Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Lupa
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. VICTOR K. MWAMBALASWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Napenda nichukue nafasi hii nimpongeze Waziri wa Fedha na Mipango, Naibu Waziri na wataalam wote kwa kazi nzuri. Nia ya kuuleta Mpango hapa Bungeni ni kuujadili na kuuboresha ikiwezekana, kwa hiyo, sidhani kama kuna Mbunge yeyote ambaye anaudhihaki na kuukejeli, kazi yetu ni kuuboresha na kuujadili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama kuna Mbunge mwenzangu ambaye hajui tunu za Tanzania nataka nirudie mimi. Tunu za Tanzania ya kwanza ni lugha yetu ya Kiswahili, ya pili Muungano wetu, ya tatu ni utu na udugu wetu na ya nne ni amani na utulivu. Hizi tunu hazikuja Tanzania kwa bahati mbaya, viongozi/waasisi wetu walitumia nguvu na resources nyingi sana kuzi-inculcate kwa Watanzania na ndiyo maana Tanzania imekuwa mfano wa kuigwa duniani kwa sababu ya hizo tunu nne. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa zinapoanza kutokea kauli za kutugawa kwa majimbo na ukanda humu ndani zinasikitisha sana. Unajua sisi Wabunge ni viongozi na kiongozi kwenye jamii yoyote watu unaowaongoza wanapenda kuiga lile unalosema na unalotenda. Kwa hiyo, tunayoyasema humu watu wetu kule wataiga. Naomba Bunge lako hizi tunu nne tuzilinde kwa nguvu zetu zote, ahsante sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa niongelee kidogo Mpango aliouleta Mheshimiwa Mpango. Ameanza na miundombinu kwamba inasaidia kuchochea maendeleo kwenye nchi kama Tanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nije kwenye umeme. Nimeona miradi mingi ya kuongeza uzalishaji wa umeme kwa sababu umeme ni driver kubwa ya kuchochea maendeleo ya uchumi. Stiegler’s Gorge itazalisha megawati 2,100 ikikamilika, na source kubwa ya maji ya mto unaokwenda kulisha Stiegler’s Gauge ni Mto Ruaha. Ukiuona Mto Ruaha ulivyokuwa mwaka 2008 na ukiuona leo, inasikitisha.
Kwa hiyo, naiomba Serikali inapopanga kwenda kuweka mtambo wa kuzalisha umeme pale Stiegler’s Gorge iweke mpango kabambe sana wa kufanya conservation ya The Great Ruaha, vinginevyo tutakuwa hatuna maji ya kuzalisha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Tanzania tumejaliwa kuwa na vyanzo vingi vya umeme, wengine wamesema asubuhi jotoardhi, jua, upepo, naomba Serikali iangalie kote huko ili tuweze kuwa na umeme mwingi wa kutosheleza viwanda vyetu na umeme mwingi wa ku-export.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wenzetu wa China wameendelea mpaka kufika hapo walipo walikoanzia ni mbali sana. Kwanza walikuwa na revolution ya kilimo, lakini baadaye wakaona waanze viwanda vidogo vidogo, wakawapeleka vijana wao kwenda kusoma kokote kule nje kwa gharama yoyote na waliporudi kwa fani ile aliyosomea, walikopeshwa fedha na vifaa waende kufanya hiyo shughuli ambayo walisomea; hao ndio wameanzisha viwanda ambavyo sasa hivi China ina mabilionea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nadhani hata sisi, juzi Mheshimiwa Rais alikuwa Kagera, Kiwanda cha Kagera Sugar kinafanya vizuri sana; kimeajiri vijana wa Kitanzania wanafanya kazi pale. Serikali inaweza ikafanya vivyo hivyo, ikawachukua vijana wa Kitanzania waliosoma, kama ni kilimo, iwawezeshe, iwakopeshe, iwape ardhi waanzie kule tuwe na mapinduzi ya kilimo kwanza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nije kwenye maji, wenzangu wengi wamesema, miaka mitano, sita ijayo maji yatakuwa ni crisis sana duniani. Naomba Serikali ianzishe Wakala wa Maji Vijijini na Mijini kama ilivyo kwa Wakala wa Barabara, kama ilivyo kwa Wakala wa Umeme na kama ilivyo TANROADS. Ni muhimu sana Serikali ianzishe Wakala wa Maji Vijijini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika miundombinu ambayo nilikuwa nimesema, nije kwenye reli ya kati ya SGR, reli ya Tanga kwenda mpaka Musoma, reli ya kutoka Mtwara kwenda mpaka Liganga, lakini reli ya TAZARA ni reli ambayo tayari ni standard gauge, inahitaji kuboreshwa tu na kuwekewa umeme. Naomba Serikali iangalie sana reli hii kwa sababu nayo itaifungua nchi yetu kwa nchi ambazo zipo kusini mwa Tanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile reli hii itakuwa inapita kwenye dry port ambayo itaanza kujengwa pale Mbeya, kwa hiyo tunakuwa na block trains za kutoka Dar es Salaam kwenda Kigali na Bujumbura. Kutakuwa na block trains kutoka Dar es Salaam kwa reli ya TAZARA kwenda Mbeya, kwenda kuwasaidia wenzetu wa Zambia, wa Malawi na wa Zimbabwe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nirudie, tunu za Tanzania ni hizo nne nilizozisema, nimesema Muungano, Lugha ya Kiswahili, utu na udugu na amani na utulivu. Bunge lako lizienzi na kuzilinda tunu hizi kama mboni za macho yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. Ahsante sana.