Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

Hon. Joseph Kasheku Musukuma

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Geita

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru sana kwa kunipa nafasi niweze kuchangia. Kwanza kabisa niipongeze Serikali ya Awamu ya Tano kwa kazi nzuri inazoendelea kuzifanya kwa kuweza kunipandishia barabara ya halmashauri ambayo iko kwenye jimbo langu yenye urefu wa kilometa 80 na kuipeleka Serikali Kuu (TANROADS). Pia, kuweza kunipandishia Kituo cha Afya Nzela na sasa kuwa Hospitali ya Wilaya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nianze kwa kutoa mfano kabla sijachangia. Jamaa wawili walikuwa wanabishana mchana kweupe, saa sita. Mmoja anamwambia mwenzie hili joto lililopo linaletwa na lile jua pale juu, mwingine anasema lile sio jua ni mwezi. Sasa wakati wanabishana jua na mwezi, wamevaa vizuri na suti na tai, akapita mama mmoja wakamuuliza mama tunaomba utuamue, hili ni jua au ni mwezi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, yule mama akawaangalia wamevaa vizuri kabisa wastaarabu, akaona dawa yao ni kuwaambia jamani mimi sijui akaondoka. Wakaendelea kubishana akapita baba mwingine, walivyomwona wakasema awaamue wakamuuliza baba tusaidie, hili ni jua au ni mwezi? Saa sita mchana, akawaangalia juu mpaka chini, ni wastaarabu kabisa, akawapa jibu tu kwamba, jamani mimi hapa ni mgeni, akaondoka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa tunachosumbuka nacho humu ndani ni huo mfano kwamba, wanaona kabisa hili ni jua, lakini wanang’ang’ana kusema huu ni mwezi. Hata mngejitetea vipi Mheshimiwa Mpango hawawezi kukuelewa hawa, watakwambia ni mwezi na wakati ni saa sita mchana. Kwa hiyo, dawa yao wewe waambie hapa ni mgeni, ili uende vizuri na safari ya kutuletea maendeleo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niseme nchi hii ina misingi mizuri sana na sisi wenzenu tumekuwa wavumilivu toka miaka ya sabini na kitu wakati nchi hii inatengenezwa. Leo ukienda Kanda ya Kaskazini utakuta lami zinaenda kuishia kwenye migomba ambako hakuna uhitaji, sisi watu wa Kanda ya Ziwa hatukupiga kelele kwa sababu, tulijua Serikali inatengeneza maendeleo kwa awamu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo ukienda Kilimanjaro unakuta kuna KIA, ukienda Moshi Mjini kuna uwanja mdogo, ukienda Arusha kuna uwanja mdogo. Sasa hapa kumetokea mambo watu wanapiga kelele katika Uwanja wa Ndege wa Chato. Nataka niwaambie, Mheshimiwa Waziri hizi kelele ziache waambie wewe hapa ni mgeni. Napendekeza mkimaliza kujenga ule uwanja wa mkakati wa Chato, jengeni mdogo Geita, kama ulivyo wa Moshi, ili tuwe na viwili hesabu ya kulilia uwanja ujengwe Geita iishe, kinachowauma mimi sikioni. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri na Serikali inisikilize katika viwanja ambavyo ni vya mikakati, ukiwemo na Uwanja wa Chato, Songwe na Mtwara, imarisheni. Huwezi kwenda kujenga uwanja wa ndege Iringa, kuna ndege inabeba magogo hapa? Tunatengeneza viwanja vyenye kupandisha uchumi wa nchi. Geita tuna dhahabu, tuna samaki ambao hata ndege ikitua itabeba, hakuna Boeing inabeba magogo kupeleka China, kwa nini tunaanza kuchambana humu ndani? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Uwanja wa Ndege wa Chato, nawashangaa sana Wabunge wa Kanda ya Ziwa, Mbunge wa Biharamulo, Mbunge wa Karagwe, Mbunge wa Kasulu, Mbunge wa Muleba, mnaacha watu wanashambulia uwanja wa Chato. Sisi tungekuwa na tamaa tungeujenga uwanja ule Geita Mjini, lakini impact ya uwanja ni biashara, hawa wote hamuwezi kwenda tena Bukoba mnakaa humu watu wasiojua hata ramani wanashambulia kwa ku-google kwenye mtandao, kwa nini msisimame mkatetea? Leo mtu wa Biharamulo utaenda Bukoba uwanja uko Chato? Mtu wa Ngara? Mtu wa Muleba? Mtu wa Kasulu? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi kwa tabia zetu Wasukuma hatuna upendeleo tunagawanaga keki na ndio maana tumeweka katikati kama mlivyoweka ninyi pale KIA. Kwa hiyo, nawaomba sana suala la ku-discuss Uwanja wa Chato acheni Mpango wa Serikali ufanye kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukienda Chato kilometa 30 tu kuna hifadhi pale inaitwa Rubondo, lakini tuna dhahabu pia, palepale Chato. Hata ukiangalia historia, msiofahamu, Chato, Mkoa wa Geita kila mahali kuna uhitaji muhimu; ukienda Geita sisi eneo lote la Geita mnalolipigia kelele kuna wazungu wanachimba under ground sasa hivi, ukienda kwangu sisi tunavua na kulima. Sasa kama tumechagua eneo ambalo lina usalama angalao wa miaka 200 mbele mnapiga kelele bila kujua, mnataka uwanja ukawekwe kwenye mahandaki yanayochimbwa under ground? Acheni Mpango wa Serikali ufanye kazi, jadilini matatizo ya mikoa yenu. Hamjatumwa humu kuja kutetea uwanja wa ndege. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana Mheshimiwa Naibu Waziri ameliweka vizuri kwamba, mtajenga na Moshi, mtajenga na Tanga; yote haya uwanja huu ungekuwa unajengwa Moshi wala kulikuwa hamna kelele humu, lakini niwaambie tumekuwa wavumilivu vya kutosha. Chuo Cha Madini ambacho kimejengwa na GGM, GGM iko Geita, kwa kuwa tu ninyi mlikuwa kwenye madaraka mka-divert mkapeleka chuo kikajengwa Moshi; dhahabu itengenezwe Geita mkajenge chuo chetu moshi, tumekaa kimya. Tusianze kufukua makaburi humu tunaelewa mengi sana. Tusianze kufukuliana makaburi na nawaona watu wa Kanda ya Ziwa mnasimama kubwabwaja kuhusu mambo ya Kanda ya Ziwa, mnatumika kama matela. Tutakutana 2020 labda ule mtindo wenu wa kunini na kunini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nichangie kuhusiana na suala la mahindi. Naiomba sana Serikali ishikilie msimamo wake wa kutokuruhusu mahindi yasiende nje, mimi nakuwa tofauti na Wabunge wenzangu. Nataka niwaambie na Serikali ina system, hebu tumeni system huko kunakolalamikiwa kuna mahindi kama utakuta mahindi ya mnyonge yako pale. Tunakuwa na Bunge la kujadili mabwanyenye walanguzi, wakulima wa mahindi..

