Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Maswa Mashariki
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
NAIBU WAZIRI WA MADINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi ili na mimi kwa upande wa Serikali basi tuanze kutoa maelezo kwa upande huu.
Kwanza kabisa nipende kushukuru kwamba Waheshimiwa Wabunge wengi wametoa mawazo mengi tofauti katika kuchangia huu mpango wa mwaka. Mawazo ni mengi na nashukuru mawazo mengi ni mazuri lakini na mimi kwa kujikita kwa upande wa madini kulikuwa kuna mawazo machache kwa Wabunge ambayo waliyatoa hasa walijikita katika upande huu wa madini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo kabla sijajibu hoja hizo awali ya yote nichukue nafasi hii kumpongeza sana Mheshimiwa Rais kwa kazi nzuri anayoifanya. Tumeona anafanya mambo mengi ambayo kwa kweli yalikuwa hayana majibu, lakini kwa uwezo wake Mheshimiwa Rais na uzalendo wake ameonesha dhahiri kwamba ana nia thabiti na ya dhati kuhakikisha kwamba analinda rasilimali ya nchi yetu, anahakikisha kwamba rasilimali ya nchi yetu inakuwa na tija kwa uchumi wa nchi yetu. Kwa hilo Mheshimiwa Rais tunampongeza sana kwa kazi nzuri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile nichukue fursa hii kumshukuru Mheshimiwa Rais kwa kuanzisha hii Wizara mpya ya Madini. Wizara hii ilikuwa imeungana na Wizara ya Nishati na Madini na ukitazama ni kwamba tunatambua kwamba madini ni sekta nyeti, ni sekta ambayo ina mchango mkubwa katika uchumi wa nchi yetu. Hivyo Mheshimiwa Rais aliniteua mimi na Mheshimiwa Angellah Kairuki tuweze kuongoza Wizara hii lakini ukitazama kwa kina ni kwamba Mheshimiwa Rais alitaka tija katika Wizara hii ya Madini. Wizara hii imeundwa kwa maana ya kwamba tuongeze efficiency ya kusimamia rasilimali ya nchi yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunatambua mchango wa uchumi katika nchi yetu rasilimali ya madini ilikuwa inachangia kiwango kidogo sana, asilimia 3.7 lakini sasa hivi kwa juhudi zake Mheshimiwa Rais ni kwamba sekta ya madini inachangia zaidi ya asilimia 4.3 katika uchumi wa nchi yetu. Hivyo basi mimi na mwenzangu tuna kazi kubwa kwa kushirikiana na wataalam wa Wizara ya Madini kuhakikisha kwamba tunaongeza tija kupitia hii sekta ya madini kuhakikisha kwamba uchumi wetu unaimarika na tunakwenda kuimarisha uchumi kwa maana ya kwamba tunakwenda kupandisha kiwango hicho kilichopo cha asilimia 4.3 na kwenda mbele zaidi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tulikuwa na Sheria ya Madini ya mwaka 2010 na tumefanya mabadiliko yake ambayo ni ya mwaka 2017. Mabaadiliko haya ni makubwa lakini yalitazama sana katika sehemu nne ambazo ni muhimu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sehemu ya kwanza ilikuwa ni kuua ile Tanzania Mineral Auditing Agency (TMAA) na jambo la pili lilikuwa ni kuunda Tume ya Madini ambayo mpaka sasa kama Wizara tupo katika kufanya restructuring kwa maana ya kuitengeneza hii Tume na kuianzisha ili sasa Tume hii iweze kusimamia sekta ya madini inavyostahili, kwa maana ya kutoa leseni, kusimamia ku-regulate sheria na kanuni za masuala ya madini ili kusudi madini yetu yaweze kuongeza tija katika uchumi wa nchi yetu. Kwa hiyo, kwa muda mfupi ujao, nadhani hadi kufikia mwisho wa mwaka huu Tume hiyo