Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Newala Vijijini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. AJALI R. AKBAR: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nachukua nafasi hii kukushukuru wewe kwa kunipa nafasi hii. Mchango wangu umegawanyika katika maeneo mawili. Kama hoja za Kamati zilivyozungumza, maana yake Mawaziri wanashauriwa kwamba miundombinu ifanye kazi kufuata utaratibu ule ambao kwa kweli unashauriwa na Kamati, nashauri miundombinu ishirikiane na Wizara nyingine. Kwa sababu leo TCRA haitaki kushirikiana na Halmashauri ambazo zipo huko Wilayani.
Mheshimiwa Naibu Spika, kama tunavyofahamu kwamba sasa hivi tunaenda kwenye bajeti, Halmashauri nyingi zinakuwa hazina mapato, lakini minara ya simu ipo katika Halmashauri zote, lakini Service Levy inakuwa hailipwi katika Halmashauri husika. Kwa hiyo, naomba Wizara ishinikize TCRA itoe takwimu ambazo ni sahihi ili Halmashauri ipate kutoza Service Levy. Kwa sababu leo minara ya simu inalipa Service Levy bila kuwa na habari, lakini TCRA ina uwezo wa kujua kwamba ni simu kiasi gani zinakuwa zinaingia kwa kila mnara.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri atakapokuja hapa atueleze, je, kulipa Service Levy ni sheria au mtu analipa kwa hiari yake? Kwa sababu kuna baadhi ya makampuni hayalipi kabisa na mengine yanalipa kwa kiwango kidogo sana. Kwa hiyo, Wizara ya Miundombinu iishinikize TCRA isaidie Halmashauri ili Halmashauri iweze kutoza ule ushuru kutegemeana na simu ambazo tunazitumia kutoka hayo maeneo ambayo yapo.
Mheshimiwa Naibu Spika, la pili, kama vile ambavyo nimezungumza kwamba Wizara ishirikiane na Wizara nyingine, vilevile tumezungumzia hapa kuhusu Wizara ya miundombinu. Ukiangalia sana kwa mfano kule Mtwara, leo ni eneo ambalo kwa kiasi kikubwa sana wanalima korosho. Kwa asilimia karibu 70 ya export ya korosho inalimwa Mtwara, lakini ukienda kuangalia kule, zile barabara zote za Kitangali, Mtopwa, Luagala na Nanyamba, zimebaki mashimo. Mapato yetu ya Export Levy, kwa mfano mwaka huu tumepata shilingi bilioni 140 na hizo fedha huwa zinapatikana kila mwaka. Hizo fedha asilimia 65 zinakwenda kule kwa ajili ya kuboresha zao la korosho, lakini zile barabara haziboreshwi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, tuangalie uwezekano wa miundombinu kwa kushirikiana na Wizara ya Kilimo kuona ni namna gani zile fedha ambazo zinapatikana zinakwenda kuboresha zile barabara ambazo zinahusiana na mambo ya kilimo.
Mheshimiwa Naibu Spika, haiwezekani leo zile fedha zote ambazo ni asilimia 65 zinaondoka halafu asilimia 35 zinakwenda katika Mfuko Mkuu. Nasema kwamba kama kila mwaka tungeamua sisi Mtwara tutumie tu Export Levy, basi barabara zote za Mtwara zingekuwa na lami. Sasa sisi hatutaki lami, tunataka angalau kifusi kiwepo katika zile barabara ambazo zinatumika na ambapo magari makubwa yanakuwa yanapita kule.
Mheshimiwa Naibu Spika, namwomba sana Mheshimiwa Waziri kwamba katika bajeti yake inayokuja, basi ashirikiane na Wizara ya Kilimo na Wizara ya Kilimo vilevile iangalie uwezekano, ni namna gani watajitoa kusaidia zile barabara zao? Wasiangalie tu kupata zile fedha asilimia 35 ambazo zinakwenda kwenye Mfuko Mkuu na asilimia 65 ambazo zinaenda kwenye Bodi. Waangalie namna gani wananchi wananufaika kwa barabara zao kuwa bora? Isiwe kama maeneo ambayo wanachimba madini, watu wanachukua yale madini wanaondoka halafu wanaacha mashimo. Namwomba sana Mheshimiwa Waziri afanye jitihada za kushirikisha maeneo yote hayo mawili. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, suala la tatu nizungumzie kuhusu REA. Mtwara ni eneo ambapo gesi inatoka kwa wingi sana, lakini mpaka leo kuna tatizo kubwa sana la umeme. Okay, sisi hatuna shida kuhusu umeme, lakini hawa wananchi wana shida ya maji. Leo maji ule umeme unaopatikana Mtwara, hauwezi kusukuma maji kwa kiwango kikubwa. Kwa hiyo, namwomba sana Mheshimiwa Waziri ule umeme uliopo Mtwara hautoshi, achukue hatua za dharura ili ahakikishe kwamba ananunua mashine za dharura ili tuweze kupata maji. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hivi leo hii huwezi kupata malalamiko ya maji kwa kuwa mvua zinanyesha. Itakapofikia mwezi wa tatu it is a crisis, itakuwa ni war. Asitake Waheshimiwa Wabunge wa Mtwara, Nachingwea au Lindi tuje tuombe hapa chini ya dharura, kwa sababu itakuwa ni tatizo kubwa sana kupita kiasi. Kama gesi ipo Mtwara, inawezekana vipi umeme ukosekane? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nachukua nafasi hii kumwomba sana Mheshimiwa Waziri afanye jitihada zote za kuleta mashine mpya za gesi aende akafunge katika station ya Mtwara. Nakuomba sana Mheshimiwa Waziri.
Mheshimiwa Naibu Spika, huo ndiyo ulikuwa mchango wangu wa leo. Ahsanteni sana na naunga mkono hoja.