Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

Hon. Cosato David Chumi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mafinga Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

MHE. COSATO D. CHUMI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi na mimi niweze kuchangia katika mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote kwanza nipende kuwashukuru na kuwapongeza wananchi wa Jimbo la Mafinga Mjini na Halmashauri ya Mji wa Mafinga, kwamba ni Halmashauri mpya tuna mwaka wa pili tu lakini katika matokeo ya darasa la saba tumeshika nafasi ya tano katika halmashauri zaidi ya 150. Ni jambo ambalo tunajivunia, ni kutokana na ushirikiano kati ya wananchi, mimi Mbunge wao, Waheshimiwa Madiwani, watumishi, walimu na wananchi kwa ujumla na ninaomba tuendelee kushirikiana ili ikiwezekana mwakani tufike tatu bora

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo napenda pia kuishukuru Serikali; tulikuwa na kilio kwa ajili ya bweni la Shule ya Msingi Maalum Makalala; ilituletea fedha milioni mia moja. Na kwa kutumia muundo wa force account tumejenga bweni zuri, Mheshimiwa Profesa Ndalichako alifika pale, tena tumetumia shilingi milioni 76 na fedha iliyobaki tutanunua samani kwa ajili ya bweni lile. Haya yote ni ushirikiano kati ya sisi viongozi na wananchi wa Mafinga.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia napenda kuishukuru Serikali kwa ajili ya ujenzi unaondelea wa tanki la maji la ujazo wa lita 500,000 pale Kinyanambo. Pia Serikali imetupa kibali tayari mkandarasia atakwenda site kuanza kujenga tanki la lita 90,000 pale Kijiji cha Maduma na mradi wa maji kule Bumilayinga.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile Serikali imetupatia shilingi milioni 500 ambazo tutaendelea na ujenzi kuimarisha kituo cha afya pale Ihongole. Haya ni mambo ambayo lazima tuyapongeze na kama hiyo haitoshi jana katika taarifa nimeona TAMISEMI inatuletea watumishi wa kada ya afya asiopungua saba ili kuendelea kuimarisha huduma za afya katika Halmashauri ya Mji wa Mafinga na Hospitali ya Mafinga ambayo inahudumia Wilaya nzima ya Mufindi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, katika Road Fund niiombe Serikali, tuna viporo, wakandarasi wamefanyakazi na wanatudai takribani shilingi milioni 212 fedha za mwaka 2016/2017.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitumie fursa hii kuwashukuru wahisani na marafiki mbalimbali ambao wanashirikiana na Ofisi ya Halmashauri ya Mji wa Mafinga katika kuimarisha huduma za afya na elimu. Napenda kuushukuru Ubalozi wa Japan wametupatia fedha tunajenga pale theatre ya kisasa kabisa. Sasa niiombe Serikali hususani Wizar ya Fedha; kwa kuwa fedha zile zilikuwa centralized sasa TBA ambao tumewapa ile kazi speed yao inakuwa ndogo kwa sababu bado hawajpelekewa fedha na yule mhisani angependa kuona maendeleo ya ile kazi.

Kwa hiyo, ningeomba Hazina watusaidie TBA wapate fedha hizo ili speed ya kazi iende sambamba na jinsi ambavyo mhisani yule alikuwa ametuelekeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimwambie Mheshimiwa Jenista Mhagama kwamba vikundi vya wajasiriamali, kama ulivyokuja ukatuelekeza tuvipike, tumevipika vimeiva, tunakusubiri kwa hamu sana uje utuletee ile mikopo ya riba nafuu.

