Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

Hon. Richard Mganga Ndassa

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Sumve

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

MHE. RICHARD M. NDASSA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru sana lakini ni kweli kama ulivyosema kwamba baadhi yetu ni wakongwe kidogo humu ndani. Kwa sababu ya ukongwe wetu nikuombe sana wewe mwenyewe lakini nimwombe pia Waziri Mkuu wetu, Mkuu wa Kambi ya Upinzani na Wabunge wote, nimesikiliza michango kuanzia mwanzo siku ya kwanza mpaka jana, siyo kawaida ya Bunge letu hata siku moja, tunatoka kujadili Mpango tunajadili ukanda. Bunge lako sasa limeshapelekwa lipande basi la ukanda kwamba kanda fulani, Kanda ya Kusini, Kanda ya Kati na Kanda ya Kaskazini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi tukishatoka kwenye ukanda tunaenda wapi? Tutakuja kwenye ukabila, tukitoka kwenye ukabila tunakuja kwenye rangi na dini zetu. Ningeomba sana Waheshimiwa Wabunge kwa sababu sisi ni wawakilishi wa wananchi na kwa sababu tukisema jambo humu ndani, wananchi wetu wanatusikiliza vizuri, tusifike mahali tukawagawa wananchi wetu kwa maana ya ukanda. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, yamesemwa mambo mengi sana kuhusu Rais sijui amefanya nini Kanda ya Ziwa, lakini ukitazama kwa nchi nzima na bahati nzuri Kanda ya Ziwa ni moja ya sehemu ya Tanzania. Rudi uangalie maeneo mbalimbali kwa mfano hata hapa Dodoma, uamuzi mzito alioutoa Mheshimiwa Rais wa kuamua kuhamishia Makao Makuu Dodoma, hakusema kuhamia Mwanza hapana.

Uamuzi mkubwa na mzito wa kuihamishia Serikali Dodoma ni uamuzi mzito, sasa tusije tukafika hapo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niwaombe sana chonde chonde Waheshimiwa Wabunge! Kwa sababu jana nimeona yale mashambulizi, watu wanatokwa mapovu kwa sababu ya ukanda. Hivi Mwalimu Nyerere ndivyo alivyotuachia maneno hayo? Tukitoka kwenye ukanda tutakwenda kwenye udini na ukabila, hatuwezi kufika. Ili tujenge nchi yetu, Wabunge lazima maneno yetu yanayotoka kwenye vinywa vyetu lazima tuyachuje kabla hatujayatoa. Naomba sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu ya mshikamano kama mnakumbuka, mwaka 1979 kwenye vita vya Kagera tulimpiga Idd Amin kwa sababu ya mshikamano na umoja. Mwalimu alitumia maneno matatu, uwezo wa kumpiga tunao, sababu ya kumpiga tunayo na nia ya kumpiga tunayo. Sababu ya umoja ule Watanzania wote Tanzania nzima mwenye kuku, mbuzi, trekta, basi na mwenye lori tukashikamana pamoja ndiyo maana ile vita tukashinda. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo vita yetu kuu siyo ya Kagera, vita yetu kuu kwa sasa ni ya kiuchumi. Vita ya uchumi tutaishinda kama tutakuwa pamoja tukaachana na mambo ya ukanda, tukawa Watanzania wamoja tukaungana kumuunga mkono Mheshimiwa Rais wetu, anatuonyesha njia kama alivyotuonesha Baba wa Taifa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Baba wa Taifa alituunganisha pamoja akasema kwa sababu huyu jamaa ametuchokoza na tunao maadui wengi wa kiuchumi Mheshimiwa Rais wetu Magufuli anatuonesha njia, ni lazima tumuunge mkono sio kwa kumbeza kwa kazi nzuri anazofanya jamani. Niwasihi sana Waheshimiwa Wabunge tumuunge mkono Mheshimiwa Rais, lakini kama Wabunge lazima tuwe wamoja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakuomba nakujua ni mtu makini, endapo itatokea mimi Mbunge na mwingine labda akasimama humu ndani na kuzungumzia ukanda, mamlaka unayo ili kulinda heshima ya Bunge na nchi yetu. Tukianza kuzungumzia ukanda tutakwenda mbali sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wenzetu jirani tu hapa kama mmesikia baada ya uchaguzi kwa sababu ya kabila hili na kabila hili, wanasema wanataka kujitenga kila mtu awe na nchi yake. Tukiruhusu kwa sababu mambo haya huwa yanamea polepole, tunaweza tukaruhusu tukafika huko. Hili ilikuwa ni ombi langu kwako na kwa Mheshimiwa Waziri Mkuu, Kiongozi wa Kambi ya Upinzani na Wabunge wote. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niende kwenye mpango, nitasema kidogo tu. Nimwombe sana Mheshimiwa Dkt. Mpango, Mheshimiwa Rais anazungumzia kuhusu uchumi wa viwanda, yeye na kila mtu anajua. Katika mpango wake humu ndani sijaona sababu za makusudi hasa upande wa umeme, hivi viwanda anavyotaka kuvianzisha anakwenda kuweka ma-generator au anaweka nini.

