Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Chato
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Naibu Spika, nami niungane na wenzangu kushukuru sana kwa kunipa fursa hii ili niweze kuchangia Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Nishati na Madini, lakini kwa upande wa Nishati. Kwanza, nampongeza Mheshimiwa Naibu Waziri, ameeleza kwa kiasi fulani mipangilio yetu kuhusiana na miradi ya umeme vijijini. Nami nampongeza sana Mheshimiwa Naibu Waziri wangu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa, naishukuru sana Serikali ya Awamu ya Tano jinsi inavyotoa pesa za kutosha katika kutekeleza miradi ya REA awamu ya tatu. Kwa takwimu tulizonazo katika kipindi kama hiki, mwaka wa fedha 2015/2016, tulipata asilimia 78.8 katika kipindi kama hiki cha miradi ya REA awamu ya tatu. Katika kipindi cha mwaka 2016/2017, tulipokea asilimia 79.3, kwa hiyo, tuliongeza asilimia moja. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nitoe taarifa mbele ya Bunge lako Tukufu katika kipindi hiki cha nusu ya mwaka, tumepokea asilimia 81.3. Kwa niaba tu ya Wizara yangu na wengine, nichukue nafasi hii kuishukuru sana Wizara yetu inavyoshirikiana na Wizara ya Fedha pamoja na Serikali ya Awamu ya Tano. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niwape tu uhakika wananchi na Waheshimiwa Wabunge kwamba kwa utaratibu huu, tuna uhakika mkubwa kwamba miradi hii itatekelezwa kwa asilimia mia moja ndani ya muda mliotupatia na sisi tutafanya kazi kwa nguvu zote kuhakikisha kwamba kazi inakamilika kwa wakati.
Mheshimiwa Naibu Spika, tumetaja mikoa ambayo tumeshaanza kutekeleza, lakini nichukue nafasi hii kuwaeleza wananchi na Waheshimiwa Wabunge, mpaka sasa tumeshawasha umeme vijiji 24 chini ya mpango huu mpya wa REA awamu ya tatu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, namshukuru sana Mheshimiwa Heche. Nitoe tu taarifa kwamba kwenye Jimbo lake tumeshawasha Kijiji cha Nyangere kwenye Jimbo lake. Kwa hiyo, tayari tumeshamwashia umeme kwenye ile awamu ya tatu. Hata kule Butiama tumeshawasha umeme Masusura; kule Mwanza tumeshawasha Ipanga na Nguge; Geita tumeshawasha Nyangomango; kule Mtwara tumewasha Nalingo; kule Arusha tunawasha Didigo; tunakwenda kuwasha kijiji hadi kijiji. Kwa hiyo, nitoe taarifa kwamba tunakwenda vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nizungumze kidogo kwenye suala la madeni ya TANESCO. Nami nawapongeza Waheshimiwa Wabunge kwa kuunga mkono kwamba Shirika letu kwa kweli linahitaji kupewa msukumo wa aina yake. Nazipongeza pia Taasisi za Serikali ambazo zilikuwa zinadaiwa kwa kiasi kikubwa, zimeanza kulipa madeni yake. Kwa hiyo, nawapongeza sana Waheshimiwa Wabunge jinsi mnavyosukuma kwenye Halmashauri zenu, kiasi ambacho sasa tumeanza kupata mapato mazuri kutoka kwenye Taasisi za Maji, Jeshi letu, Mambo ya Ndani na Taasisi nyingine za Serikali.
Mheshimiwa Naibu Spika, mpaka sasa deni kidogo limepungua. Lilikuwa shilingi bilioni 297, sasa limebaki shilingi bilioni 277. Kwa hiyo, ni maendeleo makubwa. Nawaomba tu Waheshimiwa Wabunge kupitia kwenye taasisi zetu, basi tuendelee kuliunga mkono Shirika letu ili liweze kuwahudumia vizuri na kwa asilimia ambazo wananchi wetu wana matarajio nalo.
