Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mvomero
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. SULEIMAN A. SADDIQ – MWENYEKITI WA KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE YA VIWANDA, BIASHARA NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru tena kwa kunipa nafasi kwa mara nyingine niweze kuhitimisha hoja ya Kamati ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira.
Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote, naomba niwashukuru sana wachangiaji wote waliochangia hoja hii, wale ambao wamechangia kwa maandishi na wale ambao wamechangia kwa kuzungumza Bungeni. Waliochangia kwa kuzungumza Bungeni ni wanane na naomba kwa haraka haraka niwatambue, Mheshimiwa Lulida, Mheshimiwa Kamala, Mheshimiwa Jitu, Mheshimiwa Kuchauka, Mheshimiwa Janet Mbene, Mheshimiwa Silinde, Mheshimiwa Hussein Bashe na Mheshimiwa Livingstone Lusinde.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wale ambao wamechangia kwa maandishi ni 11, naomba nao niwatambue; Mheshimiwa Pascal Haonga, Mheshimiwa Zainabu Amiri, Mheshimiwa Rhoda Edward Kunchela, Mheshimiwa Nuru Bafadhili, Mheshimiwa Tunza Issa Malapo, Mheshimiwa Oran Njeza, Mheshimiwa Mary Deo Muro, Mheshimiwa Lucy Owenya, Mheshimiwa Lucia Michael Mlowe, Mheshimiwa Suzana Chogisasi na Mheshimiwa Juma Othman Hija. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeamua niwatambue hawa kwa sababu wengi wamezungumza hoja ambazo zinafananafanana, wale ambao wameleta kwa maandishi na wale ambao wamezungumza hapa Bungeni. Pia naomba niwashukuru sana Waheshimiwa Mawaziri kwa ufafanuzi wa hoja mbalimbali. Naomba niwashukuru sana Mheshimiwa Waziri January Makamba, Mheshimiwa Mwijage na Mheshimiwa Dkt. Mpango, nawashukuru sana kwa ufafanuzi wa hoja mbalimbali. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja nyingi ambazo zimezungumzwa ziko katika maeneo tofauti tofauti. Kuna hoja ambayo imezungumzwa sana na Wabunge wengi ni kuhusu Mamlaka nyingi za Udhibiti. Wabunge wametoa michango yao, wametoa ushauri wao lakini na sisi kama Kamati tulishayaeleza haya na ni matumaini yetu kwamba Serikali itayafanyia kazi haya masuala ili kupunguza utitiri huu wa mamlaka na kuleta utaratibu mzuri wa uzalishaji katika viwanda na biashara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumezitaja zile mamlaka zote ambazo zinaingiliana katika usimamizi wa viwanda, mfano OSHA, NEMC, TFDA, TBS na wengine wengi. Kwa hiyo, ni hoja ambazo zimekuja lakini na sisi kama Kamati tulishapendekeza nini kifanyike, ni matumaini yetu Serikali itakuwa imepokea. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kulikuwa na suala lingine la ubinafsishaji wa viwanda. Katika hotuba yangu ukurasa wa 33 na 63 tumelizungumza kwa kina. Viwanda ambavyo taarifa tumeletewa kwenye Kamati viko 156 vimebinafsishwa na Serikali inaendelea kuvifanyia kazi vile viwanda lakini Wabunge wameeleza kwa masikitiko makubwa na wengine wamediriki kusema kwamba hatua kali zichukuliwe kwa wale ambao wamepewa viwanda vile lakini havizalishi, Serikali imekosa mapato kwa kipindi chote cha miaka ambayo viwanda vile vimebinafsishwa. Viwanda vingi vimebinafsishwa kati ya mwaka 1997, 1998, 1999 mpaka 2000, utaona ni miaka mingi sasa Serikali imepoteza mapato mengi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika eneo hili wapo Wabunge wamesema kwamba hatua ambazo zitachukuliwa ni pamoja na kulipa kodi kwa miaka yote ambayo viwanda vile havikufanya kazi. Wapo Wabunge wameshauri kwamba lipo suala la viwanda hivi vilivyobinafsishwa, wawekezaji wale wamechukua hati wamezipeleka benki, wamekopa na matokeo yake hati zile zimekaa benki lakini viwanda vile havikupata fedha zile, fedha zimeingia kwenye biashara zingine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, haya ni mambo ambayo Kamati ilishayapendekeza, ni matumaini yangu kwamba Serikali itayafanyia kazi. Mheshimiwa Waziri amejibu kwamba hili jambo lipo katika hatua za utekelezaji, Kamati inasisitiza utekelezaji ufanyike kwa haraka. