Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Tanga Mjini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nami nianze kwa kumshukuru Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli, kwa kuniamini kusimamia sekta hii ya afya na maendeleo ya jamii, nimhakikishie Mheshimiwa Rais nitashirikiana na Mheshimiwa Dkt. Faustine Ndungulile, Naibu Waziri ili kuhakikisha Watanzania wanakuwa na afya njema na hivyo kuweza kushiriki katika kujiletea maendeleo yao na maendeleo ya Taifa kwa ujumla.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze sana Mheshimiwa Dkt. Mpango na Naibu Waziri kwa kazi nzuri wanayofanya katika eneo hili la uchumi na fedha lakini hasa kwa kuleta mapendekezo ya mpango wa maendeleo ya Taifa kwa mwaka 2018/2019.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niwashukuru sana Waheshimiwa Wabunge kwa maoni na ushauri walioutoa hasa katika kuboresha upatikanaji wa huduma za afya nchini, ikiwemo kujenga jamii ya Watanzania inayojali na kuheshimu haki, ustawi na maendeleo ya wanawake, wazee na watoto. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda sasa kujibu baadhi ya hoja za Waheshimiwa Wabunge lakini nitajikita sana kwa Dada yangu Mheshimiwa Susan Kiwanga. Niliposikiliza mchango wake nikasema hivi huyu amesoma huu mpango au amesoma hajauelewa? Kwa sababu anasema kwamba mipango yetu haizingatii mahitaji halisi ya Watanzania. Unasema hivi huyu anazungumzia Watanzania gani?
Mheshimiwa Mwenyekiti, najua Mheshimiwa Dkt. Mpango ataeleza uhusiano mkubwa sana kati ya ujenzi wa uchumi wa viwanda na maendeleo ya watu, ikiwemo kuboresha afya, ikiwemo elimu, ikiwemo vijana na kila kitu. Lakini nataka ni-summarize kwa kitu kimoja, maendeleo ya watu, maendeleo ya jamii, msingi wake mkubwa ni maendeleo ya kiuchumi. Dkt. Mpango na timu yako songeni mbele. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunajua Tanzania ya viwanda ndani ya huu mpango ni halisi. Maana nimesoma hotuba yao wanasema Tanzania ya viwanda uhalisia au ndoto? Ni uhalisia! Tunasonga mbele wame-panic ndiyo maana sasa wanatafuta sababu zisizo na maana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili ndiyo maana nasema amesoma? Ukiangalia ukurasa wa 51, Mheshimiwa Mpango na timu yake wanasema kufunganisha maendeleo ya viwanda na maendeleo ya watu, sasa niache nimuoneshe kwenye sekta ya afya, wananchi wa Mlimba wanataka nini. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi wa Mlimba hawataki bora huduma, wanataka huduma bora za afya. Mheshimiwa Mpango katika kitabu hiki anasema kwamba kuboresha upatikanaji wa dawa, vifaa na vifaa tiba. Huu ndiyo Mpango! Sasa namshangaa Mheshimiwa Susan Kiwanga, kabla ya Serikali ya Awamu ya Tano haijaingia madarakani Ifakara walikuwa na fedha za dawa shilingi milioni 19 tu, mwaka jana tumewapa shilingi milioni 120 za dawa, mwaka huu tunawapa shilingi milioni 164, halafu anasema Mpango huu haujazingatia mahitaji ya wananchi. Najiuliza, Dkt. Mpango mimi naunga mkono hoja kwa sababu najua hata huko Mlimba, Ifakara tutaongeza fedha zaidi ya hizi ambazo umeweka. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili unajiuliza anasema siyo vipaumbele vya Watanzania. Unajiuliza, Watanzania wanataka nini? Watanzania wanataka wote tutibiwe Muhimbili siyo nje ya nchi. Mheshimiwa Dkt. Mpango anatuonesha hapa kwamba ataboresha huduma za matibabu ya kibingwa. Ndiyo maana nimesema ni kuchanganyikiwa, wanaona tunasonga mbele. Nitoe mfano, Watanzania tutatibiwa Muhimbili, nataka kutoa mfano Hospitali ya Taifa ya Muhimbili pale ICU tumeongeza vitanda vya wagonjwa mahututi kutoka 21 mwaka 2015 hadi vitanda
75. Tumeongeza vyumba vya upasuaji Muhimbili kutoka vyumba 13 hadi vyumba 20. Watu walikuwa wanasubiri miaka miwili kufanyiwa upasuaji. Sasa hivi watu wanasubiri miezi minne na tunategemea kushusha. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, upasuaji wa watoto, Muhimbili walikuwa wanafanya upasuaji wa watoto 15 kwa wiki, sasa hivi wanawafanyia watoto 50 kwa wiki. Mheshimiwa Dkt. Mpango anasema haya ni mapendekezo, nataka kuboresha huduma za matibabu ya kibingwa. Sasa unasema mpango huu haujazingatia mahitaji halisi ya wanananchi. Unajiuliza hivi huyu kweli anazungumza anachokijua kweli? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kutoa mfano mwingine. Watanzania wanataka nini kama nilivyosema?
Watanzania wanataka wote wapate huduma za matibabu ya kibingwa. Tumeanza, kuna wazazi wana watoto wana matatizo ya kutosikia, Muhimbili leo wamepandikiza vifaa vya kusikia cochlear implants, Mtanzania gani wa kawaida ataweza kutumia shilingi milioni 80 mpaka shilingi milioni 100 kwenda China? Lakini Muhimbili watapata Watanzania wote!
Mheshimiwa Mwenyekiti, habari njema, wasiwe wanasema tu, habari njema ni kwamba kabla ya tarehe 30 Desemba, tunaanza upandikizaji wa figo. Watanzania wanataka kuona huduma za matibabu ya kibingwa wote wanapata na siyo wenye fedha, huduma hizi zitapatikana nchini, Dkt. Mpango hongera sana nakuunga mkono kwa mpango huu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nani alikuwa anafahamu upasuaji lazima watu wapelekwe India? Jakaya Kikwete Cardiac Institute ilikuwa inapasua mgonjwa mmoja kwa siku, leo wagonjwa watatu kwa siku. Watanzania wote wanapata huduma hizi. Haya mambo ni kuanzia mwaka 2016 mpaka leo ndani ya miaka miwili mambo makubwa sana yamefanyika katika kuboresha sekta ya afya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo nilikuwa nasema hivi huyu anasoma nini? Watanzania wengi wanapata matatizo ya saratani. Zamani unaenda pale Ocean Road, wana vitanda 40 tu kwa ajili ya huduma ya saratani ya maji (chemotherapy) leo kuna vitanda 100, wagonjwa 100 wanatibiwa kwa wakati mmoja. Mheshimiwa Dkt. Mpango nashukuru kwamba tunaenda kununua kifaa kinaitwa PET scan kwa ajili ya tiba ya uchunguzi na uchunguzi wa matibabu ya saratani. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa nashangaa hivi huyu, lakini ninamshukuru sana kaka yangu Mheshimiwa Bobali ametoa mchango mzuri, jamani wagonjwa wengi wa saratani wanaongezeka. Mna mpango gani wa kuongeza elimu? Huu ndiyo mchango ambao ninauona una lengo la kujenga. Siyo mchango wa kusema hakuna vipaumbele. Kaka yangu Bobali nakushukuru sana. Nataka kukuhakikishia tutaendelea kutoa elimu juu ya wananchi kujikinga na saratani na tulichokifanya sasa hivi, tumeongeza pia vituo vya kuwezesha hasa wanawake kwa sababu saratani kubwa inayoongoza ni saratani ya mlango wa kizazi kwa asilimia 34 na saratani ya matiti asilimia 12. Kwa hiyo, Serikali ya Awamu ya Tano imeongeza vituo vya kuwezesha wananchi kupima kutoka 343 hadi 443, haya ndiyo wanayotaka Watanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimalizie jambo la mwisho, anazungumzia afya ya mama na mtoto wananchi wanakufa, tunajua. Lakini hivi ukijenga tu majengo ndiyo watu watapona? Sisi tumejikita kwenye kuboresha kwanza huduma. Tumesema kama kweli hiki ni kituo cha afya tunakitaka kiwe kituo cha afya na ndiyo maana kupitia Awamu ya Tano, wakati Mheshimiwa Dkt. Magufuli hajaingia madarakani, vituo vya afya 500 vya Serikali ni 109 tu vinavyotoa huduma za uzazi za dharura ikiwemo upasuaji. Mwaka wa pili wa Magufuli tunaongeza vituo 170 na Waheshimiwa Wabunge mmepata barua. Hii ndiyo tunataka, lakini kwa nini wanawake wanakufa? Kwa sababu pia wanavuja damu, wana upungufu wa damu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Dkt. Mpango anatuambia anataka kuongeza upatikanaji wa dawa na chanjo. Sasa hivi chanjo, dawa za uzazi salama (Oxytoxin) kwa ajili ya kuzuia mwanamke kuvuja damu magnesium sulphate kwa ajili ya kuzuia kifafa cha mimba na phehol kwa ajili ya kuongeza damu zinatolewa bure! Hii ndiyo wananchi wa Mlimba wanataka. Najua Mheshimiwa Jafo ataongelea ujenzi wa zahanati na vituo vya afya, lakini sisi tumejikita hizo huduma zilizokuwepo ziwe ni huduma bora siyo bora huduma. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, anasema siyo vipaumbele vya wananchi. Labda Dada yangu Mheshimiwa Susan Kiwanga wewe na familia mna hela, lakini Watanzania nikikutwa HIV positive nianze dawa mara moja. Tumeanza Sera ya Test and Treat. Mtanzania yeyote atakayepima na
kukutwa na maambukizi ya virusi vya UKIMWI anapata dawa siku hiyo hiyo tunamwanzishia, halafu anasema Mpango huu haujazingatiwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, namaliza la mwisho, Mheshimiwa Susan Kiwanga; TB kabla Mheshimiwa Magufuli hajaingia madarakani kulikuwa na kituo kimoja tu cha kutoa matibabu ya TB sugu, Kibong’oto Hospital. Leo tuna vituo 18 ikiwemo Ifakara, ikiwemo Ifakara kituo cha Kibaoni. Halafu mtu anauliza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri wa Fedha Dkt. Mpango nakuunga mkono kaka yangu, Naibu Waziri na wataalam wote wa sekta ya fedha. Endeleeni, mkisikia watu wanasema sema wame-panic kwa sababu wanajua Tanzania ya viwanda inafikiwa. Kwangu tukifikia Tanzania ya viwanda najua maendeleo ya sekta ya afya yanafikiwa na Watanzania watakuwa na afya bora na ustawi na hivyo kushiriki katika kujiletea maendeleo yao na maendeleo ya Taifa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru sana.