Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

Hon. Joram Ismael Hongoli

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Lupembe

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

MHE. JORAM I. HONGOLI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nishukuru kwa kupewa nafasi hii kuchangia kwenye Mpango wa Maendeleo wa mwaka 2018/2019. Nianze kwanza kumpongeza Mheshimiwa Rais kwa kazi kubwa ambazo anazifanya katika utekelezaji wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi ya mwaka 2015. Niwapongeze Mawaziri kwa kazi kubwa ambazo wanazifanya na wanashirikiana na Rais kuhakikisha kwamba Ilani ya Chama cha Mapinduzi inatekelezwa vizuri, niwapongeze sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze Mheshimiwa Dkt. Mpango kwa jinsi anavyosimamia shughuli nzima za mapato na matumizi kwa maana ya uchumi wa nchi hii na amekuja na hotuba nzuri ambayo inaleta matumaini kwa Watanzania, nikupongeze sana Waziri na Naibu Waziri wa Fedha na Mipango.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kuiangalia sekta ya kilimo. Sekta ya kilimo ndiyo sekta ambayo ni mhimili wa uchumi wa nchi yetu na sekta hii inachangia takribani nusu ya pato la Taifa letu kwa maana ya uchumi wa Taifa. Hivyo basi, Watanzania wengi ndio walipo huko, wameajiriwa huko wanafanya shughuli za kiuchumi, kwa hiyo ni lazima tuiangalie kwa namna ya pekee sana ili angalau iendelee kuchangia zaidi hata kuliko kuishia kwenye nusu pengine iende mpaka kwenye robo tatu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme jambo moja ni kwamba katika kilimo kuna mazao ya aina mbili, kuna mazao ya chakula na mazao ya biashara. Niseme kidogo juu ya mazao ya biashara, tuna pamba, tumbaku, kahawa na mazao mengine kama chai. Mazao mengi ya biashara yanapewa ruzuku na Serikali na angalau sasa hivi tunaona mazao mengi yanapata bei nzuri, tukiangalia kwenye korosho bei ilikuwa chini lakini sasa hivi imepanda kwa sababu ya ruzuku ambayo inatolewa na Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, bado kuna mazao mengine hatujayapa kipaumbele wakati mazazo hayo yanaweza yakatuingizia fedha nyingi sana za kigeni kama tukiamua kuwekeza huko na kuhakikisha kwamba tunawasaidia wakulima wetu waweze kuzalisha kwa wingi na kwa ubora.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue mfano wa zao la chai, sijaona likitiliwa mkazo sana, ikumbukwe kwamba zao hili katika miaka ya 1990 kurudi nyuma ndiyo zao ambalo lilikuwa linaingiza fedha nyingi sana za kigeni. Lilikuwa ni zao ambalo ni mtetea uchumi mzuri sana lakini sasa hivi ni kama tumelitelekeza hivi bado halisimamiwi vizuri na wakulima bado bei zao zipo chini na hakuna usimamizi mzuri kutoka kwa mkulima anavyoichuma chai kupeleka kiwandani na hatimaye kwenye soko.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mkulima hajui chochote, akishauza chai yake pale kwenye banda au kwenye kituo chake anachouzia hajui chochote nini kinapatikana mwisho wa siku. Kwa hiyo, ufuatiliaji katika chain nzima ya ukamilishaji wa zao la chai haupo na matokeo yake bei ya chai imeendelea kuwa chini, sasa hivi inalipwa kati ya Sh.230/= mpaka Sh.250/= ukilinganisha gharama za uzalishaji wa zao hili ni kubwa kuliko kile anachokuja kukipata mkulima.