Mheshimiwa Naibu Spika, nizungumze kidogo kuhusiana na mradi wa Stieglers. Mheshimiwa Heche amezungumza kwamba tumeanza kuutekeleza. Niseme tu, utekelezaji wa mradi wa aina yoyote una hatua zake. Hatua ya kwanza ya kawaida ya kutekeleza mradi ni maandalizi ya mradi. Hatua ya pili ni kufanya matayarisho ya miundombinu wezeshi kutekeleza mradi; na hatua ya tatu ni ya kujenga mradi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sasa tunachofanya ni kuandaa na kutayarisha mazingira wezeshi ya kuutekeleza mradi huo kabambe. Ndiyo maana hivi sasa kwa upande wa miundombinu ya umeme tumeanza kujenga miundombinu ya umeme kupitia Shirika letu la TANESCO ambalo bajeti yake ilipita katika mwaka wa fedha huu tunaoendelea nao. Shilingi bilioni 7.7 zilipitishwa kwa ajili ya miradi ya Morogoro; na mradi unaojengwa sasa kwenda kule ni kupitia bajeti ya Serikali kupitia TANESCO. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya hapo tutafanya utaratibu na tunaendelea na utaratibu sasa wa kutangaza tenda. Tutakapoukamilisha, ndipo sasa tutajua ni kiasi gani na utekelezaji wa mradi huo utaanza na taratibu za kawaida za kibajeti kuja kwenye Bunge lako Tukufu zitafuatwa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, niseme tu kwamba bado maandalizi yanaendelea, lakini nawaomba wananchi na Waheshimiwa Wabunge tuunge mkono juhudi za Serikali za Mheshimiwa Rais za kuujenga mradi huu kwa sababu utatutoa kwenye shida za upungufu wa umeme na kuwa na umeme wa uhakika wa kujenga uchumi wa viwanda tunaotarajia. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na hilo, nizungumze kidogo kuhusiana na miradi ya umeme kule Mtwara na Lindi. Nawapongeza sana Waheshimiwa Wabunge wa Mtwara na Lindi kwa jinsi ambavyo mwezi Novemba tulikuwa na shida kidogo, lakini tuliungana pamoja, mwezi Novemba Mtwara tulibaki na mashine tatu zinazofanya kazi hadi kufika Novemba, 2017. Hata hivyo, nitoe taarifa kwa Waheshimiwa Wabunge kwamba hivi sasa mashine zinazofanya kazi kwa Mtwara na Lindi, mashine zote sasa tisa sasa zinafanya kazi. Zimekarabatiwa, zinafanya kazi vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niungane na Mheshimiwa Mbunge wa Mtwara kwamba mliomba mashine mbili mpya, tumeshazileta na zimeshaanza kufungwa. Ni matarajio yetu ndani ya miezi miwili nazo zitakamilika. Kwa hiyo, Mtwara na Lindi tutaanza kupata umeme wa megawatts nne za ziada. Kwa hiyo, naipongeza sana Serikali yetu na Waheshimiwa Wabunge mnavyotuunga mkono katika jitihada hizi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu ya muda tu niseme; kweli kabisa katika Mikoa ya Ruvuma na Mtwara tuna changamoto ya miundombinu, lakini tunaendelea kukarabati na kujenga miundombinu mingine mipya. Katika Mikoa ya Sumbawanga, Kigoma pamoja na Katavi ni kweli tunatumia mafuta mazito kwa sasa, lakini Serikali Tukufu kupitia Bunge hili katika bajeti ya mwaka huu mlituidhinishia shilingi bilioni 13.2 kwa ajili ya kujenga umeme mkubwa wa kilovolts 400 wa kutoka Sumbawanga kwenda Mpanda, Kigoma, Nyakanazi, Geita mpaka Bulyanhulu. Hivi sasa utekelezaji umeshaanza. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kipande cha Geita – Nyakanazi, Mkandarasi yuko site ameshaanza ujenzi; kwa kipande cha Bulyahkhulu kwenda Geita Mkandarasi yuko site, ameshaanza ujenzi na kwa kipande cha kutoka Mbeya kwenda Sumbawanga, Mkandarasi taratibu za kwanza za kufanya survey anakamilisha; na kufika Julai mwaka huu ataanza ujenzi rasmi. Kwa hiyo, upande wa Sumbawanga napo utapata umeme mkubwa wa kilovolts 400 kwa ajili ya ujenzi wa uchumi wa viwanda vyetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, labda la mwisho kwa sababu ya muda nizungumze kidogo kuhusiana na suala la bei za umeme wa REA pamoja na TANESCO. Bei ya umeme kijijini ni Sh.27,000/= basi, hakuna bei zaidi ya hapo. Kwa miradi ya TANESCO ambayo iko katika Mitaa na katika Halmashauri za Mijini ni Sh.177,000/= basi. Hizi ni bei ambazo Serikali kwa kiasi kikubwa imechangia.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nichukue nafasi hii bado kuipongeza Serikali. Hakuna nchi kwa nchi zinazoendelea zenye gharama ya umeme Sh.27,000/= hata vijijini, hakuna. Tanzania ni bei yetu ya kwanza. Kwa hiyo, naipongeza sana Serikali kwa utaratibu huo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hakuna mteja anayelipia nguzo. Ni vizuri nikaliweka bayana suala hili. Gharama za umeme wananchi tunachangia. Gharama ya kununua nguzo moja ni Sh.200,000/= hadi Sh.250,000. Sasa kama ingekuwa ni kulipia nguzo ingekuwa gharama kubwa sana. Kinachofanyika ni kutoa huduma kwa umbali wa huduma zinazoweza kupewa kwa mteja, lakini siyo kulipa nguzo. Kwa hiyo, nguzo hazilipiwi, ni kuchangia juhudi za Serikali katika kutandaza umeme.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, nimalizie tu na kusema kwamba, kwa vile sasa hivi tunatekeleza miradi ya umeme vijijini, niwaombe sana Waheshimiwa Wabunge, lengo letu ni kupeleka umeme kijiji kwa Kijiji, Kitongoji kwa Kitongoji, nyumba kwa nyumba, taasisi kwa taasisi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo nawaomba Waheshimiwa Wabunge katika Taasisi za Umma muwashawishi na kuwashauri Wenyeviti wa Halmashauri waanze kutenga fedha kidogo ili kuzifikishia taasisi zetu umeme. Haipendezi na siyo matarajio ya mradi, nguzo kuning’inia karibu na Taasisi ya Umma halafu Taasisi ya Umma isipate umeme ndani ya nyumba. Kwa hiyo, nichukue nafasi hii kuwaelekeza na kuwashauri Waheshimiwa Wakurugenzi walipo waanze kufanya hivyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, la mwisho nachukua nafasi hii kuwaagiza Wakandarasi popote walipo, tumeshawaelekeza, mwisho wa kuanza kazi ambao hawajaanza ni tarehe 2 Machi, lakini kwa kiasi kikubwa wameshaanza kutekeleza.
Mheshimiwa Naibu Spika, nachukua nafasi hii kukupongeza kwa kunipa nafasi hii. Ahsante sana. Nashukuru kwa kunisikiliza.