Sambamba na hilo, wakati tunajadili mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa, mara zote nimesema, engine ya ufanikishaji wa utekelezaji wa mpango ni utumishi wa umma. Kama morale ya watumishi wa umma iko chini kama wanavyotumia lugha ya siku hizi kwamba vyuma vimekaza ni wazi kuwa mafanikio ya kufanikisha Mpango yatakuwa chini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo niipongeze Serikali, kwamba hatimaye baada ya uhakiki wa muda mrefu sasa imeangalia welfare ya watumishi, na ninaamini morale itapanda kwa sababu nimeona kumetengwa kiasi cha shilingi bilioni 159 kulipa malimbikizo kwa ajili ya watumishi mbalimbali ambao walishapanda vyeo na madaraja, lakini walikuwa hawajalipwa kile ambacho kinastahili kuwalipa. Kwa hiyo, naamini kwamba morale ya kazi itaendelea kupanda na kukua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini watu wengine wanabeza uchumi haukui; ukiangalia takwimu za juzi za World Bank yule Mwakilishi Mkazi wa World Bank anasema kwamba; wao kama World Bank wali-project uchumi wetu utakua kwa asilimia 6.9 lakini umekuwa kwa asilimia 6.8, ni jambo ambalo la kujivunia, ni jambo ala kujipongeza. Hata makusanyo kutoka kukusanya wastani wa asilimia 11 sasa Serikali inakusanya wastani wa asilimia 12.8 na mafanikio haya ni ndani ya miaka miwili. Lengo ni kufikia mwaka 2020/2025 tufikie makusanyo ya asilimia 19 kama ambavyo nchi zingine wameweza kufanikiwa, ni mambo ya kupongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini vile vile uthubutu wa kuanza ujenzi wa reli tena kwa gharama nafuu. Tumeona wenzetu majirani, kilometa moja ni wastani wa dola milioni 8.5, sisi kilometa moja ni chini ya dola milioni 3.5. Ni jambo ambalo unaweza kuona kwamba Serikali iko makini katika kufaya majadiliano ya kufikia makubaliano ya utekelezaji wa miradi mbalimbali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu ukuaji wa bandari. Sasa hivi tunaona wale waliokuwa wamekimbia wameanza kurejesha imani. Kwa hiyo, ni matarajio kwamba ufanisi katika bandari yetu ambao umeanza kuongezeka utachochea utendaji wa kazi na hivyo kuongeza mapato kwa Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa mwenyekiti, Tulipitisha hapa Sheria ya Madini, kulikuwa na malalmiko kwanini imekuja under certificate of urgency, lakini manufaa yake wote tunayaona. Kile kitakachopatikana maana yake ni kwamba kitakwenda kusaidia kuboresha aya, huduma za jamii kama elimu, ujenzi wa barabara na miundombinu mingineyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimesoma katika mpango na ninapongeza jitihada za ujenzi wa Kiwanda kule Mkulazi ambazo zinafanywa kwa ushirikiano wa Mifuko ya Jamii. Lakini nitoe ushauri, sisi mahitaji yetu kwa mwaka ni wastani wa tani 590,000. Katika hizi tani 300,000 ni matumizi domestic na tani 170,000 ni ile sugar for industrial.

Sasa pamoja na jitihada za uwekezaji huu ambazo zinaendelea, mimi nishauri kwamba tujaribu kuangalia katika yale mabonde muhimu tuwekeze pia kwa mfumo wa small- medium size kwamba unakuwa na kiwanda kinaweza kuzalisha tani 5,000 pale Kilombero, kiwanda kinakuwepo Rufiji hata vitatu au vinne, kwa sababu gharama zake za uwekezaji ukizi-split unaweza kuvutia wawekezaji wadogo wadogo wengi na hivyo kuongeza uzalishaji lakini pia kuongeza mapato kwa Seriakli pamoja na kupanua wigo wa ajira. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini ninasema hivi? Brazil wenzetu wanazalisha tani milioni thelathini na sita kwa mwaka na kwa takwimu hizo, Brazil globaly uzalishaji wao ni asilimia 20, lakini katika Soko la Dunia wao wanashika kwa asilimia 40.

Kwa hiyo, unaweza kuona kwamba sukali bado inahitajika kwa kiwango kikubwa na sisi ili kuimarisha shilingi yetu maana yake ni lazima tuuze nje. Kwa hiyo, licha ya kwamba tuna soko la ndani, lakini pia tuna soko ambalo lipo, limejaa tele katika global market.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nasema hivi kwa sababu ukienda katika takwimu inaonesha kwamba nchi kama Nigeria yenyewe inaagiza sukari ya thamani ya milioni 500 kwa mwaka, hilo ni soko lipo. Ukienda South Africa inaagiza sukari ya thamani ya dola milioni mia tatu na sita, maana yake ni soko lipo, ukienda Ethiopia wanagiza sukari ya dola milioni 188 kwa mwaka, maana yake ni soko lipo. Kwa hiyo pamoja na jitihada za Mkulazi tutafute pia mbinu nyingine ambayo inaweza ikachochea small-medium size factories ili tujitosheleze kama soko la ndani lakini pia tupeleke nje kusudi tuweze kuiimarisha shilingi yetu. (Makofi)

