Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mufindi Kusini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. MENDRAD L. KIGOLA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa kunipa nafasi hii ili nami niweze kutoa mchango kwenye Kamati hizi mbili; Kamati ya Miundombinu na Kamati ya Nishati na Madini.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa, nianze kutoa pongezi nyingi sana kwa Serikali. Kuna watu wengine wamekuwa wanachangia; kwanza, nimesikitika sana kwa sababu kuna kitabu hapa ambacho ni taarifa ya Kamati.
Mheshimiwa Naibu Spika, ukienda ukurasa wa 12 kuna kipengele kidogo, wameeleza vizuri Serikali imefanya nini? Imeeleza vizuri kabisa, kwamba katika miundombinu; ukichukua kipengele kimoja, sitaki nichukue vitu vingi, kwa mfano pale kwenye ujenzi wa reli na tulishaongea ili nchi iweze kusonga mbele, uchumi wa Taifa ukue ni lazima tuhakikishe kwamba tumeimarisha usafiri wa reli. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hapa nilikuwa nasoma kwamba Serikali katika mipango yake mizito kuna ujenzi wa reli wa Dar es Salaam – Morogoro kilometa 205; kuna ujenzi wa reli kutoka Morogoro – Makutupora kilometa 336; kuna ujenzi wa reli Makutupora – Tabora kilometa 295; kuna Tabora – Isaka, kilometa 133; kuna Isaka – Mwanza, kilometa 250; halafu mtu mwingine anasema haoni. Jamani, hayo ni maendeleo makubwa sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ndugu zangu Waheshimiwa Wabunge, tukitaka uchumi wa nchi uendelee lazima Serikali ijikite kwenye miundombinu ya reli ili tuweze kusafirisha mizigo mizito kwenye reli zetu na barabara za lami tuweze kusafirisha mabasi yetu na magari madogo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tulishasema ndani ya Bunge hili, Serikali imefanya mambo mengi sana na tunayaona kwa macho. Nami kama Mbunge, naiunga mkono Serikali na iendelee na mikakati mizuri. Tunategemea kwamba tukifika mwaka 2020 nadhani maswali mengi sana yatakuwa yamejibiwa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, katika ujenzi wa barabara kuna barabara nyingine zina changamoto. Naishukuru sana Serikali kwamba kwenye mipango ile ya Serikali ilishawekwa tayari. Kuna barabara moja ambayo wanaisema kila siku na huko kuna viwanda vingi na tumesema nchi yetu ni ya viwanda; kuna barabara ile ya Mafinga – Mgololo kilometa 84. Naiomba Serikali kama ilivyokuwa imeahidi, basi utekelezaji wake ukianza kwenye bajeti inayokuja nitafurahi sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine, kuna barabara ile ya Nyororo mpaka pale Mtwani. Hiyo barabara ikiwekwa kiwango cha lami itatusaidia sana kwa sababu kule kuna viwanda vingi sana halafu maeneo yale mvua zinanyesha sana kiasi kwamba magari makubwa yanashindwa kupita na kusafirisha ile mizigo mizito. Kwa hiyo, naiomba Serikali, katika ukanda huu wa Kusini, ikitujengea zile barabara za lami, basi itakuwa imefanya vizuri ili wenye viwanda vikubwa waweze kusafirisha mizigo yao. Vile vile hii barabara tunajua kabisa tuna kiwanda kikubwa cha Mgololo ambacho kinatengeneza karatasi kule, kinashindwa kusafirisha mizigo mizito, kwa hiyo, itakuwa imetusaidia. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nikienda kwenye nishati na madini kwa sababu muda ni mdogo; kwanza, nitoe pongezi kwa Serikali. Natoa pongezi kubwa sana kwa Mheshimiwa Waziri wa Nishati na Madini. Kwa kweli alifanya ziara kwenye Jimbo langu na aliongea na wananchi na kupongeza sana. Alichokiongea siku ile, utekelezaji wake umeanza. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tatizo moja la Watanzania, unataka kitu kifanyike mara moja, siku moja; lazima kuwe kuna hatua. Mimi nampongeza Waziri, sasa hivi ninavyoongea mkandarasi yuko site, kama alivyoongea. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naiomba Serikali, bahati nzuri ameandika kwenye ripoti yake; kuna maeneo yale ambayo yalirukwa. Katika survey kuna vitongoji vingine vimerukwa, naomba vile vitongoji ambavyo vimerukwa viweze kupewa survey tena ili viweze kupewa umeme kwa sababu wananchi wanalalamika, wanajua kama hawatapewa. Nakuomba kwenye majumuisho yako uwaambie wananchi kwamba yale maeneo yote ambayo yalikuwa yamerukwa, hayakufanyiwa survey kwamba mtafanya survey na watapewa umeme kama kawaida.
Mheshimiwa Naibu Spika, zile gharama za uingizaji umeme, naomba kwenye majumuisho tuwaambie wananchi zijulikane vizuri. Kwa sababu kuna watu wengine wanasema ile ya 177,000 kuna wengine kuna ile 27,000, kwa hiyo, inaleta mchanganyo kidogo. Sasa naomba Mheshimiwa Waziri anapotoa majumuisho, aliweke sawa hilo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna watu wengine wameanza kuchangia, wanasema wachangie fedha ya nguzo. Yaani mtu anataka aweke umeme pale, anaambiwa na TANESCO kwamba achangie fedha fulani. Mwananchi mmoja alisema anaambiwa achangie Sh.500,000 kwa ajili ya nguzo. Namwomba Mheshimiwa Waziri hili aliweke sawa, kwamba zile nguzo ni bure au kuna watu wengine wanatakiwa wachangie pale? Tunaona tunapata mchanganyiko sisi Wabunge tunaulizwa maswali ya namna hiyo. Kwa hiyo, leo tunategemea Mheshimiwa Waziri atupe majumuisho, masuala ya nguzo tuhakikishe kwamba kama ni bure ijulikane watu wanapelekewa bure.
Mheshimiwa Naibu Spika, halafu kuna shule nyingi tu zimerukwa. Kwa hiyo, tunaomba Mheshimiwa Waziri, zile Taasisi hasa shule, Zahanati na Vituo vya Afya, basi kama kuna exemption ya kuweka umeme kwenye hizi Taasisi, basi Mheshimiwa Waziri tunaomba majumuisho tuelezwe vizuri ili wananchi waelewe.
Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana na naunga mkono hoja. Ahsante sana.