Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Jang'ombe
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. ALI HASSAN. OMARI KING: Mheshimiwa Mwenyekiti, asante, nashukuru sana kupata nafasi hii na la kwanza nimshukuru Mwenyezi Mungu ambaye ametupa uhai tumekuwa wazima, tumekuja humu kwa pumzi ambayo ametupa yeye watu wanaongea kwa sauti kali kwa pumzi ya Mwenyezi Mungu, tunamshukuru.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine nimpongeze Mheshimiwa Dkt. Mpango ambaye amekuja na mpango huu mimi naweza kusema kwamba ni madhubuti, kwa yule ambaye alikuwa hana sikio alilopewa na Mungu la kusikia hawezi kusikia, aliyekuwa hakupewa jicho la kuona hawezi kuona. Kwa hiyo, haya mengine yatazungumzwa lakini sisi Dkt. Mpango tunampongeza, mpango ni mzuri na mwaka jana tumeona jinsi ya utekelezaji wake unavyokwenda mwenye macho haambiwi tazama. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kingine nimpongeze Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli kwa speed anayoenda. Hii kasi hii haiwezi kuzuilika kwa vitendo vile ambavyo Wapinzani wanaweza wakafanya ni kasi ambayo wao wanajaribu kupuliza kwa maneno kwamba izimike lakini haiwezi kuzimika, haiwezi kuzimika kabisa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna mfano mmoja kuna kidege kidogo kilitua juu ya mgongo wa kobe, kilivyotua juu ya mgongo wa kobe kile kidege kikawa kinamwambia kobe, kobe jiandae mimi nataka kuruka sasa. Eeh, kidege wewe? Juu ya mgongo wa kobe ulipotua kobe hajawa na habari! Leo sasa hivi unataka kuruka ndio utakuwa na nguvu za kumshtua kobe? Gamba lote lile la kobe? Kwa hiyo, haya maneno yatasemwa kutaka kuzima nuru ya Serikali hii inavyokwenda, lakini tunakwenda vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini haya maneno ya kupotosha kusema data za uongo watu kuzungumza vitu ambavyo labda vya kupingapinga tu vinajulikana. Kuna msemo wa Kiarabu unasema khalif tawrab, wewe ukitaka kujulikana nenda kinyume, ukienda kinyume utajulikana, wewe ukiambiwa uchumi unakuwa kwa 7% wewe sema unakuwa kwa 4% utajulikana kwasababu utaandikwa zile 4% unazozisema wewe, lakini hata siku moja hajatokezea mke mwenza akasifu kaburi la mke mwenziwe, umeshapata kuona hiyo na yule tayari ameshakufa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kilitokea kisa kmoja kwamba mke mwenza kapita katika kaburi la mke mwenziwe akaliona kwamba liko vizuri, alivyoliona lipo vizuri akalisifu, akaambiwa kazikwa nani hapa, aah! Alozikwa hapa ni yule mke mwenzio aaa! Kumbe kaburi baya, kaburi linanuka, hayo ni yale majibu ya maneno yenu ambayo mnaongea, mimi ninachozungumza mtoto akinyea kiganja hakikatwi, lakini tunaongeza mbele kidogo, mtoto akinyea kiganja kwanza unakosha kiganja, unamwosha na yeye na nyie ni watoto mmenyea kiganja, sasa tunakuosheni. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mpango huohuo katika hotuba ya Upinzani mlizungumza kwamba katika utawala bora, mkazungumza nyie nyote, kila aliyetoa makelele humu alizungumza hivyo kwamba mkasema polisi hawajafuatilia mpaka leo kesi ile ya Mheshimiwa Tundu Lissu lakini mnajisahau, ukiwa mwongo usiwe msahaulifu kwani si ndio nyie manaotaka polisi wa Kimataifa au sio? Sio nyie mlioambiwa mumlete dereva shahidi wa mwanzo mkasema ana msongo wa mawazo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo ni sawasawa na mtu mwenye busha, mtu mwenye busha, busha linamtatiza na daktari kamwita amfanyie operation, yeye akakataa. Halafu akasema mmeona akasema nitafanyiwa operation na madaktari wa nje, halafu anasema mnaona busha hilo madaktari wenu hawajanitibu, ndio nyie. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tukizungumzia deni la Taifa ambalo limesemwa humu sisi tunakuwa kwa 32% ya deni la Taifa, lakini ilitakiwa tuwe na asilimia zaidi 55% kwa hiyo, kiwango hicho kinakidhi tusome na ripoti za sehemu nyingine. Deni la Taifa linapimwa kwa uhimilivu wake kwa hiyo tusipotoshe watu katika masuala hayo. (Makofi)
