Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

Hon. Ally Mohamed Keissy

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nkasi Kaskazini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

MHE. ALLY K. MOHAMED: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi ili nami nichangie.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kama Serikali haina makosa, Serikali inaleta pesa lakini tatizo ni kwa wafanyakazi wa Serikali. Mfano, natolea wazi kabisa miradi ya maji Wilaya ya Nkasi. Serikali inapeleka pesa, ukiuliza kule pesa zinakwenda, Namanyere zipo pesa za kutosha, cha ajabu ukimuuliza Mkurugenzi, Mhandisi wa Maji wa Mkoa, Mhandisi wa Maji wa Wilaya, TAKUKURU na kila kitu, pesa zinakuja lakini hizo pesa zinarudi Wizarani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wanafanya mikakati, wanawapa wazabuni ambao hawana uwezo. Mzabuni uwezo wake, license yake ni bilioni 750, anapewa mradi wa bilioni saba. Tumemwambia juzi mradi wa maji Namanyere, Mfiri, mradi uko chini ya kiwango, tumezuia pesa asilipwe mkandarasi kwa ushahidi kabisa, tumeleta taarifa, lakini cha ajabu amelipwa milioni 320 bila Mkurugenzi wa Namanyere kufahamu. Baada ya muda wa siku mbili tu yule msimamizi wa mradi, mfanyakazi wa Serikali, meneja wa mradi ametoa notice ya kustaafu kazi, inaonesha wizi wa hali ya juu, mkakati mnyororo unatoka Wizarani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jana tu Namanyere kaenda Mkandarasi ambaye aliiba milioni 200 Namanyere na kitu chochote hakionekani, anataka kupewa tenda mradi wa maji Kirando, wanasema mpeni huo mradi kwa sababu tutamkata zile milioni 200, wakati milioni 200 hata chembe ya kazi haikuonekana. Nilizungumza hapa Bungeni kwa uchungu wa hali ya juu. Hizi pesa Serikali inakusanya kwa hali ya juu lakini bado kuna wizi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Rais Dokta Magufuli anajitahidi kukusanya pesa lakini bado wezi hawaogopi. Wakaone mfano Namanyere miradi ya maji inavyoibiwa, ni uchungu wa hali ya juu. Kodi ya wananchi inaibiwa, milioni 800, milioni 300, bilioni moja mradi wa maji Namanyere, lakini hakuna chochote kilichofanyika. Tukiulizia malipo, tunaambiwa malipo yanalipwa kutoka Wizarani moja kwa moja. Ndiyo kuna mafisadi Wizarani huko, hawana uchungu na nchi hii, wala hawaogopi kuiba katika nchi hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuchunguze na miradi ya gesi Pan African na Songas wanatuibia kwenye miradi ya gesi. Miradi ya gesi tunaibiwa kuliko makinikia ya dhahabu, hatuna faida na gesi, tunaibiwa. TPDC inakopa pesa lakini asilimia yake ndogo, sijui hawa ndugu zangu wasomi, wanasheria mikataba ikiandikwa wanakuwa wapi. Tunaibiwa mchana kweupe wala mikataba haisainiwi usiku, saa tatu asubuhi ofisi ziko wazi lakini tunaibiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii nchi tukikusanya pesa hazionekani kwa sababu mafisadi bado wapo. Hawa mafisadi tulishazungumza kila mara, hawa mafisadi ndugu zangu tuwe kama Korea, tuwe kama China, wataogopa. Wizi uko palepale, nguvu zote tunakusanya lakini wizi uko palepale; chunguza mwenyewe. EFD machines kila sehemu inakusanya pesa, ziko wapi? Kama mafisadi bado, mapanya wapo katika Serikali kwa nini tunaoneana huruma, tusiseme ukweli. Tuwe na uchungu, maana yake haiwezekani miradi ya hela inakuja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wilaya yangu ndugu zangu siwezi kuilaumu Serikali. Hela zinakuja, zinatiririka, lakini hakuna chochote kinachoonekana. Namanyere hela zimekuja lakini hakuna maji, hakuna mabomba yanayotoa maji, wizi uko palepale. Sasa tutafika? Hatuwezi kufika. Nataka Serikali ichunguze miradi yote ya maji. TAKUKURU nilishaandika ripoti yote mpaka imefika kwa Mkuu wa TAKUKURU lakini hakuna hatua inayochukuliwa. Tunalindana ndugu zangu, tunalindana! Kuna mnyororo wa kulindana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, umeme wa REA; Sumbawanga, miji imeongezeka, leo tumesema nchi ya viwanda. Ndugu zangu viwanda vya namna gani wakati umeme hautoshi? Leo viwanda vya kusaga tu Sumbawanga Mjini vinafungwa, vinasimama kwa sababu umeme hauna nguvu, umeme hautoshi, kiwanda kikubwa cha kusaga unga kikubwa Sumbawanga kinashindwa. Leo ndugu zangu tunasema uchumi wa viwanda, tumuinue mkulima, asilimia 75 ni wakulima, mkulima gani atalima mahindi mwaka kesho au mwaka huu wakati mahindi yameshindwa kuuzika?