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lipo suala la Mradi wa Kurasini (Kurasini Business Park), Kamati imezungumza muda mrefu na Mheshimiwa Waziri amelijibu. Ni matumaini yetu kwamba jambo hili sasa litashughulikiwa kwa uharaka mkubwa ili eneo lile sasa lianze kuzalisha Watanzania wapate ajira, Serikali ipate mapato.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo limezungumzwa na Wabunge wengi ni suala la Kiwanda cha General Tyre. General Tyre ya Arusha Kamati tumeizungumza sana, tumetoa ushauri wetu, Serikali imesikia na leo hoja hii imejibiwa ni matumaini sasa msukumo mkubwa utaanza. Nimwombe Mheshimiwa Waziri wa Fedha, katika hili la General Tyre na yeye aweke mkono wake kwani Wizara ya Viwanda peke yake hawataweza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nimuombe sana Mheshimiwa Waziri wa Fedha suala la General Tyre liwe ni suala la umoja wote Wizara ya Fedha, Wizara ya Viwanda na Wizara nyingine tushirikiane. Zipo hatua ambazo zimechukuliwa na tunaomba Serikali iandae mazingira rafiki ya uwekezaji katika General Tyre. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, limezungumzwa suala la bidhaa feki za pombe na sticker fake, hili limepokelewa na Kamati yetu na Serikali itakuwa imelisikia, imelipokea litafanyiwa kazi. Eneo hili linapoteza sana mapato. Bidhaa feki kwanza zinaharibu afya za Watanzania, lakini pia Serikali inakosa mapato. Hili limechukuliwa na litafanyiwa kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini lipo suala la TBS na TFDA, Wabunge wamelizungumza sana. Naomba niseme kwa kifupi sana, TBS wao kazi yao ni bidhaa za viwandani, TFDA wao kazi yao ni bidhaa ambazo zinakwenda moja kwa moja kwenye madawa na vyakula. Kwa hiyo, pale kuna utaratibu tofauti kabisa, sasa wanapoingiliana wale hatujui ni kwa nini wanaingiliana. Kila mmoja ana eneo lake, kuna bidhaa za madawa na bidhaa za chakula na yule ana bidhaa za viwandani. Tunaomba Mamlaka hizi zipewe eneo la mipaka ya kazi ili kupunguza urasimu ambao wafanyabiashara wanaulalamikia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nilipongeze suala la umeme. Leo asubuhi tumezungumza kwamba Mkoa wa Tanga, Mkoa wa Morogoro walikuwa wana ration ya umeme, wanaambiwa viwanda vizalishe usiku na mchana wasizalishe. Kwa taarifa niliyoipata leo kupitia kwa Waziri kwamba lile zoezi lilikuwa ni la muda, ukarabati umeshafanyika, sasa hivi viwanda vinazalisha usiku na mchana. Hili nalipongeza sana Serikali na Mheshimiwa Waziri nakupongeza sana kwa kutatua tatizo hili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala la Wakala wa Vipimo, Wabunge wameshauri Wakala huyu ashuke chini ili mazao ambayo yanakwenda sokoni wale wakulima na wazalishaji wapate haki yao ya vipimo. Vipimo viende sambamba na uzalishaji. Tunaiomba Serikali ilifanyie kazi hili na Wakala huyu aongeze nguvu katika eneo hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lipo suala limezungumzwa la utitiri wa kodi. Suala hili nimwombe sana Mheshimiwa Waziri wa Fedha, Kamati yetu kupitia CTI ambayo walikuja wametuletea orodha ndefu ya utitiri wa kodi. Kodi nyingine zinarudiarudia, wafanyabiashara wanapata shida na wakati mwingine wanapata matatizo jinsi ya kulipa zile kodi. Tunaomba Serikali ilifikirie jambo hili na wafike mahali waanze kukaa na Kamati ya Bajeti, Kamati ya Viwanda na Kamati zingine ili walifanyie kazi kwa ndani zaidi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, liko suala la mifuko ya plastiki, nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri January Makamba amelisemea vizuri na Kamati imependekeza lazima tufike mahali sasa mifuko ya plastiki iwe basi. Kamati katika eneo hili imependekeza Wizara itafute namna nyingine, tupate viwanda mbadala.