itakuwa tayari na itakuwa imeanza kazi kuhakikisha kwamba inasimamia vizuri sekta hii ya madini na tuweze kupata tija kutokana na madini ambayo tunachimba nchini kwetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sehemu nyingine ya sheria hii ilikuwa ni sehemu ya kuongeza kodi ya royalty (mrabaha), kutoka asilimia nne kwenda asilimia sita na kutoka asilimia tano kwenda asilimia sita kwenye madini ya vito na madini ya metallic. Vilevile kuongeza gharama au kuongeza kodi ya clearance ambayo ni asilimia moja. Mchakato huu hata kabla ya kuanzisha Tume hiyo, umeshaanza, sasa hivi wachimbaji wanalipa royalty asilimia sita. Hii ni hatua kubwa, ni hatua nzuri ambayo itatuongezea kipato katika mrabaha na Serikali itaweza kuneemeka zaidi na madini haya tofauti na ilivyokuwa kipindi cha mwanzo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, haya ndiyo mambo ya mwanzo, naweza kusema ni utangulizi kwa ujumla wake. Ninapenda kusema na niwaeleze Watanzania kwamba, tunakwenda kudhibiti utoroshaji wa madini kwa kuunda Tume hii na marekebisho ya sheria. Tunakwenda kuhakikisha kwamba, madini yetu tena hayatoroshwi, hayapiti njia za panya, hayapiti njia zisizo sahihi, tunataka kwamba wachimbaji wote wapitie utaratibu unaostahili ili waweze kulipa kodi zote kwa TRA na vilevile waweze kulipa mrabaha ili Serikali iweze kupata kipato chake ambacho kinastahili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ushahidi umeonesha Mheshimiwa Rais, tarehe 20 Septemba, 2017 alipokuwa Mererani, alitoa amri ya kujenga ukuta unaozuia yale maeneo yote ya machimbo ya Tanzanite. Ujenzi huo umeanza toka tarehe Sita mwezi huu na ujenzi huo unakwenda kwa kasi ya hali ya juu. Jeshi letu la JKT liko site linafanya kazi ya construction na kwa hali iliyopo sasahivi ni kwamba, kuna wanajeshi pale wa kutoka JKT zaidi ya 2,000 na wanafanya kazi hiyo na wataifanya kazi hiyo kwa mkataba unavyosema, watafanya kazi ndani ya miezi sita na fedha za ujenzi wa ukuta huo wamekwishapewa asilimia 80. Kwa hiyo, tuna hakika kwamba ukuta ule utajengwa na tutadhibiti utoroshaji wa madini kutoka eneo la Mererani. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile Mheshimiwa Rais alitoa amri ya kwamba, tujenge mnada ambao utakuwa ni Mererani ambao mnada huu utatumika kwa watu wanaokuja kununua madini ya Tanzanite katika Mnada wa Mererani. Hapa tunavyozungumza pale Mererani tumeshapata eneo la EPZA ambalo shilingi bilioni 2.2 imetolewa kwa ajili ya ujenzi wa haraka wa mnada ule, ukishakamilika ujenzi ule kwa muda mfupi ujao, basi mnada ule utafunguliwa, madini ya Tanzanite, maonesho ya madini, wanunuzi watakuja pale watanunua na watalipa mrabaha, watalipa ili tuweze kupata kipato chetu kama kinavyostahili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika michango mbalimbali kuhusiana na utoroshaji wa madini hata sheria inasema, sasa hivi tuna wataalam wazuri, wathaminishaji wa madini yetu. Ukiangalia kwenye upande wa Almasi tuna wataalam wazuri, mfano mzuri ni juzi tu hawa Wiliamson Diamond Limited (WDL) waliweza kuzalisha Almasi. Almasi ile katika kutolewa kuisafirisha Serikali kwa juhudi zake ilikamata na kuangalia, kulinganisha uthaminishaji wa mwanzo na wa pili, tukakuta thamani ya Almasi zile ni kubwa, Serikali ikazuia uuzaji