Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Muheza
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. BALOZI ADADI M. RAJAB: Mheshimiwa Mwenyekiti, na mimi nashukuru sana kupata nafasi ya kuchangia kwenye huu Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa mwaka 2018/2019.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mipango mizuri ni ile mipango ambayo inatekelezwa, tumekuwa tunatengeneza mipango mizuri sana miaka mingi sana na utekelezaji wake unakuwa sio kwenye asilimia 100.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naamini kwamba hii mipango ambayo imeandikwa kwa mwaka 2018/2019 kama utekelezaji wake unakuwa kwa ukamilifu, basi tunaweza tukawa na uchumi ambao utapaa vizuri sana. Mipango mizuri inayotekelezwa inaongeza uchumi na inapunguza mfumuko wa bei.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeona mipango mingi baadhi ya mipango ya 2017/2018, 2016/2017 imeanza kutekelezwa kwa uzuri kabisa. Tumeona standard gauge ya central line ikianza, tumeona ndege bombardier zikianza kuingia, tumeona umeme kule Rufiji - Ruaha ukianza, kwa kweli inatia matumaini na tumeona bomba la mafuta ambalo linatoka kule Hoima - Uganda mpaka kwetu kule Tanga.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vitu hivi kwa mfano kama Bomba la Mafuta la Tanga la kutoka Hoima mpaka Tanga inabidi tuongeze thamani yake, value adition. Kwamba bomba hili sehemu zote ambazo litapita watafaidika namna gani, kuna mipango gani ambayo ipo ya kusaidia kuona kwamba linaweza kuongeza thamani kwenye maeneo yote ambayo bomba hili linapita na wananchi ambao watafaidika ambao bomba hili linapita wanafaidika kiasi gani. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye huu mpango sioni central line, sioni mpango wowote wa kuanza kutengeneza SGR ya central line na nimeangalia kwa makini, lakini sijaona. Naamini kabisa kwamba Tanga line pamoja na central line zikienda simultaneously basi tunaweza tukapata mendeleo mazuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, juzi juzi Rais alikuja Tanga na aliambiwa tatizo hili na akaamuru bandari iongezewe fedha. Nilikuwa naona kwamba tusingoje mpaka Rais aje kwa sababu nchi ni kubwa, lakini ninyi Mawaziri mnapaswa kumsaidia kwenye maeneo yale ambayo ni muhimu. Sikuona namna ambavyo Kiwanja cha Ndege cha Tanga kinaweza kupanuliwa na sijaona namna ambavyo bombardier imeelekezwa kutua katika Kiwanja cha Ndege cha Tanga kwa sababu sasa hivi kutakuwa na hekaheka nyingi sana. Naomba Waziri aliangalie hili kwa makini sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini Tanga line nakumbuka kikao kilichopita tulikubaliana kwamba aliyefanya upembuzi yakinifu atalipwa fedha zake na akilipwa fedha zake basi mpango huo utaingia kwenye PPP. Wapo wawekezaji kutoka Marekani ambao wameshughulika sana kupata huo mchoro ili waanze kuleta mapendekezo ya kuanza kutengeneza Tanga line, lakini mpaka sasa mchoro huo unakuwa ni hadithi. Kwa hiyo, naomba kabisa Waziri a-take note kama tuliamua kwamba msanifu alipwe kutokana na Mfuko wa Reli basi alipwe mara moja ili huo mchoro upatikane na tuanze kuuza hiyo biashara kutengeneza Tanga line mara moja. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilizungumza katika bajeti iliyopita, hili suala la PPP, suala la road toll, duniani kote sio Marekani, Ulaya na baadhi ya nchi hapa Afrika wanatumia road toll. Hizo nchi ambazo zimeendelea zinatumia road toll sisi kwa nini hatutaki kutumia road toll? Naamini kabisa mapato ambayo yatapatikana kwenye barabara…
MWENYEKITI: Waheshimiwa Wabunge, naomba mpunguze sauti tumsikilize mchangiaji, zungumzeni taratibu.
