Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Mtwara Vijijini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. HAWA A. GHASIA – MWENYEKITI WA KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE YA BAJETI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue fursa hii kukushukuru kwa kunipa nafasi ya kuweza kutolea ufafanuzi hoja mbalimbali ambazo zimetolewa na Waheshimiwa Wabunge, ambao baadhi yao wamezileta kwa maandishi idadi yao ni nane na baadhi yao wametoa kwa kuzungumza ambao idadi yao inafikia 14 ikiwa na pamoja Waheshimiwa Mawaziri na Manaibu Mawaziri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa tuna tatizo la muda, naomba niende moja kwa moja katika hoja ambazo zimezungumzwa. Nianze na Mheshimiwa Riziki Lulida ambaye amezungumzia uwepo wa rasilimali na akaomba kwamba Serikali izisimamie rasilimali hizo ili kuhakikisha kwamba zinaleta tija katika Taifa letu. Nakubaliana naye na sina haja ya kuendelea kuijadili hoja hiyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Riziki Lulida pia aligusia pia suala la zao la korosho haswa akijikita katika eneo la uhujumu wa zao hilo, kwa kile kitendo ambacho korosho zetu zilizokwenda Vietnam kugundulika kuwa na mawe na masuala mengine. Mheshimiwa Naibu Waziri, Dkt. Mary Mwanjelwa amelitolea ufafanuzi lakini bado tunaendelea kusisitiza, naungana na Mheshimiwa Riziki Lulida kwamba bado Serikali inatakiwa ichukue hatua mbalimbali kuhakikisha kwamba suala hilo halijotokezi tena.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sisi ambao tunatoka katika maeneo ya korosho tunaona kitendo hiki kama hujuma kwa wale wanunuzi wapya ambao wamejitokeza katika zao hili na kuwezesha kupandisha bei na hata kufikia Sh. 4,000/= kwa kilo. Kwa sababu wapo ambao walikuwa wananufaika na bei zile za chini ambazo zilikuwa zinawanyonya wakulima.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tunahisi kuongezeka kwa bei za korosho ambako kumechangiwa kwa kiasi kikubwa na uwepo wa wanunuzi kutoka nchi za Vietnam, Uturuki na China kunaweza kukawa ni sababu ya kuwafanyia hizi hujuma ili kuwakatisha tamaa wasiweze kuja kununua korosho zetu na hivyo kushusha bei za korosho.
(Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tunasisitiza suala la kuchukua hatua thabiti kwa wale waliohusika lakini pia kama Serikali iwekeze kwa kujenga maghala ambayo yataweza kuhakikisha kwamba muuzaji wa korosho anavyopeleka pale, tukiwa na maghala yanayokubalika, kwa utaratibu wa ununuzi wa korosho huwa zinamwagwa na hivyo kuhakikisha kwamba zinakaguliwa kabla ya kusafirishwa kwenda kule kwa wanunuzi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia tukiwa na viwanda ambapo wale wawekezaji watakuja kubangua hapa hayo masuala mengine nadhani yataweza kuthibitiwa. Pia kwa upande wa Mkoa wa Mtwara, ilishapendekezwa kwamba korosho zote zinazozalishwa Mtwara na Lindi zitumie bandari ya Mtwara ili kuweza kudhibiti suala hili la kuziharibu korosho zetu zikiwa njiani zikielekea bandari ya Dar es Salaam.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hizi korosho ambazo zimeonekana kuwa na mawe, baada ya kuzifuatilia ni zile korosho ambazo zimesafirishwa kupitia bandari ya Dar es Salaam. Kwa hiyo, tunarudia tena kusema kwamba hatua sahihi zichukuliwe kwa wale wote waliohusika kuharibu ubora wa korosho zetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mzungumzaji wa pili ni Mheshimwa Balozi Diodorus Kamala ambaye aliomba suala la 10% kwenye mafuta ya kula kutoka nje liendelee na pia kusaidia sekta ya ngozi kama ambavyo wenzetu Ethiopia wanavyofanya. Tunaungana naye mkono hakuna haja ya kubishana naye. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mzungumzaji mwingine ambaye alichangia kuhusu Kamati yetu ni Mheshimiwa Lolesia Bukwimba ambaye alisisitiza suala la Serikali kulipa madeni yote ya ndani na pia kufanyia marekebisho Sheria ya Manunuzi na pia kuziwezesha taasisi kimitaji ili ziweze kutekeleza majukumu yake. Naungana naye mkono katika hilo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia Mheshimiwa Jitu Soni aliiomba Serikali kufanya tathmini ya gharama za uzalishaji ikiwemo tozo zinazotozwa na Mamlaka zetu za Udhibiti nadhani Mheshimiwa Waziri amelijibu, kwa hiyo, sina haja ya kulirudia. Pia mifumo ya malipo iendelee kuimarishwa ambalo pia Kamati tumelishalisema.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa David Silinde alizungumzia suala la urahisi wa ufanyaji wa biashara na uwekezaji. Pia alizungumzia kwamba tumeporomoka katika maeneo saba. Katika taarifa yangu nilisema tunaipongeza TAMISEMI pamoja na Wizara ya Ardhi, walikuja na maeneo ambayo yamewasababishia kuporomoka na wakaja pia na mikakati thabiti waliyoiweka na ambayo sisi kama Kamati tuliridhika. Bado tunaendelea kuisisitiza Wizara ya Viwanda na Biashara kuweka mikakati thabiti.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na kwamba Mheshimiwa Waziri amesema kwamba wanayo Blue Print lakini Blue Print ni maandishi yaliyopo na tumekuwa nayo muda mrefu. Tunaomba hiyo Blue Print ifanyiwe kazi kuhakikisha inaleta tija. Kwa hiyo, nimwombe shemeji yangu Mheshimiwa Mwijage apunguze maneno aongeze vitendo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Janet Mbene alizungumzia suala la magogo kutoka Congo na pia tupate mikakati ya kuinua uchumi wetu na pia pongezi ambazo alizitoa kwenye Mfuko ya Kahawa katika kuondoa tozo za Kahawa na pia kupendekeza tozo zingine ambazo zitawalenga wakulima wetu. Mheshimiwa Mwenyekiti, naungana naye sana kwa hayo aliyozungumza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Tanzanite yetu inasafirishwa kwa wingi na nchi jirani lakini sisi nchi jirani zikitaka kuleta biashara zao kama magogo au korosho kutoka Mozambique kuleta Tanzania wauze huku kwetu tunakuwa na vikwazo vingi. Kwa hiyo, tuiombe Serikali iondoe vikwazo, hivi korosho ya kutoka Kaskazini Mozambique ikiuzwa Mtwara na Mtwara ndiyo wakasafirisha kwenda nje, kuna tatizo gani?