Kwa hiyo, sasa hivi labda nizungumze kitu kimoja kuna kitu kinazungumzwa kinapotoshwa ambacho kipo katika mpango huu. Hususani kwamba kuna watu wanasema kwamba tunategemea maendeleo ya nchi hii kwa fedha za nje wakati kwamba trilioni 12.2 ndio zinatakiwa lakini trilioni
9.5 ni za ndani. Sasa wanaozungumza hivyo wanapotosha hawataki kusema ukweli, ndio hao wa kaburi la mke mwenza. Asilimia 77% ya mpango huu fedha zinatoka ndani, kwa hilo asiyejua nani? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie vipaumbele vya Serikali, katika vipaumbele vya Serikali cha kwanza ni viwanda vya kukuza uchumi na ujenzi wa msingi wa uchumi wa viwanda. Naipongeza Serikali viko viwanda vimeanzishwa na sisi wenyewe tunaona viwanda chungu mzima vinaendelea sasa hivi. Tumepita katika ziara tumeviona viwanda, watu waliokuwemo katika Kamati tofauti tofauti wamekwenda wameona hiyo tofauti, lakini bado watu wanazungumzia kwamba hakuna maendeleo yoyote.
Mheshimiwa Mwenyekiti, imezungumzwa hapa, wanabeza juhudi hizi lakini mwenye macho haambiwi tazama, tumeenda, tumeona. Wewe umeshaona mkia wa ng’ombe halafu unauliza ananyea wapi na wakati wewe mwenyewe umeenda ukakagua viwanda. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hili natoa ushauri kwa Mheshimiwa Waziri; kama Ilani ya Chama cha Mapinduzi inavyotaka, hivi viwanda vyetu tunavyovitaka ni lazima vitumie malighafi inayotoka hapa nchini kwetu ili viweze kukuza ajira, viweze kuleta multiplier effect katika wananchi wetu. Pia kupunguza kuuza malighafi nje tukaletewa bidhaa tukauziwa kwa bei kubwa, nayo pia ni tatizo kwa hiyo sisi wenyewe tuongeze thamani, tujaribu kuongeza fursa hizo katika maeneo hayo.
Pia kuna fursa za masoko ya Tanzania sisi wenyewe tunaweza kununua pia Afrika Mashariki, SADC, AGOA endapo tutazalisha, hivyo, tukizalisha tutapata kitu kizuri kabisa. Kwa hiyo, naunga mkono suala hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa wale ambao waliokuwa wanasema kwamba hili jambo la viwanda haliko vizuri kama ilivyozungumzwa katika hotuba ya Wapinzani kwamba hawa wafanyabiashara na wenye viwanda wananyanyaswa siyo kweli. Wafanyabiashara na wenye viwanda hawanyanyaswi kwa sababu kituo cha wawekezaji sasa hivi, Mkurugenzi Mkuu wa TPSF yumo mle ni Mjumbe na wanapanga kwa ushahidi wao wenyewe wamesema kwamba vile vikwazo vya biashara sasa hamna na vimeondolewa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, isitoshe, Baraza la Biashara ambalo Rais mwenyewe ndiye Mwenyekiti katika baraza hili, wao wanakaa na wanapanga na wao wenyewe wametoa ushahidi, wafanyabiashara na wawekezaji binafsi. Llingine, Rais mwenyewe amewaita wafanyabiashara katika siku zake za mwanzo kabisa akawaeleza. Kingine ambacho kwamba maneno yenu mnayosema ni ya uongo, kila mgeni katika viongozi wa nchi za nje wanaokuja hapa wanakutanishwa na wafanyabiashara, sasa wananyanyaswa vipi hawa watu? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho, Rais kila akizindua mradi wa kiwanda Mheshimiwa Rais naye pia huwa anawapa nafasi na anatoa changamoto kwa watu wanaotaka kuanzisha viwanda na yeye yuko tayari.