Mheshimiwa Spika, viwanda hivi ili viende na vizalishe lazima viwe na umeme wa kutosha na siyo vinginevyo, vinginevyo labda kama tunataka kupiga sound, well, lakini kama tunataka tutoke hapa tulipo, leo tuna megawatts 1,437, au 1,400, lakini tunasema okay, Stiegler’s Gorge mwaka 2021 tunategemea itazalisha megawatts 2,100, hivi leo tukijiuliza kwa sababu ya umeme huu tulionao tunataka viwanda vichipuke kwa haraka kwa umeme upi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, Waheshimiwa Wabunge, lakini achilia mbali viwanda, tumeanzisha REA III, ambayo ipo inakwenda Kongwa. Sasa kwa utaratibu huu wa umeme wenye mashaka hata hiyo REA III nafikiri itaishia njiani tu. Sasa ni lazima Mheshimiwa Dkt. Mpango, Waziri wa Fedha na Mipango, kwanza nimwombe, bahati nzuri Waheshimiwa Wabunge wa CCM wanamheshimu sana, lakini ana ka- arrogance fulani hivi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, natumia lugha nyepesi ya kidiplomasia, sasa hiyo arrogance hebu ajaribu kuiondoa, kwanza haisaidii Bunge, lakini haisaidii sana Serikali. Kwa sababu naweza nikaja na hoja ya msingi ya kutaka kuisaidia Serikali na nikwenda kwake mara chungu nzima, nikamwambia kuna mwanya hapa tunaweza tukapata pesa, lakini namna ya kumpata utafikiri unataka kumpata nani sijui. Sina uhakika kama hata simu za Waheshimiwa Wabunge huwa anapokea, sina uhakika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi ni Wabunge wenzake, wote humu ndani, wa upande ule kule na upande huu, sisi ni Wabunge wenzake. Tunataka tuisaidie Serikali kwa sababu yeye ndiyo amekamata mfuko wa pesa. Sasa mfuko wa pesa hawezi kwenda kutafuta pesa peke yako. Sisi ndiyo wasaidizi wa kumsaidia, mipango ambayo tunamshauri na yeye angekuwa na uwezo wa kupokea basi angalau kama siyo asilimia 75 basi hata asilimia 50, basi hata 25. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kitabu hiki nimekisoma, Mdogo wangu Peter hapa tumesoma pamoja, unajua wengine hatuna zile lugha kali, tuna lugha za kidiplomasia. Namwomba sana Mheshimiwa Dkt. Mpango wa Mipango, hebu ajitahidi kwanza kusikiliza Kamati ya Bajeti, aisikilize mipango yake, ushauri wao, ajaribu kuusikiliza pamoja na wataalam wake. Kwa sababu ilishafikia mahali wanakwenda kwenye Kamati ya Bajeti, mnakaa mnazungumza, mnaishauri Serikali, lakini hakuna kinachochukuliwa, as if Kamati ya Bajeti haipo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata ile maana ya kuwa na Kamati ya Bajeti inakuwa haipo kwa sababu yote tunayoshauri kwenye Kamati ya Bajeti yakichukuliwa sana labda ni mawili. Sasa nini maana ya kuwa na Kamati ya Bajeti ya kuishauri Serikali? Maana yake inakuwa haipo.

Mheshimiwa Spika, sasa nimwombe sana Mheshimiwa Dkt. Mpango wa Mipango, mipango yake ili iende vizuri ni lazima awasikilize Waheshimiwa Wabunge.

Peke yake na Wataalam wake watafika mahali ipo siku watakwama, watatuomba tuwasaidie kuwakwamua lakini tutafika mahali tutasema hapana na tutamwambia Mheshimiwa Spika kwa utaratibu huu hatuwezi kwenda hata siku moja kwa sababu sisi ushauri wetu tunashauri lakini hatusikilizwi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, umesema vizuri sana wakati Mheshimiwa Peter Serukamba akizungumza hapa, kwamba wasikie. Sasa nafikiri na mimi nimemwambia Mheshimiwa Dkt. Mpango asikie. Wenzake wote wanasikia isipokuwa Dkt. Mpango wa Mipango, hasikii. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, narudia tena na ukiona Seneta anasema ameshasikiliza mengi huko nje. Dkt. Mpango wa Mipango yeye siyo msikivu kwa Waheshimiwa Wabunge, ajaribu kubadilika kwa sababu wote tuko kwenye boti moja, tunataka tuifikishe hii boti yetu mahali pema, hakuna mtu hata mmoja anayetaka kutoboa mtumbwi hata mmoja, wote tunakwenda katika mtumbwi mmoja, twende salama salmini ili tuifikishe salama nchi yetu mahali ambapo patakuwa na neema. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho, nisisitize tena umeme, lakini pili suala la ukanda. Baada ya maneno hayo, nikushukuru sana kwa nafasi lakini kama nilivyoshauri na nilivyokuomba, suala la ukanda litatufikisha mahali pabaya sana endapo tutaliendekeza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi.