi maskini! Tuseme nini? Huu ndio wakati maalum wa kuweza kuboresha maisha ya wakulima, lakini nashangaa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Jenista umekaa miaka mingi, washauri wenzako hawa kwamba wakulima wanapata shida sana. Serikali ilete Bungeni tuidhinishe bajeti ya nyongeza ili mbaazi zinunuliwe ili angalau wakulima wapate manufaa wasiingie kwenye hasara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi mambo kama haya yananitia uchungu sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni suala la wavuvi. Serikali mara nyingi imekuwa ikijisifia hapa Bungeni namna ya kuchoma nyavu tu za wavuvi. Mheshimiwa Mpango utuambie una mpango gani wa kuwaboresha wavuvi wadogo wadogo kwa kuwapa mikopo, kuwasaidia wavuvi katika bahari na katika maziwa? Mpango uko wapi? Nimeangalia mpango wako huu na nilikwambia mwanzo, tathmini yako ya mpango uliopita uko wapi kuhusu maeneo mbalimbali? Wavuvi wameachwa, wametupwa, hakuna jambo lolote la kuwasaidia, hakuna mikopo kwa wavuvi wa baharini na wale wa kwenye maziwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nikuombe Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango Waziri wa Mpango utuambie una mkakati gani, una mpango gani hasa wa kuboresha maisha haya ya wavuvi wadogo wadogo? Kuna kurasa kidogo tu umeandika hapa kuhusu wavuvi, lakini tatizo ni kubwa. Mvuvi ambaye ana mtungi wake wa gesi akienda katika maeneo mbalimbali anaambiwa anafanya uvuvi haramu, anakamatwa na anachomewa nyavu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Dkt. Mpango atuambie dagaa mchele wale ambao bila shaka nawe umeshawahi kula, wanavuliwa na nyavu ya aina gani? Utuambie. Umekula dagaa mchele wewe, mara nyingi, nasikia unapenda kweli. Tuambie nyavu zile mnazochoma, dagaa mchele winavuliwa na nyavu za aina gani? Mumekuwa mabingwa wa kuchomna nyavu kila wakati mnajisifia, utuambie mikakati yao. Wavuvi mikopo hamuwapi, nyavu zao mnachoma, mikakati ya kuboresha hakuna, Serikali haina mpango wa kununua meli za kisasa na kubwa za kuvua bahari kuu, Serikali haina mpango wowote. Mnakuja na mipango, mna mpango au mna mipangilio? Shida. (Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyeiti, suala la maji hapa ni kizungumkuti cha muda wa miaka na miaka. Leo wananchi wa Tabora hawa rafiki zangu Wanyamwezi na Wakisukuma ukifika wakati wa uchaguzi kampeni yao kubwa ni maji, wanakwenda kwenye majukwaa; “nalilomba kura zing’we mnine pye bhose wadugu wanu” hawa. (Makofi/Kicheko)

Leo waambie Tabora, Bwawa la Igombe limekauka, yaani Tabora maji hakuna kabisa. Kuna Mradi wa Ziwa Victoria ni wa muda mrefu, wa muda mfupi uko wapi? Ukienda zako Njombe Mjini, Makambako, Wanging’ombe, Maswa, Buchosa huko kwa Mheshimiwa Waziri kote maji ni shida, ni malalamiko matupu, kwenye tv tunaona.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukienda kule Magu tarafa ya Ndagalu maji hakuna, nako waende wakaseme sasa; “nalilomba kura zing’we mnine pye bhose wadugu wanu” kauli ndio shida, ndio taabu kama wataipata hawa, hawapati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo la maji limekuwa la muda mrefu, tangu enzi na enzi. Sasa mkakati wa muda mrefu ni Ziwa Victoria, mkakati wa muda mfupi wa pale Tabora ni upi? Wale wenye visima vyao ni wachache sana, leo kuna shida kubwa lakini Serikali tukisema sisi eehh jamani! Serikali ichangamke, ihangaike kutafuta maeneo mengine au njia mbadala ya kuweza kupatikana kwa maji. Tatizo hakuna chochote kinachokwenda. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nataka nizungumzie suala la mafao ya wastaafu. Hamgusii mpango endelevu wa mafao ya wastaafu, hakuna, pension iliyobakia ni ile ile. Leo walimu uliwaahidi miaka kadhaa kwamba mtawapa teaching allowance, posho ya kufundishia lakini hakuna kitu, posho ya kufundishia hakuna kwa walimu na ile ndiyo motisha. Mliahidi tangu mwaka 2012, tena ni ninyi wenyewe Serikali kwamba mtatoa teaching allowance kwa walimu; hakuna kitu, mpango uko wapi? Mna mpango wa kweli wa kuboresha maslahi ya walimu? Maana mnasema elimu inashuka, tatizo kubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nadhani Serikali sasa inagalie mapungufu yake mbalimbali lakini mhakikishe kwamba wastaafu na…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)