Mheshimwa Mwenyekiti, sambamba na hilo nizungumzie pia umuhimu wa kufufua viwanda hususani mradi wa kielelezo hasa wa Mchuchuma na Liganga. Mradi huu kila mara unakuja kwenye vitabu. Sisi watu wa Nyanda za juu Kusini tunadhani kwamba kufanikiwa na kuanza kutekelezwa kwa mradi huu utasaidia sana kuchochea uchumi katika eneo hilo na hivyo si tu kuongeza mapato ya Serikali lakini pia kupanua wigo wa ajira sambamba pia na kuimarisha shilingi yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika suala la kufufua viwanda tuangalie pia jinsi ya kuwasaidia wawekezaji wa ndani. Kwa mfano mimi kule Mafinga, suala la mazao ya mistu ni jambo ambalo nimekuwa nikilisema mara kwa mara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niiombe Serikali hasa Wizara ya Maliasili na Utalii na Wizara ya Viwanda na Biashara, Maliasili na Utalii wanahusika kutupa sisi wawekezaji malighafi, lakini nimesema mara nyingi MPM kile wanachopewa wanavuna tu kama theluthi mbili. Sasa ile theluthi moja inayobaki wapewe wawekezaji wetu wa ndani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, si hivyo tu; bei imeshuka sana. Sisi hapa mbao zetu hauwezi kushindana na mbao inayotoka Malawi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, hebu Serikali ijaribu kuangalia bei za misitu kusudi tuone namna gani tunaweza kuwapa wawekezaji wa ndani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho kabisa; kama nilivyosema wakati Maliasili wanahusika kutoa malighafi, Wizara ya Viwanda na Biashara moja kwa moja inahusika katika kulea hii sekta ya mzao ya misitu. Kuna potential kubwa kwenye mzao ya misitu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nimuombe Mheshimiwa Mwijage na Naibu wake, katika miaka mwili nimemwambia sana Mheshimiwa Mwijage uje Mafinga na Mufindi. Minimum mtu kawekeza shilingi milioni 500 na tuna viwanda siyo chini ya 40, kuna watu sasa wameanza kuongeza thamani katika mazao wakitengeneza mkaa kutokana na zile pumba zinazotokana na mazao ya misitu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ile kwanza itatusaidia kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi. Vilevile hawa watu kuna fursa nyingi wangependa kuzifahamu kutoka TAB, wangeweza kufahamu mambo mengi kutokana na tozo za OSHA, NEMC, TBS na kadhalika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, haya yote tukifanya kongamano la pamoja itatuwezesha sisi kujua ni changamoto gani wanazokabiliana nazo ili tui-raise hii sekta iweze kukua, ikuze ajira lakini pia iongeze pato; kwa sababu sasa wanaongeza thamani katika mazao tuuze nje ili tuendelee kuimarisha shilingi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kumalizia, naendelea tena kuiomba Serikali katika mwaka huu wa fedha wa 2017/2018 tunaomba kwa ajili ya kuimarisha miundombinu katika Mji wa Mafinga bado hatujapokea fedha kutoka Road Fund. Tuna viporo vingi vya kuimarisha barabara ule ni mji unaokuwa kwa kasi tungependa tuwe japo na kilometa mbili, tatu za lami lakini kama hatutapata fedha itatuwia vigumu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo niiombe Serikali sambamba na kuomba fedha ambazo zinatakiwa ziende TBA kwa ajili ya mradi ule wa ujenzi wa theatre, pia ituangalie katika suala la barabara za pale Mjini Mafinga. Pia kwa ajili ya ujenzi wa tanki la mita milioni moja ambalo Mheshimiwa Waziri wa Maji namshukuru sana, ameniahidi kwamba kesho tutaonana naye ili kuweza kujua maendeleo ya kupata kibali cha kutangaza hiyo kazi yamefikia wapi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema maneno hayo, nakushukuru na niwaambie wananchi wa Mafinga nawapenda sana, ushirikiano wetu ndiyo silaha na moto wetu na slogan yetu tunasema Mafinga kazi tu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.