Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi kwa mwaka wa fedha 2016/2017.

Hon. Peter Joseph Serukamba

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kigoma Kaskazini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

3

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi kwa mwaka wa fedha 2016/2017.

MHE. PETER J. SERUKAMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nami nashukuru kwa kunipa nafasi kuchangia bajeti ya Wizara ya Kilimo. Leo ni mara yangu ya kwanza nachangia bajeti, naomba na mimi nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Rais kwa kazi kubwa anayofanya ya kurudisha nidhamu Serikalini. Nina hakika sasa tunaenda kwenye mstari ulionyooka na Taifa letu litaanza kushuhudia maendeleo kwa kasi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, niwashukuru wananchi wa Mkoa wa Kigoma hasa Kata ya Kigoma Kaskazini kwa heshima kubwa waliyonipa kunirudisha Bungeni kama Mbunge wao. Nina hakika sitawaangusha, ahsanteni sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ambalo napenda kuliongelea ni kahawa. Pale Kigoma Kaskazini tunalima kahawa hasa maeneo ya Kalinzi pamoja na Nyarubanda kwenda mpaka Buhigwe, Manyovu wanalima kahawa aina ya organic coffee. Zaidi ya wakulima 435 walichukuliwa kahawa yao, imepelekwa Kilimanjaro kwa ajili ya kubanguliwa mpaka leo hawajapata fedha zao. Nataka Waziri aje aniambie lini wananchi hawa watapata malipo yao hayo ambayo yamekaa muda mrefu sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili kwenye kahawa tatizo ni tozo. Kwenye mazao yetu tozo za wakulima ni kubwa sana na bei ya kahawa duniani imeshuka. Kwa hiyo, lazima Serikali tujipange kwa sababu bei hatuwezi ku-control lakini tozo tunaweza ku-control ili wakulima wetu waweze kupata mazao na waweze kulima na kufaidika. Kwa sababu nia yetu ni kuondoa umaskini, bei kwenye soko la kahawa hatuwezi kuisimamia kwa sababu ni suala la demand and supply, wenzetu Brazil wanaleta kahawa nyingi sana, namna ya kuwasaidia hawa wakulima wa Tanzania ni kupunguza tozo kwenye zao la kahawa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sekta ya kilimo inaendelea kushuka katika ukuaji. Mwaka 2015 kilimo kimeshuka kwa asilimia 2.3 ambapo mwaka 2014 ilikuwa asilimia 3.4 maana yake ni nini? Kama kilimo ambacho ndiyo kinabeba watu asilimia 75 ukuaji unashuka lazima tujiulize tunafanya nini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nimuombe sana Waziri tuanze na tukubali kwamba kwa asilimia 90 kilimo ni sayansi na sio juhudi. Kama ni juhudi mama yangu amelima toka nazaliwa kwa juhudi kila mwaka lakini hajawahi kujitosheleza kwenye chakula. Kama kilimo ni sayansi maana yake ni uwekezaji. Kuna Abuja declaration lazima asilimia 10 ya bajeti yetu iende kwenye kilimo kama tulivyokubaliana kwenye Azimio la Abuja. Naomba sana Waziri na Serikali tuende kule ambapo tulikubaliana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama kilimo ni sayansi tunahitaji uwekezaji, hatujapata fedha tunafanyaje kama Taifa. Lazima nimuombe Waziri tuanze sasa kuleta commercial farming in Tanzania. Tukileta commercial farming tunaunganisha na out growers. Tumeona Kilombero kuna baadhi ya maeneo unaona maisha ya watu yamebadilika kwa sababu kuna commercial farming pale na kuna wakulima wadogo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wale commercial farmer’s watakachofanya watakuja na mbegu zao, watafanya utafiti wenyewe, watatafuta wagani, hawatahitaji tuwape mbolea wala ruzuku. Kama Taifa ili tuweze kufanikiwa niombe sana tuhakikishe angalau kila mkoa tuwe na commercial farming kubwa ndiyo itawasaidia wakulima wetu wadogo wadogo. Tunaona kila mwaka tunaanza kuhangaika na mbolea na ruzuku umefika wakati wa kuleta commercial farming. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ili commercial farming Tanzania iweze kufanikiwa mambo mawili yafanyike, kwanza, ni umilikaji wa ardhi, lazima tuziangalie upya sheria zetu za ardhi. Pili, ni kuangalia namna ya kuwasaidia hawa wakulima kuweka incentive ili watu waende kwenye ukulima. Kwa sababu hiyo, tutaweza kupata malighafi kwa ajili ya viwanda vyetu. Commercial farming wataweza kufanya value addition, pia watatafuta masoko lakini tusipofanya yote haya tutasema tuna mavuno makubwa lakini wakulima wetu hayo mazao yao hawawezi kuuza popote. