Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi kwa mwaka wa fedha 2016/2017.

Hon. Joseph George Kakunda

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Sikonge

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi kwa mwaka wa fedha 2016/2017.

MHE. JOSEPH G. KAKUNDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. Napenda nichukue nafasi hii kuwashukuru sana wananchi wa Sikonge kwa kunipa heshma ya kuwawakilisha kwenye chombo hiki muhimu sana katika nchi yetu.
Pili, napenda kumshukuru sana Rais, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli kwa hatua ambazo anazichukua sasa hivi ambazo zimesaidia sana nchi yetu kuweza kurudi kwenye mstari. Naamini kwamba sasa hizi bajeti ambazo tunazipitisha hapa zote sasa zitakuwa zinafika kwenye utekelezaji. Kwa hiyo, naamini mambo mengi mazuri yanakuja. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, la tatu ambalo napenda nishukuru ni hatua ambazo Serikali na Menejimenti ya Bunge imezichukua hadi sasa ambazo zimezidi kuongeza heshima ya Bunge. Yale mambo ambayo yalikuwa yanatokea siku za nyuma yamepungua sana hata wewe mwenyewe ni shahidi. Michango ya Wabunge imezidi kuwa ni ile yenye maana kwa wananchi badala ya kuwa na mambo ambayo hayana maana yoyote. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza sana Mheshimiwa Waziri kwa hotuba yake ameiwasilisha vizuri lakini nampongeza kwa kazi zake ambazo amekuwa akizifanya katika nchi yetu ya Tanzania kwa ajili ya kuinua na kuwasaidia wakulima na wafugaji. Nakupongeza sana Mheshimiwa Mwigulu, nakupa moyo endelea kuchapa kazi na Mungu atakulinda na sisi Watanzania tutakulinda. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nianze kuchangia kuhusu wakulima. Wakulima wa Tanzania hasa wa Sikonge wanajitahidi sana kulima zao la tumbaku, kilimo cha tumbaku ni cha jasho jingi lakini wamekuwa wakikatishwa tamaa na wajanja. Kama ambavyo utaona kwenye hotuba ya Mheshimiwa Waziri ukurasa wa 23 badala ya uzalishaji kuongezeka unapungua ni kwa sababu ya kukatishwa tamaa na wajanja. Naomba sana Mheshimiwa Waziri awadhibiti hawa ili wasiendelee kumnyanyasa na kumnyonya mkulima ili hatimaye uzalishaji uongezeke na Taifa lizidi kupata manufaa kupitia kilimo cha tumbaku. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wajanja hao nitawataja wachache, kuna viongozi wa vyama vya msingi wasio makini na wasio waadilifu, kuna maafisa ushirika ambao sio waadilifu na kuna maofisa wa benki ambao sio waadilifu. Watu hawa wamekuwa wakishirikiana kwa utatu huo katika baadhi ya maeneo kuwadhulumu wakulima na kumsababishia mkulima madeni na mengine ni madeni hewa. Hadi sasa katika Mkoa wa Tabora asilimia 52 ya vyama vyetu vya msingi havikopesheki kwa sababu ya madeni. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu ya muda, naomba niende moja kwa moja kwenye kupendekeza hatua au kushauri hatua za kuchukua. Pamoja na kwamba hotuba ya Mheshimiwa Waziri imetueleza hapa pembejeo sasa zitapatikana kama soda inavyopatikana dukani, lakini najua kwamba utaratibu huo utachukua muda mrefu, hautakuwa ni utaratibu wa kuja siku moja tu, hapana. Kwa hiyo, naomba sana hatua za makusudi zichukuliwe ili kusudi haya masuala ya kumfanya mkulima na chama chake cha msingi ndiyo kuwa mkopaji kwenye mabenki wakati mkulima elimu yake ni ndogo sana kuhusu masuala ya mikopo, naomba sana mkulima aondolewe huo mzingo wa kukopa badala yake kampuni ndiyo ikope halafu impatie pembejeo mkulima. Hiyo ndiyo itasaidia kuondoa mzigo kwa wakulima wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la pili naomba sana Serikali idhibiti wizi au udanganyifu unaofanywa na baadhi ya wajanja kumuibia mkulima kupitia exchange rate. Leo dola inaweza ikawa