Magogo kutoka Congo yakisafirishwa kupitia bandari ya Tanzania au yakiuzwa Tanzania kuna tatizo gani? Kwa hiyo, tuangalie uwezekano wa kuondoa hivyo vikwazo ili tuweze kusonga mbele. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Hussein Bashe alitoa mapendekezo yake na pia alisisitiza suala la viwanda vyetu pia kuoanishwa na sekta ya kilimo ambayo inaajiri kwa kiasi kikubwa Watanzania. Tunaomba Serikali hilo ilifanyie kazi. Pia aliongelea kuweka vivutio ambavyo vitasaidia viwanda vilivyoko nje kuja kuwekwa huku ndani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Halima Mdee alizungumzia suala la kunyang’anya vyanzo vya mapato vya Halmashauri na kwamba pesa nyingi zilizoenda katika Halmashauri zimeenda kulipa madeni. Serikali eneo hili imelijibia lakini pia tukumbuke tunavyoandaa bajeti zetu huwa tunaweka na bajeti ya kulipa madeni na wazabuni. Kwa hiyo, sioni tatizo tukisema kwamba pesa zilizokwenda zimeenda kulipa madeni zaidi kwa sababu bajeti pia ilikuwa inasema hivyo hivyo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niungane na Mheshimiwa Sixtus Mapunda kwamba ATCL itazamwe na iwezeshwe, tusiangalie tu suala kwamba inaleta faida kiasi gani kwa maana ya pesa ile ya kuiona moja kwa moja, hapana, tuangalie faida za ujumla. Kwa kweli ATCL ina mchango mkubwa sana katika kuinua uchumi wetu na hasa katika sekta za utalii lakini pia hata kuharakisha usafirishaji na kuwezesha uwekezaji katika nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia niungane na wale wanaosema kwamba tuziangalie taasisi zile ambazo zina mwingiliano ili kuondoa kero za kikodi na zisizo za kikodi kama vile TFDA na TBS ikiwezekana iunganishwe na iwe taasisi moja ambayo inatoa huduma zote hizo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niwashukuru Waheshimiwa Mawaziri, Mheshimiwa Dkt. Mary Mwanjelwa kwa zile ahadi alizoahidi tunaomba basi ziharakishwe na hatua zichukuliwe.
Mheshimiwa Ashantu Kijaji, tunakubaliana naye, sina haja ya kurudia kule lakini nirudie kwa Mheshimiwa Waziri wa Viwanda na Biashara. Mheshimiwa Rais alishatoa maelekezo kwamba viwanda vyote vilivyobinafsishwa na ambavyo havifanyi kazi yake iliyokusudiwa virudishwe mara moja. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, viwanda vya korosho karibu vyote, vingi viliuzwa kwa milioni 50 na vingine waliouziwa hawakutoa hata senti tano. Sasa hivi viwanda vile vimegeuzwa kuwa maghala wanawakodisha wakulima kwa kuhifadhi korosho zao mle ndani. Nimwombe Mheshimiwa Charles Mwijage, Waziri wa Viwanda na Biashara atekeleze agizo la Mheshimiwa Rais, la kuhakikisha viwanda vile ambavyo vilibinafsishwa kwa bei nafuu zaidi ambapo wale wawekezaji wameacha kufanya yale majukumu ambayo waliagizwa basi vinarejeshwa kama Mheshimiwa Rais alivyoagiza. Kama Rais alimeshaagiza kigugumizi ni cha nini ndugu zangu? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niombe tena kwa wenzetu Wizara ya Fedha waangalie zile tozo ambazo wamepunguza lakini kama zipo tozo ambazo wanaziona ni kwa manufaa ya nchi yetu na Serikali yetu basi pia tuendelee kuzipunguza ili kuhakikisha kwamba tunaweka mazingira bora ya kufanyia biashara na kuvutia uwekezaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nirejee tena kukushukuru wewe kwa kunipa nafasi kuja kutoa ufafanuzi katika hoja zile ambazo zimechangiwa na Waheshimiwa Wabunge na pia niishukuru sana Kamati yangu ya Bajeti kwa kazi kubwa ambayo tumeifanya katika kipindi chote cha uhai wa Kamati. Niishukuru pia Sekretarieti, nimshukuru Katibu wa Bunge kwa kuiwezesha Kamati.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naomba kutoa hoja sasa kwamba mapendekezo yote yaliyotolewa na Kamati yakubaliwe ili yaweze kutekelezwa na Serikali iyafanyie kazi pia na Bunge.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kutoa hoja.