Mheshimiwa Mwenyekiti, majani mabichi sasa hivi kama nilivyosema ni Sh.230/= mpaka Sh.250/=, lakini gharama za uzalishaji zinazidi Sh.450/=. Ukiangalia kwa nchi za wenzetu, ukiangalia kwa mfano Kenya, mwaka jana kwenye kilo moja ya chai ambayo tayari ni majani makavu waliweza kupata kwa kila kilo dola 266, kwa hiyo ukii-convert katika fedha za Kitanzania pengine ni kama Sh.5,000/= hivi na zaidi. Kwa hiyo, kumbe inawezekana tukiisimamia vizuri hii sekta, tukisimamia vizuri zao linaweza likatuletea uchumi mzuri sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niiombe Serikali ijitahidi kuhakikisha kwamba kwanza inaisimamia Bodi ile ya Chai vizuri ili bei ziweze kupanda kadri ya muda unavyozidi kwenda. Ukiwauliza wenyewe wanaozalisha chai, wale wanao-process chai, wanasema haina faida lakini ukiuliza nje ya nchi kule wanakouza chai wanasema wanauza kwa bei nzuri sana. Kwa hiyo, tunajiuliza sisi wakulima wa chai kuna nini pale katikati, kwa nini bei ya chai haipandi. Bei iliyopo sasa hivi kwa mara ya mwisho iliongezwa mwaka 2012, mpaka sasa hivi bado bei ni ileile. Tunasikia tu kwamba hivi karibuni Bodi ya Chai itaenda kutangaza bei elekezi, basi tuombe hiyo bei itangazwe mapema ili wakulima wajue na waweze kupata faida.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kuna tozo ilitolewa kwenye chai, tozo ya shilingi mbili; lakini wakulima hawaioni hiyo, haiendi kwa wakulima mpaka sasa hivi. Kwa hiyo niiombe Serikali, nimwombe Waziri wa Kilimo ajaribu kusimamia ili kuhakikisha kwamba kila tozo zinavyokuwa zimeondolewa lazima zi-reflect wakulima tu na zionekane kwa wakulima ili waone kwamba zile tozo zina tija kwao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo nikuombe sana tusimamie hili na tusaidie hili, ili wananchi hawa waweze kupata fedha hizo ambazo zinawasaidia kusomesha watoto wao, zinasaidia kujenga nyumba nzuri na zinasaidia kufanya mambo mengine makubwa na mwisho wa siku kiuchumi kama wa wakulima unakuwa, lakini uchumi kama nchi pia unaongezeka. Kwa hiyo ni lazima tuanze kusimamia haya mazao tunayofikiri ni madogo ili baadaye kwa ujumla wake ndiyo yaweze kukuza uchumi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunasema viwanda, viwanda vitaongezeka kama uzalishaji utaongezeka lakini ilivyo sasa hivi kwenye zao la chai ni kama watu wanakata tamaa kwa hiyo hata viwanda havitakuwepo. Tukiongeza usimamizi katika uzalishaji wa zao la chai, naamini hata wakulima watafurahi, watazalisha kwa wingi, mashamba yataongezeka na ajira nyingi zitaongezeka kupitia mashamba na viwanda na viwanda vitaongezeka. Kwa hiyo, wazo la kufikia kwenye uchumi wa viwanda tutafika kama mazao haya ya biashara yanasimamiwa vizuri kuanzia mwanzoni mkulima anapozalisha lakini mpaka mwisho wa soko mkulima aonekane kwamba kuna faida.