Mheshimiwa Mwenyekiti, bidhaa zingine zinazobebwa zinahitaji mifuko, kwa hiyo, Wizara iharakishe kutafuta viwanda mbadala au wenye viwanda hivyo ambavyo wapo wapewe teknolojia ambayo itawasaidia kuzalisha mifuko mbadala ikiwemo mifuko ya karatasi, nguo, majani na mifuko mingine ili tunapoondoa mifuko tuweke mifuko mbadala. Kamati imependekeza hilo, ni matumaini yetu Wizara imesikia na Wizara ya Viwanda nao watakuwa wamelisikia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ambalo tunapenda sana kuliunga mkono ni suala la uchafuzi wa mazingira. Kuna viwanda kwa makusudi wanachafua mazingira kwa kutumia Tanzania ya Viwanda. Hii dhana hii wanaitumia vibaya. Tunaomba Wizara hii, Ofisi ya Makamu wa Rais Mazingira kazeni buti wale wanaochafua mazingira sheria ichukue mkondo wake. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, yamezungumzwa mengi na sisi tunasema tumeyapokea kama Kamati lakini Kamati nayo asubuhi wakati tunawasilisha taarifa yetu tulitoa maoni na mapendekezo yetu. Naomba Waheshimiwa Wabunge mapendekezo yetu yale tutayachukua pamoja na ya kwenu mliyotuletea leo kwa maandishi pamoja na kwa kuzungumza tutayachanganya pamoja ili tuyapeleke katika taasisi zinazohusika yafanyiwe kazi kwa faida ya nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, bila ya kuchelewesha muda, naomba sasa nikushukuru wewe, niwashukuru Mawaziri wote waliochangia, lakini pia niwashukuru sana Wajumbe wa Kamati yangu kwa jinsi ambavyo tumekwenda pamoja katika suala hili. Maoni yetu ya mwisho na maazimio yetu, wawekezaji wawe wakweli kwa Taifa lao. Wawekezaji watoe taarifa sahihi Serikali iweze kuwasaidia na walipe kodi Serikali iweze kuwasaidia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi kama Kamati tunawashauri wawekezaji wawe wakweli kwa Serikali, watoe taarifa sahihi na sisi kama Kamati tutawalinda na tutawasaidia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini ombi letu la pili tunaomba Watanzania wapende bidhaa za Tanzania. Unapopenda bidhaa za Tanzania, unaunga mkono juhudi za Serikali ya Tanzania ya Viwanda lakini tunamuunga mkono Mheshimiwa Rais wetu. Kwa hiyo, tunaomba Watanzania wapende bidhaa za Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho, naomba Serikali iendelee kuboresha mazingira mazuri kwa wafanyabiashara, mazingira rafiki kwa wafanyabiashara. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naomba sasa nihitimishe hoja yangu kwa kuwaahidi kwamba Kamati yetu imeyapokea masuala mbalimbali na yale ambayo tumeyatoa asubuhi pamoja na haya ya jioni ya leo tutayafanyia kazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sasa kutoa hoja, mapendekezo yote ya Kamati yapokelewe na yafanyiwe kazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kutoa hoja.