Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2017 na Kamati ya Kudumu ya Nishati na Madini kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2017.

Hon. Stanslaus Haroon Nyongo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Maswa Mashariki

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2017 na Kamati ya Kudumu ya Nishati na Madini kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2017.

NAIBU WAZIRI WA MADINI (MHE. STANSLAUS H. NYONGO): Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi hii jioni ya leo. Kwanza kabisa natoa shukrani za dhati kabisa kwa Kamati ya Nishati na Madini kwa kazi nzuri walioifanya. Kamati ya Nishati na Madini kipekee kabisa tumekuwa tukipokea mchango mkubwa, ushauri maelekezo mbalimbali kutoka katika Kamati hii. Kwa kweli ushauri wao tunaupokea na ni ushauri mzuri na tutaendelea kushirikiana na Kamati hii kwa maana kuisukuma Sekta hii ya Madini iweze kusonga mbele.

Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile nawashukuru sana Waheshimiwa Wajumbe 14 waliochangia, wametoa michango mizuri michango yenye mashiko. Namshukuru na mama yangu Mheshimiwa Anne Kilango kwa complement aliyotupa. Kweli kabisa kwamba Wizara yetu imekuwa ikikusanya maduhuli kwa hali ya juu. Tunapambana usiku na mchana kuhakikisha tunakusanya maduhuli ambayo tunayapeleka katika Mfuko wa Serikali na Watanzania wote waweze kupata fedha au kupata huduma mbalimbali kutokana na makusanyo tunayokusanya kutoka katika Wizara yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kweli tunakusanya kwa kiasi kikubwa na ni mfano tuseme wa kuigwa kwa sababu mpaka hapa tulipo tuko katika nusu ya mwaka wa fedha wa kibajeti. Tumekusanya zaidi ya asilimia 80.4 ya maduhuli. Tunashukuru sana mama kwa kuliona hilo na tunashukuru kwa pongezi ulizotupa; na tutaendelea kukaza msuli kuhakikisha kwamba tunaendelea kukusanya maduhuli ili Watanzania wote waweze kupata huduma kutokana na mapato yanayopatikana katika Sekta ya Madini. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, michango mingi imeongelewa, nami napenda kuungana na waliochangia hasa katika ukurasa wa tano wa taarifa ya Kamati kuhusiana na mradi wa Buckreef. Ni kwamba STAMICO iliingia mkataba na Buckreef na kampuni ya TAZAM 2000 wakatengeneza Kampuni ya Bacliff ambapo STAMICO wanashikilia asilimia 45.

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kama ilivyosema Kamati tumelitazama hili, huyu mbia kwa kweli havutii na tumeamua kuangalia kwa namna nyingine ambapo STAMICO inawabidi wakae chini na wanasheria waweze ku- review mkataba huu ili tuweze kuangalia na ikiwezekana tutafute mbia mwingine ili STAMICO wahakikishe kwamba yule mbia atayepatikana basi aweze kufanya kazi vizuri na uchimbaji uendelee na Serikali iweze kujipatia kipato. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna hoja nyingine ambayo imeongelewa kuhusu pesa za ruzuku pamoja na pesa za mikopo zilizokuwa zinatolewa na Wizara. Kweli kabisa kwamba kuna watu walikuwa wanapokea ruzuku kutoka Serikalini, yaani kutoka Wizara ya Madini kupitia Benki ya TIB, walikuwa wanapata fedha kwa ajili ya kuendeleza migodi. Ilikuwa ni fedha maalum kwa kuendeleza wachimbaji. Kuna wachimbaji wengine walifanikiwa, wamefanya vizuri sana. Kuna wachimbaji wengine wamekwama, lakini inaonekana kabisa walikuwa na juhudi za kufanya vizuri lakini wamekwama. Wachimbaji wengine walichukua zile fedha na kwenda kuzitumia kwa matumizi mengine.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna wachimbaki tisa kwa taarifa tulizonazo. Napenda kuchukua nafasi hii kuwaeleza kwa mara mwisho, nilitoa tamko nikiwa Singida, warudishe hizo fedha. Nachukua nafasi kusema kwamba nimetoa tena tamko la mwisho, wala sina haja ya kutoa siku nyingi, ni kwamba ndani ya hizi siku 14 zinazofuata, wajisalimishe wenyewe, wazirudishe hizo fedha kwa sababu wamewanyima Watanzania wengine kuweza kupata fedha hizo na kufanya shughuli za uchimbaji wakaweza kuendeleza Sekta hiyo ya Madini. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna suala la wachimbaji wadogo, Wizara imejipanga vizuri, sasa hivi tumeshatenga zaidi ya heka za mraba laki 238 kwa ajili ya kuwapa wachimbaji wadogo waweze kuchimba, lakini tunahakikisha kwamba wachimbaji hao wadogo wakae ndani ya vikundi, tuwatambue tuwarasimishe wachimbe ili na Serikali nayo iweze kukusanya kodi, maduhuli na Halmashauri husika ziweze kupata ushuru wa huduma (Service Levy).

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna suala la GST limezungumziwa. GST ndiyo Taasisi pekee ambayo inaweza ikafanya kazi vizuri kwa maana ya kufanya tafiti mbalimbali na kuweza kuwasaidia wachimbaji wadogo kuwapatia maeneo ambayo tayari yameshafanyiwa utafiti, yana taarifa za kutosha kwa maana maeneo ambayo yana dhahabu ya kutosha au madini mengine ambayo tayari yamefanyiwa utafiti wa kutosha ili kuepusha wachimbaji kuchimba kwa kubahatisha. Tumejipanga na GST na kuja kuleta taarifa hizo.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kumalizia. Kwa migogoro iliyopo, tunaifanyia kazi na hasa ule mgogoro wa North Mara na watu wa Nyamongo, maongezi yanaendelea. Taratibu zinafanyika na makundi yote tunayashirikisha. Tunachotaka ni Serikali itatue mgogoro wa Nyamongo ili wachimbaji waendelee na wananchi waendelee na shughuli zao za ujenzi wa Taifa.

Mheshimiwa Naibu Spika, namalizia kwa kusema kwamba Kamati imeshauri kwamba kuna wachimbaji wa Kitanzania tuwape maeneo, akiwepo mchimbaji wa Busolwa. Tunahakikisha mchimbaji huyo tunampa eneo ili aongeze muda wa mgodi, Watanzania waneemeke na ajira katika mgodi huo na Serikali tuendelee kupata kodi kutoka katika mgodi huo kwa sababu mgodi huo unafanya kazi. Hakuna haja ya kumnyima eneo ambalo tunadhani Serikali tunaweza tukampa na kukamsaidia mchimbaji mdogo na wa kati.

Mheshimiwa Naibu Spika, Watanzania wengine wote wanaotaka kuwekeza katika Sekta ya Madini, tuko tayari kuwasaidia kuwapa maeneo mazuri wachimbe na tutaweza kuwasaidia kwa namna ambayo watatoa ajira kwa Watanzania wengine…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)