(Hapa baadhi ya Wabunge waliongea bila mpangilio)

MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Mnisikilize nyie mmechangia mie nimekaa kimya; wakulima wa mahindi kuna mabwanyenye wanaowekesha gunia 15,000/= wakati wanaanza kupanda, wakishamaliza kuvuna yanachukuliwa yale mahindi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hata huko Sumbawanga kuna watu tunanunua nao mahindi 35,000/=. Yaani tunakuja na katimu ka kutetea mabwanyenye, tumeni watu mkaone mkulima mwenye magunia 150 au 30, 10 kama ana mahindi. Halafu mimi ni Mbunge wa Kanda ya Ziwa ambapo mahindi yalikuwa yanauzwa Sh.110,000/= leo tunauziwa mahindi Sh.60,000/=, nikubali mahindi yaende nje ili turudi kwenye Sh.110,000/=? Shikilia msimamo, mtu anayetaka kufanya biashara koboa unga, peleka nje. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, bahati nzuri Mheshimiwa Keissy ametoka, wakati tunatetea ng’ombe alisema mang’ombe yauzwe, sasa yeye kwenye mahindi hatutoi mahindi, Serikali isilegeze kaza uzi. Mnaona kama mzaha, ruhusuni, fanyeni hesabu kuyaruhusu haya mahindi yaende nje, yakienda nje haya mahindi mwezi wa kwanza hili Bunge tunaanza kujadili njaa.