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la mkonge, sasa hivi duniani mkonge umepanda bei sana. Tani moja ya singa ya mkonge ni dola 2500, hata ukiondoa gharama za kuzalisha hiyo tani moja hazizidi dola 1,000 kuna faida zaidi ya dola 1,500. Leo watu wanakuja kununua mkonge shambani, wanalipa pesa in advance. Niiombe Serikali na Waziri wa Kilimo sasa hivi tuhangaike kuhakikisha kila shamba ambalo linaweza kulima mkonge tupande mkonge. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tukipanda mkonge tutapata fedha za kigeni, tutaajiri watu wengi sana kwenye kiliomo kwa sababu mkonge unahitaji watu wengi sana kwenye yale mashamba, lakini hauhitaji mvua, ni kitu rahisi kulima. Ukisoma hapa hotuba ya Wizara ya Kilimo suala la mkonge limetajwa paragraph moja tu wakati ndiyo zao ambalo leo lingeleta pesa nyingi kuliko zao lolote Tanzania. Zao la mkonge ukishaondoa singa yale yaliyobaki yote unaweza ukaanzisha viwanda vya kutengeneza tikira kwa ajili ya pombe, syrup kwa ajili ya wangonjwa wa sukari, kwa ajili ya umeme, kwa ajili ya mbolea haya yote yanawezekana kama tutajielekeza kwenye suala la mkonge. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niongelee mifugo, hapa ni masikitiko makubwa. Ukisoma hotuba ya Waziri katika mifugo anaongelea majosho, dawa, migogoro ya wakulima na wafugaji. Kama kuna jambo ambalo tukiamua kufanya tutabadilisha nchi hii kimaendeleo ni suala la mifugo. Mifugo tusiione ni dhambi. Leo hii ukitaka kujua thamani ya mifugo hebu fikirieni kama Taifa tungekuwa hatuna mifugo ingekuwaje? Leo ingekuwa Tanzania hakuna ng‟ombe, kuku wala mbuzi Taifa hili lingekuwaje, mngetumia mabilioni ya pesa kuagiza nyama duniani. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hii biashara ya nyama ili ziweze kufanikiwa naombeni kama Serikali tuanzishe National Abattoir kubwa na kama Serikali haiwezi tutafute private sector waanzishe National Abattoir kubwa ambayo kazi yake itakuwa ni kuchinja mifugo na kusambaza nyama nchini na kuuza nje ya nchi na kuchukua zile ngozi kuwapelekea wenye viwanda vya ngozi. Kazi nyingine wawepo watu katikati wafugaji ambao watafanya kazi ya kunenepesha ng‟ombe, hiyo ndiyo itakuwa kazi yao. Kwa kufanya hivyo chain ya biashara ya mifugo itakuwa kubwa sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la NFRA, kila mwaka tunatafuta kuongeza hela kwa ajili ya strategic reserve. Sasa imefika wakati tuanzishe private sector ambao na wao watanunua mazao ya wakulima wetu. Ikitokea leo mavuno ni wengi hakuna mnunuzi wa mahindi yao kwa sababu mnunuzi ni mmoja. Kwa hiyo, tutafute mtu mwingine ambaye anaweza akafanya biashara hiyo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho uvuvi, mnaenda mnawachomea nyavu wavuvi wetu wa Kigoma, Lake Victoria, Lake Nyasa, swali langu ni moja naomba Waziri atujibu nyavu hizo zinatoka wapi? Kwa nini nyavu hizo wasizizuie toka kiwandani? Nyavu zinazalishwa viwandani au zinakuwa imported wanauziwa wavuvi wetu ndiyo mnakwenda kuwakamata mnawachomea, hapana. Naomba Mheshimiwa Waziri mpige marufuku kuleta nyavu hizo, mpige marufuku kuzalishwa na hiyo ndio itaondoa suala hili la nyavu mbaya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho ni tumbaku, naomba tupunguze tozo kwenye zao hili. Pia wakulima wangu wa kule Matendo, Kidaghwe anayekuja kununua tumbaku ni mtu mmoja anapanga bei anayotaka matokeo yake wakulima wetu wanaendelea kuwa maskini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naomba nimalizie kwa kusema naunga mkono bajeti lakini naomba Serikali ijielekeze kwenye kuamini bila sayansi kilimo hakiwezi kuondoka hapa. Hata tukisema kilimo ndiyo uchumi, ni mgongo wa Taifa, mali ipo shambani kama huweki sayansi yatakuwa maneno matupu, hatuwezi kwenda tunakotakiwa kwenda. Zama hizi ni za mabadiliko, naombeni tubadilike, tuamini kulima ni sayansi, bila sayansi hatuwezi kwenda tunapotaka kwenda. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naomba kuunga mkono hoja.