Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CHADEMA
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. JOYCE B. SOKOMBI: Mheshimiwa Mwenyekiti, niane na sekta ya uvuvi.
Katika Mpango wa Maendeleo wa Taifa 2017/2018 kuhusu rasilimali za uvuvi, Serikali ilitenga shilingi bilioni 2.2, na shilingi milioni 400 tu kama fedha za ndani kwa ajili ya ukarabati wa miundombinu ya uvuvi pekee. Fedha hii ni ndogo sana ukilinganisha na matokeo tunayoyatarajia katika sekta ya uvuvi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli usiopingika kwamba Serikali hii ya Awamu ya Tano inataka kuwekeza kidogo huku ikitarajia matokeo makubwa sana. Sekta ya uvuvi ni sekta nyeti ambayo inachangia katika uchumi wa Taifa na pato la mtu mmoja mmoja katika maeneo mengi ya nchi yaliyozungukwa na maji. Jambo la kushangaza jamii za wavuvi zimekuwa ni jamii zinazoishi maisha duni sana pamoja na ugumu na changamoto nyingi wanazopitia wavuvi ikiwa ni pamoja na upatikanaji wa zana bora na za kisasa katika kufanya uvuvi wenye tija.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wavuvi wamekuwa wakitozwa kodi nyingi huku miundombinu ikibaki vilevile. Wavuvi wa Tanzania hususani wa Mkoa wa Mara wamekuwa wakinyanyasika kwenye kulipa tozo nyingi, hawana uhakika wa mikopo na pia usalama wa kutosha wawapo katika shughuli zao usiku.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nchi kama Norway imekua sana kiuchumi kwa kuwekeza katika sekta ya uvuvi pekee. Leo hii katika nchi za Ulaya, Norway ni nchi inayoongoza kwa kuwa na GDP kubwa ambapo sehemu kuwa ya Pato la Taifa hutokana na uvuvi tofauti na hapa nchini ambapo jamii ya wavuvi ndio jamii maskini wa kutupwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu usafiri wa anga, uwanja wa ndege wa Musoma, katika mpango huu wa maendeleo 2017/2018 hakuna mahali panapoonesha mkakati maalum wa ukarabati wa uwanja wa ndege wa Musoma. Ni dhahiri uwanja huu ni muhimu sana katika kukuza sekta ya utalii kwa Kanda ya Serengeti. Uwanja wa Ndege wa Musoma ni wa muhimu sana katika kuchochea ukuaji wa uchumi wa Kanda ya Ziwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na sababu za kiuchumi uwanja wa ndege wa Musoma ni muhimu katika historia ya ukombozi wa nchi yetu. Uwanja huu umebeba historia ya Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere. Hivyo ni muhimu kwa wageni wanaokuja nchini
kutembelea makazi ya Hayati Baba wa Taifa ambaye aliipigania ukombozi wa nchi hii kwa gharama kubwa sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo ni vema sasa Serikali ione umuhimu wa kuuweka uwanja huu katika vipaumbele vyake ikiwa ni pamoja na kuutengea fedha za kutosha na kukamilisha ukarabati kwa wakati kama vile ilivyofanya kwenye uwanja wa ndege wa Chato. Pamoja na hilo, uwanja huu utakuwa kichocheo kikubwa cha uchumi kwani hata shughuli za uchimbaji madini zinazofanyika Mkoani Mara zitaimarika zaidi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, bado naamini Mkoa wa Mara una wasafiri au watumiaji wengi wa ndege wanaofanya biashra katika maeneo mbalimbali ya ndani na nje ya nchi ikiwemo nchi jirani ya Kenya. Hivyo Serikali itueleze ni lini itakamilisha uboreshaji wa uwanja huu ili wananchi hawa waweze kunufaika. Naomba kuwasilisha.