Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mpanda Mjini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
2
Ministries
nil
MHE. SEBASTIAN S. KAPUFI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Na mimi nianze kuchangia Mpango huu kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la kwanza ni eneo la kilimo. Mimi eneo la kilimo naomba niliweke katika sura zaifuatazo. Namwomba Mheshimiwa Waziri mipango yetu na kama ambavyo mmeeleza hapo iendelee kujikita katika kuzingatia tafiti mbalimbali. Nalisema hilo kwa sababugani?
Leo hii isitokezee kwamba kwa sababu korosho ina bei kubwa basi kila mtu akatamani kulima korosho, twende kwa tafiti. Kwa misingi hiyo kama ambavyo nimeendelea kusema hapo kwa kupitia tafiti tunaweza tukafahamu ni kanda zipi zinafaa kitu gani na isitokezee tu kwamba kwa sababu leo pamba ina bei nzuri basi kila mmoja akataka kulima pamba, naomba mipango ituelekeze huko.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo, eneo hilo hilo la kilimo upande wa mahindi ambao kila mmoja amezungumzia hapa, mimi nitatoa mfano na wanasema kama huna vielelezo, haujafanya utafiti usiongee, naomba niongee kwa vielelezo na kwa utafiti.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nililima maharage lakini baada ya kulima maharage nikafanya maoteo kwamba mahindi yatanipatia pesa nzuri, kwa hiyo, nikabilisha maharage kununua mahindi. Ni mkulima mimi niliyelima maharage, lakini nikanunua mahindi, nikayahifadhi kwa maana nipate fedha nzuri kwa maana ya maoteo. Leo hii nisipopewa nafasi ya kuuza mahindi yangu, sitokuwa na nafasi ya kulima tena hata maharage, nitakuwa nimekatwa miguu.
Kwa hiyo, naomba sana katika maeneo hayo, wale wote ambao wamelima mahindi wapewe nafasi vinginevyo tutakwenda kutengeneza mazingira ya watu hao kutoweza kusimama kwa miguu yao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, natambua kwamba nusu ya 2017 kilimo kilichangia kutoka asilimia 2.7 mpaka 3.1, umuhimu wa kilimo uko pale pale. Nafahamu kwamba kwa kupitia kilimo ni sehemu kubwa ambayo inaajiri Watanzania walio wengi, lakini mipango iendelee kutusaidia. Kilimo hiki ambacho ni cha kijungujiko (hand to mouth) sort of economy, tunatakiwa tutoke huko. Haiwezekani ikawa Watanzania wengi wako kwenye kilimo lakini mwisho wa siku kilimo hiki kisifanye watu tujitegemee. Ni bora hata wachache wakalima lakini wakalima kilimo chenye tija.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sasa niongelee suala la afya. Nilishauri mara ya mwisho, ni kweli nimeona hospitali kama ya Muhimbili na Bugando tunaendelea kuzipa vifaa tiba na kuongeza vifaa mbalimbali. Ushauri wangu unabaki pale pale, tuna mipango ya kuboresha Hospitali za Mikoa, mimi binafsi natoka Mkoa wa Katavi, tukiboresha Hospitali za Mikoa tunapunguza msongamano wa watu kwenye Hospitali hizo za Bugando, Muhimbili na kwingineko. Kwa hiyo, niliombe sana hilo tuendelee kufanyia kazi kwa maana ya kuboresha maeneo haya ya chini. Ukiniboreshea mimi Katavi, ukimboreshea wa Kigoma na wa Tabora tutapunguza watu kutegemea maeneo hayo. Eneo la afya naomba nitoke kwa sura hiyo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la maji. Itakuwa ni kichekesho, mara ya mwisho nilizungumza hapa pia nikasema nchi hii tuna uwezo wa kufanya muunganiko wa maji kuwa kama design ya buibui. Mtu wa Nyasa akiunganishwa kupitia Ziwa Nyasa na Viktoria wakiunganishwa kupitia Ziwa Viktoria, Tanganyika tukiunganishwa kwa kupitia Ziwa Tanganyika, nchi hii itakuwa na mtandao wa mabomba ya maji. Hatuna sababu ya kwenda kwenye vyanzo ambavyo siyo vya uhakika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi leo hii katika Mkoa wa Katavi tunazungumzia habari ya Bwawa la Milala na chanzo kingine cha Ikorongo wakati Ziwa Tanganyika lipo kilometa 120 kufika Manispaa ya Mpanda. Miradi mingine tunayoiona ya kutoa maji VI-ictoria iwe ni dira kwenye maeneo mengine. Hatuna sababu, nimesema kwingineko duniani watu wanabadilisha mpaka maji ya bahari kuwa maji safi ya kunywa, sisi hatutakiwi kufika huko kwa sababu vyanzo vingine vya maji safi, baridi ya kutumia tunavyo, ni mipango tu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la misitu, naomba eneo hili nilizungumze kwa kina. Leo tunazungumzia miradi mbalimbali, tukizungumzia hata suala la Stiegler’s Gorge na kwingineko. Nilifarijika sana mtaalam mmoja majuzi katika semina ile tulipokuwa tunazungumzia suala la Sera ya Taifa ya Misitu alipotuambia pasipo misitu hata suala la umeme tunaouhitaji hautokuwepo, habari ya Stiegler’s Gorge na kwingineko kwa sababu maji hayatapatikana. Hata tukizungumzia suala la utalii, lina uhusiano wa moja kwa moja na misitu kwa sababu kwa kupitia misitu kuna biodiversity ambayo hiyo moja kwa moja inakwenda na masuala ya ecosystem, tukikosea hapo iko shida kubwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nikuombe Mheshimiwa Waziri kwenye mipango yetu tuendelee kuboresha suala hilo la misitu. Leo mkizungumzia mipango yote, yawe ni mabwawa ama vitu vingine bila kujikita kwenye kuhifadhi misitu, tatizo ni kubwa, umeme hatutokuwa nao na wakati mwingine hata kilimo pia itakuwa shida na eneo hili naomba tuendelee kupewa elimu pana. Wakati mwingine ukiona miti imetunzwa sehemu, sio kwa sababu anatakiwa mnyama awe pale, ni kwa ajili ya kutengeneza biodiversity pamoja na ecosystem ambayo ina nafasi kubwa kwenye kumsaidia binadamu.