Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2017 na Kamati ya Kudumu ya Nishati na Madini kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2017.

Hon. Prof. Norman Adamson Sigalla King

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Makete

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2017 na Kamati ya Kudumu ya Nishati na Madini kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2017.

MHE. PROF. NORMAN A. S. KING - MWENYEKITI WA KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE YA MIUNDOMBINU: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nawashukuru sana Waheshimiwa Wajumbe wote ambao wametoa michango yao. Naomba uniruhusu niwatambue kwa majina hasa wale ambao wameandika, kwa sababu wale ambao wamechangia hapa ndani wote mliwaona.

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kumshukuru Mheshimiwa Ritta Kabati, Mheshimiwa Shelukindo, Mheshimiwa Oran Njeza, Mheshimiwa Juma Othman Hija, Mheshimiwa Aida Joseph Khenani, Mheshimiwa Eng. Ramo Makani, Mheshimiwa Rhoda Edward Kunchela, Mheshimiwa Silafu, Mheshimiwa Mashimba Ndaki, Mheshimiwa Mary Deo Muro, Mheshimiwa Lucia, Mheshimiwa Zainab na Mheshimiwa Lucy Owenya.

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kuweka kumbukumbu sawasawa, nadhani ni Mheshimiwa Shekilindi badala ya Mheshimiwa Shelukindo. Umetaja Shelukindo hapo, nadhani ni Mheshimiwa Shekilindi. Sasa sema ili kumbukumbu rasmi za Bunge ziwe na jina linalotuhusu kwa sasa.

MHE. NORMAN A. SIGALLA KING - MWENYEKITI WA KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE YA MIUNDOMBINU: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na michango mingi ya Wabunge pia nichukue nafasi hii kipekee kuwapongeza Mawaziri kwa maana Waziri Mheshimiwa Profesa Mbalawa pamoja na Naibu wake kwa michango yao kwenye hoja hii. Nitoe ufafanuzi katika mambo machache. Kwanza Waheshimiwa Wabunge wote waliochangia wameipongeza Serikali ya Chama cha Mapinduzi kwa kazi kubwa inayofanya, nasi tunapokea pongezi hizo. Pia wengi wameongelea umuhimu wa kuunganisha barabara za lami, nashukuru kwamba Mheshimiwa Wazirri amefafanua vizuri jambo hilo.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia kuna hoja ya kuangalia uwezekano wa kuunganisha barabara za mikoa, nashukuru Mheshimiwa Waziri pia ametoa ufafanuzi mkubwa kwenye hilo. Pia kuna hoja ya uwanja wa Chato na pia hoja ya kujenga uwanja Mkoa wa Mara; nafikiri haikujibiwa na ni vizuri nitoe ufafanuzi.

Mheshimiwa Naibu Spika, ni vizuri Waheshimiwa Wabunge na Bunge lako lifahamu; mimi nimeshiriki kwenye uwekaji wa jiwe la msingi uwanja wa Chato. Shilingi bilioni 39 zilizotajwa ni gharama za ujenzi mradi ukikamilika. Kilichofanyika Chato ni kuweka jiwe la msingi. Kuhusu fedha za bajeti kwa mwaka huu wa fedha kwa mfano, 2018/2019, wale Wajumbe watakaokuwa kwenye Kamati ya Miundombinu wataona bajeti hiyo. Kinachoonekana sasa ni kama vile umeshajengwa. Haujajengwa, tulichofanya ni kuweka jiwe la msingi. Hilo ni la kwanza.

Mheshimiwa Naibu Spika, la pili, pia aliuliza vizuri rafiki yangu, Mbunge wa Sengerema kwamba kwa nini uwanja haujajengwa Mkoa wa Mara? Je, kwa nini Serikali inapeleka nguvu upande wa Chato?

Mheshimiwa Naibu Spika, Waheshimiwa Wabunge na Bunge lako Tukufu, ni vizuri watu wafahamu, mpaka Mwalimu Nyerere anatoweka tarehe 14 Oktoba, 1999 viwanja ambavyo vilikuwa vimejengwa Tanzania hii ni vichache sana na hasa viwili vikubwa ni uwanja wa KIA na uwanja wa Dar es Salaam. Viwanja vingine vya Kigoma na Tabora na kwingineko, wote tulikuwa tunatua na ndege kwa mashaka, siyo kwa kujengwa. Kwa hiyo, lawama ziende kwa nani?

Mheshimiwa Naibu Spika, Rais Dkt. Magufuli ameingia wakati Mheshimiwa Rais wetu Mwasisi wa nchi hii alishaondoka katika nchi hii. Kwa hiyo, siyo sawa hata kidogo kwa hekima yote ile kupeleka lawama kwa Rais wa Awamu ya Tano wakati, Rais wa Awamu ya Pili alikuwepo, ya Tatu alikuwepo, ya Nne alikuwepo na muda huo viwanja havikujengwa kwa sababu ya uwezo wa uchumi kuwa mdogo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu utangazaji wa tenda labda nayo niifafanue kidogo. Ni vizuri Bunge lako Tukufu likafahamu, utangazaji wa tenda wa viwanja au miradi mingine ya Serikali imegawanyika katika sehemu kuu mbili; unaweza ukafanya kitu kinachoitwa open tender kwa maana ya kwamba unatafuta Mkandarasi wa ujenzi wa uwanja au jambo lolote ndani ya Serikali au restricted tender.