Mheshimiwa Mwenyekiti, huwa kunakuwa kuna malipo ya pili baada ya kuuza yale majani mabichi lakini wananchi wengi hawayapati haya. Kwa mfano, wakulima wangu wa Lupembe kule hawapati mauzo ya pili au ile fedha inayokuja baada ya kuuza majani makavu, wakilipwa tu yale majani mabichi inakuwa ni mwisho wa malipo. Kwa hiyo, niiombe Serikali, niombe Wizara isimamie vizuri jambo hili ili wakulima hawa waweze kuongeza uzalishaji na wakione kilimo kama kina tija na mwisho wa siku tutaongeza uchumi wa nchi lakini pia tutakuwa tumeongeza Pato la Taifa kupitia hili zao la chai.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine nije kwenye upande wa kilimo cha mazao ya chakula, niseme kidogo kuhusu zao la mahindi. Kama walivyosema wenzangu kwamba zao la mahindi kwetu sisi sio zao tu la chakula bali ni zao la biashara. Kuna wananchi wanalima mahindi kwa ajili ya chakula, lakini pia kwa ajili ya kuuza kuweza kupata fedha kwa ajili ya kusomeshea watoto wao. Hivi sasa baada ya hili zuio, kama walivyosema wenzangu zuio la kuuza mahindi nje ya nchi, wakulima wetu wamebakiwa na mahindi na wengine wanauza kwa bei ndogo sana kati ya Sh.3,000/= mpaka Sh.5,000/-.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo, ukipiga hesabu ya gharama za uzalishaji wa zao la mahindi na bei wanayouzia mahindi kwa gunia kwa maana ya Sh.20,000/= mpaka Sh.25,000, bei hiyo inawapa hasara kubwa sana. Kwa hiyo sasa hivi wanashindwa kununua mbolea ambapo msimu wa kuanza kilimo cha mahindi ndiyo huu umeanza, sasa hivi wameshaanza kulima mashamba, mwisho wa mwezi huu wanatakiwa waanze kupanda. Hata hivyo, hawawezi kulima vizuri na kupanua kilimo chao kwa sababu hawajauza mazao yao kwa bei nzuri na hawajapata fedha za kutosha za kuweza kununulia hizi mbolea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaishukuru Wizara, mbolea imeshafika na bei imepungua tumeshaiona, lakini wakulima wetu hawawezi kununua zile mbolea kwa sababu hawana fedha za kutosha. Kwa hiyo nimwombe Mheshimiwa Waziri wa Kilimo na Serikali kwa ujumla wakae wajaribu kulitafakari hili na wajaribu kuangalia jinsi gani tutawasaidia wale wakulima.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunashukuru Serikali imenunua kupitia Hifadhi ya Chakula (NFRA) imenunua mahindi, lakini imenunua kiasi kidogo sana. Mahindi yapo mengi, sisi Waheshimiwa Wabunge na viongozi wengine tulihamasisha wananchi walime kiasi cha kutosha ili waweze kuuza tuki-refer soko la mwaka jana, kwamba mkiuza mtauza kwa bei nzuri na mtapata faida kubwa. Hata hivyo, sasa hivi ilivyo inaonekana kama sisi Waheshimiwa Wabunge na viongozi wengine tulikuwa tunawadanganya. Hivyo, wawakilishi wa wananchi na viongozi wengine tunalaumiwa kwa sababu wananchi hawana sehemu ya kupeleka yale mahindi na kuweza kuuza ili waweze kupata fedha na kuweza kufanya mambo yao mengine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nimwombe Waziri, hebu wajaribu kuliangalia kwa jicho la pekee ili wajaribu kujadili na tuweze kuangalia jinsi gani tutaweza kuwasaidia wale wakulima wetu waweze kuuza yale mazao yao lakini wauze kwa bei nzuri. Ikiwezekana, wakifungua mipaka inakuwa rahisi kwetu kwa sababu wafanyabiashara wakubwa wanakuja na bei inapanda kwa sababu kunakuwa na ushindani wa ununuzi wa mahindi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo nimwombe sana Waziri na niiombe pia Serikali kwa ujumla wajaribu kutafakari hili na tuangalie jinsi gani tutaweza kuwasaidia wale wakulima wa mahindi waweze kuuza mazao yao ili wakishauza waweze kupata fedha za kununulia mbolea, lakini pia wapate fedha za kuweza kusomeshea watoto wao. Januari shule zinafungua wanategemea wauze hayohayo mahindi, watashindwa kupeleka watoto wao kwa sababu ya ada na michango mbalimbali ambayo inatakiwa kwenye shule kwa kule watakakokuwa wamepeleka watoto wao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme juu ya miundombinu. Kilimo au shughuli zote za maendeleo zinategemeana sana na miundombinu. Kwa hiyo miundombinu kama barabara, reli, mambo ya viwanja vya ndege na mambo mengine vikiboreshwa vizuri ndiyo vinasaidia kukua kwa uchumi. Niipongeze Serikali na nimpongeze Rais kwa jinsi ambavyo anapigania uboreshaji wa barabara, uboreshaji wa miundombinu ya reli na uboreshaji wa viwanja vya ndege, ni jambo jema.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kuna baadhi ya maeneo bado uboreshaji haujafanyika sana. Kwa mfano kwenye Jimbo langu mimi la Lupembe; nishukuru kwamba barabara kwa maana ya zile za vumbi zinapitika sehemu kubwa, lakini kuna tatizo la barabara ile ya lami ambayo ilitakiwa ijengwe. Ilikuwa ni ahadi kwenye Ilani ya Uchaguzi ya mwaka 2015, kwamba Barabara ya Kibena – Lupembe – Madeke itajengwa kwa kiwango cha lami.

Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara hii tunaitumia sana sisi wananchi wa Lupembe kwa maana ya kusafirisha mazao mbalimbali, hasa mizigo mizito kama ya mbao, kusafirisha mizigo kama ya nguzo za umeme na kusafirisha mazao ya mahindi, maharage, matunda – mananasi, maparachichi na mazao mengine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, hii barabara ikifika wakati wa kifuku huwa inakuwa ni ngumu sana kusafirisha mizigo kama hii. Wakati wa kifuku, wakati inaisha mvua ndivyo mazao haya yanapotolewa. Kwa hiyo, niombe katika bajeti ya mwaka jana, mwaka 2016/2017 zilipitishwa bilioni nane lakini bado haikutangazwa na mwaka huu tumepitisha bilioni mbili kuanza kujengwa kwa kiwango cha lami lakini bado haijatangazwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nimwombe Waziri mwenye dhamana atusaidie kutangaza barabara hii ili ianze kujengwa kwa kiwango cha lami ili tuweze kuhakikisha kwamba mazao yaliyopo kule kwenye maeneo yetu, kule vijijini, yaweze kusafirishwa kuweza kufikia soko. Maana yake nguzo kwa kutumia barabara za vumbi zikishapita gari ndani ya wiki moja au mbili tayari barabara zimeharibika, lakini ikiwa lami tunaamini kwamba mazao haya yatasafirishwa na uchumi wa maeneo haya utakuwa lakini mwisho wa siku, uchumi la Lupembe utachangia uchumi wa Taifa na uchumi wa nchi kwa ujumla utakua kupitia uzalishaji unaofanyika kwenye maeneo yale. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine niseme juu ya umeme. Nnashukuru sana kwamba mpango wa umeme, hasa umeme vijijini, unaendelea vizuri kwa maana tumeshaanza kuona baadhi ya maeneo kuna nguzo zinachomekwa, lakini kwetu sisi ujenzi wa line bado
haujaanza. Tunashukuru kwamba kuna line ile ya Makambako – Songea, wameshapitisha line lakini bado hawajaanza kusambaza umeme kwenye vile vijiji kadiri tulivyoahidiwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba, katika mipango ya fedha ya Serikali hii nayo tuiwekee kipaumbele ili sasa umeme huu uweze kwenda huko vijijini, vijiji vingi viwe na umeme. Tunajua kwamba umeme unachochea maendeleo, unachochea shughuli za kiuchumi nyingine kwa sababu tukiwa na umeme itakuwa rahisi kuanzisha viwanda vidogovidogo, tukiwa na umeme itakuwa rahisi hata kusukuma maji. Kwa mfano, Lupembe maji yapo chini – kusukuma maji yaweze kupandisha majumbani na kuweza kufanyia shughuli mbalimbali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo umeme una manufaa makubwa sana endapo vijiji vyetu hivi vitakuwa na umeme. Namwomba Mheshimiwa Waziri, hebu tupate utaratibu mzuri, maana yake sasa hivi ni kama haieleweki vizuri ni lini umeme utaanza kusambazwa. Tukipita huko tunaulizwa na wananchi kwamba mlituahidi umeme wa REA lakini hatuoni hata nguzo zikisambazwa kwenye vijiji vyetu zaidi ya ile line ambayo imepita inayokwenda Songea. Kwa hiyo nimwombe sana Mheshimiwa Waziri atusaidie haya, katika mipango ijayo angalau maeneo haya ile mipango ambayo tumeipanga kwamba itatekelezwa kuanzia mwaka huu, wananchi waanze kuiona ikitekelezwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, nikushukuru sana na naunga mkono hoja iliyopo Mezani kwa asilimia mia moja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.