Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

Hon. Albert Ntabaliba Obama

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Buhigwe

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

MHE. ALBERT O. NTABALIBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ili na mimi niweze kuchangia mpango wetu wa 2018/2019. Kwanza kabisa nichukue nafasi hii kupongeza Wizara, kumpongeza Waziri na Naibu wake kwa kutuletea mpango ili tuweze kuuboresha. Mpango huu umekuja kama mapendekezo kwa hiyo, ni kazi yetu kuuboresha. Badala ya kuuboresha wala tusiweke majembe, tuuboreshe mpango wetu ili uweze kwenda kutekelezwa 2018/2019.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kipekee niipongeze Serikali hii nzima kwa mafanikio ambayo wameyapata 2017/2018 ni juhudi ambazo zinatokana na michango yetu Wabunge lakini na usimamizi mkubwa wa Serikali. Kwa hiyo, niwapongeze kabisa sitaki kuingia kwa yale waliyoyaandika, yote ni mazuri tusonge mbele, twende mbele!

Mheshimiwa Mwenyekiti, kipekee napenda tu nirudi jimboni kwangu, kwanza niishukuru Serikali. Wizara ya Uchukuzi kwa kutupandishia hadhi ya barabara zetu ambazo zilikuwa zinatuletea shida, barabara ya Buhigwe-Muyama- Katundu imepandishwa kuwa TANROADS, tunawashukuru sana. Pia tunawashukuru kwa kutupandishia barabara nyingine ya Mnanila mpaka Janda ambayo kwa kweli tunategemea fedha nyingi kupatikana ili tuweze kuitengeneza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niishukuru Serikali kwamba tunajenga hospitali yetu ya wilaya. Tunachokiomba sasa kwenye Serikali ni kutuongezea fedha. Mmetupa shilingi milioni 500, tumeanza na ujenzi, Kikosi cha Jeshi la Kujenga Taifa wako wanajenga pale lakini sasa ile milioni 500 ni kidogo. Tunaomba mtuongezee angalau bilioni moja na nusu mkupuo ili twende na ujenzi wa hospitali yetu kwa haraka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niendelee kupongeza kwamba vituo vyetu vya afya vimeendelea kuboreshwa. Tuwashukuru World Vision kwa kuendelea kutuchangia sana kwenye kituo chetu kile cha Muyama lakini tuishukuru Serikali nao wametupatia milioni 500 kwa ajili ya kituo chetu cha Janda. Tunaomba kwa kweli mwendelee kutu-support ili tuweze kuendelea na ujenzi huo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunalo tatizo la ujenzi wa Halmashauri yetu ya Wilaya, ofisi zetu za watendaji tumewapata hawa TBA, tumeshawalipa karibu milioni 400 lakini speed yao ya kutengeneza ni ndogo sana. Kwa hiyo, tunaomba kwa sababu tunapowalipa sisi kama Halmashauri fedha zinaenda Benki Kuu. Zinapokwenda Benki Kuu nafikiri wana tatizo la kurudishiwa fedha ili shirika liweze kuendelea na mradi. Kwa hiyo, tunawaomba kwa kweli muweze ku- release fedha ili waweze kuendelea na mradi na tunaomba mwendelee kutu-support. Tumewalipa pesa zote karibu bilioni moja na milioni 200 tumewalipa cash lakini ujenzi unasuasua. Tunaomba Wizara ya Fedha muweze kuruhusu waweze kupata fedha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunayo miradi ya maji. Mheshimiwa Waziri kwa bahati nzuri wewe unatokea jimbo langu, mimi ndiye Mbunge wako wa Jimbo. Kwa hiyo, ningetegemea kwamba miradi iliyoko pale na fedha ambazo mnatupa ni kidogo sana tunaomba fedha ziweze kuongezwa kwenye miradi yetu ya maji katika vijiji vyetu mbalimbali tunalo tatizo la maji sitaki kwenda mbali kwa sababu mengine tutayaongea kwa sababu ni mpango; mengine tutayaleta na mengine tutayaweka kwenye bajeti zetu za halmashauri, lakini generally tuna matatizo makubwa ya maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkoa wa Kigoma sasa hivi mnaposikia kwamba, Mpango umeandika kwamba kuleta umeme vijijini. Sisi Mkoa wa Kigoma hatujazindua mpango wa REA III na hatujazindua walitupa barua ya kuhudhuria uzinduzi lakini baadaye ukaahirishwa lakini kwa taarifa tulizonazo ni kwamba, kuna mgogoro uliopo kati ya CCRB na wakandarasi. Tunaomba Wizara ya Uchukuzi, Wizara ya Nishati na Madini na Wizara ya Fedha, hebu ingilieni mgogoro huu, mkoa mzima unaadhibiwa na mradi wa vijiji haufanyiki, hatuna umeme!