wa zile Almasi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, WDL waliendelea kuzalisha. Walizalisha tena carat 39,000 na zikathaminishwa kwa kiasi cha shilingi bilioni nane na wataalam wetu, lakini kupeleka Almasi ile kwenye soko la Almasi, soko la mnada la Antwerp, kwa mara ya kwanza tumeweza kuuza Almasi yetu kwa njia ya mnada kwa dola za Marekani bilioni 10. Hii ni hatua kubwa ambayo Serikali imechukua na ni ya kumpa moyo Mheshimiwa Rais kwa kazi kubwa anayoifanya. Kwa kweli hiyo ni hatua kubwa na Mheshimiwa Mwenyekiti na wewe ni shahidi unalielewa hili. Kwa kweli, utoroshaji wa Almasi ulikuwa ni wa hali ya juu, lakini kwa namna tunavyokwenda tunakwenda kudhibiti. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa taarifa yako katika ule mzigo wa pili uliokwenda kuuzwa kwa dola milioni 10, ndani ya almasi zile ilikuwepo almasi adimu ambayo inapatikana Tanzania ambayo tunasema inaitwa pink diamond, iliuzwa kwa dola milioni mbili, kipande kimoja tu chenye carat tano. Kwa hiyo, tunaweza tukaona kwamba, kumbe tulikuwa na pink diamonds nyingi ambazo zinakwenda bila kuwa recorded katika zile takwimu ambazo zilikuwa zinaandikwa, kwa hiyo, hiyo ni hatua kubwa tumeweza kufikia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, bado tunaendelea na hatua za ku-control utoroshaji wa madini. Juzi tumekamata kilo nne za dhahabu katika Bandari ya Zanzibar, tumezikamata dhahabu ambazo zina thamani ya milioni 500. Tunaendelea kuimarisha ulinzi mipakani kuhakikisha kwamba utoroshaji wa dhahabu unasimamishwa, lakini wakati huo huo Serikali ina juhudi ya kuanzisha minada mitano mikubwa ambayo itakuwa inauza dhahabu. Tutauza dhahabu kwa njia ya wazi ili watu waje wanunue dhahabu na waweze kulipa ushuru, waweze kulipa na mrabaha. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile minada yetu hii tunatakiwa tuitengenezee miundombinu mizuri kwa maana ya usalama, miundombinu ya umeme, miundombinu ya maji, miundombinu ya usafirishaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mjadala uliokuwa unaendelea watu wamepiga sana kelele kuhusu kutengeneza Uwanja wa Ndege Chato. Kule Chato tunahitaji usafirishaji wa madini yetu, tunahitaji kusafirisha watu, tunahitaji kusafirisha vifaa, uwanja wa ndege wa Chato ni muhimu sana kujenga pale Chato. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukienda pale Bulyanhulu wana uwanja wa ndege. Wale mabwana wamejenga uwanja wao wa ndege wa kuweza kusafirisha bidhaa zao, Kwa nini Serikali tusiwe na uwanja wetu? Kwa nini Serikali tusiweke uwanja wa kisasa wa kuweza kusafirisha bidhaa zetu za madini kupitia uwanja wa Chato? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, watu wameongelea kuhusu umbali wa kutoka Mwanza. Kutoka Mwanza hadi Geita ni kilometa 185, kutoka Geita kwenda Chato ni zaidi ya kilometa
120. Kwa hiyo ni kilometa 120 na hizo 180 ni zaidi ya kilometa 300 kutoka uwanja wa ndege wa Mwanza, hapa katikati usafirishaji wa dhahabu ni hatari sana kusafirisha dhahabu umbali wa zaidi ya kilometa 300.
Kwa hiyo, uwanja wa Chato ni muhimu kuuweka pale na hii ni kwa manufaa ya Watanzania wote na wala sio kwa manufaa ya watu wachache kama wenzetu walivyokuwa wakieleza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, naunga mkono hoja.