Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CUF
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. KIZA H. MAYEYE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Napenda nikushukuru kwa kunipa nafasi hii ya leo. Nikiwa kama Mwanakamati wa Kamati ya Nishati na Madini, napenda kuipongeza Kamati ya Nishati na Madini kwa kazi nzuri ambayo wameifanya. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nianze kuongelea suala la TANESCO. TANESCO ni taasisi ambayo tunaitegemea katika nchi yetu, lakini imeshindwa kufanya kazi yake ipasavyo kwa sababu ya haya madeni. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niongelee suala la Kigoma. Mpaka leo mikoa hii ya Magharibi ambayo ni Katavi, Kigoma, tunatumia umeme wa dizeli ambao kwa namna moja ama nyingine unasababisha hasara kubwa kwa Serikali yetu. Sasa naiomba Serikali ijitahidi kadri inavyoweza, kwa sababu tayari wameanza mpango huu wa Gridi ya Taifa, basi mikoa hii ya Magharibi, Kigoma na Katavi tuweze kuingia katika Gridi ya Taifa haraka inavyowezekana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pia niongelee suala la wachimbaji wadogo wa madini. Wachimbaji wadogo wengi wa madini ni vijana wa Kitanzania ambao wengi wameamua kujishughulisha wasiingie katika wizi na wafanye kazi. Naiomba sasa Serikali iwasaidie vijana hawa, iwasaidie elimu, iwasaidie vifaa. Leo tumeona vijana wengi wamekuwa wakifunikwa na vifusi katika migodi kwa sababu hawana uelewa wanapoingia kule chini. Kwa hiyo, naiomba Serikali ijitahidi kadri inavyoweza itoe elimu kwa vijana hawa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine niongelee kuhusu REA. Naipongeza sana Serikali, pamoja na kufanya kazi vizuri katika REA II lakini kuna changamoto ambazo zimejitokeza. Naomba wanapokwenda katika REA III wajitahidi changamoto zile zisirudie. Kwa sababu tumeona vijiji vingine umeme unapita barabarani, lakini hauendi katika hospitali na shule. Umeme unakwenda Kijiji ‘A,’ lakini unaruka unakwenda Kijiji ‘C’, Kijiji ‘B’ kinakosa umeme. Kwa hiyo, naiomba sana Serikali, pamoja na kazi nzuri ambayo wanafanya katika Mradi huu wa REA, REA III iende vizuri na vijiji vyote vipate umeme. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niongelee suala la Chuo hiki cha Madini cha MRI. Tunahitaji wasomi ambao wamebobea katika suala zima la madini. Leo Tanzania tunatengeneza Tanzanite, lakini Tanzanite hii ambayo tukiipeleka katika Soko la Dunia ambayo imechachuliwa hapa Tanzania, inaonekana haina hadhi sawa na ile ya India au South Africa. Naiomba sasa Serikali iwasomeshe watu, iwapeleke nje, wakapate ujuzi ili kesho Tanzanite yetu hii ionekane sawa na ile ya India au ya South Africa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho kabisa, Waswahili wanasema mnyonge, mnyongeni haki yake mpeni. Nampongeza Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuweka ukuta huu Mererani ambao unalinda madini yetu ya Tanzanite yasiweze kuibiwa. Leo madini yetu hayataweza kuibiwa, yatatoka na yatapelekwa moja kwa moja kwa asilimia 100 na hakuna wezi ambao watapitisha tena haya madini kwa njia ya chocho. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, naomba kuunga mkono hoja. Ahsante.