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumemsikia Mheshimiwa Rais akisema, Wakuu wa Mikoa waangalie ujenzi wa viwanda sasa mkoa mzima hamna umeme unaoenda pale unategemea yeye hapo afanye namna gani? Kwa hiyo, tunamwomba kabisa Mheshimiwa Waziri na ni kilio cha mkoa. Mkoa wa Kigoma ikifikia maendeleo tunataka kuendelea kuna watu wanatokea ku-sabotage maendeleo yetu. Sasa ifike mwisho na Mheshimiwa Waziri yuko hapo na wao ndio wanakaa kwenye Baraza la Mawaziri, hebu ashughulikie hilo, tuna uchungu nalo sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine tumeanzisha TARURA, ni jambo jema, mimi napongeza kwa sababu ubora wa barabara zetu utakuwa mzuri. Tatizo langu, kuna Sheria ya TARURA ambayo hairuhusu kupasua barabara mpya. Sasa ningeomba hilo nalo waliangalie. Kwenye maeneo yetu tuna barabara ambazo tunatakiwa kupasua ni mpya kwa sababu wilaya zenyewe ni mpya ili kuleta mawasiliano mazuri, lakini Sheria inawabana kwamba hawawezi kufanya namna hiyo. Kwa hiyo, tunaomba Sheria nayo ya TARURA ya kupasua barabara mpya iweze kuongezwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini upande wa elimu, kwenye mpango tunakokwenda sasa hivi watu wa kidato cha nne wanafaulu vizuri, kwa hiyo, watatakiwa kwenda kidato cha tano. Sioni kama Taifa kwenye mpango na kupitia kwa Waziri wa Elimu kama tuna bajeti ya kuweza sasa kujenga majengo ya kidato cha tano angalau kila kata kwa sababu sasa tumeshatoka kwenye sekondari kila kijiji sasa angalau kidato cha tano kila kata. Kwa hiyo tunategemea mpango huu uweze kuongeza bajeti ya ujenzi wa madarasa hayo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye bajeti iliyopita hotel levy tuliitoa, tulisema kwamba, haitakuwepo, lakini sasa nimeona kwa Dar-es-Salaam na sehemu nyingine kuna waraka ambao unafuta ile waive tuliyoitoa ndani ya Bunge letu. Sasa tungependa Waziri atuambie hotel levy bado ipo au ameifuta? Maana upo waraka, watu wanatozwa hela, watu hatuelewi, tunaomba a seme.

Mheshimiwa Mwenyekiti, msukumo wa viwanda nakubaliana nao na hakuna ambaye anaubishia, ila wito wangu ni kwamba, intelligence ya masoko na ubora wa mazao ambayo sasa yataanza kuzalishwa ni lazima uwe makini kwa sababu, tutakuja kuwa na bidhaa ambazo watu wataanza kulia hawana mahali pa kuuza. Kwa hiyo, ni vizuri sana sasa watu wa masoko waweze kuwa macho na kuanza kujua namna ya ku-market bidhaa zetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, viwanda vya SIDO. SIDO tumeipa jukumu kubwa sana la kusimamia viwanda vidogo vidogo, lakini ubora wa bidhaa zinazozalishwa na viwanda vya SIDO ni mdogo. Kwa hiyo, tungependa eneo hilo Waziri wa Viwanda aweze kulisimamia vizuri ili ubora wa bidhaa zetu uweze kwenda vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho sijaona kwenye mpango wa Mheshimiwa Mpango kwenye kilimo, msukumo wa zao la michikichi. Sioni akiliongelea kabisa na ni zao ambalo linawafaidisha watu wa Kigoma, watu wanaokula mawese pamoja na kahawa. Kwa hiyo, ni vizuri nayo iweze ku-reflect kwenye mpango huo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, upande wa barabara za lami ambavyo tumeahidiwa na Mheshimiwa Rais. Kwanza tunampongeza, tunamtia moyo, nia yake ya kuufungua Mkoa wa Kigoma tunaipongeza kwelikweli. Tunamshukuru alikuja kwenye ziara, tulimpokea vizuri, kwa hiyo, tunaomba msukume maendeleo na watu wa Kigoma waweze kubadilika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naomba niunge mkono hoja hii tuweze kwenda na maendeleo zaidi. Nakushukuru sana.