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ambalo katika vipaumbele ni ujenzi wa mazingira wezeshi kwa uendeshaji wa biashara na uwekezaji; kwanza hapa niipongeze Serikali, mazingira ya uwekezaji sasa hivi yanajengwa:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza, kwa hizo Taasisi ambazo zipo zinafanya kazi ikiwemo Baraza la Biashara, ikiwemo Tanzania Investment Center (TIC). Kwa hiyo, hivi vinafanya kazi vizuri; Pili, pia kuanza kwa reli hii ya standarg gauge itakuza; na tatu ndege ambazo tumewekeza, ujenzi wa viwanja vya ndege na vitu vingine hivi vyote vinakuza mazingira ya biashara. Kwa hiyo hapa naipongeza sana Serikali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia naipongeza kwa mpango wa kuja kuendeleza katika mpango huu. Wataendeleza Stiegler’s Gorge, wataendeleza reli ya kati, viwanja vya ndege, Shirika la Ndege litaendelea kuimarishwa na mengine ambayo yanazungumzwa, kwa hiyo haya yatatengeneza mazingira ya biashara na uwekezaji. Kwa hiyo, wakati yamo humu na mwanzo yameshaendelea kufanyika katika kipindi kilichopita ina maana kwamba tunajua kwamba, haya mazingira yatakuwa. Hivyo, ukilinganisha haya mazingira ya biashara na ukuaji wa kipato chetu. Sasa naomba tulinganishe na ukuaji wa kipato chetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukuaji wa kipato chetu sasa hivi per capita ni dola 979, tumetoka hapo tumekuwa kwa 2017 kwa dola 1,025 na sisi tunataka kufikia katika lengo mwaka 2020 - 2025 kwa dola 3,000. Kwa hiyo ili tuweze kwenda speed kama hiyo, sekta binafsi hapa ishirikishwe na ikishirikishwa sekta binafsi tutakwenda vizuri na pia Serikali iweke mazingira katika sekta ya miundombinu. Wakiweka mazingira mazuri hayo pia yatatusaidia katika kufikia mambo ambayo tunaweza tukayafikia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mengine ni ushauri mbalimbali katika sehemu ya mapato; Mashirika ya Umma yale ambayo yanajiendesha kwa hasara tunaiomba Serikali kwanza ifanye utafiti ikihisi kwamba wanaweza wakaendelea nayo yanaweza yakageuka, sawa, lakini ikiona hayawezi kugeuka, yabinafsishwe ili yatakapobinafsishwa Serikali itakuwa inakusanya kodi na Serikali itakapofanya study itajua nini ifanye.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ni mfumo wa tozo za wharfage katika Bandari; Bandari yetu inazalisha mapato zaidi ya asilimia 40, lakini mfumo wa wharfage unaweza ukaturudisha nyuma. Sasa mfumo wa wharfage urekebishwe lakini kwa kufanya utafiti. Tufuate njia ipi? Tutakapofanya utafiti tukaona njia tutakayoweza kufuata, hiyo njia inaweza ikatusaidia, inaweza ikawa ni mwarobaini katika kuzidisha mapato. Tunashukuru kwamba bandari itaongezeka na itajengwa. Tulipita Mtwara kule tumeona Bandari inaendelea, Dar es Salaam sasa hivi tumeona. Kwa hiyo, kwa mazingira ya kujenga Bandari tuweke na mazingira mengine katika mambo ya wharfage ili tuweze kupata kipato kikubwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ni katika urasimishaji wa sekta binafsi na urasimishaji wa biashara ndogo ndogo. Kwenye urasimishaji huu tunaomba ufanyike katika ngazi za mikoa kwa sababu utakaposema unafanya katika ngazi ya Taifa kwamba ni lazima TRA ndiyo awe anashughulika na suala hili kidogo itakuwa tabu na ndiyo maana sasa hivi katika huo urasimishaji imefanyika kwa Dar es Salaam peke yake, mikoani bado haijaweza kufika. Kwa hiyo zoezi hili lifanyike mpaka mikoani ili tuweze kuona ile convenience na economy ya kukusanya kodi na wale ndiyo wanaowajua, mkaa na mgonjwa ndiyo anamjua mihemo yake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naiomba Serikali yangu Tukufu ifanye haya, vinginevyo nawapongeza sana na Mwenyezi Mungu atatusogeza mbele ili jambo lingine ambalo watu wanazungumza haya maneno kwa ajili ya kupata umaarufu, tuyasikilize tu. Ahsante.