Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi kwa mwaka wa fedha 2016/2017.

Hon. Juma Selemani Nkamia

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Chemba

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi kwa mwaka wa fedha 2016/2017.

MHE. JUMA S. NKAMIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nami nakushukuru kwa kunipa nafasi hii ili niweze kuchangia hotuba hii ya bajeti ya Mheshimiwa Waziri wa Kilimo. Kwanza nimshukuru Mwenyezi Mungu Subhanahu Wataala kwa kuwa salama.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nina mambo makubwa matano. Kwanza, nimshukuru Mheshimiwa Waziri kwa kumpongeza yeye binafsi na Naibu wake mtani wangu pale Mheshimiwa Ole-Nasha na wataalam wote wa Wizara hii kwa kazi nzuri wanayoifanya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, niwashukuru sana wakulima wote wa Wilaya ya Chemba na Mkoa mzima wa Dodoma kwa juhudi wanazozifanya kujikwamua pale walipo na kusonga mbele. Tuna migogoro kidogo ya ardhi kwa wakulima wetu. Kuna mgogoro ambao sasa umedumu kwa takribani miaka 11 kati ya Kiteto, Kondoa na Chemba. Mheshimiwa Waziri nikuombe tu kama umeweza kwenda kukutana na wafugaji kutana pia na wakulima na siyo kukutana nao tu bila kuwa na strategic plans za kuondoa matatizo hayo. Ningeomba sana jambo hili ulizingatie kwa kina sana. Tumekuwa na matatizo haya siyo kule Kiteto tu hata kule Lahoda ambako ni jirani sana na anapotoka Mheshimiwa Waziri, hebu tushughulikie matatizo haya yaishe. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, la tatu ni masoko ya wakulima. Mwaka 2011 Benki ya CRDB ilitaka sana kuwainua wakulima wa alizeti katika Mkoa wa Dodoma, Iringa, Manyara na Singida. Ilifanikiwa hata kutoa mikopo kwa baadhi ya watu ili waweze kupandisha bei ya alizeti. Kutokana na mfumo wa Serikali kuruhusu mafuta ghafi kutoka nje yaingie Tanzania bei ya alizeti ikashuka, hata hao wakulima wa alizeti wakapoteza mwelekeo na hata wale ambao walikuwa wanafanya biashara hii ya kuwanyanyua wakulima na wao wakaingia hasara ikiwa ni pamoja na benki na wale waliokopa na wafanyabiashara wengi wameingia kwenye madeni bila sababu ya msingi na yote haya yamesababishwa na Serikali. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Rwanda pale na Uganda, wameongeza kodi ya mafuta ghafi kutoka nje kwa lengo la ku-boost kilimo cha mazao yao ambayo yanazalisha mafuta. Let us be serious, tufanye jambo hili kwa nia njema ya kuwasaidia wakulima wetu. Mheshimiwa Waziri bahati nzuri unatoka Singida, wazalishaji wakubwa sana wa alizeti ni Dodoma, Iringa, Manyara, Arusha na kwingineko lakini bado Serikali imeruhusu uagizaji wa mafuta kutoka nje tena kwa watu wachache ambao leo ndiyo wanasababisha matatizo makubwa kwa wakulima wetu halafu tunakaa tunalalamika. Nilidhani hili jambo lazima tuwe serious sana, sisi tunashauri tu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mifugo, Dar es Salaam imejaa watu sana lakini tumefikia hatua sasa na mifugo nayo angalau iende ikaangalie Jiji kabla ya kupelekwa kwenye machinjio. Magazeti yanaweza kufika Mbeya au Mwanza saa 12 asubuhi nyama inashindwaje kufika Dar es Salaam tunapeleka ng‟ombe mzima? Kama gazeti linachapishwa Dar es Salaam saa 12 unalisoma Mbeya, unashindwaje kupata figo ya ng‟ombe iliyochinjwa Shinyanga ikapatikana Dar es Salaam asubuhi? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza mimi nashangaa, Wizara ya Kilimo inakuaje na Makao Makuu yake Dar es Salaam, hameni, mnakaa pale kufanya nini? Hameni tu, nendeni Arusha, nendeni Shinyanga, nendeni Mwanza hata Dodoma.
MHE. JUMA S. NKAMIA: Hata Geita nendeni, hata Bukene sawa, hata Chemba njooni.