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumezungumza lakini Waziri anatujibu kama vile yeye hana habari, hana uchungu na wakulima. Mkulima hata hawezi kununua mbolea wala hawezi kulima mwaka huu, mahindi yameshindikana kuuza. Tunazungumza kila siku mtu auze mnasema asage, apeleke unga wapi, watu wenyewe wengine wanataka kula dona, wengine wanataka kula kande, utamlazimisha mtu kula sembe? (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ndugu zangu, kwa hiyo naomba waangalieni wakulima ndio wapiga kura, asilimia 75 unasema ni wakulima, nani atalima shamba sasa? Kazi ya ajira hapati, kwenda shambani mnamnyanyasa mkulima, mbona ninyi mishahara yenu mnatumia mnavyotaka?

Mheshimiwa Mwenyekiti, mishahara yenu mnanywea pombe, mnaongeza wake hakuna mtu anawauliza! Mkulima akilima hukumsaidia kupanda, hukumsaidia kupalilia, hukumsaidia kuvuna, akivuna unampa masharti ya ajabu ajabu kwa nini? Kwa nini unampa masharti mkulima wakati hukumsaidia kulima? (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hakuna kazi ngumu kama kilimo, mvua isipokuja hapati kitu, mbolea unamuuzia, sasa ndugu zangu, tutafika? Ninyi aah, mnapata posho hapa mnaingia kwenye mabaa hakuna mtu anawauliza!

Mheshimiwa Mwenyekiti, lazima tuwaonee huruma wakulima wetu wauze mahindi. Hawana cha kuuza katika Mkoa wa Rukwa. Mnaona wivu akiuza mahindi ajenge nyumba ya bati, kitu cha ajabu kabisa. Hatuwezi tukakutana na Waziri, sijui tukakutana na wanaolima mahindi, tuambizane ukweli hapa wananchi wajue kama mwaka kesho njaa itakuja kwa sababu ninyi mmeshindwa kununua mahindi na mkulima hana hela ya kununua pembejeo wala hana uwezo wa kulima. Tusianze kutafuta mchawi hapa, mchawi ni ninyi kwa sababu mmezuia kuuza mahindi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo Zambia wanauza mahindi mpaka 20,000 wanaingiza kule sehemu za Matai, Kalambo, wanauza mahindi wanavyotaka sisi tunazuia mahindi. Kulikuwa na njaa Kenya, kuna njaa tumesikia DRC Congo, kuna njaa Sudan, kwa nini mmeshindwa kupeleka mahindi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama sijakosea jana, kazungumza Mheshimiwa Mbunge mmoja hapa kuhusu Rais kutoa tenda. Ndugu zangu, wapi Rais anatoa tenda? Mimi nimeshangaa, toa ushahidi. Unasema kwamba Rais anampa rafiki yake au ni kampuni yake, toa ushahidi. Naomba aliyesema jana, Hansard ipo atoe ushahidi. Kama Rais anahusika na kutoa tenda ya uwanja wa ndege wa Geita na kama Rais ni rafiki yake, atoe ushahidi. Sio kwenye Bunge hapa kuropoka kuhusu Rais, ni makosa ya hali ya juu. Huna ya kuzungumza kaa, weka akiba ya maneno, siyo unakuja hapa Bungeni unaropoka wewe unavyotaka kwa sababu ni Bunge, hapana. Toa ushahidi, Kamati ya Maadili ikuite utoe ushahidi, kama hukutoa ushahidi uchukuliwe hatua za kinidhamu. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, unazungumza kuhusu Rais, Rais ana makosa gani? Vitanda vya Muhimbili Rais hakuchukua hela kupeleka kule Dar es Salaam? Muhimbili ni Kanda ya Ziwa kule? Amejenga flyover Dar es Salaam ni Kanda ya Ziwa? Ndugu zangu, tuwe tunaweka akiba ya maneno, siyo unazungumza, unabwata kama uko Manzese, hapa siyo Manzese. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nawaambia ukweli, utoe ushahidi. Mimi nashangaa, Waziri anasema anaropoka kuhusu Rais hakuna mtu alisema tukakaa kimya kama tumepumbazwa. Nashauri Mheshimiwa Waziri atoe ushahidi kamili kama Rais alihusika na tenda. Naishukuru Serikali, wananchi wangu wa Kazogo walikuwa hawaoni gari, mwaka huu wanaona gari. Tangu uhuru hawajaona gari, nimepewa hela wanaona gari, nikose kuishukuru Serikali? Barabara ya lami imekwisha toka Tunduma mpaka Kibaoni kupitia Namanyere, sitaishukuru Serikali? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ndugu zangu inafanya kazi, tatizo ni wasimamizi wanakula hela kama watu wa maji. Kuna wizi mkubwa kila Wilaya, kila Mkoa, tena wanaohusika ni Wizarani moja kwa moja. Nataka mfuatilie wala sina utani na hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nasema kwamba, Rais siku akija Namanyere, nitawasema waondoke na wafanyakazi ambao wanakula hela katika Wilaya ya Nkasi wakiongozwa na Idara ya Maji. Haiwezekani hela inafika Namanyere inarudi Dar es Salaam wanagawana Wakandarasi. Wanawapa Wakandarasi tenda wana briefcase, hawana uwezo, hata tipa hana, wala mashine hana, unampa tenda ya milioni 500 au 600 kwa sababu mjomba wako au shangazi yako, hilo haliwezekani!

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.