Mheshimiwa Naibu Spika, wakati gani unatumia restricted tender? Ni pale ambapo Wakandarasi ambao tayari unao wanafanya miradi mingine; unataka mradi mwingine unaofanana na kazi ambazo tayari Wakandarasi wapo, unataka utekelezwe. Badala ya kupoteza muda kufanya open tender, unafanya kitu kinachoitwa restricted tender, kwa maana ya kwamba unachagua katika wale ambao tayari wapo na unaangalia nani mwenye bei ndogo halafu unampa kazi.

Mheshimiwa Naibu Spika, Procurement Act iko wazi na wala siyo kwamba ni jambo linafanywa kwa kificho, liko wazi kwenye kufanya hivyo, kwa hiyo, chochote utakachofanya katika hivyo, ni sahihi. Kwenye Halmashauri zetu tunafanya hivyo na kwenye Serikali Kuu tunafanya hivyo pia.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nitumie dakika chache kupongeza kwa dhati taasisi ambazo Kamati hii inazisimamia. Nianze na taasisi kama TCRA; siwezi kuzitaja zote 37 na CEOs kokote waliko wajue kwamba nazitaja hizi tu kama mfano. TCRA, Kamati iliagiza kwamba watekeleze utaratibu wa TTMS ili tuwe na hakika ya mapato ambayo Serikali inapata. Wameshirikiana na wenzao wa TRA na sasa kazi inafanyika vizuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, Kamati ilielekeza TPA kwamba wajaribu kurekebisha kero za Bandari ya Dar es Salaam ikiwa ni pamoja na ucheleweshaji na siku zinazochukuliwa katika kupakua na kupakia pamoja na tozo mbalimbali. TPA wamerekebisha jambo hilo na sasa mambo yamekwenda vizuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, wanaoagiza mizigo kwa kutumia Bandari ya Dar es Salaam kwa sasa watakuwa ni mashuhuda kwamba hata vitu vilivyokuwa vinanyofolewa kwenye magari au kwenye magari tunayoagiza, sasa hivi wizi huo haupo tena. Pongezi sana kwa TPA pongezi sana kwa CEO wa TPA pia.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia Tanzania Buiding Agency (TBA) ambayo ndiyo taasisi iliyopewa madaraka ya kujenga miradi mbalimbali ya Serikali na hasa majengo, imefanya kazi nzuri sana. Kwa mfano, imejenga hostel pale Chuo Kikuu Dar es Salaam. Gharama za kampuni ya Kichina iliyokuwa ime-tender ilikuwa shilingi bilioni 80 kumaliza mradi ule. Wao wametumia shilingi bilioni 10. Pia ukienda kwa mradi wa hostel za Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ndiyo kama hivyo, lakini ukienda mradi mwingine kama wa Ihungo, wengine wali-tender shilingi bilioni 60, lakini wao wamemaliza kwa shilingi bilioni 11. Wameenda hivyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, nenda Mlonganzila, hivyo hivyo; wamekwenda wakitekeleza miradi mingi kwa karibu ten percent of the entire total ukilinganisha na Wakandarsi wengine. Lazima tuwapongeze sana TBA na CEO wake kwa kazi kubwa na nzuri wanayofanya katika kutekeleza miradi mbalimbali. Unakuja bodi za Wakandarasi na za Wahandisi; wote wamefanya kazi nzuri sana. Wakandarasi ambao wamekuwa wakizembea kutimiza viwango wameondolewa kwenye roster ya Wakandarasi Tanzania. Ni kazi nzuri sana inayofanywa na taasisi hizi.

Mheshimiwa Naibu Spika, nikitaja MSL pale Mwanza, ameteuliwa Kaimu Mkurugenzi. Kwa muda mfupi tu wa miezi michache aliyokaa, ameweza kuifanya meli ya MV. Liemba ambayo ilionekana kama haifai pale Kigoma na ilikuwa inaripotiwa kwamba imeleta hasara kila trip ya shilingi milioni nne. Yeye kwa trip moja ameweza kusimamia na kupata shilingi milioni 15. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika na Waheshimiwa Wabunge wa Bunge lako Tukufu, kwa hiyo, hii inaonesha kwamba kuna vitu viwili muhimu ambavyo lazima Wizara hii iendelee kufanya. Moja, ni uteuaji kwa kufuata weledi wa Watendaji wanaosimamia taasisi mbalimbali zilizo chini ya Wizara hii; lakini pili, kufuatilia kwa makini ili kuona jinsi gani ambavyo tunaweza kuisaidia Tanzania na Serikali kwa ujumla kupata maendeleo. Ndiyo maana nimesema nizitaje taasisi kwa uchache.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, nitakuwa nimekosa fadhila kama nisiporudia kusema nashukuru sana Waheshimiwa Wabunge wa Bunge hili kwa michango yao kutoka pande zote kwa vyama vyote. Michango yenu imekuwa ya muhimu sana na tumeichukua, tutazidi kuisheheni na kuiweka vizuri ili kwamba kwenye vikao vijavyo tuweze kuisaidia Serikali yetu kutekeleza mipango yake.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, naomba sasa kutoa hoja kwamba taarifa ya utekelezaji ya shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu kwa kipindi cha Januari, 2017 hadi Januari, 2018 sasa ipokelewe na Bunge lako Tukufu kama taarifa rasmi.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kutoa hoja.