Kwa hiyo, mimi nadhani upo umuhimu wa Serikali kuwa serious na jambo hili. Tafuteni utaratibu wa kuwa na viwanda vya nyama katika mikoa ambayo ina wanyama wengi hasa ng‟ombe. Ukipita barabara hii magari yanayosafirisha ng‟ombe kwenda Dar es Salaam masaa 12/13 what is that? Mimi sijaona duniani ng‟ombe na wao wanakwenda kuangalia Jiji ni Tanzania peke yake. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilitaka nizungumzie kidogo Maafisa Ugani. Maafisa Ugani wengi waliopelekwa na Serikali vijijini wameajiriwa kwa ajili ya kupata kazi lakini hawafanyi kazi yao. Mbunge leo anaweza kufanya ziara kwenye kijiji fulani anaambatana na Afisa Ugani wananchi hawamjui, anafanya nini? Kwa Kiswahili rahisi ni kwamba hapa mtu kapata kazi siyo kazi imepata mtu. Hebu waangalieni hawa, zaidi ya kwenda kupima nyama asubuhi anachukua figo anaenda nyumbani hana kazi nyingine. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine nilitaka kuzungumzia Wizara kwa kushirikiana na TAMISEMI mwezi wa tatu mwishoni mwishoni hivi wakati mvua zinaishaisha ilisaidia Mkoa wa Dodoma hela kidogo kama shilingi milioni 10 kwa ajili ya kununua mbegu za mihogo na mbegu za ule mtama mfupi. Hivi mlitaka wakulima hawa wapande mihogo ile ife au ule mtama usifike ili keshokutwa mseme mmepata njaa hatuwezi kuwaletea chakula kwa sababu tuliwapa mbegu? Unawezaje kupeleka mbegu wakati msimu umeisha? Hebu niambie kule Chemba unawapelekea mbegu mvua imeisha, kule Mvumi kwa Lusinde umewapelekea mbegu mvua imeisha, watafanya nini? Let us be serious! Mtu anakaa ofisini Dar es Salaam hajui hata mvua inaisha lini Dodoma anasema pelekeni milioni 10 hizi wakanunue mbegu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikuombe Mheshimiwa Mwigulu, mimi nakujua wewe ni mchapakazi mzuri sana na mimi nakupenda tu kama rafiki yangu na ndugu yangu, pamoja na juhudi zote unazofanya za kukutana na wakulima na wafugaji, kukutana nao peke yake siyo solution. Mnaweza mkakutana mkapiga soga, mkamaliza na wakafurahi sana kwamba atatekeleza, ukipeleka kwa wataalam wako hawashughulikii jambo hili. Kesho na keshokutwa atakayepoteza umaarufu ni wewe na siyo wale wataalam wako. Pamoja na kukutana nao chukua hatua, shirikiana vizuri sana na TAMISEMI. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, siku ya kwanza hapa nilisema tuna-problem kidogo katika mfumo wetu, huu mfumo wa kugatua madaraka. Leo huyu Afisa Ugani aliyeko kule huna mamlaka naye yuko chini ya TAMISEMI, chini ya Mkurugenzi, Mkurugenzi huna mamlaka naye wewe. So let’s get somewhere the government should sit down and see hivi mfumo wa ugatuaji wa madaraka huu kweli umetusaidia? Lazima tuu-review, nchi zingine zinafanya hivyo kwani ku-review kuna dhambi gani? Tu-review ili tuone umuhimu wake, kama tunaona kuna mahali pamekwenda ndivyo sivyo turekebishe. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho kabisa ni bei za mazao ya wakulima. Mwaka jana wakulima wa Mkoa wa Dodoma waliouza mahindi NFRA wengi walikopwa na walichelewa sana kulipwa. Naomba mwaka huu Serikali iwasaidie wakulima hawa, alhamdulilah wamebahatisha mahindi na alizeti kidogo basi tukichukua mazao yao tuwalipe kwa wakati.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini nakupongeza pia kwa kwenda Kondoa kule japo Chemba ulipita tu kwenda kuangalia ndege iliyokuwa inamwagia ndege dawa, ahsante sana. Nakushukuru sana kwa sababu hata Chemba wale ndege japo waliendelea kutuumiza kidogo lakini wengine waliohamia Kondoa walikufa, ahsante sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikuombe hasa kwenye alizeti hebu kuwa very serious, tafuteni altenative ya kujenga viwanda iwe Singida hata Dodoma sisi hatuna tatizo. Tukiwa na kiwanda hapa naamini alizeti inayozalishwa central corridor hii inaweza kusaidia sana nchi yetu ya Tanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kuyasema haya na mimi naunga mkono hoja, ahsanteni sana.