T A A R I FA . . .

MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, namheshimi sana. Mimi ni Mbunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na bahati nzuri kwenye jimbo lake mimi nanunua mahindi. Hawa watu muwe mnatafuta reference twende ukatuoneshe, mkulima tunayemtetea humu ndani ni mkulima anayelima kwa jembe la mkono, hatuwezi kutetea walanguzi...

(Hapa baadhi ya Wabunge walizungumza bila mpangilio)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nizungumzie kidogo suala la mazao na maliasili. Nimpongeze sana Mheshimiwa Kigwangalla ameanza vizuri, hakuna Waziri atakayepambana na wanyonge akabaki kuwa Waziri. Wanyonge wana machozi na machozi yanasikilizwa na Mungu na mifano mmeiona. Simamia uzi huohuo wa kutetea wanyonge. Kumeibuka mambo tunaomba atusaidie; watu wana miaka 10 wanaishi maeneo ya porini, halafu leo wanaibuka tu wataalam wanaenda wanachoma nyumba, tunakubali chomeni nyumba, chakula ambacho kimebakiza mwezi mmoja kivunwe wanafyeka na kuchoma. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, namhakikishia Mheshimiwa Waziri asipodhibiti hili, hii ndio laana yake ya kwanza kabisa. Awaambie wawaache wananchi wetu wavune kwanza chakula ndani ya miezi miwili, halafu wawadhibiti kuingia mle ndani. Sisi kama Wabunge wawakilishi hatuwezi kuwa na wananchi ambao wana njaa. Bahati mbaya sana tumetoka kwenye njaa, Mungu ametupa neema watu wamelima, chakula kimebaki miezi miwili, mitatu DC anaonekana kwenye TV anafyeka chakula na kuchoma tena kama shujaa, halafu sisi Wabunge tumekaa kimya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sana Mheshimiwa Waziri Kigwangalla tumeona aliyoyafanya Loliondo.
Achunguze, hata hizi operations…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nishauri kwenye dhahabu. Niliwahi kumshauri Mheshimiwa Waziri kwamba, mzee huwezi kupambana na wafanyabiashara wadogowadogo ambao wanatorosha dhahabu yetu ambayo ni nyingi kuliko hata inayosafirishwa na migodi. Ushauri wangu, hebu aondoe ile asilimia tano ya kodi ya wachimbaji wadogowadogo, a-deal na watu wa migodi mikubwa ambao wao hawawezi kukwepa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hawa watu wa mifukoni kuwadhibiti ni ngumu sana na yeye kwenye bajeti yake aliwahi kukusanya milioni 88 tu, hebu aruhusu dhahabu iwe free market kama ilivyo Dubai, kama ilivyo Uganda, watu wa Kongo, wa Zaire, wa Burundi walete dhahabu Tanzania, sisi tupate asilimia moja peke yake ya kusafirisha dhahabu, hatapambana na hao watu anaowakamata bandarini na watu watamwonesha kila kitu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, namshauri sana watalaam wake wakubali kuachia free kwenye dhahabu humu ndani liwe soko la uhuru, Waganda walete. Leo hii Uganda ni asilimia 0.5 nani atakubali kuja kulipa asilimia 6.0, si afadhali niifiche kwenye soksi, sasa atakamata wangapi kwa mwaka?

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu ajaribu kuangalia kama anaweza kutoa hiyo asilimia tano abakize asilimia moja tu ya kusafirisha. Hatakamatana na watu tutamletea dhahabu kama anavyotaka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru.