Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

Hon. Eng. Isack Aloyce Kamwelwe

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Katavi

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijalia afya njema na kunipa pumzi. Pili nimshukuru Mheshimiwa Rais, ameniamini miezi 23 katika nafasi ya Naibu Waziri, lakini baadae ameniamini zaidi na kunikabidhi nafasi ya Waziri wa Maji na Umwagiliaji. Ninamshukuru sana na ahadi yangu kwake na ahadi kwa wananchi wa Tanzania ni kwamba nitawatumikia kuhakikisha wanapata huduma ya maji safi na salama. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninampongeze sana Waziri wa Fedha, ndugu yangu Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango, kwa kuleta mpango mzuri huu ambao hauna maneno mengi, lakini ukiuangalia unatupeleka moja kwa moja kwenye uchumi wa kati ili tuhakikishe kwamba, wananchi wetu wanakuwa na maisha bora. Niwashukuru sana Waheshimiwa Wabunge kwa michango yenu ndani ya Wizara ya Maji na Umwagiliaji na michango hii yote kwetu ni dira, tutaifanyia kazi, tutashirikiana na ninyi na tunaomba muendelee kutu- support ili tuweze kutekeleza majukumu yaliyo mbele yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza ninayo michango ya kiujumla kwenye Wizara yangu ya Maji na Umwagiliaji na nianze na tatizo ambalo tumekuwanalo nab ado tunalo sasa hivi kuhusiana na utoaji wa huduma ya maji vijijini na mijini, hasa kupitia katika mamlaka. Tunazo mamlaka za aina tatu, tuna mamlaka ya daraja la tatu, mamlaka daraja la pili na mamlaka daraja la kwanza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, daraja la kwanza wanajihudumia kwa asilimia 100, ikiwa ni kulipa mishahara, kununua madawa na kulipa gharama za umeme. Madaraja ya pili na daraja la tatu ni kwamba madaraja haya inabidi yasaidiwe hasa katika kulipa bili za umeme. Daraja la pili linasaidiwa kwa asilimia 50, daraja la tatu linasaidiwa kwa asilimia 100.

Mheshimiwa Mwenyekiti, iko changamoto katika mamlaka hizi, zipo mamlaka ambazo zipo chini ya Wizara ya Maji na ambazo zipo chini ya Wizara ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tayari tulishakaa na Serikali tukayaainisha medeni na tukakubaliana kwamba Serikali sasa hivi inaendelea kutafuta fedha ili iweze kulipa madeni yote ya nyuma. Tumejipanga kuhakikisha kwamba hatuendelei kuzalisha deni jingine na ndio maana tumekuja na mfumo wa mita za LUKU upande wa maji ili tukishaiweka mwananchi unalipia ndio uweze kupata huduma ya maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mchango wangu katika hili, Waheshimiwa Wabunge na Serikali kwa ujumla ni kwamba sasa tunajadili mapendekezo ya maendeleo ya mwaka ujao wa fedha pamoja na mwongozo wa bajeti, Serikali tuhakikishe watu wote wanatenga bajeti kwa ajili ya kuzihudumia hizi mamlaka za daraja la tatu na daraja la pili ili mwaka ujao wa fedha tena isitokee kwamba mtu anakatiwa umeme kwa sababu hajalipa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, najua Nzega sasa hivi wamekatiwa na maeneo mengine pia lakini kama alivyosema Mheshimiwa Waziri wa Nishati kwamba tutakaa tuhakikishe kwamba wananchi hawa wanapata huduma ya maji. Changamoto ninayoipata ni kwamba umeme ukikatika, maji yakikosekana hatuangalii kwamba ni umeme linarudi kwa Waziri wa Maji na Umwagiliaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, niwaombe sana hasa Serikali tuhakikishe kila mtu kwenye Taasisi yake mwaka ujao wa fedha atenge bajeti kwa ajili ya kulipia gharama hizo za umeme.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kuweza kutekeleza azma ya kuhakikisha wananchi wa Tanzania wanapata maji safi na salama, bajeti ya mwaka 2006/2007 tulianzisha programu ya maendeleo ya sekta ya maji. Katika programu hiyo tulipanga kutekeleza miradi 1,810, hadi sasa kupitia progamu hiyo ya awamu ya kwanza ambayo ilikamilika mwezi Juni mwaka 2017, tumefanikiwa kutekeleza miradi 1,423, miradi iliyobaki ni miradi 378 lakini tunaendelea na utekelezaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, matokeo ya utekelezaji wa miradi hiyo, tumetengeneza vituo 117,000 vya kuchotea maji, kama vituo vyote vingetoa maji, sasa hivi tungekuwa na asilimia 78 ya upatikanaji wa maji safi na salama katika maeneo ya vijiji. Bahati mbaya sana kutokana na changamoto mbalimbali, asilimia 35 ya hivi vituo havitoi maji na matokeo yake sasa huduma ya maji inayopatikana kwa sasa ni asilimia 63.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kupitia bajeti ya mwaka huu wa fedha tulionao 2017/2018 Waheshimiwa Wabunge vile vitabu mlivyopewa kwenye bajeti za Halmashauri tumeweka kifungu cha fedha kwa ajili ya Halmashauri kuhakikisha kwamba wanarejesha huduma kwa kukafuta vyanzo vingine. Tumeweka incentives kwamba ukirejesha huduma ya kituo kutoa maji, unapata sterling pound 50 na ukiweka kituo kipya unapata sterling pound 1,500. Fedha mnazo zimeainishwa kwenye bajeti, kwa hiyo tujitahidi kuhakikisha kwamba tunarejesha hiyo huduma ambayo tumeweka vituo lakini vile vituo havitoi maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto ambayo imejitokeza mpaka hivyo vituo vikakosa kutoa maji hadi sasa tumebaini kuna changamoto za aina tatu. Kwanza ni wananchi kushindwa kuendesha miradi hasa miradi ambayo unakuta kwamba mradi umewekwa katika kijiji wakaweka jenereta ambayo inatumia diesel, wananchi wanafikia mahali wanashindwa kumudu gharama ya kununua mafuta na matokeo yake ni kwamba mradi ule upo lakini hautoi maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimekutana na mradi wa namna hiyo wakati wa ziara zangu nikiwa Manispaa ya Mji wa Singida nikakuta kuna mradi una vituo vya kuchotea maji zaidi ya 19, maji yapo lakini wamesitisha huduma kwa sababu mashine iliyowekwa ya kusukuma maji inatumia diesel na hawana uwezo wa kununua hiyo diesel, sasa hivi tumeelekeza kwamba miradi yote ambayo inatumia jenereta za diesel tuhakikishe kwamba tunaweka solar na ndio maana tuna bajeti.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilishangaa Manispaa hiyo bajeti ya mwaka 2016/2017 walikuwa na shilingi bilioni mbili lakini hawakutumia hata senti tano na bado walishindwa kununua umeme wa kutumia nguvu ya jua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto nyingine ni mabadiliko ya tabianchi na sisi wananchi kulima kwenye vyanzo vya maji, matokeo yake vyanzo vimekauka na miradi tuliyotekeleza tukiwa tunatarajia kwamba chanzo kitakuwa mahali fulani, maji hakuna na matokeo yake sasa maji hayatoki katika hiyo miradi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto ya tatu ni pamoja na usanifu mbaya, tumekutana na usanifu mbaya. Wataalam wanakwenda kusanifi kipindi cha mvua, kwa hiyo, kwa vyovyote maeneo yote unakuta yana maji, baada ya kiangazi lile eneo ulilobaini linakuwa halina maji. Kwa hiyo, sasa hivi tunasimamia kuhakikisha usanifu unafanyika wakati wa kiangazi ili chanzo kikipatikana kinakuwa na uhakika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hivi tumeanza awamu ya pili ambayo itakamilika mwaka 2020. Katika awamu hiyo, tunatarajia kutumia zaidi ya dola bilioni 3.3 na tunalenga kutengeneza miradi ya maji vijijini 4,015 na hadi sasa tayari tumeshasaini miradi 150 na tunaendelea vizuri kabisa. Hii ni miradi itakayotekelezwa katika vijiji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia tuna miradi zaidi ya 33 ambayo tunatarajia tuitekeleze miradi ambayo ni mikubwa. Miradi hii ni pamoja na mradi wa ujenzi wa bwawa la Kidunda, tuna mradi wa maji wa Mtwara Mikindani, tuna mradi wa usambazaji wa maji kutoka visiwa vya Kimbiji na Mpera na tuna miradi ya maji 17 katika miji 17 ambayo itafadhiliwa na mkopo nafuu kutoka Serikali ya India. Fedha hii imeshapatikana, taratibu za kukamilisha kusaini financial agreement ziko mbioni na wakati wowote ikishasainiwa basi tutaendelea na utekelezaji wa miradi hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia tuna mradi mkubwa wa maji utakaopeleka Wilaya zote za Simiyu, huu ni mradi mkubwa utakaotumia zaidi ya dola bilioni 300 na tender tumeshatangaza tayari. Kwa hiyo, tunasimamia kuhakikisha kwamba wananchi wanapata huduma ya maji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunao mradi tunaendelea na usanifu wa kutoa maji Mto Malagarasi kupeleka Tabora na kama tutaufanikisha mradi huu na maji yakawa mengi, tuna malengo ya kupanua huduma hii ili iweze kusambaa na mikoa mingine kama tulivyofanya maji ya kutoka Ziwa Victoria. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna mradi wa maji wa uondoaji wa majitaka katika Mji wa Dodoma nao pia tunaendelea nao kutafuta fedha. Pia tuna mradi wa maji kupeleka Mji wa Kisarawe na juzi meagiza ikifika mwezi wa tano mkataba wake uwe umeshasainiwa ili wananchi wa Kisarawe waweze kupata huduma ya majisafi na salama. Pia Kisarawe sasa hivi kuna eneo ambalo viwanda vinaendelea kujengwa na tayari tuna kiwanda cha cement pale kinafanya kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna mradi wa maji kwa ajili ya Mji wa Kilolo. Tuna mradi wa maji wa HTM nao pia taratibu zinaendelea…

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa Mzungumzaji