MHE. BALOZI ADADI M. RAJAB: Mapato ambayo yatapatikana kwenye barabara ni makubwa na mfano upo wa Daraja la Kigamboni ambalo limeingia PPP na NSSF, mapato ambayo yanapatikana pale Kigamboni yangeweza pia yakapatikana kwenye barabara zetu kama tungeanzisha mpango wa road toll. Naamini kabisa kama Mataifa makubwa wanatumia road toll kwa nini hapa tusitumie, tuna tatizo gani? Mheshimiwa Mpango naomba kabisa hili suala aliangalie kwa makini sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la maji tumelizungumza na kila mtu hapa ndani ana tatizo la maji, viwanda na kilimo haviwezi kupatikana bila maji. Kuna mpango upo wa miradi mikubwa 17, kuna mradi wa dola milioni 500 kutoka China lakini sasa hivi imekuwa ni hadithi tu tunaambiwa financial agreement, sasa financial agreement mpaka lini? Naambiwa financial agreement ipo Wizarani kwake Mheshimiwa Mpango. Naomba kabisa atakapokuja ku-windup atuambie kwamba hii miradi na hiyo financial agreement imefikia wapi, kwa nini haianzi? Mimi ni mdau na Muheza ipo kwenye huo mradi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kilimo, ukiangalia ukurasa wa tisa tumeambiwa kuna ongezeko kutoka asilimia 2.7 mpaka 3.1, hili ni ongezeko dogo sana. Naamini mkazo mkubwa tungeweka kwenye kilimo sasa hivi tungeweza kuwa mbali sana. Mheshimiwa Mpango ningependa sana wataalam wa kilimo watembelee hata hapo Zimbabwe na South Africa ili waone mashamba ya kisasa ambayo yapo, waone system za umwagiliaji ambazo zinatumika kule boreholes na kadhalika, unakwenda kwenye shamba wewe mwenyewe hutaki kutoka kwa raha ambayo unaoina pale.
Mheshimiwa Mwenyekiti, unakwenda kwenye shamba unakuta kuna viwanda vidogo vidogo kama tumbaku hii ambayo tunasema wanakausha, wana viwanda vidogo vidogo ndani ya mashamba. Tumbaku ikitoka pale inakwenda moja kwa moja airport na maua yakitoka shambani yanakwenda moja kwa moja airport. Vitu kama hivi ndiyo vya kujifunza, naamini kabisa kwamba tutakapopeleka wataalam na Serikali ikiweka nia kwenye kilimo tutakuwa mbali sana.
Mheshimiwa Spika, hapa juzi nchi moja hapa chini tu walitoa bure mbolea na mbegu wakawapa wakulima na mazao ambayo wamevuna huwezi kuambiwa kwa sababu yale mavuno yalikuwa ni mengi mwisho ikabidi wawauzie WHO. Kwa hiyo, vitu kama hivyo ni muhimu sana kuweza kujua kwamba unawawezesha wakulima, unawapa mikopo ya vifaa vya kisasa, hatuwezi kuendelea kulima na jembe mpaka leo, kuna ma-harvester na kila kitu.
Mheshimiwa Spika, hapa kamati yangu ilikwenda Songwe, Mbeya kule, wapo wafungwa wanasema hatuna trekta, hatuna vifaa tuleteeni vifaa, Songwe ndiyo ambayo inalisha Mbeya yote ile, tuleteeni vifaa tulime na ardhi ipo. Tukaweka kwenye bajeti kwani walipata hata senti tano? Hivi ni vitu vya kuangalia kwa sababu vina umuhimu wake. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hivi kuna tatizo kubwa sana kwenye zao la chai. Kule Amani sisi tunalima chai sana lakini tatizo ambalo linajitokeza sasa hivi ni kwamba wale walimaji wanatakiwa wa-export hiyo chai moja kwa moja au waingie kwenye mnada Mombasa, hawaruhusiwi ku- blend wala ku-pack, parking na blending vyote vifanyike nje, sasa hii nini? Wanakwenda Mombasa kwenye mnada, Kenya wananunua chai yetu wana-pack Kericho, Kericho wanaleta chai hiyo hiyo hapa nchini.
Mheshimiwa Spika, hili suala siyo sahihi tunasema tulime na tu-dd value sasa hawa hawaruhusiwi, ni suala la kuliangalia. Nimeongea na Waziri wa Kilimo na nime-set appointment naye ili tuweze kuona tutafikia wapi lakini ni muhimu suala hilo liangaliwe kwa umakini wake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vivyo hivyo na pamba, nchi kama Zimbabwe inalima pamba kidogo sana ukilinganisha na sisi, lakini grade ya kwake ni kubwa ukilinganisha na grade ya kwetu hapa. Ni kwa sababu ya utunzaji na ulimaji wake ambao unafanyika kwa umakini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la mwisho ambalo nataka kuongelea ni la kuhamia Dodoma. Wizara zimeshahamia Dodoma, Dodoma imeshakuwa makao makuu lakini sijaona kwenye mpango namna ya kutengeneza huu Mji uonekane kweli ni makao makuu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, miji mingi ambayo imehamiwa Serikali inakuwa na mipango, nenda Rwanda na Abuja kaangalie, wanakuwa na mipango kabisa wameshapanga kwamba wanajenga site fulani, wana- prepare certain site, wanaweka kila kitu nyumba na maofisi everything. Sasa hapa sijaona chochote kwenye mpango huu namna gani ambavyo tutaboresha Makao Makuu ya Dodoma iweze kuonekana kweli ni makao makuu kama nchi nyingine. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, nakushukuru sana.