shilingi 2,200 lakini mkulima ataambiwa ni shilingi 1,800, hapo anakuwa ameibiwa shilingi 400 au ataambiwa dola ni shilingi 2000 hapo atakuwa ameibiwa shilingi 200. Kwa sababu mkulima hana utaalamu anakuwa ameibiwa fedha nyingi sana kupitia njia hizi. Naomba sana Serikali ichukue hatua kudhibiti wizi unaofanyika kupitia thamani ya ubadilishaji wa fedha kutoka dola kwenda kwenye shilingi yetu ya Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, la tatu, naomba sana Serikali isiendelee kujiweka pembeni kwenye suala la kupanga bei ya tumbaku. Najua Sheria ya Tumbaku imesema Serikali ijiweke pembeni iwaachie sijui Baraza la Tumbaku, kule kuna wajanja ambao ni makampuni, hao ndiyo ajenda yao wakiileta huwa inapitishwa vilevile kama ilivyoletwa. Bila Serikali kuingilia kati mkulima atabaki kunyanyasika kupitia bei ndogo sana ya tumbaku. Mbona kwenye sukari mnapanga bei? Kwenye sukari mbona mnajishirikisha kusema kilo ya sukari ni shilingi kadhaa, kwa nini kwenye bei ya tumbaku mnasema tunawaachia wakulima wenyewe matokeo yake wakulima hawawezi kupambana na wajanja. Naomba sana Serikali iwe makini katika suala hilo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, la nne ni kuhusu mbolea, ninapendekeza Serikali iongeze uratibu wake wa uingizaji wa mbolea kutoka nje. Utaratibu wa sasa wa kuingiza mbolea pale bandarini halafu ndiyo inaanza kusambazwa nchini kutoka bandarini pale unamsababishia mkulima gharama kubwa. Kwa sababu bei ambayo wana-charge wasafirishaji kutoka bandarini hadi mkulima anapoipata inakuwa kubwa mno badala yake napendekeza vianzishwe vituo maalum vya kupokeleana mbolea mikoani. Kwa mfano, Tabora pale unaweza ukajenga warehouse kubwa ikapokelewa mbolea yote ya Mikoa ya Tabora, Kahama na baadhi ya maeneo ya Kigoma halafu kutoka hapo kwenda kwa mkulima bei itakuwa ndogo kuliko kusafirisha mbolea kutoka Dar es Salaam. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, la tano ni makato kwenye sekta ya tumbaku yamekuwa makubwa mno na mengi hayakubaliki. Waziri Mkuu alipokuwa anatoa hotuba yake alizungumzia kuondoa au kupunguza makato kwenye zao la korosho. Naomba sana dhana aliyoitumia Mheshimiwa Waziri Mkuu kupunguza makato kwenye zao la korosho hiyo hiyo itumike kupunguza makato kwenye zao la tumbaku. (Makofi)
Mhesimiwa Mwenyekiti, kuna makato mengi, kwa mfano, mkulima ameuza tumbaku yake kwenye ghala lakini anakatwa fedha ya kusafirishia tumbaku kutoka kwenye ghala mpaka kwenye kiwanda Morogoro, ni kwa sababu gani? Kama mimi nikinunua cement Dar es Salaam hivi yule mwenye duka la cement niliponunua atalipia gharama za kusafirisha cement kwenda kwangu Tabora? Naomba hapo tubadilike na Serikali iwe makini. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, makato ya APEX ambayo yalishafutwa bado mkulima anakatwa. Shilingi milioni 575 za mwaka jana zipo lakini sasa hivi wamezipangia matumizi kwamba hizo fedha badala ya kumrudishia mkulima wanataka wazitumie watu wa Wizara ya Kilimo eti kwa ajili ya kuja kutoa mafunzo. Kwa nini Serikali itumie fedha za mkulima kuja kutoa mafunzo, Serikali si imeweka bajeti na tulishawapa! Naomba sana fedha hizo warudishiwe wakulima wenyewe kama walivyokatwa. Pia kuna makato ya kuchangia union na kuchangia gharama za utafiti nayo yaondolewe kwa sababu utafiti ni kazi ya Serikali. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nina mawili kwa wakulima, naomba sana kilimo cha mkataba kirejeshwe, wakulima wanataka sana kilimo cha mkataba. Kama ni pembejeo wapewe na mnunuzi, hiyo itasaidia kuondoa mambo ya riba ambayo wanakabiliana nayo kwenye masuala ya kukopa benki.
MHE. JOSEPH G. KAKUNDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana, naunga mkono hoja.